Masada Je! Ni Ithibati ya Kwamba Mesiya Alikuwa Amekuja?
UMWAGAJI-DAMU kwa jina la dini umekuwa tauni yenye kutukia-tukia katika historia. Masada haikuwa tofauti, kwa maana wenye kuikinga walikuwa na motisha imara za kidini. Ukiyazuru machimbuo huko Masada, waweza kuona magofu ya sinagogi moja ambako wanaume watumia-sime walikutana kwa ajili ya ibada na miogo ya kidesturi iliyotumiwa kwa usafishaji wa kidini.
Vijipande vya Biblia vimepatikana pia huko Masada. Huenda wewe ukashangaa, ni jinsi gani ujumbe wa Kibiblia uliokuwa na wanaume watumia-sime ulivyolingana na tusomayo katika Biblia leo? Dakt. Yigael Yadin, katika kitabu chake Masada, aliandika juu ya ugunduzi wa kwanza wa jinsi hiyo:
“Uchunguzi wa karibu mahali hapo watuonyesha mara hiyo kwamba hapa palikuwa na kipande kimoja kutokana na Book of Psalms, nasi tungeweza hata kuzitambua sura: kisehemu hicho kilianzia Zaburi 81 hadi Zaburi 85. . . . Iliwezekana kujua tarehe yacho bila kishaka chochote. Haingeweza kuwa baada ya mwaka 73 AD, mwaka ambao Masada ilianguka. . . . Kama vile ilivyo na hati-kunjo nyingine za kibiblia tulizopata baadaye, kisehemu hiki cha kutoka Book of Psalms chakaribia kulingana kabisa . . . na maandishi ya vitabu vya kibiblia tuyatumiayo leo.”
Kwa wazi, wale wanaume watumia-sime waliamini kwamba Mtungaji wa Kimungu wa Maandiko ya Kiebrania angebariki uasi wao dhidi ya Roma. Kama vile The Universal Jewish Encyclopedia kielezavyo: “Bidii ya ushupavu wa Wayahudi katika ile Vita Kubwa dhidi ya Roma (66-73 W.K.) iliimarishwa na imani yao kwamba ile enzi ya Kimesiya ilikuwa ikikaribia sana. Kulipoteza Hekalu kuliyaongezea makisio tu juu ya kuja kwa Mesiya.”
Kuja kwa Mesiya
“Wayahudi waliokuwa na hamu nyingi ya kumwona Mesiya,” chataarifu The Encyclopedia of Religion, “walikuwa mara nyingi wakitegemeza makadirio yao juu ya Book of Daniel.” Ni kweli kwamba nabii Danieli alitabiri kuja kwa “Mesiya yule Kiongozi.” (Danieli 9:25, NW) Katika masimulizi mengine mawili, Danieli alisema kwamba Mesiya angekuwa Mtawala wa ulimwengu na kwamba Ufalme Wake ungeharibu serikali zote za kibinadamu zenye upinzani.—Danieli 2:44; 7:13, 14.
Wanamapinduzi Wayahudi wa karne ya kwanza walihisi kwamba wakati ulikuwa umefika kwa utimizo wa njozi hizo za kiunabii. “Zaidi ya kinginecho chote kilichowachochea kwenye vita,” ataarifu Yosefo, “ilikuwa [ile imani] ya kwamba wakati huo mtu mmoja wa kutoka nchi yao angekuwa mtawala wa ulimwengu.” Lakini Danieli alitabiri kwamba ni lazima Kiongozi wa Kimesiya ‘akatiliwe mbali’ na kwamba baada ya kifo chake Yerusalemu na hekalu lalo vingeharibiwa na ‘watu wa kiongozi mwingine aliyekuwa anakuja.’—Danieli 9:25, 26, NW.
Maoni ya Kiyahudi ya Utawala wa Wasio Wayahudi
Yudea ya karne ya kwanza iligawanywa kati ya matajiri wachache na maskini wengi. Wayahudi fulani matajiri, hasa miongoni mwa Masadukayo na Mafarisayo, walithamini mamlaka ambayo Roma iliwaruhusu kuwa nayo katika bara, nao waliwadharau watu wa kika-waida. Hivyo, wao walipinga wazo lolote la mapinduzi, na badala yalo wakafanya kazi kutafuta mahusiano yenye amani pamoja na Roma.—Luka 16:14; 19:45, 46; Yohana 2:14; 7:47-49; 11:47, 48.
Kwa upande mwingine, Wayudea wa kawaida waliteseka chini ya mzigo wa kutozwa kodi na Waroma na kuonewa na wananchi wao wenyewe. Hawakupata faraja kwa kuwa chini ya ile iliyoitwa Pax Romana (Amani ya Kiroma) bali walitaka badiliko. Hitilafiano hili la mapendezi lilitokeza ugomvi mbaya sana wa wao kwa wao. “Kikundi kimoja kiliazimia sana kupata utawala,” akaandika Yosefo, “kile kingine kikaazimia sana kufanya jeuri na kuwanyang’anya matajiri.”
Kwa kielelezo, wale wanaume watumia-sime walipora vitu vya Wayahudi wenzao na kuwaua na kutetea vitendo hivyo vya ugaidi kuwa ni adhabu kwa Wayahudi waliosemekana kupanga njama na Roma. Rabi mmoja wa karne ya pili, Johanan ben Torta, alitoa sababu hii kwa afa lililowapata Wayahudi wa karne ya kwanza: “Wao walitamani pesa mno na wakachukiana.”
Si ajabu kwamba Wayahudi wale waliokuwa wahofu Mungu kikweli walitamani sana kutokea kwa Mesiya, ambaye walitumaini angepindua utawala wa Kiroma na kuanzisha Ufalme wa Mungu wenye haki. Lakini watu wasioongozwa na dhamiri walitumia matumaini hayo kwa faida zao wenyewe.
Wamesiya Bandia
Karibu na mwaka 33 W.K., kiongozi mmoja Myahudi jina lake Gamalieli aliwakumbusha hivi watawala wenzao wa Yerusalemu: “Kabla ya siku hizi . . . aliondoka Yuda [Yudasi, NW] Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha [za usajili, NW], akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika.”—Matendo 5:36, 37.
‘Usajili’ uliotokeza uasi wa Yudasi ulitengenezwa katika 6 W.K. kwa kusudi la kuinua kodi kwa ajili ya Roma. Yosefo atuambia kwamba Yudasi alipiga mbiu kwamba Wayahudi “walikuwa waoga ikiwa walijitiisha kuwalipa Waroma kodi.” Jina Yudasi hutokana na jina Yuda, likidokeza kwamba yeye alikuwa wa kabila ambalo Mesiya alitarajiwa kutokana nalo. (Mwanzo 49:10) “Ufasaha wake moto-moto na umaarufu wa mafundisho yake ulivuta idadi kubwa za watu kwenye kiwango chake, na wengi walimchukua kuwa ndiye Mesiya,” yataarifu Cyclopædia ya McClintock na Strong.
Angalia kwamba Matendo 5:37 yaripoti kwamba wafuasi wa Yudasi huyu hawakuangamia pamoja naye. Harakati yake, kulingana na mwanachuo Myahudi Gaalya Cornfeld, “ilitia mizizi ya kina kirefu na matumaini ya kimesiya.” Kwa uhakika, viongozi wawili wa wale wanaume watumia-sime, Menahemu na Eleazari, walikuwa wa asili ya huyo Yudasi Mgalilaya. Mwanzoni mwa maasi ya Kiyahudi katika 66 W.K., Menahemu aliwapa wafuasi wake silaha zilizokuwa zimewekwa akiba Masada. Halafu, “alirudi akiwa kama mfalme Yerusalemu” na “akawa kiongozi wa mapinduzi hayo.” Encyclopaedia Judaica yaongezea kwamba, “Ni kama jambo la hakika kwamba Menahemu [mwana wa] Yuda alionwa kuwa Mesiya.”
Hata hivyo, katika mwaka huo huo, Menahemu aliuawa na washiriki wa harakati ya ushindani ya wanamapinduzi Wayahudi. Wafuasi wake walikimbia wakarudi Masada, ambako Eleazari alichukua amri juu ya wale wanaume watumia-sime mpaka 73 W.K. Hotuba ya Eleazari juu ya kujiua yafanana na yale mafundisho yenye makosa ya Yudasi baba yake wa zamani: “Muda mrefu tangu wakati huo, enyi waandamani wangu mashujaa, sisi tulipiga moyo konde tusitumikie wala Waroma wala mtu mwingine yeyote isipokuwa Mungu tu.”
Kutokuwamo kwa Wakristo Wayudea
Kabla ya maasi ya Kiyahudi katika 66 W.K., makundi ya Kikristo yalikuwa yameanzishwa katika Yudea, bila shaka kutia na kundi la Yerusalemu. (Matendo 9:31) Yalifanyika kutokana na Wayahudi walioamini kwamba Yesu wa Nazareti alikuwa Mesiya ambaye kifo na ufufuo wake vilikuwa vimetabiriwa. (Matendo 2:22-36) Wakristo Wayahudi walieneza imani zao kwa bidii, wakingojea kwa amani kuja kwa pili kwa Mesiya, akiwa mtawala wa ulimwengu. Yesu alikuwa ameonyesha kwamba angerudi “baada ya muda mrefu.”—Mathayo 25:19, 31, HNWW; 28:19, 20; Matendo 1:8-11, UV.
Lakini maasi ya Wayahudi yalipofoka katika 66 W.K., ni nini kilichowalinda Wakristo hao Wayudea wasisisimuke bure kuhusu mafanikio yayo ya kwanza? Bila shaka walikumbuka onyo la Bwana-Mkubwa wao: “Wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.” (Mathayo 26:52) Yesu alikuwa pia amewapa maoni yenye usawaziko juu ya mamlaka ya kiserikali: “Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari,” akasema, “na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu.” (Marko 12:17) Zaidi ya hilo, Yesu alikuwa ametabiri kwamba wenye kusingizia kwamba wao ndio mesiya wangekuja, wakisema, “Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia,” lakini akaonya hivi: “Msiwafuate hao.”—Luka 21:8.
Yesu hata alikuwa ametabiri tokeo la maasi ya Kiyahudi, akisema: “Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi [yaliyopiga kambi, NW], ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie . . . kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili. Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote.”—Luka 21:20-24.
Lile furiko baya sana la uharibifu lililofuata maasi ya Kiyahudi lilikuwa utimizo wa kutazamisha wa unabii wa Yesu! Na bado Wakristo Wayudea waliepuka kwa kutii “wakimbilie milimani.” “Kabla ya mazingiwa ya Yerusalemu yaliyofanywa na Tito [katika 70 W.K.],” yataarifu Encyclopaedia Judaica, “jumuiya yalo ya Kikristo ilihamia Pella.” Kwa kupendeza, Pella ilikuwa kuelekea kaskazini, katika vilima vya chini vya msafa wa milima ng’ambo ya Mto Yordani na hivyo basi Bonde la Yordani liliitenganisha kabisa na Yudea. “Ni vigumu kutegemea usimulizi wa mkimbio huu ikiwa unabii [wa Yesu] uliandikwa baada ya tukio hilo,” ataarifu G. A. Williamson katika utangulizi wake kwa Josephus—The Jewish War.
Kwa kweli, mkimbio huo wenye mafanikio wa Wakristo Wayudea ni uthibitisho thabiti kwamba wao walikuwa wafuasi wa yule Mesiya wa kweli. Hilo latokeza maswali ya maana. Lilikuwa nini kusudi la kuja kwa Mesiya mara ya kwanza? Na je! yale maasi ya Kiyahudi yenye msiba yavumisha onyo gani kwetu leo, hasa kile kisehemu cha wanadamu kibandikwacho jina la kwamba ni “cha Kikristo”? Maswali haya yatazungumzwa zaidi katika gazeti hili.