Kumtegemea Yehova Huleta Furaha
KAMA ILIVYOSIMULIWA NA JACK HALLIDAY NATHAN
Labda wewe umeusikia usemi huu (wa Kiingereza ulio wa kitamathali), “Kazaliwa na kijiko cha fedha kinywani mwake.” Basi, mimi nilipozaliwa huko nyuma katika 1897, karibu iwe hivyo kihalisi katika kisa changu.
ULIKUWA mwaka wa 60 wa utawala wa Malkia Victoria, yubile yake ya kialmasi. Watoto waliozaliwa mwaka huo katika Uingereza walituzwa kijiko cha fedha. Milki ya Uingereza ilikuwa katika utukufu wayo, ikivuna manufaa za Vuvumko la Viwanda nyumbani na biashara yenye ufanisi iliyotokana na koloni zenye kusitawi ng’ambo.
Babu yangu alikuwa Myahudi, na baba yangu akawa mwanachuo Mwebrania, mwenye maarifa ya kutosha katika Maandiko ya Kiebrania. Lakini nyanya yangu alikuwa binti ya askofu Mwanglikana, na kwa sababu ya uvutano wake, baba yangu alimkubali Yesu Kristo kuwa Mesiya. Miandiko ya Charles Taze Russell ilivutia wazazi wangu wote wawili, kwa hiyo sisi hatukuamini kamwe Utatu wala fundisho la moto wa helo.
Wakati wa utoto wangu, farasi walikuwa wangali ndiyo njia kuu ya usafiri katika Uingereza, na mikokoteni isiyovutwa na farasi, au magari, ilikuwa michache. Katika 1913, kwa sababu ya mimi kupenda farasi, nilijiunga na kikosi cha usafirishaji wa kutumia farasi cha jeshi la eneo (jeshi la mgambo). Ilipofoka Vita ya Ulimwengu 1, nilihamishwa nikawa kwenye jeshi la kawaida na kusafirishwa kwa meli kwenda kwenye kikosi cha kukabili Ugiriki, ambako nilipata maleria. Baadaye, nilipelekwa kwenye kikosi cha magharibi katika Ufaransa nikiwa mtumiaji wa bunduki-mimina-risasi na hatimaye nikachukuliwa na Wajeremani nikiwa mfungwa katika 1917.
Kupata Kusudi Maishani Katika India
Baada ya vita kwisha katika 1918, hakukupatikana kazi yoyote katika Uingereza, kwa hiyo nikajiunga tena na jeshi na kwenda zangu India nikiwa sehemu ya jeshi la kukaa mjini wakati wa amani. Katika Mei 1920 maleria iliwaka tena, nami nikapelekwa vilimani nikapate nafuu. Huko nikasoma vitabu vyote ambavyo ningeweza kuvipata, kutia na Biblia. Kuyasoma Maandiko kulizidisha sana upendezi wangu katika kurudi kwa Bwana.
Miezi kadhaa baadaye, nikiwa huko Kanpur, nilianzisha kikundi cha funzo la Biblia, nikitumainia kujifunza mengi zaidi juu ya kurudi kwa Bwana. Huko ndiko nilikokutana na Fredrick James, askari Mwingereza wa hapo zamani ambaye sasa alikuwa Mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii. Alinieleza kwamba Yesu alikuwa amekuwapo tangu 1914, bila kuonekana na binadamu. Hiyo ilikuwa ndiyo habari yenye kusisimua kabisa niliyokuwa nimepata kusikia. Himizo langu la kwanza lilikuwa kuondoka jeshini. Umwagaji damu na vifo vya vita ya Ulaya vilikuwa vimeninyarafisha. Nilitaka kuwa misionari mwenye amani na kuhubiri habari njema hizi juu ya kuwapo kwa Kristo.
Hata hivyo, jeshi halikukubali kuniachilia. Badala ya hivyo, walinipeleka India magharibi, sasa Pakistan. Nikiwa huko, nilisoma Studies in the Scriptures, kilichotungwa na Charles Taze Russell, nami nikasadiki hata zaidi kwamba nilipaswa kuitikia wito wa kuhubiri. Nilianza kuwa na majinamizi yaliyoniacha nimeshuka moyo. Kwa vumaiko la kutatizika nikamwandikia Ndugu James, naye akanialika nyumbani kwake katika Kanpur. Siku niliyowasili ilikuwa ndiyo Ukumbusho wa kifo cha Bwana. Siku hiyo ilikuwa na uvutano mkubwa juu ya maisha yangu—niliazimia kubaki mseja na pia kufanya huduma ya wakati wote iwe mradi wangu maishani.
Kurudi Uingereza
Mwishoni-mwishoni mwa 1921, nilihamishwa kurudi Uingereza, na katika masika ya 1922, nikaruhusiwa kutoka jeshini. Kiangazi hicho J. F. Rutherford, msimamizi wa pili wa Watch Tower Society, alikuja Uingereza, nami nikaenda pamoja na wazazi wangu kusikia hotuba yake kwenye Royal Albert Hall, London. Baadaye, nilisukumwa na moyo kutoa huduma zangu Betheli, kama vile maofisi ya tawi ya Watch Tower Society yaitwavyo, lakini nikatiwa moyo kwa fadhili nifanye kadiri fulani ya kazi ya kolpota (kuhubiri wakati wote) kwanza. Kwa hiyo nikaacha kazi yangu na kukubali mgawo wa eneo kusini mwa Uingereza. Nikiwa bila ujuzi, nikiwa na krauni moja (senti 50 za United States) mfukoni mwangu, na kwa kumtegemea Yehova, nikaanza kazi-maisha yangu nikiwa mhudumu wa wakati wote. Karibu na Machi 1924, nilialikwa Betheli.
Ingawa hivyo, mwaka uliofuata niliombwa niondoke Betheli, nami nikahisi nimevunjika moyo kweli kweli, nikihisi kwamba nilikuwa nikitiwa nidhamu kwa jambo ambalo sikuwa wa kulaumiwa kwalo. Katika muda huo mfupi, Betheli ilikuwa imekuwa maisha yangu. Lakini kwa kuweka tatizo hilo mbele za Yehova katika sala na kutegemea kwamba mapenzi yake yangefanywa, niliweza kuendelea kwa shangwe katika mgawo wa upainia niliopewa. Katika Mei 1926, nilialikwa kurudi Betheli, ambako nilibaki kwa miaka 11 iliyofuata.
Ndugu Rutherford alizuru Uingereza tena katika 1936 na kunialika niende Kanada kushiriki katika kazi ya Ufalme huko. Hata hivyo, kwa sababu ya jambo fulani la kutoelewana, nilipoteza kibali cha Ndugu Rutherford kwa kufunua habari fulani ya siri. Ningali nakumbuka maneno yake hususa: “Jack, mimi siwezi kukutegemea. Zirarue tikiti zako!” Lo, tukio lenye kuponda kama nini! Lakini ilikuwa nidhamu iliyohitajiwa sana, na baadaye, nikiwa pamoja na ndugu mwingine, niligawiwa kuwa painia kwa miezi minane iliyofuata. Pendeleo hilo la utumishi lilininyanyua kutoka uzito wangu wa moyo, nami nikajifunza kutokana na nidhamu hiyo.
Huduma Iliyopanuliwa Katika Kanada
Karibu mwaka mmoja baadaye wakati wa ziara yake iliyofuata ya Uingereza, Ndugu Rutherford alitaja tena ile habari ya Kanada. Nilikuwa mwenye hamu nyingi ya kupata fursa hiyo na kwa uharaka nikakubali mgawo huko. Baada ya kutumikia miezi michache kwenye Betheli ya Kanada, niligawiwa kuwa mwakilishi mwenye kusafiri wa Sosaiti kusini-magharibi mwa Ontario. Yaliyo mengi ya makundi huko yalikuwa madogo na yalihitaji sana kitia-moyo. Lakini miaka hiyo ya mapema ilikuwa ya shangwe kama nini, kujapokuwako magumu ya kimwili kutokana na hali kali za halihewa na usafiri wa kiwasiwasi!
Mimi sitasahau kamwe uchangamfu na uthamini wa kiroho wa kundi moja dogo la Wahindi wenyeji karibu na Brantford. Ulikuwa wakati wa kipupwe, na theluji zilikuwa za kina kirefu, zikifanya iwe vigumu gari langu la “Model T Ford” kupita. Hakuna aliyekuwa ananitarajia, nami nilipowasili, nilipata kwamba akina ndugu walikuwa wameingia vichakani kutafuta kuni. Hivyo basi nikaenda kuwatafuta, theluji ikiwa ya kina cha kunifika kiunoni. Nilipowakuta mwishowe, walishangaa, hata hivyo wakafurahi, kuniona. Waliangusha chini kila kitu, wakaja nyumbani, na kupanga mkutano jioni hiyo hiyo.
Kwenye Beamsville ya karibu, ndugu waaminifu na mimi tuling’ang’ana miezi mingi na wazee wa kuchaguliwa na waasi-imani. Lilikuwa pendeleo kama nini kuona jinsi roho ya Yehova ilivyoendesha mambo ili kuisafisha hali hiyo! Tegemeo katika Yehova na uaminifu-mshikamanifu kwa tengenezo lake vilitokeza baraka nyingi kwa makundi wakati wa miaka hiyo ya mapema. Watoto wengi kutoka makundi hayo walikua wakawa wakubwa kuingia upainia, kwenda Betheli, kuona shangwe ya migawo ya kimisionari, na kuwa waangalizi wanaosafiri. Mimi sijasahau kamwe shangwe za kukaa pamoja na familia za Kikristo zenye uaminifu-mshikamanifu ambazo ziliwatokeza vijana wazuri jinsi hiyo. Familia hizo zikawa familia yangu, na watoto wazo wakawa watoto wangu.
Miaka ya Kuwa Chini ya Marufuku
Wakati wa kivumbi cha vita ya 1940, kazi ya Mashahidi wa Yehova iliwekwa chini ya marufuku. Lo, mshtuko ulioje! Matangazo yenye kudhaminiwa na serikali yalituagiza tuwape polisi fasihi zetu, maandishi yetu ya kundi, na funguo zetu za Jumba la Ufalme. Kwa kung’amua uharaka wa hali hiyo, nilizunguka kwenye makundi nikayahimiza yafiche fasihi na maandishi yao. Akina ndugu walitiwa moyo kukutana katika nyumba za faragha, kwenye nyumba tofauti kila juma. Baada ya muda makundi yakaanzisha tena huduma ya mlango kwa mlango, yakitumia Biblia tu. Hiyo ilithibitika kuwa baraka, kwa maana sisi sote tulijifunza kutumia Biblia zetu vizuri zaidi.
Baadaye mwaka huo tulipokea ugavi mkubwa wa kijitabu End of Nazism (Mwisho wa Unazi) kutoka United States. Kuingiza Kanada fasihi hiyo iliyopigwa marufuku kulitaka akili nyingi. Akina ndugu waliwabeba askari walioomba lifti, nao wakakalia vile vibweta (katoni), hivyo wakilinda kijitabu hicho marufuku bila kujua. Halafu asubuhi moja katika Novemba, kati ya saa tisa na kumi na mbili, nchi nzima ilitifuliwa kivumbi na Mashahidi walioacha nakala moja ya kijitabu hicho kwenye sakafu ya mlango wa nyumba zilizo nyingi katika Kanada.
Wakati wa miaka hiyo ya marufuku, mimi niliendelea katika huduma ya painia katika mkoa wa British Columbia, magharibi mwa Kanada. Kabla ya marufuku, akina ndugu walitumia mashua wakiwazuru watu vijijini katika vipenyo vya mahali pa upweke kutoka Vancouver (Vankuva) hadi huko mbali Alaska. Marufuku ilipotokea, fasihi nyingi sana zilikuwa mashuani, kwa hiyo Mashahidi wakaipakua kwa kuwaachia watu wenye urafiki wakiwa njiani kwenda kwenye bandari ambako mashua ingepelekwa ikatunzwe. Baadaye, mimi nilipanda mashua ya uvuvi ili nikatafute fasihi hizo, halafu, wakati wa majira ya kuvua salmoni, nikapanga akina ndugu wakaichukue kutoka kwa watu hao wenye kupendezwa. Baada ya muda fasihi hizo zililetwa Vancouver kwa ugawaji mpana zaidi, zikiwa zimefunikwa katika sehemu za tumboni mwa mashua za uvuvi.
Mwishoni-mwishoni mwa 1943, tulipokea habari kwamba marufuku juu ya Mashahidi wa Yehova imeondolewa. Hata hivyo, haikuondolewa kwa Watch Tower Society. Kwa hiyo tukaendelea kama hapo mbele, tukitumia Biblia tu katika huduma yetu ya nyumba kwa nyumba. Lakini sasa tungeweza kujitambulisha wenyewe kuwa Mashahidi wa Yehova. Marufuku ilipoanza, tulikuwa na Mashahidi karibu 6,700; ilipoondolewa, tulikuwa 11,000 barabara!
Maisha Nikiwa Mwangalizi Anayesafiri
Nikiwa mwakilishi anayesafiri wa Sosaiti, nilifanya mwendo wa kilometa zisizohesabika wakati wa miaka michache iliyofuata, nikifanya kazi pamoja na makundi na kuyatia moyo. Katika kipupwe, niliandamana na akina ndugu katika gari la ajabu liitwalo kabusi. Hilo lilikuwa gari la kuteleza chini-chini lililofunikwa na lenye kuburutwa na farasi, likiwa kamili kwa kuwekewa jiko la kutumia kuni lisilovuja hewa lenye bomba la kutoa moshi nje. Mara nyingi, kwa kuanza kabla ya mapambazuko kukiwa na watu wafikao sita humo ndani, tulisafiri kupitia theluji ya kina kirefu kwa kilometa 35 au zaidi, tukitembelea mashamba ya kando za njia. Ilikuwa lazima dereva awe chonjo kwa sababu mimomonyoko ya theluji ingeweza kuipindusha kabusi kwa upande, ikimwaga waliomo pamoja na makaa moto kutoka kwenye jiko la kuni.
Katika 1947, niliwekwa niangalie wilaya ya kwanza nchini, ambayo ilihusisha nchi nzima. Nilikuwa na kusanyiko la mzunguko la kutumikia karibu kila wiki. Makusanyiko yalifanywa katika nyanja za michezo ya barafuni, nyanja za mpira, nyanja za mashindano ya mbio, majumba ya ushirika, na majumba ya kijumuiya. Mipango kwa ajili ya makusanyiko haya ilitaka uangalifu mwingi kabla ya programu kuweza kuanza. Katika 1950, Frank Franske aliwekwa kuwa mwangalizi wa wilaya wa pili katika Kanada, na baadaye wakaongezewa watano zaidi wa hawa waangalizi wanaosafiri.
Muda wa miaka iliyopita, mimi nimesafiri kwa ndege nyepesi, kwa mashua za uvuvi, kwa magari makubwa ya kusafiri katika theluji yakiwa na vikanyagio na vitelezo viitwayo mabombadia, kwa ndege-theluji (visafirio vilivyo na rafardha nyuma na vitelezo upande wa mbele kutumika kama usukani), na kwa njia zilizo za kikawaida—gari-moshi, basi, na motakaa. Nyakati fulani, tukiwa katika ndege tulikuwa tukipita karibu sana na vilele vya Milima Rocky yenye fahari, halafu ndege inashuka ghafula kwa kichwa kuingia katika mabonde ya kina kirefu yaliyofichika ili kuvifikia vikundi vya akina ndugu walio peke yao.
Nimepitapita sehemu nyingi za Kanada mara nyingi. Nimekaa katika nyumba zilizojengwa kwa magogo yakiwa na baridi sana hivi kwamba tungeweza kuona pumzi yetu asubuhi na katika nyumba za mashambani zisizo na vifaa vya ki-siku-hizi. Hata hivyo, kwa kuyapita yote hayo, nilipata hisi kubwa ya uradhi, nikijua nilikuwa nikifanya kazi ya Yehova, nikiwatia moyo watu wa Yehova.
Mapendeleo Zaidi ya Utumishi
Kwa miaka 33 iliyopita, nimepata pendeleo la kuwa mshiriki wa familia ya Betheli ya Kanada, na pia kutumikia nikiwa msemaji wa mkusanyiko katika Uingereza, Ulaya, Afrika, Australia, New Zealand, na Mashariki ya Mbali. Katika Australia, nilikutana na binti ya Ndugu James, aliyekuwa amenitia moyo sana katika India. Ndugu James hakuwa kamwe misionari, bali alipitishia familia yake urithi mzuri wa kiroho.
Leo nimezungukwa na mamia ya wanaume na wanawake vijana katika Betheli ya Kanada. Njia ambayo wao hutumia sulubu yao ya ujana katika utumishi wa Yehova ni yenye kutia moyo na kusisimua. Macho yangu yamefifia, lakini hao wenye ujana zaidi hunisomea. Miguu yangu ni dhaifu, lakini wao huenda pamoja nami katika huduma ya shambani. Baadhi yao huuliza ni jinsi gani mimi hukabili matatizo ya afya yashirikishwayo na uzee. Kwanza, mimi hujifunza Neno la Mungu kila siku. Hilo huweka akili na moyo wangu juu ya mambo ya kiroho.
Kwa kweli, limekuwa pendeleo kubwa kutembea na kuongea na Baba yangu wa kimbingu, Yehova, kwa miaka 69 ya maisha yangu ya wakfu, miaka 67 kati yayo ikiwa imetumiwa katika utumishi wa wakati wote. Sikuzote mimi nimempata Yehova kuwa mwenye upendo na huruma, mwenye kusamehe manyonge ya kibinadamu na kuwapa nguvu na imara wale wanaomtegemea. Tumaini langu ni kudumisha ukamilifu-maadili wangu na uaminifu-mshikamanifu kwa Yehova na tengenezo lake hadi mwisho, nikitumainia ahadi ya kwamba katika wakati ufaao nitaungamana na Bwana wangu mpendwa, Yesu Kristo, na pamoja na wengi wa ndugu na dada zangu waaminifu katika utukufu wa kimbingu.—Zaburi 84:12.
[Picha katika ukurasa wa 12]
Ndege-theluji zilisafiri kwenye nyika za nchi kwa miendo ya kufikia
kilometa 80 kwa saa
[Picha katika ukurasa wa 13]
Wakati wa kipupwe, kabusi yenye kuburutwa na farasi ilitumiwa kutoa ushahidi juu ya nyanda pana za manyasi (preiri) ya Kanada