Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w90 7/15 kur. 21-23
  • ‘Dhidi ya Maarifa—Yaitwayo Hivyo kwa Ubandia’

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • ‘Dhidi ya Maarifa—Yaitwayo Hivyo kwa Ubandia’
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maisha na Huduma ya Mapema
  • Dhidi ya Maneno ya Uzushi
  • ‘Wasiotambua Mungu na Waangamie!’
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • “Injili ya Yuda” Ni Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Sehemu 12: 100-476 W.K.—Kuizima Kabisa Nuru ya Gospeli
    Amkeni!—1990
  • Je, Tatian Alitetea Imani au Alikuwa Mwasi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
w90 7/15 kur. 21-23

‘Dhidi ya Maarifa—Yaitwayo Hivyo kwa Ubandia’

UKWELI ni wa maana kwako kadiri gani? Je! wewe husumbuka fikira kwamba ubandia umepotosha, hata ukaficha, ukweli juu ya Muumba wa mbingu na dunia? Jambo hilo lilimsumbua sana fikira Irenayo, mtu mwenye kudai kuwa Mkristo wa karne ya pili ya Wakati wa Kawaida wetu. Alijaribu kufichua mambo hatari yasiyo sahihi ya Ugnosti, namna fulani ya Ukristo wa uasi-imani. Mapema kidogo, mtume Paulo alionya Timotheo aepuke hayo ‘yaitwayo maarifa kwa ubandia.’—1 Timotheo 6:20, 21, NW.

Irenayo alisema kwa ujasiri dhidi ya fundisho lenye makosa. Mathalani, fikiria alilosema katika utangulizi wa maandishi yake yenye maelezo marefu yenye kichwa “Kukanushwa na Kupinduliwa kwa Maarifa Yaitwayo Hivyo kwa Ubandia.” Aliandika hivi: “Watu fulani, kwa kuukataa ukweli, wanaingiza miongoni mwetu hadithi za ubandia na nasaba za vizazi zilizo batili, ambazo hutumika kama zenye kuleta vibishanio, kama vile mtume alivyosema [1 Timotheo 1:3, 4], kuliko kuleta kazi ya Mungu ya kujenga katika ile imani. Kwa ufasaha wao uliotungwa kwa hila ya kiufundi wao hukengeusha akili za wasio na ujuzi, na kuwachukua mateka, wakifisidi mafunuo thabiti ya Bwana, na kuwa wafafanuzi waovu wa kile kilichokuwa kikisemewa mema.”

Wagnosti (kutokana na neno la Kigiriki gnoʹsis, linalomaanisha “maarifa”) walidai kuwa na maarifa bora zaidi kupitia ufunuo wa siri na wakajisifu kwamba ndio waliokuwa “wasahihishaji wa mitume.” Ugnosti ilichanganya falsafa, makisio, na mafumbo ya kipagani pamoja na Ukristo wa uasi-imani. Irenayo alikataa kushiriki lolote la mambo hayo. Badala ya hivyo, alianza kupambana na mafundisho ya uzushi muda wote wa maisha. Bila shaka alijua sana uhitaji wa kutumia onyo hili la mtume Paulo: “Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu [falsafa, NW] yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo.”—Wakolosai 2:8; 1 Timotheo 4:7.

Maisha na Huduma ya Mapema

Ni machache yajulikanayo juu ya maisha ya mapema na historia ya kibinafsi ya Irenayo. Kwa ujumla hudhaniwa kwamba yeye alikuwa mwenyeji wa Esia Ndogo, aliyezaliwa kati ya 120 W.K. na 140 W.K. katika au karibu na jiji la Smirna. Irenayo ashuhudia kibinafsi kwamba katika ujana wake wa mapema, alifahamiana na Polycarp, mwangalizi katika kundi la Smirna.

Alipokuwa akijifunza chini ya ualimu wa Polycarp, yaonekana Irenayo alipata kuwa rafiki ya Florino. Polycarp alikuwa kiunzi hai kwa mitume. Yeye aliyafafanua Maandiko kwa wingi sana na akapendekeza kwa uthabiti kushikamana na mafundisho ya Yesu Kristo na mitume Wake. Hata hivyo, kujapokuwa na mazoezi haya mazuri ya Kimaandiko, Florino baadaye alipotoka akaingia katika mafundisho ya Valentino, kiongozi aliye mashuhuri kabisa wa harakati ya Kignosti!

Irenayo alitaka Florino aliyekuwa rafiki na mshirika wake hapo kwanza arudishwe kwenye fundisho timamu la Kimaandiko na kuponyoshwa kutoka kwenye Uvalentino. Kwa hiyo, Irenayo alisukumwa na moyo kuandikia Florino barua, akisema: “Mafundisho haya, Florino, . . . hayana uelewevu timamu; mafundisho haya hayapatani na kanisa, nayo yawahusisha wale wayafuatao katika ukosefu mkubwa kabisa wa kustahi Mungu; . . . ma-fundisho haya hayakupokezwa na wazee wa kikale waliotutangulia, na waliojuana sana na mitume.”

Akijitahidi kukumbusha Florino juu ya mazoezi mazuri yaliyopokewa kwenye miguu ya Polycarp aliye mashuhuri, Irenayo aliendelea kusema hivi: “Mimi nakumbuka matukio ya nyakati hizo . . . hivi kwamba naweza kupajua mahali ambapo Polycarp mbarikiwa alikuwa na desturi ya kupakaa na kutoa hotuba . . . Pia jinsi yeye alivyokuwa akihutubu juu ya uhusiano wake wa kufahamiana vizuri na Yohana, na pamoja na wale wengine waliokuwa wamemwona Bwana; pia jinsi alivyokuwa akisimulia maneno yao.”

Florino alikumbushwa kwamba Polycarp alifundisha mambo aliyokuwa amepokea “kutoka kwa mashahidi wenye kujionea kwa macho wa Neno la uhai, [na akawa] amesimulia yote kupatana na Maandiko. Mambo haya, yalinifikia kupitia rehema ya Mungu, halafu nikayasikia, nami nikayaandika, si juu ya karatasi bali katika moyo wangu; na kwa neema ya Mungu mimi naendelea kuikumbusha akili yangu mambo haya kwa usahihi. Na [kuhusu Uvalentino] mimi naweza kutoa ushahidi machoni pa Mungu kwamba kama mzee huyo wa kikale [Polycarp] angalisikia jambo la jinsi hiyo, angalilia kwa kupaaza sauti na kuziba masikio yake . . . Angalikimbia kutoka mahali ambamo, iwe ni kwa kuketi au kusimama, yeye alikuwa amesikia maneno ya jinsi hiyo.”

Hakuna maandishi ya kuonyesha kwamba Florino wakati wowote aliijibu barua yenye kugusa moyo na yenye uthabiti ya Irenayo. Lakini maneno ya Irenayo hufunua hangaikio lake halisi kwa rafiki mpenzi aliyekuwa ameiacha njia ya kweli ya na kujiachilia afuate uasi-imani.—Linganisha 2 Wathesalonike 2:3, 7-12.

Haijulikani ni wakati gani Irenayo alipoanza kukaa katika Gaul (Ufaransa). Katika mwaka 177 W.K., yeye alikuwa akitumikia akiwa mwangalizi katika kundi huko Lyons. Yaripotiwa kwamba huduma yake huko ilikuwa na matunda sana. Kwa uhakika, mwanahistoria Gregori wa Tours aliripoti kwamba kwa muda mfupi Irenayo alikuwa amefanikiwa kuongoa Lyons yote ifuate Ukristo. Bila shaka, hiyo ilikuwa taarifa yenye kutiliwa mkazo kupita kiasi.

Dhidi ya Maneno ya Uzushi

Maandishi makuu ya Irenayo, “Kukanushwa na Kupinduliwa kwa Yale Maarifa Yaitwayo Hivyo kwa Ubandia,” yalirejezewa sana-sana kwa lile jina “Dhidi ya Maneno ya Uzushi.” Yamegawanywa kuwa vitabu vitano. Vya kwanza viwili vina maelezo ya umaana mkubwa juu ya imani za madhehebu mbalimbali za wazushi, hasa ule uzushi wa Kivalentino. Katika vile vitabu vitatu vilivyobaki, Irenayo hujaribu kuonyesha wazi “hoja za kutoka kwenye Maandiko.”

Katika utangulizi wa kitabu chake cha tatu “Dhidi ya Maneno ya Uzushi,” Irenayo aandika hivi: “Kwa hiyo kumbukeni yale ambayo nimesema katika vitabu viwili vilivyotangulia; na kwa kuongezea hiki kwavyo nyinyi mtapata kutoka kwangu jibu kamili dhidi ya wazushi wote, nanyi mtaweza kuwakinza kwa uaminifu na kwa ujasiri kwa ajili ya ile imani moja ya kweli yenye kupatia uhai, ambayo Kanisa limepokea kutoka kwa mitume na ambayo huwapa watoto walo. Kwa maana Bwana wa wote aliwapa mitume wake nguvu ya ile gospeli, na kwa njia yao sisi pia tumejifunza ukweli, yaani, fundisho la Mwana wa Mungu—kama vile Bwana alivyosema kwao, ‘Yeye awasikiaye nyinyi hunisikia mimi, na yeye ambaye huwadharau nyinyi hunidharau mimi, na huyo aliyenituma mimi.’”

Ingawa Irenayo alikiri kwamba yeye hakuwa mwandikaji mzuri, alipiga moyo konde kufichua mambo yote ya “mafundisho maovu” ya Ugnosti. Yeye afanya manukuu na kutoa maelezo juu ya maandiko mengi na kutoa hoja kwa ustadi dhidi ya “walimu bandia” wa zile “madhehebu zenye uharibifu.” (2 Petro 2:1-3, NW) Yaonekana kwamba Irenayo alitatizika kuunga maandishi yake yawe namna moja yenye kuridhisha. Kwa nini? Kwa sababu alikuwa amekusanya habari nyingi mno.

Ni dhahiri kwamba ufichuzi wa Irenayo ulitokezwa baada ya jasho jingi na uchunguzi mwingi. Hoja zake ndefu hutoa utajiri wa habari juu ya vyanzo na ajabu za Ugnosti. Miandiko hii ya Irenayo ilikuwa pia faharisi yenye thamani kubwa ya angalau baadhi ya maoni ya Kimaandiko ambayo bado yalishikiliwa na wenye kudai kuwa washikamani wa Neno la Mungu mwishoni mwa karne ya pili W.K.

Irenayo hurudia-rudia kuthibitisha imani katika “Mungu mmoja, yule Baba Mweza Yote, aliyefanya mbingu, na dunia, na zile bahari, na vyote vilivyo ndani yazo, na katika Kristo Yesu mmoja, yule mwana wa Mungu, aliyefanywa mnofu kwa ajili ya wokovu wetu.” Wagnosti waliyakana hayo mambo ya uhakika!

Akisema dhidi ya Udoseti wa Kignosti (fundisho la kwamba Kristo hakuja kamwe akiwa na umbo la kibinadamu), Irenayo aliandika hivi: “Ni lazima Kristo awe binadamu, kama sisi, kama angetufidia kutoka kwenye uharibifu na kutukamilisha. Kama vile dhambi na kifo viliingia ulimwenguni kwa njia ya binadamu mmoja, hivyo ndivyo kwa uhalali na kwa faida yetu vingeweza kufutwa na binadamu mmoja tu; ingawa, bila shaka, si na mmoja aliye mzao wa kikawaida tu wa Adamu, na hivyo yeye mwenyewe akiwa ana uhitaji wa kufidiwa, bali na Adamu wa pili, aliyezaliwa kwa nguvu zenye kuzidi zile za kiasili, babu mpya wa jamii yetu.” (1 Wakorintho 15:45) Kwa upande mwingine, Wagnosti walikuwa Wenye Imani Mbili, wakiamini kwamba mambo ya kiroho ni mema lakini kwamba vitu vyote vyenye umbo la kimwili na mnofu ni viovu. Kwa hiyo, wao walimkataa binadamu Yesu Kristo.

Kwa kusababu kwamba mnofu wote ni mwovu, Wagnosti walikataa ndoa na uzazi, wakidai kwamba Shetani ndiye mwanzilishi wa vitu hivyo. Hata walimhesabia nyoka katika Edeni sifa ya kuwa na hekima ya kimungu! Maoni haya yalitokeza mitindo ya maisha yenye kupita kiasi, ama ule wa kujinyima raha yoyote ama ule wa kujitia katika anasa ya kimnofu. Wakidai kwamba wokovu ulikuja kupitia Ugnosti, au maarifa ya kibinafsi yenye mafumbo, hawakuuachia nafasi ukweli wa Neno la Mungu.

Tofauti na hilo, hoja za Irenayo zilitia ndani kuiamini Mileani na zikaonyesha ufahamu wa kadiri fulani juu ya tazamio la kupata maisha ya wakati ujao yenye amani duniani. Yeye alijitahidi kuungamanisha vikundi vya mafarakano vyenye kuongezeka vya wakati wake kwa kulitumia Neno la Mungu lenye nguvu nyingi. Naye hukumbukwa kwa ujumla kwa sababu ya ufahamivu wake wenye fikira safi za uelewevu sahihi sana, na uamuzi timamu.

Ingawa watu fulani humpa Irenayo (aliyekufa karibu 200 W.K.) sifa ya kusitawisha mafundisho ya kweli ya imani ya Kikristo, ni lazima ikumbukwe kwamba wakati wake ulikuwa wa badiliko na wa uasi-imani uliotabiriwa. Nyakati fulani, hoja zake hukosa kidogo kupambanuka waziwazi, hata huwa zenye kujipinga. Hata hivyo, sisi twathamini sana ushuhuda wa watu waliosema kwa ujasiri wakipendelea Neno la Mungu lililovuviwa na kuandikwa badala ya kupendelea mapokeo ya wanadamu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki