Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 3/15 kur. 3-6
  • Kifo cha Yesu Chamaanisha Nini Kwako?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kifo cha Yesu Chamaanisha Nini Kwako?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Hicho?
  • Kwa Nini Wahitajiwa?
  • Unachofanya Kiwezekane
  • Ni Nani Hukombolewa?
  • Sababu za Shukrani
  • Wewe Utafanya Nini?
  • Fidia​—Zawadi Bora Kutoka kwa Mungu
    Biblia Inatufundisha Nini?
  • Fidia—Zawadi Bora Zaidi Kutoka kwa Mungu
    Biblia Inafundisha Nini Hasa?
  • Yehova Atoa “Fidia Katika Kubadilishana kwa Ajili ya Wengi”
    Mkaribie Yehova
  • Fidia ya Kristo Njia ya Mungu ya Wokovu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 3/15 kur. 3-6

Kifo cha Yesu Chamaanisha Nini Kwako?

“MAJESHI yote yaliyopata kupiga mwendo, majeshi-bahari yote yaliyopata kujengwa, mabunge yote yaliyopata kuketi, na wafalme wote waliopata kutawala, wakiwekwa pamoja, hawajaathiri maisha ya mwanadamu juu ya dunia hii kwa nguvu nyingi kama mtu mmoja huyu peke yake.”Ndivyo alivyoandika mtungaji James A. Francis kuhusu Yesu Kristo.

Watu humwona Yesu kwa njia mbalimbali, lakini Biblia humtambulisha kuwa Mwana wa Mungu na mwanadamu mwenye upendo wa kujidhabihu. Yesu alitaja njia kuu ambayo yeye alionyesha upendo huo aliposema hivi juu yake mwenyewe: “Mwana wa binadamu alikuja, si ahudumiwe, bali kuhudumia na kutoa nafsi yake ukombozi kwa kubadilishana na wengi.”—Mathayo 20:28, NW.

Ni nini umaana wa ukombozi huu? Kwa nini ulihitajiwa? Ni nani mwenye kukombolewa? Kwa kweli, kifo cha Yesu chamaanisha nini kwako?

Ni Nini Hicho?

Ukombozi ni kitu ambacho hufungua. Kukomboa mtu humaanisha kumkomboa kutoka utekwa au adhabu kwa kulipa bei. Katika maana ya kiroho, “kukomboa” humaanisha kuokoa kutoka kwenye dhambi na adhabu yayo. Ndiyo sababu Yesu alikufa. Kama vile mtume Mkristo Paulo alivyoandika: “Mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.”—Warumi 6:23.

Bei ya kukomboa (kufidia) hushirikishwa Kimaandiko na kulipa ukombozi. Zaburi 49:6-9 yasema hivi: “Hao wanaozitumainia mali zao, na kujisifia wingi wa utajiri wao; hakuna mtu awezaye kumkomboa ndugu yake, wala kumpa Mungu fidia [ukombozi, NW] kwa ajili yake, (maana fidia ya nafsi zao ina gharama, wala hana budi kuiacha hata milele;) ili aishi sikuzote asilione kaburi.” Ukombozi ni fidia ambayo hufanywa na Mungu, wala si na mwanadamu yeyote asiyekamilika.

Kwa Nini Wahitajiwa?

Ukombozi wahitajiwa kwa sababu baba yetu wa kwanza wa kibinadamu, Adamu, alitenda dhambi. Hivyo yeye alipoteza uhai mkamilifu usio na mwisho, akahukumiwa kwa haki kufa, na hatimaye akafa. (Mwanzo 2:15-17; 3:1-7, 17-19; 5:5) Sisi tukiwa wazao wake, tumerithi dhambi na kifo. “Kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti,” akaandika Paulo, “na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi.” (Warumi 5:12) Ndiyo, “katika Adamu wote wanakufa.” (1 Wakorintho 15:22) Kwa hiyo mtunga zaburi Daudi alisema hivi kwa usahihi: “Mimi naliumbwa katika hali ya uovu; mama yangu alinichukua mimba hatiani.”—Zaburi 51:5.

Kukombolewa kutoka laana ya dhambi na kifo kwahitajiwa sana ikiwa mzao yeyote mwenye dhambi wa Adamu atapokea uhai wa milele. Ijapokuwa wanadamu wasiokamilika hawawezi kuandaa ukombozi huu, Yehova alifanya hivyo kwa upendo kupitia Yesu Kristo. Hata hivyo, ni nini chenye kununuliwa kwa ukombozi? Basi, Adamu alipotenda dhambi, alipoteza uhai wa milele wa kibinadamu ulio mkamilifu, ukiwa na haki na matazamio yao yote. Hivyo, kitu icho hicho kililipiwa fidia kwa njia ya dhabihu ya ukombozi wa Yesu.

Unachofanya Kiwezekane

Haki ilitoshelezwa kwa kupatwa kwa ainabinadamu na kifo, iliyo adhabu ya dhambi. Kwa hiyo ukombozi ni kitendo cha rehema na fadhili-upendo za Mungu. Uhai mkamilifu wa kibinadamu wa Yesu, pamoja na haki na matazamio yao yote, ulitolewa katika kifo na haukutwaliwa urudishwe kamwe, kwa maana yeye hakufufuliwa akiwa mwanadamu wa mnofu na damu bali akiwa kiumbe roho asiyekufa. (1 Wakorintho 15:50; 1 Petro 3:18) Kwa hiyo uhai wa kibinadamu wa Yesu Kristo uliodhabihiwa uliendelea kuwa na nguvu ya kufidia, au kukomboa.

Akiwa mwanadamu asiye na dhambi, Yesu alisimama katika cheo kama kile kilichokaliwa na Adamu mkamilifu hapo kwanza. Yesu alifanywa Kuhani wa Juu mkubwa kwa sababu ya kutii Mungu hadi kifo, na alitoa thamani ya dhabihu yake kamilifu ya kibinadamu mbinguni. (Waebrania 9:24-26) Kwa sababu Mungu alikubali bei hii ya fidia, Yesu angeweza kufidia wazao wa Adamu wenye kuamini watoke kwenye dhambi na kifo kwa kutumia ustahili wa dhabihu yake kwa ajili yao. (1 Wakorintho 6:20; 7:23; 1 Yohana 2:1, 2) Hivyo Yesu “akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.” (Waebrania 5:8, 9) Hii yafanya iwezekane wao kupata msimamo wa uadilifu mbele za Mungu kupitia Mwanae.

Ni Nani Hukombolewa?

Basi, ni nani hunufaika na ukombozi? Ni wanadamu ambao hujizoeza imani katika uandalizi huu na hivyo kuja katika upatano na Mungu. Kwa kumtumikia kwa uaminifu, wao waweza kuwekwa huru kutoka kwenye dhambi na adhabu yayo kifo na kupokea uhai wa milele.—Yohana 17:3.

Mwanadamu wa kwanza angeweza kuamua kama angetii au hangetii Mungu. Yeye alichagua kutotii. “Adamu hakudanganywa,” bali alikufa akiwa mtenda dhambi wa kupenda. (1 Timotheo 2:14) Hata hivyo, namna gani wazao wa Adamu? Wangeweza kuchagua ama kutumikia Mungu kwa kadiri ya uwezo wao usiokamilika ama kutotii Muumba wao.—Yoshua 24:15.

Yesu alikuja “kutoa nafsi yake iwe fidia [ukombozi, NW] ya wengi.” (Marko 10:45) Lakini “wengi” hao ni nani? Kwa wazi Adamu hahusishwi ndani kwa sababu alikuwa mwanadamu mkamilifu aliyechagua kimakusudi kutotii Mungu na akafa akiwa mtenda dhambi wa kupenda, asiyetubu. Lakini namna gani familia yake kubwa, inayofikia hesabu ya maelfu ya mamilioni? Kwa bei yenye kulingana, Yesu Kristo huondoa laana kali iliyorithiwa ambayo inakalia familia ya Adamu. (Linganisha 1 Timotheo 2:5, 6.) Kwa ajili ya waamini “wengi” hao, Yesu hutumia ustahili wa bei yake ya kufidia.

Waamini wenye kukombolewa ni kuhusisha ndani Wayahudi na Wasio Wayahudi pia, au watu wa mataifa. Paulo asema: “Kama kwa kosa moja watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki [uadilifu, NW] watu wote walihesabiwa haki [uadilifu, NW] yenye uzima.” (Warumi 5:18) Kwa kufa juu ya mti, ‘Kristo alikomboa Wayahudi katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yao; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti.’ (Wagalatia 3:13; Kumbukumbu 21:23) Warumi 4:11 hudokeza juu ya Wasio Wayahudi lisemapo kwamba Abrahamu, babu ya Wayahudi, alipokuwa angali hajatahiriwa, akawa “baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa.” Kwa hiyo, basi, dhabihu ya ukombozi ya Yesu hunufaisha Wayahudi na Wasio Wayahudi wanaoamini.

Mwendo uliofuatwa na kila mtu waamua kama atanufaika na dhabihu ya Yesu. Kama Adamu, walio waovu kwa kupenda hawalazimishwi kupata ustahili wa ukombozi na uhai wa milele. Kama Kristo alivyosema: “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.” (Yohana 3:36) Ukombozi hufanya ufufuo uwezekane pia kwa wafu wale walio katika kumbukumbu ya Mungu. (Yohana 5:28, 29) Wakithibitika kuwa watiifu na wenye uthamini, utumizi wa manufaa za ukombozi kwao wamaanisha kwamba wataishi milele. Lakini kwa wale wanaoishi katika “siku za mwisho” hizi, kuna uwezekano wa uhai wa milele bila uhitaji wa kufa hata kidogo.—2 Timotheo 3:1-5; Mathayo 24:3-14, 21, 34; Yohana 11:25, 26.

Sababu za Shukrani

Ni lazima mtu yeyote anayetamani kunufaika na ukombozi awe na uthamini wa kina kirefu kwao. Nazo shukrani za jinsi hiyo zafaa kama nini! Ingawaje, ukombozi ulitaka upendo mwingi sana upande wa Mungu na Kristo.

Yehova Mungu alionyesha upendo mkubwa katika kuandaa ukombozi kupitia kifo cha Mwanae. Yesu alisema: “Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwanae wa pekee, ili kila mtu anayemwamini asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16, 17, HNWW) Je! haikupasi uthamini udhihirisho huu wa upendo wa Mungu?

Fikiri zaidi juu ya kina cha upendo wa Yehova katika kuandaa ukombozi. Kabla Mwana wa Mungu hajatumwa duniani aishi na kufa akiwa mwanadamu mkamilifu, alikuwako kabla ya kuwa mwanadamu. Alikuwa ndiye “mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” ambaye kwa njia yake “vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana.” (Wakolosai 1:13-16) Lo, Yehova alipenda Mwanae kama nini! Hata hivyo, Mungu hakutuma yeyote tu wa mamilioni ya malaika waadilifu aje duniani. Upendo wake kwa ainabinadamu ulikuwa mkubwa sana hata akatuma Mwanae mzaliwa wa kwanza.

Fikiria, pia, upendo wa kina kirefu ambao Yesu alionyesha kuhusiana na ukombozi. Akiwa kiumbe roho mbinguni, yeye alikuwa “stadi wa kazi” wa Mungu. Ni kweli, “vitu ambavyo [Mwana wa Mungu] alipenda sana vilikuwa pamoja na wana wa wanadamu.” (Mithali 8:22-31, NW) Hata hivyo, haikuwa rahisi kwake kuondoka mbinguni, kwenye hali za kupendeleka sana akiwa katika ushirika na Baba yake na miriadi za malaika waadilifu. Akiwa katika mahali pake pa kimbingu penye mwono mzuri, Mwana wa Mungu angeweza kuona hali za uovu duniani na maangamizi ya dhambi na kifo juu ya ainabinadamu. Pia alijua kwamba kuandaa ukombozi kungetaka yeye afe. Hata hivyo, “akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, . . . alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti.” Kwa uaminifu huo, Yesu aliinuliwa kwenye uhai mtukufu wa mbingu. (Wafilipi 2:5-11) Alionyesha upendo ulioje kuhusiana na ukombozi! Je! Wewe kathamini aliyofanya Yesu?

Wewe Utafanya Nini?

Askofu Mwingereza Richard wa Chichester (c. 1198-1253) alisali wakati mmoja kwamba wanaume na wanawake wapate “kujua Yesu Kristo kwa uwazi zaidi, kumpenda kwa upenzi mwingi zaidi, na kumfuata kwa ukaribu zaidi.” Kwa uhakika dhabihu ya ukombozi ya Yesu huandaa sababu moja timamu ya kupata kumjua, kumpenda, na kumfuata.

Kama haingekuwa ni kwa sababu ya ukombozi, sisi watenda dhambi tungekufa bila tumaini, kwa maana “uchungu wa mauti ni dhambi.” (1 Wakorintho 15:56) Hivyo, ili kuokolewa kutoka kwenye kifo ambacho kingetokea kwa sababu ya kuwa umetiwa uchungu na dhambi, ni lazima ufanye nini? Wahitaji kujifunza juu ya uandalizi wa Mungu kwa ajili ya wokovu kupitia Yesu Kristo. Halafu ni lazima uonyeshe kwamba wewe hujizoeza imani katika ukombozi. Jinsi gani? Kwa kuuonyesha uthamini wenye kuhisiwa moyoni, kujitoa mwenyewe kwa Mungu, na kuambia wengine juu ya uandalizi huu mzuri ajabu wa wokovu.

Mwendo huu waweza kukutia wewe miongoni mwa “mkutano mkubwa” ambao “ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo,” Yesu Kristo. (Ufunuo 7:9, 14) Tumaini lao ni uhai wa milele katika paradiso ya kidunia. (Luka 23:43, ZSB) Ndiyo, nawe waweza kuwa sehemu, ya songamano hilo lenye furaha, ikiwa kweli kifo cha Yesu ni kitu cha bei kubwa kwako.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Yesu asiye na dhambi alisimama katika cheo kile kilichokaliwa na Adamu mkamilifu

[Picha katika ukurasa wa 6]

Je! wewe wathamini maana halisi ya kifo cha Yesu?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki