Maswali kutoka kwa Wasomaji
■ Ni vitu gani vinavyopasa kutumiwa viwe mifano kwenye utukuzo wa Chakula cha Bwana cha Jioni, na mifano hiyo inapasa kuonwaje (kuchukuliwaje)?
Ukumbusho wa kila mwaka wa Chakula cha Bwana cha Jioni ndio utukuzo wa pekee ambao Wakristo wanaamriwa na Maandiko waufuate. Yesu aliuanzisha usiku wa Nisani 14, mwaka wa 33 W.K., baada ya kufanya sherehe ya kuikumbuka sikukuu ya Kiyahudi ya Kupitwa. Mbele yake vilikuwako vyakula vidogo vilivyokuwa vikitumiwa katika ulaji wa sikukuu ya Kupitwa. Masimulizi ya Luka yanasema:
“[Yesu] akachukua mkate mmoja, akatoa shukrani, akauvunja, na akapa wao huo, akisema: ‘Huu maana yake ni mwili wangu ambao ni wa kusudi la kutolewa kwa ajili yenu. Endeleeni kufanya hili katika ukumbusho wa mimi.’ Pia, kile kikombe kikawa kwa, njia ile ile baada ya wao kuwa wamepata kile chakula cha jioni, yeye akisema: ‘Hiki kikombe maana yake ni lile agano jipya kwa nguvu za damu yangu, ambayo ni ya kusudi la kumwagwa itoke kwa ajili yenu.’—Luka 22:19, 20, NW.
Mungu alikuwa amewaelekeza Wayahudi watumie ‘mikate isiyotiwa chachu’ wakati wa sikukuu ya Kupitwa. (Kutoka 12:8) Basi ‘mikate’ ambayo Yesu alikuwa nayo ilikuwa isiyotiwa chachu. Ilitengenezwa kwa kutumia unga wa ngano bila chumvi yo yote wala kikolezo (kiungo) cha namna yo yote, kwa maana ilifananisha “mikate ya mateso.”—Kumbukumbu la Torati 16:3.
Leo Mashahidi wa Yehova wanatumia ‘mkate’ unaofanana na hiyo ya siku hizo. Nyakati nyingine matzos (mikate) ya Kiyahudi inanunuliwa na kutumiwa, lakini kunakuwa na uangalifu wa kununua matzos ambayo haikutengenezwa kwa kutumia vitu vya ziada, kama vitunguu, nafaka za kuchachisha pombe wala mayai. Mikate matzos iliyo tambarare, mikavu, isiyokolezwa (isiyotiwa kiungo) inafaa. Au mkate usiochachishwa unaweza kutengenezwa (kuokwa). Kiasi kidogo cha unga-dona wa nganoa (unga-ngano usiochekechwa) kinaweza kuchanganywa na maji machache. Kisha mkando ulio na umajimaji mchache unaviringishwa uwe mwembamba halafu unaokwa ukiwa katika karatasi iliyo tambarare ya kupikia (ukiwa na mafuta machache tu) mpaka mkate utakapokuwa mkavu na wenye kuvunjika vyepesi.
Namna gani ule mfano mwingine? Kufikia karne ya kwanza W.K. Wayahudi walikuwa wamekubali kutumia divai katika chakula cha sikukuu ya Kupitwa. Yesu aliutaja “ule uzao wa mti wa zabibu” uliotumiwa katika utukuzo huo. (Luka 22:18, NW) Watu wengine wanasema kwamba Yesu hakuwa akisema habari za divai bali za majimaji ya zabibu yasiyotiwa chachu. Walakini, majimaji ya zabibu yasiyotiwa chachu yasingaliweza kukaa bila kuchacha tangu mavuno ya majira ya vuli mpaka sikukuu ya Kupitwa iliyokuwa katika majira ya masika, kwa hiyo pasipo shaka Yesu aliimaanisha divai. Divai nyekundu ya zabibu ingefananisha damu ya Yesu kwa njia yenye kufaa. Kwa kuwa “damu ya thamani” ya Kristo ilikuwa kamili isihitaji kuongezewa kitu cho chote, kwenye Ukumbusho isingefaa kutumia divai iliyotiwa nguvu au iliyogeuzwa ladha kwa kuchanganywa na brandi, kama vile “sherry,” “port” na “muscatel,” au divai nyingine zinazotumiwa kujiburudisha baada ya chakula. (1 Petro 1:19) Wala isingefaa kutumia divai yenye viungo au mimea ya kuikoleza, kama vile “Vermouth” na “Dubonnet,” au divai nyingine nyingi zinazonywewa kabla ya chakula ili kumfanya mtu atake sana kula chakula. Bali, divai nyekundu isiyoongezewa utamu kama vile Chianti, Burgundy au claret inafaa, au divai nyekundu iliyotengenezwa nyumbani bila kutiwa utamu (sukari hivi), bila kutiwa kiungo (kikolezo) wala kuongezewa nguvu kwa kutumia kitu kingine.
Inawapasa wazee walio katika kundi la Mashahidi wa Yehova wapange mapema kuwe na mkate usiotiwa chachu na divai nyekundu, nao wachunguze wahakikishe kwamba vitu wanavyojipatia vinafaa kwa matumizi. Katika siku za baada ya utukuzo wa Chakula cha Bwana cha Jioni hakuna haja ya kuuona mkate na divai kuwa vitu vya pekee au vitu vilivyotakaswa, kwa maana vinaendelea tu kuwa vyakula vya kawaida. Pia, hakuna sababu ya kuihifadhi (kuiweka sana) chupa fulani yenye divai tangu mwaka huu mpaka mwingine ili itumiwe kwenye utukuzo, isipokuwa kama ni vigumu kujipatia divai nyingine inayofaa kwa matumizi.
Watu wengine wamekuwa wakijifanya kama kwamba wameshika vitu vyenye nguvu za kufanya maajabu wakati wanapopitishiwa mifano kwenye utukuzo wa Ukumbusho. Kwa mfano, watu kadha wamenyosha shingo zao wakaribishe vichwa vyao kwenye ile mifano au kuinusa. Haifai kufanya hivyo.
Wakati wa utukuzo wa Chakula cha Bwana cha Jioni, ule mkate na ile divai ni vitu vinavyofananisha mwili wa Yesu na damu yake yenye thamani kubwa. (Mathayo 26:26-28) Kwa hiyo, wakati mifano hiyo inapopitishwa, inampasa kila mtu afikirie kwa heshima kile kinachofananishwa na ule mkate na ile divai. Wale wasioshiriki kula wala kunywa wanaweza kwa wepesi tu kumpitishia aliyeketi karibu nao sahani na bilauri inayopitishwa, wakiikumbuka hasa dhabihu ya Yesu, ambayo inaweza kufunika dhambi zetu na inayotuwezesha tuwe na tazamio la kupata uzima wa milele.—1 Yohana 2:2; 1 Wakorintho 11:23-26.
[Maelezo ya Chini]
a Ni afadhali zaidi kutumia unga wa ngano, kwa maana huo ndio uliotumiwa na Wayahudi kutengeneza mikate yao isiyotiwa chachu. Lakini ikiwa ni vigumu sana kupata unga wa ngano, ‘mkate’ usiotiwa chachu uliotengenezwa kutokana na mchele, mahindi au unga wa nafaka nyingine unaweza kutumiwa.