Mandhari Kutoka Bara Lililoahidiwa
Kula Chakula —Kula Mkate
PINDI moja wakati Yesu na wanafunzi wake walipokuwa ndani ya nyumba, hawakuweza “kupata nafasi ya kula chakula” kwa sababu ya umati wa watu. (Marko 3:20, HNWW) Wakati mwingine Yesu aliingia nyumba ya Farisayo “ale chakula.” (Luka 14:1) Ni chakula cha aina gani unachofikiria?
Waisraeli wa kale huenda wakafikiria mkate kwa sababu maneno ya Kiebrania na ya Kigiriki ya “kula chakula” humaanisha kihalisi “kula mkate.” Hilo laeleweka, kwa kuwa mkate uliofanyizwa kutoka ngano au shayiri ulikuwa sehemu kuu ya chakula chao.
Watu wengi huwafikiria wazee wa ukoo Waebrania kuwa wachungaji na wanafunzi wa Yesu kuwa wavuvi. Na baadhi yao walifanya kazi hiyo, lakini si wote. Ngano ilikuwa chakula kikuu katika maisha ya wengi. Yaonekana ilikuwa hivyo nyakati nyingine kwa habari ya Isaka na Yakobo, kama tuwezavyo kuona kutokana na Mwanzo 26:12; 27:37; na 37:7. Na kwa kuwa ukulima ulikuwa ndio kazi kuu katika Galilaya wakati wa Yesu, je, baadhi ya wale waliokuja kuwa mitume wangalikuwa wakulima wa ngano?
Kuna uwezekano, kwani upandaji wa ngano ulienea sana katika Bara Lililoahidiwa, na kuna marejezeo mengi ya Kibiblia ya jambo hilo. (Kumbukumbu la Torati 8:7-9; 1 Samweli 6:13) Ni nini kilichohusika?
Baada ya mvua ya mapema ya Oktoba na Novemba kulainisha udongo, mkulima wa ngano angelima kwa plau na kisha kupanda mbegu zake. Mvua za baadaye zingesaidia mimea yake ikue na kisha, katika Aprili na Mei, iive kuwa rangi ya kahawia-dhahabu kabla ya joto la kiangazi. Uvunaji wa ngano ulijulikana sana hivi kwamba twasoma juu yao kuwa ishara ya hayo majira. (Mwanzo 30:14; Waamuzi 15:1) Je! waweza kujua ni wakati gani wa mwaka picha hiyo kwenye upande wa kushoto, ilipigwa?a Na ni majira gani wanafunzi wa Yesu walipovunja punje mbichi?—Mathayo 12:1.
Kuvuna ngano kulimaanisha kazi nyingi kwa wakulima. Wavunaji wangekata vikonyo kwa mundu wa mkono na kuvifunga miganda-miganda, kama uonavyo chini. Bila shaka, vikonyo vingine huenda visikatwe au huenda vikaanguka chini, ndiyo sababu Ruthu angeweza kuokota masazo kwa mafanikio. (Ruthu 2:2, 7, 23; Marko 4:28, 29) Baadaye miganda ya ngano ilipelekwa kwenye kiwanja cha kupuria, kama vile cha Arauna. Ni nini kilichotukia huko? Biblia hutaja “vyombo vya kupuria, na vyombo vya ng’ombe.” (2 Samweli 24:18-22; 1 Mambo ya Nyakati 21:23) Miganda ya ngano ilitapanywa mahali tambarare penye jiwe au ardhi ngumu. Fahali au mnyama mwingine angezunguka-zunguka, akikanyaga ngano. Huyo mnyama angeweza kuvuta gari la mbao la kupuria ambalo lingesaidia kuvunja-vunja vikonyo na kuiacha nafaka peke yake.—Isaya 41:15.
Kisha nafaka ilikuwa tayari kupepetwa, kulikofanywa kwa kurusha nafaka hewani kwa kolego au kwa uma, kama ionwavyo juu. (Mathayo 3:12) Mkulima angeweza kupepeta jioni wakati upepo ungepulizia mbali makapi (maganda kutoka kwa punje) na kuyapeleka kando majani makavu. Nafaka ilipokusanywa na kuchungwa kuondoa vijiwe vyovyote, ilikuwa tayari kuwekwa akibani—au kutengenezwa kuwa kile chakula chenye umaana sana, mkate.—Mathayo 6:11.
Ikiwa ungekuwa mke wa nyumbani mwenye ile kazi ngumu ya kutengeneza mkate, kila siku ungetumia kinu na mchi kutwanga nafaka kuwa unga, labda unga wa ngano usio laini. Au ungeweza kutwangwa uwe “unga safi,” kama ule ambao Sara alitumia kuwatengenezea wale malaika waliojivika miili, “keki za mviringo,” NW au ambao Waisraeli walitumia katika matoleo ya nafaka kwa Yehova. (Mwanzo 18:6; Kutoka 29:2; Mambo ya Walawi 2:1-5; Hesabu 28:12) Sara aliutia maji unga huo wa ngano na kuukanda kwa kinyunya.
Chini, waweza kuona madonge ya unga na bofulo moja bapa, iliyo nyembamba, ambayo imetandazwa tayari kupikwa. Keki za mviringo zilizo kubwa jinsi hiyo zingeweza kuokwa kwenye mawe au kwenye vikaango vya chuma, kama anavyofanya mwanamke huyu. Je! hilo linakusaidia kuona akilini kile ambacho Sara aliwafanyia wageni wake wa kimalaika na kile ambacho familia ya Loti ilifanya wakati fulani baadaye? Twasoma hivi: “[Malaika] nao wakaja, wakaingia nyumbani mwake. Akawafanyia karamu, akawapikia mikate [keki, NW] isiyochachwa, nao wakala.”—Mwanzo 19:3.
[Maelezo ya Chini]
a Linganisha na 1992 Calendar of Jehovah’s Witnesses.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Pictorial Archive (Near Eastern History) Est.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Garo Nalbandian