Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 2/1 kur. 26-31
  • Nimeiona Ikikua Kusini mwa Afrika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nimeiona Ikikua Kusini mwa Afrika
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mambo Yalianza kwa Msiba
  • Miaka ya Mapema ya Kupainia
  • Katika Nchi Nyinginezo
  • Mapendeleo ya Betheli
  • Badiliko Katika Cheo
  • Kukabili Mnyanyaso wa Wakati wa Vita
  • Ofisi Mpya ya Tawi
  • Mgawo Mwingine wa Kuhubiri
  • Mibaraka na Mambo ya Kuridhisha
  • Kulea Watoto Afrika Wakati wa Magumu
    Amkeni!—1999
  • Nilichagua kazi inayofaa
    Amkeni!—2007
  • Sehemu ya 2—Kuwa Mashahidi Hadi Sehemu ya Mbali Zaidi Sana ya Dunia
    Mashahidi wa Yehova—Wapiga-Mbiu wa Ufalme wa Mungu
  • ‘Twaishi Si kwa Ajili Yetu Wenyewe Tena’
    Amkeni!—1998
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 2/1 kur. 26-31

Nimeiona Ikikua Kusini mwa Afrika

Kama ilivyosimuliwa na Robert Albert McLuckie

UTENDAJI wa kuhubiri Ufalme katika Afrika Kusini wasonga mbele kwa njia yenye fahari. Kutoka kwenye wale mia moja hivi waliokuwa wakihubiri mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1920, sasa kuna karibu 45,000 wenye kujulisha wazi habari njema katika Afrika Kusini. Na wengine 150,000 hivi wanahubiri katika nchi nyinginezo ambako ni tawi letu la Afrika Kusini lililokuwa likifanya uangalizi hapo kwanza.

Mimi nimekuwa na shangwe ya kuona ukuzi huu wa ajabu kusini mwa Afrika wakati wa miaka 60 iliyopita! Acha nikueleze kifupi kuhusu jambo hilo na kuhusu ushiriki ambao jamaa yangu na mimi tumependelewa kuwa nao.

Mambo Yalianza kwa Msiba

Siku ya Juni 22, 1927, mke wangu mpendwa, Edna, alikufa, akimwacha nyuma binti yetu, Lyall, mwenye miaka mitatu na mwana wetu, Donovan, mwenye miaka miwili. Mimi nilikuwa na miaka 26 tu. Kifo cha mke wangu kiliniacha na kihoro kingi sana nami nikawa nimetatanishwa mawazo. Yeye alikuwa wapi? Kwa kutoamini kwamba alikuwa katika helo, usiku nilipata kiasi fulani cha faraja kwa kuota kwamba alikuwa mbinguni.

Julai hiyo Donovan mdogo alinipa kijigazeti kilichokusudiwa anwani ya mtu mwingine lakini kwa njia fulani kikachanganyika na barua zetu. Kilikuwa na hotuba moja iliyotolewa na Joseph Rutherford, msimamizi wa pili wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi. Yaliyokuwamo yalinipendeza sana hata nikaharakisha kuagiza vichapo vyote vilivyoorodheshwa. Wakati huo sikung’amua kwamba kufanya hivyo kungebadili maisha yangu.

Miongoni mwa vijitabu vilivyofika, kile kimoja chenye kichwa Hell​—What Is It? Who Are There? Can They Get Out? kilikumbana na macho yangu. Nilisisimuka kama nini kuona kijitabu hicho! Baada ya kurasa mbili tatu tu, kwa kweli nikacheka kwa upendezo mwingi.

Nikiwa na hamu ya kushiriki mambo niliyokuwa nimejifunza, niliwaandikia barua au nikanena na wazazi wangu na washiriki wengine wa jamaa. Tokeo ni kwamba, ndugu zangu wanne, Jack, Percy, William, na Sydney, walipendezwa baada ya muda mfupi na wakaanza kuhubiria wengine. Miaka kadhaa baadaye, baba yangu, mama, na dada zangu wawili, Connie na Grace, waliikubali imani pia.

Katika sehemu yetu ya Afrika Kusini sikuweza kupata Mwanafunzi wa Biblia mwingine, kama vile Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo. Nilihamia Rhodesia ya Kusini, sasa Zimbabwe, nikafanya kazi kwa karibu mwaka mmoja katika shamba kubwa la ng’ombe nikiwa pamoja na Jack ndugu yangu. Kutokana na kusoma fasihi za Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, punde si punde nikahisi tamaa yenye kunihimiza niingie huduma ya wakati wote.

Kufikia hapo sikuwa nimekutana na waamini wenzi wowote isipokuwa wale ambao mimi nilikuwa nimewapa ushahidi. Kwa hiyo nilifunga ile safari ya kilometa 2,300 kwenda ofisi ya tawi la Sosaiti kule Cape Town, Afrika Kusini. Nilipokea upokezi mchangamfu kama nini kutoka kwa George Phillips, aliyekuwa akisimamia kazi kusini mwa Afrika! Siku ya Januari 10, 1930, nilibatizwa.

Miaka ya Mapema ya Kupainia

Ingawa nilikuwa nimeongea na mamia ya watu kuhusu Biblia wakati wa miaka mitatu iliyotangulia, nilikuwa sijashiriki katika huduma ya nyumba kwa nyumba. Hata hivyo, niliandikishwa katika huduma ya wakati wote kuwa painia. Hakukuwa na programu ya mazoezi siku hizo. Kwa uhakika, ni mara chache ambapo wahubiri wangeenda pamoja kwenye nyumba ile ile moja. Kwa maana tulikuwa na wahubiri wachache sana, haikuonekana kabisa ikifaa kufanya hivyo.

Kiasili, mimi nilihangaikia hali njema ya watoto wangu, Lyall na Donovan, waliokuwa wakitunzwa na babu yao na nyanya yao. Kwa maana walikuwa wakipokea utunzi mwema, wakati huo nilihisi ilifaa nijitumikishe katika kueneza ujumbe wa Ufalme kwa wengine. Basi nikafanya hivyo.

Wakati wa miaka mitatu iliyofuata ya kupainia, nilipata wafanya kazi watano wenzangu, kutia na Syd ndugu yangu. Baadaye yeye alipata homa mbaya ya tumboni akiwa katika upainia na akafa. Kupainia hakukuwa rahisi siku hizo za mapema. Tulitumia gari la kibiashara lenye nafasi ya mizigo, likiwa na vitanda vilivyojengwa kwa ndani, vilivyofanyizwa kwa njia ya kuweza kukunjwa upande huu na huu wa gari hilo. Hiyo ilituwezesha kulala, kuketi, kupika, na kula tukiwa ndani.

Tukio lililo la kutokeza zaidi la siku zangu za mapema za upainia ni wakati tulipopokea jina letu jipya, Mashahidi wa Yehova, katika 1931, pamoja na kile kijitabu The Kingdom​—The Hope of the World. Nakumbuka wazi sana kwamba nilijawa mno na hofu nilipofikiri juu ya kutumia jina hilo lenye fahari nyingi, nikishangaa kama ningeweza kulitumia kwa ustahiki.

Tukio jingine lenye kukumbukika katika miaka hiyo ya mapema ni kwamba mimi nilibatiza ndugu yangu Jack na mke wake, Dorrell, katika yale maji yenye mamba wengi ya Mto Nuanetsi katika Rhodesia ya Kusini. Kabla ya uzamisho huo, tulitupa miamba fulani ndani ya mto huo ili kufukuza mamba wowote wenye kuotea. Baadaye, katika miaka ya 1950, nilibatiza mama yangu katika kiogeo cha bafu.

Katika Nchi Nyinginezo

Katika 1933 mfanya kazi mwenzangu wa tano, Robert Nisbet, na mimi tuligawiwa kwenda kwenye eneo bichibichi, lisiloguswa​—visiwa vya Mauritius na Madagascar kando ya pwani ya kusini-mashariki ya Afrika. Tulitumia sehemu kubwa ya miezi minne katika visiwa viwili hivyo, tukipanda mbegu za ukweli wa Biblia. Sasa ni shangwe iliyoje kuona kwamba Mauritius ina wahubiri wa Ufalme 800 hivi na Madagascar ina wapatao 3,000! Tuliporudi Afrika Kusini, Robert na mimi tuliacha uandamani wetu. Baadaye yeye alipainia pamoja na Syd ndugu yangu na baadaye zaidi akatumikia akiwa mwangalizi wa tawi katika Mauritius.

Kabla ya kurudi kwetu Afrika Kusini, nilipanga kukutana na Lyall na Donovan nyumbani kwa baba yangu. Baada ya kumtembelea, ulikuja ule mtengano usioepukika, ukiandamana na machozi. Nikasonga mbele na safari yangu nikakutane na mwangalizi wa tawi, Ndugu Phillips, ili nipokee mgawo wangu ufuatao. Ulikuwa Nyasaland, sasa Malawi. Nilinunuliwa gari la muundo wa 1929 wa Chevrolet ili nilitumie huko.

Kwa hiyo, katika 1934, nikafunga ile safari ya kilometa 1,900, sana-sana nikipita katika barabara za mavumbi, kutoka Johannesburg, Afrika Kusini, kwenda Zomba, mji mkuu wa Nyasaland. Hatimaye nikafika nilikokuwa nikienda, kwenye nyumba ya ndugu mmoja Mwafrika, Richard Kalinde. Akawa mwandamani wangu wa karibu na mkalimani wakati wa kukaa kwangu Nyasaland. Baada ya muda, nilipata vyumba viwili katika hoteli moja ya zamani isiyokuwa ikitumiwa tena. Nilitumia kimoja kuwa ofisi-bohari, na kile kingine kuwa mahali pa kulala.

Mgawo wangu katika Nyasaland ulikuwa hasa kuleta utengemano katika hali zenye msukosuko uliotokana na zile zenye kuitwa harakati za Kitawala (“Watchtower”) eti. Miaka kadhaa kabla ya hapo, Mwafrika mmoja, mwenye kuzoeana na miandiko ya msimamizi wa kwanza wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, Charles Taze Russell, alikuwa amekuwa na daraka la usitawi wa harakati hizi, hata ingawa yeye mwenyewe hakupata kamwe kuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.​—Ona 1976 Yearbook of Jehovah’s Witnesses, kurasa 71-4.

Nilizuru makundi ya wale waliokuwa wanatumia fasihi za Mnara wa Mlinzi na nikasoma azimio moja kuhusu jina letu jipya, Mashahidi wa Yehova. Wote wenye kupendelea azimio hilo waliombwa waonyeshe hivyo kwa kuinua mikono. Ingawa walio wengi walionyesha kukubali, wengi hawakuelewa kikamili mambo yaliyohusika hasa. Hivyo, muda wa miaka iliyofuata, ingawa baadhi yao hawakufanya maendeleo ya kiroho, wengine waliacha kabisa kumuunga mkono mmoja ambaye walikuwa wamemwona kuwa kiongozi na wakawa kikweli Mashahidi wa Yehova.

Baada ya kuwa katika Nyasaland karibu miezi sita, nilivuka nikaingia Msumbiji, ambako ujumbe wa Ufalme ulikuwa bado haujapigiwa mbiu. Huko nikakuta ofisa kijana Mreno ambaye Robert Nisbet na mimi tulikuwa tumeonana naye tukiwa katika mashua ya kwenda Mauritius. Alinialika kwenye mlo, nami nikaweza kunena naye zaidi.

Katika pindi nyingine, nilipokuwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Msumbiji, gari moja lilisimama karibu nami. Kumbe ikawa ni gavana wa eneo lile. Aliuliza kama angeweza kunisaidia na akanialika kwenda nyumbani kwake, ambako alikubali vingi vya vichapo vya Mnara wa Mlinzi. Hata ingawa sasa kazi ya kuhubiri ni marufuku katika Msumbiji na Nyasaland (Malawi), inanisisimua kujua kwamba kuna ndugu na dada wengi waaminifu walio watendaji huko.

Mapendeleo ya Betheli

Baada ya mimi kurudi Nyasaland, nilipokea mshangao ulioje! Nilialikwa nijiunge na wafanya kazi wa ofisi katika tawi la Afrika Kusini kule Cape Town, na William ndugu yangu mchanga alitumwa akachukue mahali pangu katika Nyasaland. Kwa hiyo mimi nikafunga ile safari ya kilometa 3,500 nikiwa katika Chevrolet. Nikiwa njiani nilizuru Donovan na Lyall. Sasa walikuwa na umri wa miaka 11 na 12, na ungepita mwaka mwingine mmoja kabla sijawaona tena.

Niligawiwa kusimamia ofisi ya tawi wakati wowote ambapo Ndugu Phillips, mwangalizi wa tawi, hakuwapo. Ingawa sikuwa nimeshirikiana kwa ukawaida pamoja na kundi lolote moja la Mashahidi wa Yehova tangu nilipojifunza ukweli miaka tisa mapema, katika 1936 niliwekwa rasmi kuwa mwangalizi-msimamizi wa Kundi la Cape Town, la wahubiri karibu 20.

Badiliko Katika Cheo

Sikutaka kudhabihu mapendeleo yangu ya utumishi, lakini Lyall na Donovan walikuwa karibu kuingia miaka yao ya utineja, nami nilihangaikia hali njema yao, kutia na hali njema yao ya kiroho. Shukrani ni kwamba utatuzi fulani wa jambo hilo ulikuwa karibu.

Siku ya Juni 6, 1936, Ndugu Phillips alinijulisha kwa wawasili wapya kutoka Australia, Dada Seidel na binti yake mwenye kuvutia wa miaka 18, Carmen. Kabla mwaka huo haujaisha Carmen na mimi tukawa tumefunga ndoa. Kwa hiyo mimi nikajipatia kazi ya kimwili na kuanzisha makao.

Kwa mwaka mmoja nilikuwa na kazi fulani katika Afrika Kusini, lakini Carmen na mimi na mwana wetu mchanga, Peter, tukahamia Rhodesia ya Kusini, ambako Jack ndugu yangu alikuwa amenialika nijiunge naye katika jasirio la kuchimba mgodi wa dhahabu. Tulipokwisha kutulia, Lyall na Donovan, waliokuwa wamebaki nyuma pamoja na mama ya Carmen, walijiunga nasi.

Kukabili Mnyanyaso wa Wakati wa Vita

Katika Septemba 1939, Vita ya Ulimwengu 2 ilitokea ghafula, na mwaka uliofuata fasihi zetu za Biblia zikapigwa marufuku. Sisi tulipiga moyo konde tutahini uhalali wa sheria hiyo kwa kugawanya fasihi liwe lolote liwalo. Visa vya kukamatwa na kushtakiwa vikafuata, na vitabu vyetu na Biblia vikachukuliwa kwa nguvu na kuchomwa.

Asubuhi moja baada ya kazi yetu ya kuhubiri, tulialikwa na kachero (mpelelezi) mmoja tukachukue watoto wetu kwenye kituo cha polisi walikokuwa wamepelekwa. Sisi tulikataa, tukionyesha wazi kwamba kwa sababu ilionekana wachanga hao walikuwa wamekamatwa, ilikuwa juu ya polisi kuwatunza. Alasiri hiyo, baada ya kurudi kutoka huduma ya shambani, tuliwapata watoto nyumbani wakiwa salama lakini hakuonekana hata polisi mmoja!

Katika pindi nyingine, katika 1941, Carmen alihukumiwa kifungo cha miezi mitatu gerezani hata ingawa alikuwa mja mzito. Hata hivyo Estrella alizaliwa kabla Carmen hajaanza kutumika kifungo chake. Badala ya kuniachia mtoto mchanga huyo, Carmen alichagua kwenda naye gerezani. Hivyo, Estrella akapata kuwa na yaya aliye mwanamke Mwafrika aliyekuwa ameua mume wake. Carmen alipoachiliwa, mwanamke huyo muua-mtu alisumbuka sana mawazo hata akalia kwa uchungu mwingi. Haya basi, Estrella alianza kupainia katika 1956 akiwa na miaka 15. Baadaye, akafunga ndoa na Jack Jones na kwa miaka zaidi ya 20 sasa ametumikia pamoja na mume wake katika Afrika Kusini na wakati uliopo kwenye makao makuu ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi katika Brooklyn, New York.

Baada ya muda mfupi mimi pia nilikaa miezi kadhaa gerezani kwa sababu ya kuhubiri. Nilipokuwa huko, katika Januari 1942, Joseph Rutherford alikufa. Nilishindwa kujizuia nisitokwe na machozi kadhaa usiku huo nikiwa katika seli yangu. Nilikuwa na fursa za kutoa ushahidi, na asubuhi moja ya Jumapili, kila mtu mwingineye akiwa katika ua wa nje ili kufanya mazoezi, nilibatiza mwanagereza mwenzangu aliyekuwa ameitikia ujumbe wa Ufalme.

Ofisi Mpya ya Tawi

Baada ya mimi kuachiliwa gerezani, nilijipatia kazi ya reli katika Bulawayo. Carmen alikuwa amejifunza kushona nguo akiwa gerezani na alitumia ujuzi huo kusaidia kuruzuku jamaa. Lyall alirudi kutoka Afrika Kusini, alikokuwa amekuwa akipainia, na pia akasaidia gharama mbalimbali. Tokeo ni kwamba, baada ya muda mfupi tulichuma mapato mengi zaidi ya tuliyohitaji, kwa hiyo tukaongea jambo hilo, na mwafaka ukafikiwa kwamba mimi ningeweza tena kuchukua huduma ya wakati wote.

Kwa sababu nilikuwa na cheti cha kuniwezesha kusafiri kwa reli, katika 1947 nilienda kwa gari-moshi hadi Cape Town nikamwone Ndugu Phillips. Acha nishangae nilipogawiwa kufungua bohari la kushughulikia fasihi za Sosaiti katika Bulawayo. Halafu, mwaka uliofuata, Nathan H. Knorr, msimamizi wa tatu wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, akazuru na kupanga kwamba bohari hilo liwe ofisi ya tawi siku ya Septemba 1, 1948, huku Eric Cooke akiwa ndiye mwangalizi wa tawi la Rhodesia ya Kusini. Kwa miaka 14 iliyofuata, mimi nilipendelewa kufanya kazi kwenye tawi, bila shaka nikiwa ninaishi nyumbani pamoja na jamaa yangu yenye kukua. Nashukuru sana kwa tegemezo la kimwili ambalo Carmen na watoto wetu wenye umri mkubwa walitoa, wakiniwezesha kuendelea kufanya kazi kwenye ofisi ya tawi.

Mgawo Mwingine wa Kuhubiri

Kufikia 1962 Carmen na mimi tulitamani kusonga mbali zaidi katika shamba tukafanye kazi kwenye uhitaji mkubwa zaidi. Kwa hiyo tukauza nyumba yetu na kwenda pamoja na Lindsay na Jeremy, watoto wetu wawili walio wachanga zaidi​—wale wengine watano walikuwa wamekua wakaondoka nyumbani​—nasi tukaelekea kwenye Visiwa vya Ushelisheli.

Kwanza, tulisafiri kwa gari, sana-sana kwa kufuata barabara za mavumbi, kwa karibu kilometa 2,900, tukawasili Mombasa, Kenya. Tuliachia ndugu mmoja gari hilo tukapanda meli kwenda Ushelisheli. Mtu mwenye kupendezwa alitujulisha kwa wengine, na baada ya muda mfupi tukawa tunaongoza mikutano pale pale karibu na nyumba ya askofu. Tulifanya mikutano mingine katika kisiwa cha karibu katika nyumba-mashua ya mtu fulani iliyozungukwa na mitende mirefu na huku mawimbi yakikumba-kumba ufuo.

Baada ya muda mfupi utendaji wetu ukajulikana, na hatimaye wenye mamlaka wakatuagiza tuache kuhubiri, nasi tukawa hatuwezi kamwe kukubali kufanya hivyo. (Matendo 4:19, 20) Kwa kweli, basi, sisi tuliondoshwa nchini, lakini kwa wakati huo tukawa tumebatiza watu watano. Wakati wa kukaa kwetu miezi mitano katika Ushelisheli, Carmen akawa mja mzito kwa kumbeba Andrew, mtoto wetu wa mwisho. Tuliporudi Rhodesia ya Kusini, Pauline binti yetu alitualika tukae pamoja na yeye na mume wake tukingojea kuzaliwa kwa Andrew.

Mibaraka na Mambo ya Kuridhisha

Nina furaha kusema kwamba wanane kati ya watoto wetu, kutia ndani Lyall na Donovan, wamejihusisha katika kupainia nyakati fulani fulani. Kwa uhakika, wanne kati ya wana na wana-wakwe zetu ni wazee sasa, na wawili ni watumishi wa huduma. Kwa kuongezea, sisi twaterema kama nini kwamba wengi wa wajukuu na vitukuu vyetu pamoja na wazazi wao wanapiga mbiu ya taarifa za kuteremesha katika nchi zisizopungua nne na kwamba korija za washiriki wengine pia wa jamaa ya McLuckie wanatumikia Yehova. Mimi nasadiki kwamba matokeo hayo yamekuwapo kwa sababu ya jamaa kuhudhuria mikutano bila ugeugeu na kujihusisha kwa ukawaida katika utendaji wa kuhubiri.

Sasa nikiwa na miaka 89, ningali na lile pendeleo la kuwa mzee katika kundi letu katika Pietermaritzburg, Afrika Kusini. Yaniletea uradhi wa kweli kutazama nyuma kwenye miaka zaidi ya 60 nikiwa katika utumishi mbarikiwa wa Yehova. Hasa ni baraka kuwa nimeona vizazi vitano vya jamaa yetu, kutia ndani wazazi wangu, vikimletea sifa Yehova, yule Mungu mkubwa wa ulimwengu wote mzima.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki