Jumuiya ya Wakristo na Ile Biashara ya Kununua na Kuuza Watumwa
WAKATI wa karne ya 19, wamishonari Wakatoliki na Waprotestanti waliungana katika kupinga kwao biashara ya kununua na kuuza watumwa. Hata hivyo, huo haukuwa umekuwa msimamo wao sikuzote. Katika karne kadhaa kabla ya hiyo, walikubali na kushiriki katika biashara ya kununua na kuuza watumwa ijapokuwa kule kuteseka kubaya sana kulikotokezwa na biashara hiyo.
Wamishonari walianza kuja kwenye pwani ya mashariki na pwani ya magharibi ya Afrika wakati njia ya biashara kupitia bahari kwa kuzunguka Rasi ya Good Hope ilipovumbuliwa katika karne ya 15. Hata hivyo, baada ya karne tatu, kazi ya mishonari katika Afrika ilikuwa karibu imefika mwisho wayo. Kulikuwako waongofu wachache Waafrika. Sababu moja ya kutofaulu huko ilikuwa kule kuhusika kwa Jumuiya ya Wakristo katika biashara ya kununua na kuuza watumwa. C. P. Groves hueleza hivi katika The Planting of Christianity in Africa:
“Ufuatiaji wenye bidii wa biashara ya kununua na kuuza watumwa uliandamana na utume wa Kikristo na haukuonwa kuwa jambo baya. Kwa kweli, misheni ilikuwa na watumwa wayo yenyewe; Jumba la watawa la Kiyesuiti katika Loanda [sasa Luanda, jiji kuu la Angola] lilipewa watumwa 12,000. Biashara ya kununua na kuuza watumwa ilipoanzishwa kati ya Angola na Brazili, askofu wa Loanda, akiwa kwenye kiti cha mawe karibu na gati, alitoa baraka zake za kiaskofu kwenye mizigo hiyo iliyokuwa ikiondoka, akiwaahidi wakati ujao wenye fanaka wakati ambapo majaribu hayo ya maisha yaliyokuwa kama dhoruba yangepita.”
Wamishonari Wayesuiti hawakutoa “upinzani wowote dhidi ya utumwa wa Watu Weusi,” ahakikisha C. R. Bokser kama alivyonukuliwa katika kitabu Africa From Early Times to 1800. Katika Luanda, kabla ya watumwa kupanda meli zilizoelekea koloni za Kihispania na Kireno, aongeza Bokser, “walipelekwa kwenye kanisa la karibu . . . na kubatizwa na padri wa parishi katika vikundi vya mia-mia kwa wakati moja.” Kisha, baada ya kunyunyizwa “maji matakatifu,” watumwa hao waliambiwa: “Tazameni nyinyi tayari ni watoto wa Mungu; mnaenda nchi ya Wahispania ambapo mtajifunza mambo ya Imani [ya Kikatoliki]. Msifikiri tena juu ya mlikotoka . . . Enendeni na nia njema.”
Bila shaka, si wamishonari wa Jumuiya ya Wakristo peke yao waliokubali biashara ya kununua na kuuza watumwa. “Mpaka nusu ya mwisho ya karne ya kumi na nane,” aeleza Geoffrey Moorhouse katika kitabu chake The Missionaries, “huo ulikuwa ndio mtazamo wa watu wengi.” Moorhouse ataja mfano wa mishonari mmoja Mprotestanti wa karne ya 18, Thomas Thompson, aliyeandika trakti yenye kichwa The African Trade for Negro Slaves Shown to Be Consistent With the Principles of Humanity and With the Laws of Revealed Religion (Biashara ya Afrika ya Kununua na Kuuza Watumwa Weusi Yaonyeshwa Kuwa Yapatana na Kanuni za Ubinadamu na Sheria za Dini Iliyofunuliwa).
Hata hivyo, kwa kuhusika kwayo Jumuiya ya Wakristo hushiriki daraka la kule kuteseka kubaya sana kulikoelekezwa kwa mamilioni ya watumwa Waafrika. “Bila kutia ndani wale watumwa waliokufa kabla ya wao kuabiri kutoka Afrika,” yataarifu The Encyclopœdia Britannica, “asilimia 12 1\2 walikufa wakati wa safari yao kuelekea West Indies; katika Jamaika asilimia 4 1\2 walikufa walipokuwa bandarini au kabla ya kuuzwa na theluthi moja zaidi katika ‘yale mazoezi waliyopewa wapya ili kuwafanya wawe watumwa wafaao.’”
Hivi karibuni Yehova Mungu atatoza hesabu Jumuiya ya Wakristo na pia namna nyinginezo za dini bandia kwa ajili ya vile vitendo vyote vibaya vya hatia ya damu ambavyo zimeachilia na hata kubariki.—Ufunuo 18:8, 24.
[Mchoro katika ukurasa wa 8]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa.)
Mchoro unaoonyesha jinsi watumwa walivyopakiwa ndani ya meli ya watumwa
[Hisani]
Schomburg Center for Research in Black Culture / The New York Public Library / Astor, Lenox and Tilden Foundations