Ufuataji Haki Ndiyo Sera Bora Zaidi
UFUATAJI haki hupendekezwa sana katika Biblia na ni takwa kwa Wakristo wa kweli. (Mathayo 22:39; 2 Wakorintho 8:21) Zaidi ya hilo, kwa kweli ufuataji haki ndiyo sera bora zaidi, kama ionyeshwavyo katika maisha za wengi leo ambao akili na mioyo yao imegeuzwa na maarifa sahihi ya Biblia. Kielelezo cha jambo hili chatoka Liberia.
Baada ya ufikirio mwingi wa sala, mzee Mkristo na mke wake walifunga duka lao la kushona kwa cherehani. Kwa nini? Kwa sababu lilikula muda mwingi sana wao na kuzuia utendaji wao wa kihuduma na funzo la kibinafsi. Waliafikiana kuridhika na mapato ya kiasi yaliyotokana na mauzo ya rangi za kupaka nguo. Hata hivyo, mara baada ya wao kuchukua hatua hii, bei za rangi za kupaka nguo zilishuka katika soko la kwao. Sasa mapato yao hayangetosheleza jamaa. Wangefanya nini?
Waliiomba kampuni yenye kugawa rangi za kupaka nguo zishushe bei, hivyo iruhusu kuwe na faida kubwa zaidi. Hiyo ilikataliwa. Hata hivyo, kampuni ilijitoa kupeleka invoisi mbili, moja ikionyesha bei halisi na ile nyingine bei iliyopunguzwa ambayo wangeweza kuonyesha Forodhani ili walipe kiasi kidogo zaidi cha kuingiza bidhaa. Hiyo ingeruhusu mzee huyo shangwe ya kupata faida haramu ya dola 2,000 kwa kila fungu la bidhaa.
Ndugu huyo alikataa kuwa sehemu ya utendaji usiofuata haki na ambao ungepunja serikali. Maafisa wa kampuni walishangaa. Waliandika hivi: “Sisi twastahi dhamiri yako,” nao wakaweka mzee huyo awe ndiye mwakilishi mmoja tu wa bidhaa yenye kutengenezwa nao katika Liberia. Mahitaji ya kimwili ya jamaa yakiwa sasa yaweza kutoshelezwa vya kutosha, mzee huyo na mke wake wameweza kufanya upainia msaidizi, wakifanya kazi kwa ukaribu pamoja na akina ndugu ili kulijenga kundi. Kwa kweli, kufuata kwao haki kulithibitika kuwa baraka kwao.
Alfonso, katika Hispania, alipata pia kwamba ufuataji haki ndiyo sera bora zaidi. Kivulana huyu aliondoka nyumbani akiwa na umri wa miaka 12, na muda si muda akawa akiuza dawa za kulevya, na pia kuiba katika magari, nyumba, na maduka. Nyakati fulani aliiba katika maduka mengi kufikia kumi kwa siku moja. Akiwa na miaka 21, wanne wa washirika wake walimpiga vibaya sana, wakaiba dawa zake zote za kulevya, na kutisha kumuua kama angewaripoti kwa polisi. Kwa kuwa yeye alijulikana sana na polisi, hata aliogopa kwenda hospitali kwa matibabu.
Akiwa anapata nafuu polepole kutokana na majeraha yake, Alfonso alifikiria kwa uzito njia yake ya maisha. Alikumbuka mambo kuhusu Biblia na kanuni za Kikristo ambazo mama yake alikuwa amemwambia akiwa mtoto. Halafu, yeye akawa amepuuza maneno hayo, lakini sasa aliomba funzo la Biblia kwa Mashahidi wa Yehova. Katika muda wa miezi sita akawa amebadili kabisa mwenendo na utu wake na akastahili ubatizo.
Hata hivyo, katika siku iliyokuwa kabla ya ubatizo wake, alipokea maandishi yenye kumwita mahakamani akakabili shtaka la wizi wa kutumia silaha. Huo ulikuwa uhalifu aliokuwa ametenda zamani kidogo. Hata hivyo, Alfonso aliungama wazi kosa hilo na akatiwa gerezani akingojea kesi. Loya mwenye kumtetea alihimiza ataarifu kwamba hakuwa ameiba chochote na kwamba hakuwa akichukua bunduki. Lakini Alfonso alisisitiza juu ya kusema ukweli. Kwa sababu ya kosa hilo na rekodi yake mbaya kwenye polisi, kiongozi wa mashtaka alidai kifungo cha miaka 13. Lakini kwa sababu ya mwenendo wake mwema na mtazamo wa ufuataji haki, alipewa miezi sita, wakati aliokuwa tayari ametumikia huku akingoja kesi.
Sasa Alfonso na mke wake watumikia Yehova kwa uaminifu, wakiwa na furaha kwamba walipata kusudi halisi maishani na kwamba kwa mambo yaliyowapata wao wenyewe walithibitisha kwamba ufuataji haki ndiyo sera bora zaidi.