Baraka ya Yehova Imenitajirisha
Kama ilivyosimuliwa na Elsie Meynberg
“BARAKA ya BWANA [Yehova, NW] hutajirisha, wala hachanganyi huzuni nayo.” (Mithali 10:22) Mimi nimejionea kibinafsi ukweli wa mithali hii ya Biblia. Niruhusu nikusimulie ni kwa jinsi gani.
Nilipokuwa na miaka sita tu, nilisikiliza mazungumzo ya mama yangu pamoja na mwalimu mmoja wa Biblia aliyetuzuru, nami nikaona jinsi mama alivyosisimuliwa sana na mambo aliyokuwa akijifunza. Usiku mmoja wa kipupwe baridi, niliteremka chini katika vidato vya nyumba ili nikapate bilauri ya maji baridi nami nikamkuta Mama akisoma karibu na mlango wazi wa joko. Badala ya kunigombeza kama nilivyotarajia, alinizungushia mkono akanieleza kwamba jina la Mungu ni Yehova. Uchangamfu uliokuwa katika sauti yake uliniambia kwamba jambo alilokuwa amejifunza lilikuwa la maana sana kwake.
Baada ya mazungumzo machache zaidi pamoja na yule mwalimu wa Biblia, mama alishika njia kwenda kushiriki pamoja na majirani habari njema alizokuwa amejifunza. Hata hivyo, si sikuzote alipopokewa vizuri. Sisi tuliishi mashambani karibu na Beatty, Saskatchewan, Kanada, na sana-sana jirani zetu walikuwa ni watu wa ukoo wetu, Walutheri au Waevanjeli thabiti. Hata hivyo, Mama aliendelea kuwazuru.
Mimi nilikuwa nikitazama kupitia madirisha yenye baridi kali ya theluji huku Mama akijikaza sana kuwatoa farasi kwenye ghala ya nafaka, nikijua kwamba hakuzoea kuwafunganisha na gari. Nyakati fulani alikuwa akienda zake mikutanoni au kwenye huduma ya shambani ijapokuwa Baba alitoa malalamiko. Yeye hakuafikiana na imani mpya ya Mama, lakini Mama alipiga moyo konde. Sikuzote yeye alikuwa akirudi na furaha ya ndani iliyoonekana wazi kwa wote. ‘Baraka ya Yehova ndiyo hutajirisha,’ akawa akisema. Mimi nilikuwa nikishangaa alimaanisha nini kwa kusema hivyo. Ingawa nilikuwa na miaka sita tu, mimi pia nilitaka kumtumikia Yehova.
Siku moja nilikuwa paani pamoja na baba yangu, ambako alikuwa akitengeneza mbao zilizoezekwa. Mama na Eileen dada yangu walikuwa wakiondoka pamoja na kikundi kimoja wakiwa katika motakaa ya “Model T Ford” ili wakashiriki “matembezi ya kupasha habari.” Wao wangepiga gwaride kupitia mjini wakiwa na mabango yenye kutangaza hotuba moja ya Biblia.
“Wewe hutakuwa mpumbavu hivyo, au sivyo?” Baba akaniuliza. Lakini hata ingawa nilikuwa msichana aliyefurahia kupanda juu ya vitu tu, niliona ingalikuwa afadhali kama nilikuwa katika hayo matembezi ya kupasha habari kuliko kuwa juu ya paa hiyo. Hata hivyo, wao walisema nilikuwa mfupi mno kuchukua bango la matangazo.
Kukabili Mwito wa Ushindani wa Marufuku
Mwishowe, fursa yangu ya kwanza ya kushiriki katika kuhubiri Ufalme ikaja katika Novemba 1940. Lo, msisimuko ulioje! Kwa kuwa wakati huo kazi ya kuhubiri ya Mashahidi wa Yehova ilipigwa marufuku katika Kanada, tulienda nje katikati ya usiku na kuacha kijitabu End of Nazism (Mwisho wa Unazi) kwenye mlango wa kila nyumba.
Nilipokuwa na miaka tisa, nilipiga moyo konde kuweka maisha yangu wakfu kwa Yehova na kubatizwa. Kwa sababu ya mnyanyaso ule, hatukuambiwa mahali pa mkutano, lakini tuliongozwa mahali fulani katika msitu ambapo kikundi kikubwa cha Mashahidi kilikuwa na shangwe ya kufanya “mandari” (pikniki). Huko dada yangu wa umri mkubwa zaidi Eleanor na mimi tukawa miongoni mwa wengi waliobatizwa katika maji baridi ya ziwa la hapo karibu.
Shule siku hizo ilianza huku darasa likisalimu bendera na kuimba wimbo wa taifa. Wanadarasa wenzetu wajapotukodolea macho yenye mashtaka, kwa staha sisi tulikuwa tukikataa kushiriki kwa sababu ya fundisho la Biblia juu ya ibada ya sanamu. (Danieli, sura ya 3) Binamu yangu Elaine Young, aliyekuwa Shahidi pia, alilazimika kutembea kilometa 6 kwenda shuleni, lakini kila siku msichana huyo alikuwa akifukuzwa kwa kutosalimu bendera. Baada ya hapo alikuwa akitembea mwendo wote ule kwenda nyumbani tena. Alifanya hivyo kwa nusu ya mwaka wa shule ili asiandikiwe kukosa masomo na kuanguka mtihani.
Baada ya kuondoka shuleni, nilifanya kazi katika benki. Lakini mtihani ukaja niliponyimwa ombi la kuhudhuria ule mkusanyiko wa kimataifa wa Mashahidi wa Yehova huko New York katika 1950. Nilikuwa na akiba fulani nami nikaamua kuacha kazi na kuanza huduma ya wakati wote. Kwa hiyo Elaine na mimi tukahamia jiji la Regina. “Atarudi nyumbani akiwa mwombaji masika yafikapo,” watu fulani wakanidhihaki vikali. Hata hivyo, niliweza kujiandalia mimi mwenyewe kwa kufanya kazi nikiwa yaya wa nusu-wakati. Utajiri wa mibaraka ya Yehova umeniendeleza katika huduma yake ya wakati wote muda wote tangu hapo.
Kufikia Mradi Wetu
Katika 1955 Elaine na mimi tulisisimukia kualikwa kwenye darasa la 26 la Gileadi na baadaye kupokea migawo ya kwenda Bolivia, Amerika Kusini. Wakati huo katika nchi mzima kulikuwako Mashahidi karibu 160 tu. Hatimaye, tulielekea Tarija ili tukajiunge na wamisionari wengine wawili katika mgawo wetu wa kwanza.
Tarija ulikuwa mji wa kupendeza. Ilipendeza sana kuona wanawake katika mavazi yao ya kitamaduni wakiwa wamechukua mizigo juu ya vichwa vyao. Watu wa huko walikuwa wa kupendeza nao hawakutaka kamwe kutuambia hawakupendezwa. Ni wazi kwamba walihisi lilikuwa jambo la uungwana zaidi kutuambia tuwatembelee tena wakati ambapo walijua hawangekuwa nyumbani. Ilichukua muda kuzoea jambo hilo.
Siku moja tulikuwa tukiongea na mwanamume mmoja kwenye mlango wake wakati gari aina ya “jeep” liliposimama halafu akaruka nje padri aliyebadilika sura kwa kasirani nyingi. “Usipoacha kuongea na wasichana hao, utaondolewa katika ushirika!” akampigia kelele mwanamume huyo. Akitugeukia sisi, akatisha hivi: “Hamna haki ya kuhubiri hapa. Msipoacha, nitachukua hatua zaidi.” Kufikia hapo jirani wengi walikuwa wamekuja nje kutazama. Kwa hiyo sisi tukaendelea tu na kazi yetu, tukiangusha vitabu vingi na Biblia kwa watazamaji wenye kuulizia kulikuwa na nini.
Tukiisha kutumia miaka miwili katika bonde hili lenye sura nzuri ambako mafyulisi (matunda), njugu, na zabibu husitawi, kwanza hatukufurahi kupokea badiliko la mgawo kwenda Potosí, jiji la uchimbaji migodi lenye baridi kali sana lililo kwenye mwinuko wa meta 4,000. Sisi tulikuwa tumezoea vipupwe vya Kikanada vyenye baridi nyingi, lakini tofauti ilikuwa kwamba katika Potosí kwa kawaida nyumba hazikuwa na joto. Hata hivyo, katika Potosí kulikuwako ule ushirika mchangamfu wa kundi la Kikristo, hali hakuna kundi lililokuwa limefanyizwa katika Tarija.
Kufungua Eneo Jipya
Halafu, Elaine na mimi tukagawiwa kwenda Villamontes kufungua kazi ya kuhubiri huko. Lori tulilopanda lilikuwa limejazwa sukari haramu, kwa hiyo ili kuepuka matatizo na polisi kwenye vizuizi vya kukagua magari, dreva hakuanza safari mpaka usiku ulipoingia. Tuliona ni laiti tungalileta tochi, kwa maana kwa ghafula kitu fulani kilisukasuka kando yetu chini ya chandarua! Alikuwa ni msaidiaji wa dreva wa lori.
Saa kumi na moja asubuhi, tulisimama. Tukiwa twajihisi vibaya kutokana na mioshi yenye kutoka katika bomba la gari na kukumbwa na vumbi, tulitambaa tukatoka nje. Poromoko la ardhi lilikuwa limefunga njia yetu. Mwishowe, baada ya saa nne za kazi ngumu, mwenyewe aliagiza msaidiaji wake avushe gari kwenye ukingo mwembamba uliokuwa umeondolewa ardhi. Mwenyewe hata hakutaka kutazama wakati lori hilo lilipopita ukingoni kuvuka mahali hapo huku magurudumu yalo mawili-mawili ya nje yakizunguka hewani juu ya ile iliyoonekana kama abiso ya kina kisicho na mwisho kando ya barabara. Elaine na mimi tulivuka kwa miguu. Tulipoendelea kuelekea Villamontes katika lori hilo, zile kona nyembamba kali sana kwenye mapito ya mlimani zilikuwa ngumu sana hata dreva akalazimika mara nyingi kurudi nyuma na kutafuta maarifa ya kuzizungukia. Mwishowe, baada ya saa 35 za kuchoka sana, tukawasili.
Lilikuwa ono jipya kwa Elaine na mimi kuwa peke yetu kabisa. Pia jambo jipya kwetu lilikuwa wadudu wa kitropiki. Mbawakavu wakubwa wenye magamba magumu wakawa wakituangukia baada ya kugonga mwanga uliokuwa juu ya vichwa vyetu. Mainzi wadogo sana wakawa wakituuma vikali, wakisababisha mifuro yenye kuwasha iliyotoka umajimaji laini. Usiku wa kwanza kukaa katika makao yetu mapya, mimi nilienda nje kutumia choo cha nje. Lakini nilipowasha tochi yangu, sakafu nzima ikawa kana kwamba ndiyo makao ya kombamwiko. Mijusi walikimbia wakajibanze, na vyura wakubwa sana wakanipigia jicho wakiwa kwenye konakona. Nikaamua ningeweza kungojea mpaka asubuhi.
Baadaye, tulikuwa kando ya mto tukafikiri tungepumzika kwa kukalia gogo tuliloona hapo. Hata hivyo, tuliamua kwanza tufanye ziara ya kurudia hapo karibu. Tuliporudi, gogo halikuwapo. Wapita-njia wenye taharuki wakatuambia kwamba pandikizi la nyoka limekuwa hapo. Nina nderemo kwamba hatukujaribu kukalia “gogo” hilo!
Jambo tuliloonea shangwe zaidi juu ya Villamontes lilikuwa kuzuru watu jioni. Tulikuwa tukiwakuta wamekalia viti vya kusukwa wakiwa nje kando za njia, wakikonga kinywaji cha mimea kiitwacho maté. Tulitumia saa nyingi zenye kufurahisha tukieleza juu ya ahadi za Ufalme katika mazingira ya jinsi hiyo. Lakini nyakati ngumu zaidi zilikuja baada ya Elaine kuolewa na mimi nikapewa mgawo mpya kwenda Vallegrande nikiwa na mwenzi mpya.
Tabia Kama Uhayawani wa Magharibi!
Ili kufika Vallegrande, safari nyingine ya kuchosha ya siku tatu ilitakwa, na wakati huu mimi nilikuwa peke yangu. Zile barabara nyembamba za mavumbi zilionekana zikijipinda-pinda kuingia jangwani kana kwamba hazina mwisho. Mwishowe nikawasili jua likitua. Basi lilivuruga utulivu wa mji ambako farasi wali-kuwa wa kawaida kuliko magari. Watu walikodoa macho wakiwa chini ya vipenu vya nyumba zao vilivyochomoza juu ya kandokando za nyumba na kutegemezwa na viguzo vya miti. Baadhi ya wanaume walioegemea viguzo hivyo walivaa mishipi ya bastola. Karibu kila mtu alionekana amevalia nguo ya rangi nyeusi. Mimi nikawaza hivi: ‘Lo, tabia za huku ni kama zile za uhayawani wa Magharibi!”
Na kwa kweli ndivyo ilivyokuwa. Mabishano yalimalizwa kwa kutumia bunduki. Hata ingawa ulikuwa mji wenye watu kumi elfu tu, uuaji na jeuri yalikuwa mambo ya kawaida wakati huo. Idadi ya watu ilitawaliwa na genge la watu lililomiliki kinguvu nyumba ya pombe kwenye mwingilio wa mji. Wanagenge walijipatia riziki kwa kusimamisha mabasi na kuyanyang’anya vitu. Pia wakulima walinyang’anywa vitu vyao walipoleta mazao yao mjini. Wasichana wachanga walilalwa kinguvu mbele ya macho ya wazazi wao kwa kuelekezewa bunduki. Akina mama hata hawakutaka kuacha binti zao waende mwendo mfupi sana kununua vitu wakiwa peke yao.
Ebu fikiria jinsi tulivyowaza na kuwazua wakati kiongozi wa genge hilo alipoingia katika Jumba la Ufalme siku moja. Alikuwa amelewa. Mwangalizi wa mzunguko, aliyekuwa akitoa hotuba, alififia uso. “Mimi huamini!” ndivyo kapiga kelele huyo kiongozi wa genge huku akigota-gota nyuma ya benchi ya kukalia kwa nguvu sana hata ikavunjika. Kisha akambamba mwangalizi wa mzunguko. Lakini kwa ghafula akatulia, na mmoja kati ya wasikilizaji ambaye hapo zamani alikuwa rafiki yake shuleni akaweza kumwondosha hapo.
Hatimaye, jemadari wa jeshi alimkaidi huyo kiongozi wa genge kwamba wataonana. Jemadari aliagiza mbwa mfu aangikwe juu katika uwanja wa watu wote kukiwa na ishara yenye kusema: “Ondoka mjini, au sivyo utakiona kiki hiki.” Mwanagenge huyo aliondoka, na hali zikawa nafuu katika Vallegrande.
Nyakati fulani tulisafiri kwa saa 12 tukiwa tumepanda farasi ili kuhubiri katika vijiji vya nje-nje. Mwalimu mmoja wa shule katika kimoja cha vijiji hivyo alitupokea kwa ukaribishaji-wageni na baadaye akawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Wakati mmoja niliazima nyumbu ili niende huko nje, lakini kila wakati alipopita kwenye nyumba ya mmoja wa wenyewe wake wa zamani, alielekea huko, na ikawa lazima wao watuongoze kurudi njiani.
Kuna Miito ya Ushindani—Lakini Ningali Tajiri
Kama ilivyo kweli kuhusu wamisionari wengine wengi, mimi nimepata kwamba mwito wa ushindani ulio mkubwa kabisa huenda usiwe ni joto wala wadudu, baridi wala kimo cha usawa wa nchi, wala hata ugonjwa na umaskini. Bali, yaweza kuwa ni migongano ya nyutu. ‘Kwa nini magumu ya jinsi hiyo hutokea katika tengenezo la Yehova?’ Nilijiuliza hivyo kwa mshangao, na hata nikaanza kutia shaka kwamba Yehova alikuwa akinifanya tajiri kwa kunipa mibaraka. Ndipo nikakumbuka lile andiko juu ya baraka ya Yehova kwenye Mithali 10:22. Sehemu ya pili ya mstari huo husema, “Wala hachanganyi huzuni nayo.” Kwa hiyo haitupasi kumlaumu Yehova kwa magumu haya. Nilikuja kung’amua kwamba hayo ni sehemu ya kile ambacho Adamu alitupitishia nayo hutiwa ndani ya mambo ambayo Paulo husimulia kwenye Warumi 8:22: “Viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa.”
Nilikuwa nimekuwa nikiandikiana na Walter Meynberg wa Betheli ya Kanada, nami nilipokuwa likizoni Kanada katika 1966, tukafunga ndoa na kupewa mgawo kwenda La Paz, jiji kuu la Bolivia. Imekuwa baraka iliyoje kuona makundi hapa yakizidika kutoka moja tu nilipowasili katika Bolivia na kufikia 24, katika kila kona ya jiji. Imekuwa hivyo hivyo katika majiji mengine ya nchi. Kwa kweli, kikundi cha karibu wahubiri 160 waliokuwa wakihubiri habari njema katika Bolivia nilipowasili kwanza katika 1955 kimekua kikawa 7,000 hivi!
Kielelezo cha kupiga moyo konde ambacho mama aliweka zamani sana kimekuwa na tokeo la kufanya zaidi ya kumi wa familia yetu wenyewe wawe katika utumishi wa wakati wote. Mimi nafurahi sana kusema kwamba baba yangu alikuja kuwa Shahidi aliyejiweka wakfu, na watu zaidi ya 30 niliokuwa na pendeleo la kujifunza nao Biblia wamebatizwa. Je! huo si utajiri? Naam, mimi naamini ndivyo ilivyo. Kwa kweli, ‘baraka ya Yehova imenitajirisha.’