Milki Iliyopotea Ambayo Iliwaaibisha Wahakiki wa Biblia
“Zamani historia ya milki ya Kiashuru ilikuwa habari iliyofichika zaidi katika historia ya ulimwengu.” “Yale yote yaliyojulikana juu ya Ninawi la kale yalitiwa ndani ya mitajo na unabii mbalimbali uliotawanyika katika Biblia ambao ulirejezea jiji hilo, na zile taarifa za juujuu na za sehemu-sehemu za historia ya Kiashuru katika maandishi ya Diodorus Siculus . . . na wengine.”—Cyclopædia of Biblical Literature, Mabuku 1 na 3, 1862.
MWANAHISTORIA Mgiriki Diodorus Siculus aliishi miaka 2,000 iliyopita. Alidai kwamba Ninawi lilikuwa jiji lenye pande nne; zile pande nne zilikuwa na urefu wa ujumla wa stadia (kimo cha Kiroma cha kale) 480. Huo ni mduara wa kilometa 96! Biblia hutoa masimulizi ayo hayo, ikisimulia Ninawi kuwa jiji kubwa “mwendo wa siku tatu.”—Yona 3:3.
Wahakiki wa Biblia wa karne ya 19 walikataa kuamini kwamba jiji lisilojulikana la ulimwengu wa kale lingaliweza kuwa kubwa jinsi hiyo. Walisema pia kwamba ikiwa Ninawi lilipata kuwako wakati wowote, ni lazima iwe lilikuwa sehemu ya ustaarabu wa kale uliotangulia Babuloni.
Maoni hayo yalikuwa kinyume cha Mwanzo sura 10, inayosema kwamba kitukuu wa Noa, Nimrodi, alianzisha serikali ya kwanza ya kisiasa katika mkoa wa Babeli, au Babuloni. “Akatoka katika nchi ile,” Biblia yaendelea, “akaenda mpaka Ashuru, akajenga Ninawi, na Rehoboth-Iri, na Kala; na Reseni, kati ya Ninawi na Kala, nao ni mji mkubwa.” (Mwanzo 10:8-12) Ona kwamba, andiko hilo husimulia yale majiji mapya manne ya Kiashuru kuwa ‘jiji kubwa’ moja.
Katika 1843 mwakiolojia mmoja Mfaransa, Paul-Émile Botta, aligundua mabomoko ya jumba la kifalme yaliyothibitika kuwa sehemu ya jiji la Kiashuru. Habari ya ugunduzi huo ilipofikia umma, ilisababisha msisimuko mwingi. “Kupendezwa kwa umma kuliongezeka zaidi,” aeleza Alan Millard katika kitabu chake Treasures From Bible Times, “ilipothibitishwa kwamba jumba hilo la kifalme lilikuwa la Sargon, yule mfalme wa Ashuru anayetajwa katika Isaya 20:1, ambaye kuwako kwake kulikuwa kumetiliwa shaka kwa sababu hakuwa amejulikana vingine.”
Wakati uo huo, mwakiolojia mwingine, Austen Henry Layard, alianza kuyachimba mabomoko kwenye mahali paitwapo Nimrud karibu kilometa 42 kusini-magharibi mwa Khorsabad. Mabomoko hayo yalithibitika kuwa Kala—mojawapo yale majiji manne ya Kiashuru yanayotajwa kwenye Mwanzo 10:11. Halafu, katika 1849, Layard alifukua mabomoko ya jumba kubwa mno ya kifalme kwenye mahali paitwapo Kuyunjik, kati ya Kala na Khorsabad. Jumba hilo la kifalme lilithibitika kuwa sehemu ya Ninawi. Kati ya Khorsabad na Kala kuna mabomoko ya makao mengine, kutia na rundo liitwalo Karamles. “Tukichukua marundo hayo makubwa manne ya Nimrúd [Kala], Koyunjik [Ninawi], Khorsabad, na Karamles, yakiwa kona za mraba,” akaonelea Layard, “itaonekana kwamba pande zalo nne zinalingana kiasi fulani kwa usahihi na zile stadia 480 au maili 60 za yule mwanajiografia, zinazofanyiza ule mwendo wa siku tatu wa nabii [Yona].”
Basi yaonekana, Yona alitia ndani makao hayo yote kuwa ‘jiji kubwa,’ moja akiyaita kwa jina la lile jiji linalotajwa kwanza kwenye Mwanzo 10:11, yaani, Ninawi. Ndivyo ifanywavyo leo. Kwa kielelezo, kuna tofauti kati ya lile jiji la awali la London na maeneo yalo ya mashambani, ambayo hufanyiza lile linaloitwa nyakati nyingine “London Kubwa Zaidi.”
Mfalme wa Ashuru Mwenye Majivuno
Lile jumba la kifalme huko Ninawi lilikuwa na vyumba zaidi ya 70, vikiwa na karibu kilometa 3 za kuta. Kwenye kuta hizo kulikuwa mabaki yaliyochomeka ya sanamu zilizochongwa zikiwa ukumbusho wa ushindi mbalimbali wa kijeshi na mafanikio mengine. Nyingi zayo zilikuwa zimeharibika vibaya. Hata hivyo, kuelekea mwisho wa ziara yake, Layard aligundua kichumba kimoja kilichokuwa kimehifadhiwa vizuri ajabu. Kwenye kuta zacho kulikuwa michoro iliyoonyesha kutekwa nyara kwa jiji lililozingirwa vizuri, mateka wakipelekwa kwa miguu mbele ya mfalme huyo mwenye kushambulia, aliyekuwa ameketi juu ya kiti cha utawala nje ya jiji. Juu ya mfalme huyo kuna mchoro ambao wastadi wa maandishi ya Kiashuru wanatafsiri ifuatavyo: “Senakeribu, mfalme wa ulimwengu, mfalme wa Ashuru, aliketi kwenye kiti cha utawala cha nimedu na akakagua kirasmi nyara (zilizotekwa) kutoka Lakishi (La-ki-su).”
Leo wonyesho na mchoro huo waweza kuonwa katika British Museum. Unakubaliana na tukio la kihistoria uliorekodiwa katika Biblia kwenye 2 Wafalme 18:13, 14: “Katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa. Basi Hezekia, mfalme wa Yuda, akapeleka wajumbe waende Lakishi kwa mfalme wa Ashuru, kusema, Nimekosa; uniache ukarudi kwako; cho chote utakachoweka juu yangu, nitakichukua. Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia, mfalme wa Yuda, talanta za fedha mia tatu, na talanta za dhahabu thelathini.”
Michoro mingine ilipatikana miongoni mwa mabomoko ya Ninawi ikiongeza maelezo madogo-madogo juu ya shambulio la Senakeribu la Yuda na juu ya ushuru uliolipwa na Hezekia. “Labda mojawapo mambo yenye ulinganifu wa ajabu zaidi katika uthibitisho wa kihistoria ambao umerekodiwa ni kwamba, kiasi cha hazina ya dhahabu kilichochukuliwa kutoka kwa Hezekia, talanta thelathini, chakubaliana katika masimulizi hayo mawili yasiyotegemeana hata kidogo,” akaandika Layard. Bwana Henry Rawlinson, aliyesaidia kufasiri hayo maandishi ya Kiashuru, alitangaza kwamba michoro hiyo “ilithibitisha pasipo shaka utambulisho wa kihistoria wa [Senakeribu].” Zaidi ya hayo, Layard auliza hivi katika kitabu chake Nineveh and Babylon: “Kabla ya magunduzi hayo, ni nani ambaye angaliamini yawezekana kwamba chini ya rundo la ardhi na takataka lililotia alama mahali pa Ninawi, kungepatikana historia ya vita kati ya Hezekia na Senakeribu, iliyoandikwa na Senakeribu mwenyewe wakati uleule vilipotukia, na kuthibitisha hata katika mambo madogo sana rekodi ya Kibiblia?”
Bila shaka, mambo mengine madogo-madogo ya rekodi ya Senakeribu hayakubaliani na Biblia. Kwa kielelezo, mwakiolojia Alan Millard asema hivi: “Jambo lenye kutokeza zaidi laja mwishoni mwa [rekodi ya Senakeribu]. Hezekia alimtuma mjumbe wake, na ushuru wote, kwa Senakeribu ‘baadaye, huko Ninawi’. Jeshi la Kiashuru halikuupeleka nyumbani kwa ushindi katika njia ya kawaida.” Biblia husema kwamba ushuru huo ulilipwa kabla ya mfalme wa Ashuru kurudi Ninawi. (2 Wafalme 18:15-17) Kwa nini tofauti hiyo? Na kwa nini Senakeribu hakuweza kujivuna juu ya kushinda jiji kuu la Yuda, Yerusalemu, kwa njia ile ambayo alikuwa amejivunia ushindi wake juu ya lile jiji la ngome la Yuda Lakishi? Waandishi watatu wa Biblia wanatoa jibu. Mmoja wao, aliyekuwa shahidi aliyejionea mwenyewe aliandika hivi: “Basi malaika wa BWANA [Yehova, NW] alitoka, akaua watu mia na themanini na tano elfu katika kituo cha Waashuri, na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe, hao walikuwa maiti wote pia. Basi Senakeribu, mfalme wa Ashuru akaenda zake, akarudi Ninawi, akakaa huko.”—Isaya 37:36, 37; 2 Wafalme 19:35; 2 Mambo ya Nyakati 32:21.
Katika kitabu chake Treasures From Bible Times, Millard amalizia hivi: “Hakuna sababu nzuri ya kutilia shaka ripoti hii . . . Kwa kueleweka, Senakeribu asingerekodi msiba kama huo usomwe na waandamizi wake, kwani ungempa sifa mbaya.” Badala yake, Senakeribu alijaribu kuonyesha kwamba shambulio lake juu ya Yuda lilikuwa limefanikiwa na kwamba Hezekia aliendelea kujinyenyekeza kwake, akipeleka ushuru Ninawi.
Asili ya Ashuru Yathibitishwa
Maktaba zenye makumi ya maelfu ya mabamba ya matope yaligunduliwa pia katika Ninawi. Hati hizo zinathibitisha kwamba Milki ya Kiashuru ilikuwa na mianzo upande wa kusini katika Babuloni, kama vile Mwanzo 10:11 ionyeshavyo. Kwa kutumia habari hiyo, waakiolojia walianza kukaza jitihada zao upande wa kusini zaidi. Encyclopædia Biblica yaeleza hivi: “Mabaki yote ya Waashuri hufunua asili yao ya Kibabuloni. Lugha yao na njia yao ya kuandika, fasihi yao, dini yao, na sayansi yao ilitoka kwa majirani wao wa kusini ikiwa imerekebishwa kidogo tu.”
Magunduzi kama yale yaliyo juu yamewalazimisha wahakiki wa Biblia wasawazishe maoni yao. Kwa kweli, uchunguzi wa moyo mweupe wa Biblia hufunua kwamba iliandikwa na waandishi waangalifu, wenye kufuatia haki. Aliyekuwa hakimu mkuu wa Mahakama ya Juu Zaidi ya United States, Salmon P. Chase, alisema hivi baada ya uchunguzi wake wa Biblia: “Hilo lilikuwa funzo refu, lenye uzito, na lenye kina: na kwa kutumia kanuni zilezile za uthibitisho katika habari hii ya kidini kama nifanyavyo sikuzote katika mambo ya kilimwengu, nimefikia uamuzi kwamba Biblia ni kitabu kinachozidi nguvu za kibinadamu, kwamba kimetoka kwa Mungu.”—The Book of Books: An Introduction.
Kwa kweli, Biblia ni zaidi ya historia sahihi tu. Ni Neno la Mungu lililopuliziwa, zawadi ya kuinufaisha ainabinadamu. (2 Timotheo 3:16) Uthibitisho wa hilo waweza kuonwa kwa kuchunguza jiografia ya Biblia. Hilo litachunguzwa katika toleo lifuatalo.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]
Kwa hisani ya Trustees of The British Museum
[Picha katika ukurasa wa 6, 7]
Juu: Sehemu tatu zenye mambo mengi zilizochukuliwa kutoka kwenye mchoro wa ukuta
Chini: Mchoro wa maandishi ya Kiashuru yaliyochongwa ukutani yakionyesha mazingiwa ya Lakishi
[Hisani]
(Kwa hisani ya The British Museum)
(Kutoka The Bible in the British Museum, kilichotangazwa na British Museum Press)