Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 10/22 kur. 20-24
  • Kulea Watoto Afrika Wakati wa Magumu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kulea Watoto Afrika Wakati wa Magumu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwenda Afrika, Kisha Ndoa
  • Twahamia Rhodesia Kusini
  • Mimi na Bertie Twatiwa Gerezani
  • Huduma Yetu Baada ya Vita
  • Mgawo Mpya wa Kuhubiri
  • Safari ya Kurudi Yenye Hatari Sana
  • Nabarikiwa Kuwa na Familia Yenye Upendo
  • Nimeiona Ikikua Kusini mwa Afrika
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Naimarishwa na Udugu Wetu wa Ulimwenguni Pote
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Kukua Pamoja na Tengenezo la Yehova Katika Afrika Kusini
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
  • Kufurahia “Uzima wa Sasa” Kikamili
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 10/22 kur. 20-24

Kulea Watoto Afrika Wakati wa Magumu

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA CARMEN MCLUCKIE

Ulikuwa mwaka wa 1941. Vita ya Ulimwengu ya Pili ilikuwa imechacha. Nilikuwa mama mwenye umri wa miaka 23 kutoka Australia, huku mimi na mtoto wangu mwenye umri wa miezi mitano tukiwa gerezani huko Gwelo, Rhodesia Kusini (ambayo sasa ni Gweru, Zimbabwe). Mume wangu alikuwa gerezani huko Salisbury (ambayo sasa ni Harare). Watoto wetu wengine—mwenye umri wa miaka miwili na mwingine umri wa miaka mitatu—walikuwa wakitunzwa na watoto wangu wa kambo wawili matineja. Acha nieleze jinsi nilivyojikuta katika hali hiyo.

NILIISHI na Mama na Baba katika Port Kembla, karibu kilometa 50 kusini ya Sydney, Australia. Mwaka wa 1924, Clare Honisett alimtembelea Mama na kuamsha kupendezwa kwake katika mafundisho ya Biblia kwa kumwuliza kama alielewa maana ya Sala ya Bwana. Clare alimweleza kinachomaanishwa na kulitukuza jina la Mungu, kisha akamwambia jinsi Ufalme huo utakavyofanya mapenzi ya Mungu duniani. (Mathayo 6:9, 10) Mama alishangaa. Ujapokuwa upinzani wa Baba, Mama alianza kuchunguza sana kweli hizo za Biblia.

Muda mfupi baada ya hapo, tulihamia kiungani cha Sydney. Tukiwa huko mimi na Mama tungetembea karibu kilometa tano ili kufika kwenye mikutano ya Wanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo. Ijapokuwa Baba hakuwa Shahidi kamwe, aliruhusu mafunzo ya Biblia yafanywe nyumbani kwetu. Ndugu zake wawili Max na Oscar Seidel—wakawa Mashahidi, na pia washiriki wengine wa familia ya Max na vilevile ndugu yangu mchanga, Terry, na dada yangu mchanga, Mylda.

Mwaka wa 1930 Sosaiti ya Watch Tower ilinunua mashua yenye urefu wa meta 16, ambayo baadaye ilikuja kuitwa Lightbearer. Kwa miaka miwili mashua hiyo ilikuwa ikitiwa nanga karibu na makao yetu katika Mto Georges. Ikiwa huko, ilifanyiwa marekebisho ili Mashahidi wa Yehova waitumie katika kazi yao ya kuhubiri kwenye visiwa vya Indonesia. Nyakati nyingine mimi na dada yangu Coral tungesafisha kijumba na sitaha, na kuomba taa ya ncha ya mlingoti twende kuvua kamba.

Kwenda Afrika, Kisha Ndoa

Australia ilikumbwa na upungufu wa kiuchumi miaka ya katikati ya 1930, mimi na Mama tukasafiri kwenda Afrika Kusini kuona kama ingefaa familia yetu kuhamia kule. Tulikuwa na barua ya kutujulisha kutoka katika ofisi ya tawi ya Australia ya Mashahidi wa Yehova kumpelekea George Phillips, ambaye wakati huo alisimamia kazi ya kuhubiri katika sehemu ya kusini mwa Afrika. George alikuwa gatini huko Cape Town kungoja meli yetu. Alikuwa na kitabu cha Watch Tower Society Riches chini ya mkono wake ili tumtambue. Siku hiyohiyo, Juni 6, 1936, alitujulisha kwa washiriki watano wa ofisi ya tawi, kutia ndani Robert A. McLuckie.a Katika kipindi cha mwaka mmoja, tukaoana na Bertie, kama sote tulivyomwita.

Baba ya babu ya Bertie, William McLuckie alikuja Afrika mwaka wa 1817 kutoka Paisley, Scotland. Katika safari zake za kwanza, William alijuana na Robert Moffat, mwanamume aliyeanzisha kuandikwa kwa lugha ya Kitswana na kutafsiri Biblia katika lugha hiyo.b Katika miaka hiyo ya mapema, William na mwenzake Robert Schoon walikuwa tu ndio wazungu waliotumainiwa na Mzilikazi, shujaa mashuhuri wa jeshi la chifu mashuhuri wa Zulu, Shaka. Ilitokea kwamba, William na Robert walikuwa ndio wazungu pekee walioruhusiwa katika boma la Mzilikazi, ambako jiji la Pretoria, Afrika Kusini liko sasa. Baadaye, Mzilikazi akawa mkuu wa serikali na mnamo katikati ya karne ya 19 aliyaunganisha makabila mengi kuwa ufalme mmoja mkuu wa Afrika.

Nilipokutana na Bertie, alikuwa mjane mwanamume mwenye binti aliye na umri wa miaka 12, Lyall, na mwana mwenye umri wa miaka 11, Donovan. Bertie alikuwa amejifunza kweli za Biblia mara ya kwanza katika mwaka wa 1927 miezi michache baada ya mke wake Edna kufa. Miaka tisa iliyofuata, alihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu katika visiwa vya Mauritius na Madagaska na vilevile kotekote Nyasaland (ambayo sasa ni Malawi), Afrika Mashariki ya Ureno (ambayo sasa ni Msumbiji), na Afrika Kusini.

Miezi michache baada ya Bertie na mimi kuoana, tulihama pamoja na Lyall na Donovan hadi Johannesburg, ambapo ilikuwa rahisi kwa Bertie kupata kazi. Kwa muda fulani, nilitumikia nikiwa painia, kama vile ambavyo wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova huitwa. Kisha nikapata mimba ya Peter.

Twahamia Rhodesia Kusini

Hatimaye, kaka ya Bertie, Jack, alitualika tujiunge naye katika kazi hatari ya migodi ya dhahabu karibu na Filabusi, huko Rhodesia Kusini. Mimi na Bertie tulisafiri huko pamoja na Peter, wakati huo akiwa na umri wa mwaka mmoja, huku mama yangu akitunza Lyall na Donovan kwa muda. Tulipofika kwenye Mto Mzingwani, ulikuwa umefurika, nasi tulipaswa kuuvuka tukiwa katika sanduku lililovutwa kwa waya iliyonyooka kutoka ufuo mmoja wa mto hadi ule mwingine. Nilikuwa na mimba ya Pauline ya miezi sita na ilinibidi nimkamate Peter kwa nguvu kifuani pangu! Iliogopesha sana, hasa wakati waya hiyo ilikuwa karibu iguse maji katikati ya mto. Mbali na hilo, ilikuwa usiku wa manane, na mvua ilikuwa inanyesha sana! Baada ya kuvuka mto huo, ilitubidi tutembee kilometa mbili hivi ili tufikie nyumba ya mtu wetu wa jamaa.

Baadaye tulikodi nyumba iliyojaa mchwa kwenye shamba la mifugo. Fanicha zetu zilikuwa chache—baadhi yake zilikuwa zimetengenezwa kwa masanduku yaliyotumiwa kwa baruti na fyuzi. Mara nyingi Pauline alikuwa na ugonjwa wa kifaduro, nasi hatukuweza kununua dawa. Nilivunjika moyo sana, lakini tulishukuru kwamba kila mara Pauline alipona.

Mimi na Bertie Twatiwa Gerezani

Tulisafiri hadi jiji la Bulawayo mara moja kwa mwezi, umbali wa kilometa 80 hivi, kuuza dhahabu yetu katika benki. Pia tulikwenda Gwanda, mji mdogo karibu na Filabusi, kununua vyakula na kushiriki katika huduma. Katika 1940, mwaka ambao Vita ya Ulimwengu ya Pili ilianza, kazi yetu ya kuhubiri ilipigwa marufuku katika Rhodesia Kusini.

Muda mfupi baada ya hapo, nilikamatwa nikihubiri huko Gwanda. Wakati huo nilikuwa na mimba ya mtoto wangu wa tatu, Estrella. Wakati rufani yangu ilipokuwa ikifikiriwa, Bertie alikamatwa kwa sababu ya kuhubiri na kutiwa gerezani katika Salisbury, zaidi ya kilometa 300 kutoka mahali tulipokuwa tukiishi.

Hii ndiyo iliyokuwa hali yetu wakati huo: Peter alikuwa hospitalini huko Bulawayo akiwa na dondakoo, na kulikuwa na shaka kama angepona. Nilikuwa nimetoka tu kumzaa Estrella, na rafiki yangu alikuwa amenichukua kutoka hospitalini hadi gerezani kumwonyesha Bertie binti yake aliyetoka tu kuzaliwa. Baadaye, rufani yangu ilipokataliwa, Mhindi tajiri mwenye duka aliyekuwa mwenye fadhili alilipa dhamana yangu. Baada ya muda, maofisa watatu wa polisi walikuja kwenye mgodi kunipeleka gerezani. Waliniambia nichague. Ningeenda na mtoto wangu wa miezi mitano gerezani au nimwache na watoto wetu matineja, Lyall na Donovan. Niliamua kumchukua.

Niligawiwa kazi ya kushona nguo na kusafisha. Pia, nilipewa mtunzaji wa kumwangalia Estrella. Alikuwa mfungwa mchanga aitwaye Matossi, aliyekuwa akitumika kifungo cha maisha kwa kumwua mume wake. Matossi alilia nilipoachiliwa, kwa kuwa hangemtunza Estrella tena. Askari wa gereza wa kike alinipeleka nyumbani kwake tupate chakula cha mchana kisha akanipeleka kwenye garimoshi nimtembelee Bertie katika gereza la Salisbury.

Mimi na Bertie tulipokuwa gerezani, Peter na Pauline walitunzwa na Lyall na Donovan. Ijapokuwa Donovan alikuwa na umri wa miaka 16 tu, aliendeleza kazi zetu za migodi. Bertie alipoachiliwa kutoka gerezani, tuliamua kuhamia Bulawayo, kwa kuwa migodi haikuwa ikiendelea vizuri. Bertie alipata kazi kwenye reli, nami niliongezea mapato yetu kwa kutumia stadi zangu mpya nilizopata nikiwa mshonaji.

Kazi ya Bertie akiwa mpiga-ribiti kwenye reli ilionekana kuwa ya muhimu, kwa hiyo akaepushwa na utumishi wa kijeshi. Wakati wa miaka hiyo ya vita, Mashahidi Wazungu wapatao 12 hivi katika Bulawayo walikutana kwenye mikutano katika nyumba yetu ndogo yenye chumba kimoja cha kulala, na wachache kati ya ndugu na dada zetu Waafrika walikutana kwingineko jijini. Lakini sasa, kuna makutaniko zaidi ya 46 ya Mashahidi wa Yehova yaliyo na Waafrika pamoja na Wazungu katika Bulawayo!

Huduma Yetu Baada ya Vita

Baada ya vita Bertie aliomba shirika la reli limhamishe hadi Umtali (ambayo sasa ni Mutare), mji wenye kupendeza mpakani mwa Msumbiji. Tulitaka kutumikia mahali palipo na uhitaji mkubwa zaidi wa wahubiri wa Ufalme, na Umtali palionekana kuwa mahali pafaapo, kwa kuwa jiji hilo halikuwa na Mashahidi. Katika kipindi hicho kifupi tulichokaa huko, familia ya Holtshauzen, ambayo ilitia ndani wana watano, ikawa Mashahidi. Sasa kuna makutaniko 13 katika jiji hilo!

Mwaka wa 1947 familia yetu ilizungumzia uwezekano wa Bertie kurudia kazi ya upainia. Lyall, ambaye alikuwa amerudi kutoka kupainia kule Afrika Kusini, aliunga mkono wazo hilo. Donovan alikuwa akipainia Afrika Kusini wakati huo. Wakati ofisi ya tawi ya Cape Town ilijua tamaa ya Bertie ya kupainia tena, walimwomba afungue depo ya vichapo huko Bulawayo badala yake. Kwa hiyo alistaafu kutoka shirika la reli, na tukahamia huko. Punde baada ya hapo, wamishonari wa kwanza kwenda Rhodesia Kusini walifika Bulawayo, kutia ndani Eric Cooke, George na Ruby Bradley, Phyllis Kite, na Myrtle Taylor.

Mwaka wa 1948, Nathan H. Knorr, msimamizi wa tatu wa Watch Tower Society, pamoja na mwandishi wake, Milton G. Henschel, walitembelea Bulawayo na kupanga depo iwe ofisi ya tawi, Ndugu Cooke akiwa mwangalizi. Mwaka uliofuata, binti yetu Lindsay alizaliwa. Kisha mwaka 1950, ofisi ya tawi ilihamishwa hadi Salisbury, jiji kuu la Rhodesia Kusini, nasi tukahamia kule pia. Tulinunua nyumba kubwa mno ambamo tuliishi kwa miaka mingi. Sikuzote mapainia na wageni walitutembelea na kukaa nasi, kwa hiyo mahali petu pakajulikana kuwa hoteli ya McLuckie!

Mwaka wa 1953, mimi na Bertie tulihudhuria mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova katika Yankee Stadium huko New York City. Hilo lilikuwa tukio lisilosahaulika kama nini! Miaka mitano baadaye, Lyall, Estrella, Lindsay, na Jeremy mwenye umri wa miezi 16 walikuwa pamoja nasi kwenye mkusanyiko huo wa kimataifa mkubwa mno wa siku nane mwaka wa 1958 katika Yankee Stadium na Polo Grounds iliyo karibu na hapo. Idadi kubwa ya watu zaidi ya robo milioni walihudhuria hotuba ya watu wote siku ya kumalizia!

Mgawo Mpya wa Kuhubiri

Bertie alitumikia kwa miaka 14 akiwa mfanyakazi mwenye kusafiri kila siku kwenye ofisi ya tawi ya Salisbury, lakini tukaamua kutumikia mahali penye uhitaji mkubwa zaidi huko Shelisheli. Tuliuza makao yetu na fanicha zetu na kupakia vitu vilivyobaki katika gari dogo la abiria na mizigo aina ya Opel. Tukiwa na Lindsay, mwenye umri wa miaka 12, na Jeremy, mwenye umri wa miaka 5, tulisafiri karibu kilometa 3,000 kwenye barabara mbaya zaidi zenye vumbi kupitia Rhodesia Kaskazini (ambayo sasa ni Zambia), Tanganyika (ambayo sasa ni sehemu ya Tanzania), na Kenya, mwishowe tukafika kwenye jiji la bandari, Mombasa.

Mombasa lilikuwa na joto jingi sana, lakini lilikuwa na fuo zenye kupendeza. Tulimwachia Shahidi wa mahali hapo gari letu tukaanza safari ya siku tatu kwa mashua hadi Shelisheli. Tulipofika, tulipokewa na Norman Gardner, mwanamume aliyekuwa amepokea ujuzi wa msingi wa kweli ya Biblia kutoka kwa Shahidi mmoja katika Dar es Salaam, Tanganyika. Alipanga tukodi nyumba kwenye Sans Souci Pass ambayo ilikuwa imejengewa polisi waliomlinda Askofu Mkuu wa Othodoksi ya Kigiriki, Makarios, ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Saiprasi mwaka wa 1956.

Kwa kuwa nyumba yetu ilikuwa peke yake, baada ya mwezi mmoja tulihamia kwenye nyumba karibu na ufuoni kwenye Beau Vallon. Tukiwa huko tulialika watu kwenye hotuba ambazo Bertie alitoa kwenye veranda yetu. Tulianzisha funzo la Biblia na akina Bindschedler, na baada ya miezi michache, Bertie aliwabatiza na binti yao waliyeasilisha na vilevile Norman Gardner na mke wake. Pia tulisafiri na Norman katika mashua yake hadi Kisiwa cha Cerf, ambapo Bertie alitoa hotuba za Biblia katika nyumba ya mashua.

Tulipokuwa Shelisheli kwa miezi minne hivi, mkuu wa polisi alituambia kwamba ilikuwa lazima tuache kuhubiri ama sivyo tungefukuzwa nchini. Fedha zetu zilikuwa zimepungua, nami nilikuwa na mimba tena. Tuliamua kuendelea na mahubiri yetu ya hadharani. Hata hivyo, tulijua kwamba tulikuwa tuondoke upesi kwa vyovyote vile. Meli iliyofuata ilipofika kutoka India wapata mwezi mmoja baadaye, tulifukuzwa nchini.

Safari ya Kurudi Yenye Hatari Sana

Tulipofika Mombasa, tulichukua gari letu na kuelekea kusini kupitia barabara ya pwani yenye changarawe. Tulipofika Tanga, injini ya gari letu ilizima. Fedha zetu zilikuwa karibu kwisha, lakini mtu wa jamaa na Shahidi mwingine walitusaidia. Tulipokuwa Mombasa, ndugu mmoja alijitolea kutusaidia kifedha kama tungeenda kaskazini hadi Somalia kuhubiri. Hata hivyo, sikuwa mzima, kwa hiyo, tulitaka tu kurudi nyumbani Rhodesia Kusini.

Tulivuka kutoka Tanganyika hadi Nyasaland na kusafiri hadi upande wa magharibi wa Ziwa Nyasa, sasa liitwalo Ziwa Malawi. Nilikuwa mgonjwa sana hivi kwamba nikamwomba Bertie aniweke kandokando ya barabara nife! Tulikuwa karibu na jiji la Lilongwe, kwa hiyo alinipeleka hospitalini huko. Sindano za afyuni zilinipa kitulizo kidogo. Kwa kuwa sikuweza kuendelea na safari kwa gari, Bertie na watoto waliendesha gari kilometa 400 hivi hadi Blantyre. Mtu fulani wa jamaa alipanga nisafiri kwa ndege siku chache baadaye ili nijiunge nao. Kutoka Blantyre nilisafiri kwa ndege kurudi Salisbury, na Bertie na watoto walisafiri kwenda nyumbani kwa gari.

Sisi sote tulifurahi kama nini kufika Salisbury nyumbani kwa binti yetu Pauline na mume wake! Mwaka wa 1963 mwana wetu wa mwisho, Andrew, alizaliwa. Alikuwa na tatizo la pafu naye hakutazamiwa kuishi, lakini kwa tokeo zuri akaishi. Hatimaye, tulihamia Afrika Kusini na mwishowe makao yetu yakawa huko Pietermaritzburg.

Nabarikiwa Kuwa na Familia Yenye Upendo

Bertie alikufa kwa utulivu akiwa na umri wa miaka 94 katika 1995, na tangu hapo nimekuwa nikiishi peke yangu katika nyumba yetu hapa. Lakini siko peke yangu kwa vyovyote! Lyall na Pauline wanamtumikia Yehova pamoja na familia zao hapa Afrika Kusini, na baadhi yao wanaishi papa hapa Pietermaritzburg. Lindsay na familia yake wako California, Marekani, wote ni Mashahidi watendaji. Watoto wetu wadogo zaidi, Jeremy na Andrew, walihamia Australia, ambako wameoa na wanaishi kwa furaha na wanatumikia wakiwa wazee katika makutaniko yao.

Watoto wetu wote wanane walipata kushiriki katika huduma ya painia wakati mmoja au mwingine, na sita wamepata kutumikia katika ofisi za tawi za Watch Tower Society. Donovan alihitimu kutoka katika darasa la 16 la Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower katika Februari 1951 na akatumikia akiwa mwangalizi asafiriye katika Marekani kabla ya kurudi kufanya kazi katika ofisi ya tawi ya Afrika Kusini. Sasa yeye ni mzee Mkristo katika Klerksdorp, karibu kilometa 700 kutoka Pietermaritzburg. Estrella huishi na mume wake, Jack Jones, kwenye makao makuu ya Mashahidi wa Yehova huko Brooklyn, New York.

Mwana wangu wa kwanza, Peter, alikuwa katika huduma ya wakati wote kwa miaka kadhaa, katika kazi ya painia na kwenye ofisi ya tawi ya Watch Tower huko Rhodesia. Hata hivyo, miaka kadhaa iliyopita, nilihuzunika sana alipoacha ushirika wa kutaniko la Kikristo.

Nikifikiria maisha yangu ya nyuma, naweza kusema kwamba kwa kweli nina furaha kwamba nikiwa tineja nilikwenda Afrika na mama yangu. Ni kweli kwamba, maisha hayajawa rahisi, lakini nilikuwa na pendeleo la kumwunga mkono mume wangu na kulea familia ambayo imesaidia kuendeleza habari njema za Ufalme wa Mungu sehemu ya kusini mwa Afrika.—Mathayo 24:14.

[Maelezo ya Chini]

a Masimulizi ya kibinafsi ya Robert McLuckie yapatikana katika Mnara wa Mlinzi la Februari 1, 1990, ukurasa wa 26-31.

b Ona ukurasa wa 11 wa broshua Kitabu kwa Ajili ya Watu Wote, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Ramani katika ukurasa wa 22, 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

AFRIKA KUSINI

Cape Town

Pietermaritzburg

Klerksdorp

Johannesburg

Pretoria

ZIMBABWE

Gwanda

Bulawayo

Filabusi

Gweru

Mutare

Harare

ZAMBIA

MSUMBIJI

MALAWI

Blantyre

Lilongwe

TANZANIA

Dar es Salaam

Tanga

KENYA

Mombasa

SHELISHELI

SOMALIA

[Picha katika ukurasa wa 20]

Nikiwa na Peter, Pauline, na Estrella,

kabla ya kwenda gerezani pamoja na Estrella

[Picha katika ukurasa wa 21]

Lyall na Donovan mbele ya nyumba yetu ya shamba la mifugo karibu na Filabusi

[Picha katika ukurasa wa 23]

Bertie, Lyall, Pauline, Peter, Donovan, na mimi mwaka wa 1940

[Picha katika ukurasa wa 24]

Carmen na watoto wake watano (kushoto hadi kulia): Donovan, alipokuwa Gileadi mwaka wa 1951, na Jeremy, Lindsay, Estrella, na Andrew leo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki