Kodeksi Washington ya Zile Gospeli
KATIKA Desemba 1906, Charles L. Freer, mwanaviwanda tajiri na mkusanya-sanaa aliye Mwamerika, alinunua hati-mkono fulani za zamani kutoka kwa mwuzaji Mwarabu jina lake Ali, katika Giza, Misri. Ali alisema kwamba zilikuwa zimetoka White Monastery (Makao ya Kitawa) yaliyo karibu na Sohâg, lakini yaelekea zaidi kwamba zilipatikana katika magofu ya Monastery of Vinedresser (Makao ya Kitawa ya Mtunza-mizabibu) karibu na piramidi ya tatu ya Giza katika vijito vyenye rutuba nyingi vya Naili (Nile Delta).
Freer alipewa hati-mkono tatu na “kibunda cha kitabu-ngozi kilichogeuka cheusi kwa kuoza kikawa kigumu na chenye kuvunjika kwa urahisi kwa kukakamaa nje kama gundi.” Kilikuwa na urefu wa sentimeta 17, upana wa sentimeta 11, na maki (unene) ya sentimeta 4 na kiliuzwa pamoja na hati-mkono hizo kwa sababu tu kilihusiana nazo, wala si kwa sababu hicho chenyewe kilidhaniwa kuwa na thamani yoyote. Ilikuwa kazi-jasho yenye kuhitaji uangalifu mwingi sana kutenganisha mtungamano huo wa sahifa (kurasa) zilizo vijipande, lakini hatimaye 84 kati yazo zilifunuliwa, zote zikiwa zimetokana na kodeksi ya karne ya tano au sita W.K. ya barua za Paulo.
Moja ya hati-mkono tatu zilizobakia ilikuwa ya vitabu vya Kumbukumbu la Torati na Yoshua. Nyingine ilikuwa ya Zaburi, kutokana na tafsiri ya Septuagint ya Kigiriki. Hata hivyo, ya tatu iliyo ya maana zaidi ilikuwa hati-mkono ya zile Gospeli nne.
Hati-mkono hii ya mwisho ina sahifa (kurasa) 187 za kitabu-ngozi laini, sana-sana ngozi ya kondoo, zilizoandikwa kwa herufi kubwa za Kigiriki zenye kulala. Ni mara haba ambapo alama za vituo na mikato zimewekwa, lakini mara kwa mara kuna nafasi ndogo-ndogo kati ya vifungu vya maneno. Kingo zote za hati-mkono zilikuwa zimeoza vibaya, lakini sehemu kubwa ya maandishi hayo imehifadhiwa. Baadaye hati hiyo ilipokezwa kwa Freer Gallery of Art (nyumba ya hifadhi) ya Smithsonian Institution, katika Washington, D.C. Ikiwa yaitwa Kodeksi Washington ya zile Gospeli, ilipewa herufi ya utambulishi “W.”
Kitabu-ngozi hicho kimepewa tarehe ya kufikia mwishoni mwa karne ya nne au mapema karne ya tano W.K., hivi kwamba hakikupata cheo kilicho mbali sana na zile hati-mkono tatu za maana za Sinaitic, Vatican, na Alexandrine. Zile Gospeli (ambazo ni kamili isipokuwa sahifa [kurasa] mbili zilizopotea) zimo katika ule uitwao mpangilio wa Magharibi wa Mathayo, Yohana, Luka, na Marko.
Kusoma hati-mkono hiyo hufunua mchanganyiko usio wa kawaida wa namna za kimaandishi, kila moja ikiwakilishwa na visehemu vikubwa vyenye kuendelea. Yaonekana ilinakiliwa kutokana na vijipande vilivyoendelea kuwako vya hati-mkono kadhaa, kila moja ikiwa na namna tofauti ya maandishi. Profesa H. A. Sanders alidokeza kwamba huenda hiyo ingeweza kurudi nyuma kwenye mnyanyaso ambao Maliki Diocletian aliwatenda Wakristo katika mwaka 303 W.K., na kwa amri yake nakala zote za Maandiko zikaagizwa kuteketezwa peupe. Twajua kutokana na maandishi ya kihistoria kwamba hati-mkono fulani zilifichwa wakati huo. Yaonekana kwamba miongo kadhaa baadaye mtu asiyejulikana alinakili sehemu zi-lizoendelea kuwako za hati-mkono tofauti-tofauti ili kuyatokeza maandishi ya Kodeksi Washington. Baadaye, kikundi cha kwanza cha sahifa (kurasa) za Yohana (Yohana 1:1 hadi 5:11) kilipotea wakati fulani ikawa lazima kiandikwe upya katika karne ya saba W.K.
Kuna mitofautiano fulani ya kupendeza katika maandishi na nyongeza isiyo ya kawaida, lakini isiyoaminiwa kabisa, kwenye Marko sura ya 16 ambalo labda lilianza likiwa maelezo ya pambizoni. Thamani maalumu ya hati-mkono hiyo imo katika uhusiano wayo na fasiri zile za zamani za Kilatini na Kisiriaki. Alama-alama zilizosababishwa na mmwagiko wa mafuta ya mishumaa katika kitabu-ngozi hicho zaonyesha kwamba kilitumiwa sana.
Ijapokuwa kumekuwa na mnyanyaso na upinzani na hali ambazo zingeweza kuiharibu Biblia baada ya muda mwingi kupita, imehifadhiwa vizuri ajabu kwa ajili yetu katika namna nyingi za hati-mkono. Kwa kweli, “Neno la Bwana [Yehova, NW] hudumu hata milele.”—1 Petro 1:25; Isaya 40:8.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 15]
Kwa hisani ya Freer Gallery of Art, Smithsonian Institution