Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 3/15 kur. 28-31
  • Masimulizi ya Matukio ya Yosefu Yenye Kuvutia

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Masimulizi ya Matukio ya Yosefu Yenye Kuvutia
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maisha Yake ya Mapema
  • Kwenda Roma na Kurudi
  • Vitabu vya Flavio Yosefu
  • Utambuzi wa Ndani ya Neno la Mungu
  • Ule Uasi Mkubwa Dhidi ya Roma
  • Baada ya Vita
  • Je, Kweli Yosefo Ndiye Aliyekiandika?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Je, Wajua?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • Kitabu Kinachotegemeka—Sehemu ya 6
    Amkeni!—2011
  • Je, Yohana Mbatizaji Alikuwa Mtu Halisi?
    Habari Zaidi
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 3/15 kur. 28-31

Masimulizi ya Matukio ya Yosefu Yenye Kuvutia

KWA muda mrefu wanafunzi wa historia wamechunguza maandishi ya Yosefu yenye kuvutia. Akiwa amezaliwa miaka minne tu baada ya kifo cha Kristo, yeye alikuwa shahidi mwenye kujionea utimizo wa unabii wa Yesu wenye kuogofya juu ya taifa la Kiyahudi la karne ya kwanza. Yosefu alikuwa kamanda wa kijeshi, mjumbe, Farisayo, na msomi.

Maandishi ya Yosefu yajaa habari nyingi yenye kunasa fikira. Hayo yaelimisha juu ya uasilia wa Biblia huku yakitoa mwongozo wa usomi kwenye hali ya mazingira na ya jiografia ya Palestina. Si ajabu kwamba wengi huona vitabu vyake kuwa nyongeza ya thamani kwenye maktaba yao!

Maisha Yake ya Mapema

Yusufu ben Matayo, au Yosefu, alizaliwa katika 37 W.K., mwaka wa kwanza wa utawala wa maliki Waroma Kaligula. Baba ya Yosefu alikuwa wa familia ya kikuhani. Yeye alidai kwamba mama yake alikuwa mzao wa kuhani mkuu Yonathani wa Hasmonae.

Akiwa tineja, Yosefu alikuwa mwanafunzi mwenye bidii wa Sheria ya Kimusa. Yeye alichanganua kwa uangalifu madhehebu matatu ya Uyuda—Mafarisayo, Masadukayo, na Waesene. Kwa kupendelea hao wa mwisho, yeye aliamua kuishi kwa miaka mitatu akiwa na mtawa wa jangwani aitwaye Bannus, yaelekea akiwa Mwesene. Akiacha hilo akiwa na umri wa miaka 19, Yosefu alirudi Yerusalemu na kujiunga na Mafarisayo.

Kwenda Roma na Kurudi

Yosefu alisafiri hadi Roma katika 64 W.K. ili kuwatetea makasisi Wayahudi ambao kiongozi Myudea Feliki alikuwa amewapeleka kwa Maliki Nero ili wahukumiwe. Akivunjikiwa meli njiani, Yosefu aliponea chupuchupu. Ni maabiria 80 tu kati ya 600 waliokuwa melini waliookolewa.

Wakati wa ziara ya Yosefu kwenda Roma, mchezaji mmoja Myahudi alimjulisha kwa mke wa Nero, malkia Popia. Yeye alikuwa na fungu muhimu katika kufanikiwa kwa mradi wake. Uzuri wa jiji lile uliacha Yosefu akiwa na kumbukumbu lenye kudumu.

Yosefu aliporudi Yudea, uasi dhidi ya Roma ulikazwa kikiki akilini mwa Wayahudi. Yeye alijaribu kuwaonyesha wananchi wenzake ubatili wa kupigana na Roma. Akishindwa kuwazuia, na yaelekea akihofia kwamba angeonwa kuwa msaliti, yeye alikubali kuteuliwa kuwa kamanda wa majeshi ya Wayahudi katika Galilaya. Yosefu alikusanya na kuwazoeza watu wake na kupata ugavi uliohitajiwa katika kujiandaa kwa ajili ya vita dhidi ya majeshi ya Roma—lakini walishindwa. Galilaya ilitwaliwa na jeshi la Vespasian. Baada ya mazingiwa ya siku 47, ngome ya Yosefu katika Jotapata ilitwaliwa.

Alipojisalimisha, Yosefu alitabiri kwa werevu kwamba karibuni Vespasian angekuwa maliki. Akiwa amefungwa jela lakini bila kuadhibiwa kwa sababu ya utabiri wake, Yosefu aliachwa huru wakati utabiri wake ulipotimia. Huo ulikuwa wakati wa maana zaidi maishani mwake. Kwa sehemu iliyobaki ya vita ile, yeye alitumikia Waroma akiwa mkalimani na mpatanishi. Akionyesha kuunga mkono Vespasian na wanae Tito na Domitiani, Yosefu aliongeza jina la familia Flavio kwa jina lake.

Vitabu vya Flavio Yosefu

Kitabu cha kale zaidi cha Yosefu chaitwa The Jewish War. Yaaminiwa kwamba aliandika simulizi hilo la mabuku saba ili kuonyesha Wayahudi picha kamili ya uweza mkuu wa Roma na kutoa kizuizi dhidi ya uasi wakati ujao. Mabuku hayo yalichunguza historia ya Wayahudi tangu kutwaliwa kwa Yerusalemu na Antiokasi Epifane (katika karne ya pili K.W.K.) hadi msukosuko wa 67 W.K. Halafu akiwa shahidi aliyejionea, Yosefu azungumzia vita iliyofikia kilele katika 73 W.K.

Kitabu kingine cha Yosefu kilikuwa The Jewish Antiquities, kikiwa historia ya Wayahudi ya mabuku 20. Kikianzia Mwanzo na uumbaji, chaendelea hadi kuzuka kwa vita na Roma. Yosefu afuata kwa ukaribu utaratibu wa masimulizi ya Biblia, akiongeza mafafanuzi ya kimapokeo na uchunguzi wa nje.

Yosefu aliandika juu ya simulizi la kibinafsi lenye kichwa sahili Life. Ndani yacho yeye ajaribu kutetea msimamo wake wa wakati wa vita na ajaribu kukinza mashtaka yaliyotolewa dhidi yake na Yusto wa Tiberio. Kitabu cha nne—mabuku mawili yenye kutetea yenye kichwa Against Apion—chatetea Wayahudi dhidi ya maoni mabaya juu yao.

Utambuzi wa Ndani ya Neno la Mungu

Hakuna shaka kwamba sehemu kubwa ya historia ya Yosefu ni sahihi. Katika kitabu chake kiitwacho Against Apion, yeye aonyesha kwamba Wayahudi hawakutia ndani kamwe vitabu vya Apokrifa kuwa sehemu ya Maandiko yaliyopuliziwa. Yeye atoa ushuhuda kwenye usahihi na upatano wa ndani wa maandishi ya kimungu. Yosefu asema: “Sisi hatuna vitabu vingi miongoni mwetu, vinavyotofautiana na kupingana, . . . bali vitabu ishirini na viwili tu [vinavyolingana na mgawanyo wetu wa kisasa wa Maandiko katika vitabu 39], vyenye rekodi ya nyakati zote zilizopita; ambavyo vinaaminiwa kwa kufaa kuwa vya kimungu.”

Katika The Jewish Antiquities, Yosefu aongeza jambo lenye kupendeza kwenye masimulizi ya Biblia. Yeye asema kwamba “Isaka alikuwa mwenye miaka ishirini na mitano” Abrahamu alipomfunga mikono na miguu ili kumtoa dhabihu. Kulingana na Yosefu, baada ya kusaidia katika ujenzi wa madhabahu, Isaka alisema kwamba “‘hakustahili kuzaliwa kwanza, iwapo akataa makusudi ya Mungu na ya baba yake’ . . . Kwa hiyo alienda mara hiyo kwenye madhabahu ili atolewe dhabihu.”

Juu ya masimulizi ya Kimaandiko ya kuondoka kwa Israeli kutoka Misri ya kale, Yosefu aongeza mambo haya madogo-madogo: “Idadi ya wale waliowafuatia ilikuwa magari ya farasi mia sita, pamoja na wapanda farasi elfu hamsini, na wenye kupiga miguu elfu mia mbili, wote wakiwa na silaha.” Yosefu pia asema kwamba “Samweli alipokuwa mwenye miaka kumi na miwili, yeye alianza kutoa unabii: na wakati mmoja alipokuwa amelala, Mungu alimwita kwa jina lake.”—Linganisha 1 Samweli 3:2-21.

Maandishi mengine ya Yosefu yalitoa utambuzi wa ndani kwa habari ya kodi, sheria, na matukio. Yeye ataja Salome kuwa ndiye mwanamke aliyecheza dansi kwenye karamu ya Herode na ndiye aliyeomba kichwa cha Yohana Mbatizaji. (Marko 6:17-26) Sehemu kubwa juu ya yale tunayojua juu ya Maherode ilirekodiwa na Yosefu. Yeye hata asema kwamba “ili kusitiri umri wake mkubwa, [Herode] alipaka nywele zake rangi nyeusi.”

Ule Uasi Mkubwa Dhidi ya Roma

Miaka 33 tu baada ya Yesu kutoa unabii wake juu ya Yerusalemu na hekalu lalo, utimizo wa unabii huo ulianza. Mafarakano ya Wayahudi yenye mabadiliko makubwa katika Yerusalemu yaliazimia kupindua kongwa la Waroma. Katika 66 W.K., habari hizo zilifanya majeshi ya Waroma yakusanywe na kutumwa chini ya gavana wa Ashuru Sestio Galo. Kusudi lao lilikuwa ni kuvunja uasi huo na kuadhibu wenye kuuanzisha. Baada ya kuleta uharibifu katika viunga vya Yerusalemu, majeshi ya Sestio yalipiga kambi kuzunguka jiji hilo lenye kuta. Wakitumia njia iitwayo testudo, Waroma waliunganisha ngao zao kwa mafanikio kama mgongo wa kasa ili wajilinde kutoka kwa adui. Akishuhudia mafanikio ya njia hiyo, Yosefu asema: “Mishale iliyotupwa ilianguka, na kuteleza bila kuwadhuru kwa vyovyote; kwa hiyo askari-jeshi hao waliushambulia ukuta, bila kuumizwa wao wenyewe, na wakatayarisha mambo yote ili wawashe moto malango ya hekalu.”

“Ndipo ikatukia,” asema Yosefu, “kwamba Sestio . . . aliwaita askari-jeshi wake kutoka mahali hapo . . . Aliondoka kwenye jiji, bila sababu yoyote.” Kulingana na ithibati, bila kukusudia kumtukuza Mwana wa Mungu, Yosefu aliandika juu ya tendo ambalo Wakristo katika Yerusalemu walikuwa wamengoja. Lilikuwa utimizo wa unabii wa Yesu Kristo! Miaka mingi mapema, Mwana wa Mungu alikuwa ameonya hivi: “Hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia. Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie. Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.” (Luka 21:20-22) Kama vile Yesu alivyoagiza, wafuasi wake waaminifu walikimbia upesi kutoka jijini, wakaendelea kukaa mbali, na wakaepushwa ubaya uliolipata baadaye.

Majeshi ya Waroma yaliporudi katika 70 W.K., matokeo yalirekodiwa kirefu na Yosefu. Mwana wa kwanza wa Vespasian, Jenerali Tito, alikuja kuutiisha Yerusalemu, pamoja na hekalu lalo tukufu. Jijini kwenyewe, mafarakano yenye kupigana yalijaribu kutwaa udhibiti. Yalitumia njia za kupita kiasi, na damu nyingi ilimwagwa. Baadhi yao “walikuwa katika masumbuko makubwa kwa sababu ya msononeko wa wao kwa wao, kiasi cha kwamba walitamani Waroma wawavamie,” wakitumaini “waondolewe taabu zao za kindani,” asema Yosefu. Yeye aita waasi hao “majangili” walioharibu mali za matajiri na kuwaua kimakusudi watu wa maana—wale walioshukiwa kuwa tayari kuridhiana na Waroma.

Kujapokuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, hali za maisha katika Yerusalemu zilishuka vibaya sana, na wafu wakabaki bila kuzikwa. Wahaini “walipigana wao kwa wao, huku wakikanyaga maiti zilizorundikana moja juu ya nyingine.” Waliwanyang’anya watu wa kawaida vitu, wakiua kimakusudi ili wapate chakula na utajiri. Vilio vya waliosononeka sana vilikuwa vyenye kuendelea.

Tito aliwahimiza Wayahudi wausalimishe mji na hivyo wajiokoe wenyewe. Yeye “alimtuma Yosefu azungumze nao katika lugha yao wenyewe; kwani aliwazia wangesikiliza usadikisho wa mwananchi mwenzao.” Lakini walimsuta Yosefu. Halafu Tito akajenga ukuta wa miti michonge kuzunguka jiji zima. (Luka 19:43) Tumaini lote la kutoroka likiwa limeondolewa, na mwendo kuzuiwa, njaa kali “iliwamaliza watu wakiwa nyumba na familia nzima-nzima.” Vita iliyoendelea iliongeza idadi ya vifo. Bila kujua kwamba anatimiza unabii wa Biblia, Tito alilitiisha Yerusalemu. Baadaye, akichunguza kuta zalo kubwa na minara yenye ngome, yeye alisema hivi kwa mshangao: “Haikuwa mwingine ila Mungu aliyewatoa Wayahudi kutoka ngome hizi.” Wayahudi zaidi ya milioni moja waliuawa.—Luka 21:5, 6, 23, 24.

Baada ya Vita

Baada ya vita, Yosefu alienda Roma. Akipata kibali cha Waflavio, yeye aliishi akiwa raia wa Roma katika jumba lililokuwa la Vespasian na akapokea malipo ya serikali pamoja na zawadi kutoka kwa Tito. Halafu Yosefu akafuatia kazi-maisha ya uandishi.

Yapendeza kuona kwamba yaonekana Yosefu alibuni neno “Theokrasi.” Kuhusu taifa la Kiyahudi, yeye aliandika hivi: “Serikali yetu . . . yaweza kuitwa Theokrasi, kwa kurejezea mamlaka na uwezo kwa Mungu.”

Yosefu hakudai kamwe kuwa Mkristo. Yeye hakuandika chini ya upulizio wa Mungu. Lakini, kuna thamani ya kihistoria yenye kuelimisha katika masimulizi ya matukio ya Yosefu yenye kuvutia.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Yosefu kwenye kuta za Yerusalemu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki