Masada Kwa Nini Ilitukia?
“MUDA mrefu tangu hapo, enyi waandamani wangu wa karibu, sisi tulipiga moyo konde tusitumikie wala Waroma wala mtu mwingine yeyote isipokuwa Mungu tu . . . Njoni, maadamu mikono yetu iko huru kuushika upanga . . . Acheni tufe kabla hatujawa watumwa chini ya adui zetu, na tuyaache maisha haya pamoja tukiwa wanaume huru pamoja na watoto na wake zetu!”
Himizo hili la kuvumaika laripotiwa kuwa lilitolewa na Eleazari, mwana wa Yairi (au Ben Ya’ir), kwa wenye kukinga Masada. Lilirekodiwa na mwanahistoria wa karne ya kwanza Yosefo katika kichapo chake The Jewish War. Kwa nini kiongozi huyo Myahudi akahimiza waandamani wake wafanye uuaji na ujiuaji wa kihalaiki, kinyume cha sheria ya Mungu? (Kutoka 20:13) La maana zaidi, maarifa juu ya hali hizo yaweza kukusaidiaje uendelee kuwa hai katika ulimwengu wa leo wenye jeuri?
Wanaume Watumia-Sime wa Masada
Kabla ya mfoko wa uasi wa Kiyahudi katika 66 W.K., boma la askari lilikuwa huko Masada, kilele cha kilima chenye ngome karibu na Bahari ya Chumvi. Ingawa Masada ilikuwa katika mahali papweke, Herode Mkubwa alikuwa amejengesha jumba zuri la kifalme la kukaliwa wakati wa kipupwe. Alijengesha mfumo wa maji hivi kwamba miogo ya maji moto ingeweza kuonewa shangwe. Ingawa hivyo, chini ya ukaliwa wa Kiroma, ngome hiyo ilikuwa akiba ya silaha nyingi. Wakati misisimuko ilipochacha dhidi ya kukaliwa kwa Palestina na Waroma, silaha hizo zikawa katika hatari ya kuingia mikononi mwa wanamapinduzi Wayahudi. Kikundi kimoja cha jinsi hiyo kilikuwa Wasikarii, kumaanisha “wanaume watumia-sime,” watajwao katika Biblia kuwa walihusika katika maasi.—Matendo 21:38, NW.
Katika 66 W.K. wanaume hao watumia--sime waliteka Masada. Wakiwa na silaha zao walizojipatia karibuni, walipiga miguu kwenda Yerusalemu kuunga mkono uasi dhidi ya utawala wa Kiroma. Machinjo makubwa ambayo wanamapinduzi Wayahudi walifanya kwenye maboma ya askari Waroma huko Masada na Yerusalemu pia yalileta hasira kisasi ya Milki ya Kiroma juu ya wananchi wao. Kabla ya kumalizika kwa 66 W.K., Lejioni ya Kumi na Mbili ya Kiroma ikiwa chini ya Sesho Gallo ilipiga miguu ikaingia Yudea na kupiga kambi nje ya Yerusalemu. Waroma walishambulia jiji kutoka pande zote hata kufukia misingi ya kaskazini ya hekalu. Kwa ghafula Gallo aliondoa askari wake na bila sababu yoyote ijulikanayo wazi akaondoka Yudea. “Kama tu angalidumu na mazingiwa hayo muda kidogo zaidi angaliteka Jiji hilo mara ile,” akaandikia Yosefo shahidi aliyeona kwa macho.
Lakini Waroma hawakumalizia hapo. Miaka minne baadaye jemadari Mroma Tito alipiga miguu kwenda Yerusalemu akiwa na malejioni manne.a Wakati huu jiji zima liliharibiwa, na Yudea ikarudishwa chini ya utawala chuma wa Roma. Yote isipokuwa Masada.
Wakiwa wamepiga moyo konde kufutilia mbali kipingamizi hiki cha mwisho, Waroma waliizungushia ngome hiyo ukuta wa mawe wenye maki makubwa na kambi nane zenye kuta za mawe. Hatimaye walijenga mapandio ya ardhi yenye kuongoza hadi juu—mwegemo uliofanyizwa na binadamu wenye kutandaa meta 197 na kuinuka meta 55! Juu yao walijenga mnara na kuweka mtambo wa kutwanga ukuta wa Masada ili waubomoe. Muda si muda jeshi la Kiroma lingepita kama mafuriko liiteke ngome hii ya mwisho ya Kiyudea!
Leo ule muundo wazi wa kambi za Kiroma, ule ukuta wa mazingiwa wenye kuzunguka, na yale mapandio makubwa yashuhudia jinsi uasi wa Kiyahudi ulivyoisha. Uchimbuzi mwingi wa kiakiolojia uliofanywa Masada ulimalizwa katika 1965. Ikieleza juu ya mapato, The New Encyclopedia Britannica (1987) yataarifu hivi: “Maelezo ya Yosefo mwanahistoria Mroma-Myahudi, ambayo mpaka wakati huo ndiyo tu yaliyokuwa chanzo chenye maelezo mengi juu ya historia ya Masada, yalikutwa kuwa sahihi mno.”
Lakini Waroma wakiwa karibu kuvunja wazipenye kuta, wanaume watumia-sime waliitikiaje hotuba ya ujiuaji ya Eleazari, mwana wa Yairi? Yosefo arekodi hivi: “Wote kabisa walizimaliza familia zao; . . . halafu, wakiisha kuchagua wanaume kumi kwa kura ili wawe wafishaji wa wale wengine, kila mmoja akajibwaga chini kando ya mke wake na watoto, na, kwa kuwarushia mikono kuwakumbatia, wakaziacha wazi koo zao kwa wale waliolazimika kutekeleza jukumu hilo la hisia chungu.b Hawa wa mwisho waliwachinja wote bila msito wowote, halafu wakafuata mtindo uo huo kwa mmoja na mwenzake, . . . lakini mwanamke mmoja mzee, akiwa pamoja na mwingine . . . wakaponyoka . . . Wahanga walikuwa mia tisa na sitini hesabu yao, kutia na wanawake na watoto.”
Kwa nini uasi wa Kiyahudi ukamalizika kwa msiba hivyo? Je! kwa njia fulani ulihusiana na maisha na kifo cha Yesu wa Nazareti?
[Maelezo ya Chini]
a Huko Masada, waakiolojia walipata mamia ya sarafu zenye miandiko ya Kiebrania zikiadhimisha uasi huo, kama vile “Kwa ajili ya uhuru wa Sayuni” na “Yerusalemu Takatifu.” Dakt. Yigael Yadin katika kitabu chake Masada aeleza hivi: “Shekeli tulizopata zawakilisha miaka yote ya uasi, kuanzia mwaka wa kwanza hadi ule mwaka wa tano wa shida, mwaka wa mwisho ambapo shekeli hiyo iliundwa, ukilingana na mwaka 70 AD ambapo Hekalu la Yerusalemu liliharibiwa.” Angalia sarafu iliyo juu.
b Kwenye mahali pamoja pa mwoteo mzuri karibu na malango ya Masada, vijipanda 11 vya vyungu vilipatikana, kila kimoja kikiwa kimeandikwa jina fupi la ubandiko la Kiebrania. Wanacho kadhaa hudokeza kwamba huenda hizo zikawa ni zile kura ambazo hurejezewa na Yosefo. Kimoja kiliandikwa “Ben Ya’ir,” kumaanisha “mwana wa Yairo.” “Mgunduo wa Yadini wa kura, kutia na moja yenye jina Ben Yairi, ni uhakikisho wa kiajabu juu ya usimulizi wa Yosefo,” ataarifu Louis Feldman katika Josephus and Modern Scholarship.
[Picha katika jalada]
Masada—Ithibati ya Kwamba Mesiya Alikuwa Amekuja?
[Picha katika ukurasa wa 4]
Sarafu ya Kiyahudi ya 67 W.K., ikitaja “Mwaka wa 2” wa ile vita pamoja na Roma
[Hisani]
Pictorial Archive (Near Eastern History)