Misiba ya Asili-Je! Mungu Ndiye Huisababisha?
“MUNGU, umetufanyia nini?”
Hilo lilikuwa itikio lililoripotiwa la mwokokaji mmoja aliyechunguza uharibifu ulioletwa na mlipuko wa mlima wenye kufunikwa kwa theluji wa Nevado del Ruiz katika Kolombia mnamo Novemba 13, 1985. Poromoko la matope lililotokea lilizika jiji lote la Armero na kuua watu zaidi ya 20,000 katika usiku mmoja.
Yaeleweka kwamba mwokokaji aweza kuitikia hivyo. Wakiwa hoi wanapokabili kani za asili zenye kuogopesha, tangu nyakati za mapema zaidi watu wamemwona Mungu kuwa ndiye husababisha matukio hayo yenye kuleta msiba. Watu wa kale sana walitoa matoleo, hata dhabihu za kibinadamu, ili kutambikia vijimungu vyao vya bahari, anga, dunia, mlima, volkano, na vyanzo vinginevyo vya hatari. Hata leo, wengine huyaona matokeo ya matukio ya asili yenye kuleta maafa makuu kuwa ajali au tendo la Mungu.
Je! kweli Mungu ndiye husababisha misiba iletayo kuteseka kwingi sana kwa binadamu na hasara kotekote ulimwenguni? Je! yeye ndiye mwenye kulaumika? Ili kupata majibu, twahitaji kuchunguza kwa ukaribu zaidi yale yanayohusika katika misiba hiyo. Kwa kweli, twahitaji kuchunguza tena mambo fulani ya hakika yanayojulikana.
“Msiba wa Asili” Ni Nini?
Tetemeko la dunia lilipopiga Tangshan, Uchina, na kuua watu 242,000 kulingana na ripoti rasmi za Uchina, na Kimbunga Andrew kilipopiga kwa kishindo Florida Kusini na Louisiana katika United States na kusababisha uharibifu wenye kugharimu mabilioni ya dola, misiba hiyo ya asili ilikuwa habari kuu ya vyombo vya habari ulimwenguni kote. Lakini, namna gani ikiwa tetemeko hilo la dunia lingalipiga Jangwa la Gobi lisilokaliwa na watu, lililoko kilometa 1,100 kaskazini-magharibi mwa Tangshan, au namna gani ikiwa Kimbunga Andrew kingalifuata kijia tofauti na kumalizikia baharini, bila kugusa bara hata kidogo? Hayo yasingalikumbukwa hata kidogo sasa.
Basi, ni wazi kwamba tusemapo juu ya misiba ya asili, hatusemi tu juu ya kule kutukia kwa kani za asili zenye kutokeza. Kila mwaka kuna maelfu ya matetemeko ya dunia, makubwa kwa madogo, na dhoruba nyingi, tufani, vimbunga, pepo zenye nguvu nyingi, milipuko ya volkano, na matukio mengineyo yenye nguvu nyingi mno ambayo hurekodiwa yakiwa takwimu tu. Hata hivyo, matukio hayo yanakuwa misiba wakati yasababishapo uharibifu wa uhai na mali na kuvuruga njia ya maisha ya kawaida.
Yapaswa kuonwa kwamba uharibifu na hasara inayotokana nao hazilingani sikuzote na kani za asili zinazohusika. Msiba ulio mkuu zaidi si lazima uwe ni tokeo la kani za asili zenye nguvu nyingi kabisa. Kwa kielelezo, katika 1971 tetemeko la dunia lenye kiwango cha 6.6 kwenye kipimo cha Richter lilikumba San Fernando, Kalifornia, United States, na kuua watu 65. Mwaka mmoja baadaye tetemeko lenye kiwango cha 6.2 katika Managua, Nikaragua, liliua watu 5,000!
Hivyo, kwa habari ya uharibifu wenye kuongezeka wa misiba ya asili, ni lazima tuulize, Je! hali za asili zimekuwa zenye nguvu nyingi zaidi? Au visababishi vya kibinadamu vimechangia tatizo hilo?
Ni Nani Huisababisha?
Biblia humtambulisha Yehova Mungu kuwa Muumba Mtukufu wa vitu vyote, kutia na kani za asili za dunia hii. (Mwanzo 1:1; Nehemia 9:6; Waebrania 3:4; Ufunuo 4:11) Hilo halimaanishi kwamba yeye ndiye husababisha kila msogeo wa upepo au kila manyunyu ya mvua. Badala ya hivyo, ameweka sheria fulani ambazo huongoza dunia na mazingira yayo. Kwa kielelezo, kwenye Mhubiri 1:5-7, twasoma juu ya utendaji tatu kati ya utendaji mbalimbali wa msingi ambao hufanya maisha yawezekane duniani—macheo na machweo ya jua ya kila siku, mwendo wa pepo usiobadilika, na kawaida ya maji. Iwe ainabinadamu yatambua au la, mifumo hiyo ya asili, na mingine kama hiyo, inayohusisha halijoto, jiolojia (uso wa dunia), na mazingira ya dunia, imefanya kazi kwa maelfu ya miaka. Kwa kweli, mwandikaji wa Mhubiri alikuwa akielekeza fikira kwenye ile tofauti kubwa iliyo kati ya njia za uumbaji zisizobadilika na zilizo nyingi mno, na hali ya uhai wa kibinadamu isiyodumu na ya muda tu.
Yehova si Muumbaji tu wa kani za asili bali pia ana nguvu za kuzidhibiti. Kotekote katika Biblia twapata masimulizi juu ya Yehova kudhibiti au kutumia kani hizo ili kutimiza makusudi yake. Hayo yatia ndani kuyatenganisha maji ya Bahari Nyekundu katika siku ya Musa na kusimamisha jua na mwezi katika vijia vyavyo mbinguni katika wakati wa Yoshua. (Kutoka 14:21-28; Yoshua 10:12, 13) Yesu Kristo, aliye Mwana wa Mungu na Mesiya aliyeahidiwa, alionyesha pia nguvu zake juu ya kani za asili, mathalani, alipotuliza dhoruba katika Bahari ya Galilaya. (Marko 4:37-39) Masimulizi kama hayo hayaachi shaka lolote kwamba Yehova Mungu na Mwanae, Yesu Kristo, waweza kudhibiti kabisa mambo yote yanayoathiri maisha duniani.—2 Mambo ya Nyakati 20:6; Yeremia 32:17; Mathayo 19:26.
Kwa kuwa hiyo ni kweli, je, twaweza kumwona Mungu kuwa ndiye amesababisha hasara na uharibifu ulioongezeka ambao umetokana na misiba ya asili katika nyakati za karibuni? Ili kujibu swali hilo, ni lazima kwanza tuchunguze kama kuna ithibati kwamba kani za asili zimekuwa zenye nguvu nyingi zaidi kwa njia ya kutokeza hivi karibuni, hata labda kuwa zisizodhibitika.
Kwa habari hiyo, angalia yale ambayo kitabu Natural Disasters—Acts of God or Acts of Man? chasema: “Hakuna ithibati yoyote kwamba taratibu za kihalijoto ambazo huhusianishwa na ukame, mafuriko, na tufani zinabadilika. Na hakuna mwanajiolojia yeyote anayedai kwamba minyambuko ya dunia inayoshirikishwa na matetemeko ya dunia, volkano na tsunami (mawimbi ya tetemeko la dunia) yanakuwa yenye nguvu nyingi zaidi.” Vivyo hivyo kitabu Earthshock chaonelea hivi: “Miamba ya kila kontinenti ina rekodi ya matukio mengi mno ya kijiolojia makubwa kwa madogo, ambayo kila moja yayo yangalikuwa misiba yenye kuleta maafa makuu kwa ainabinadamu ikiwa yangalitukia leo—na ni jambo la hakika kisayansi kwamba matukio hayo yatatukia tena na tena katika wakati ujao.” Yaani, kwa kadiri fulani dunia na kani zayo zenye nguvu zimeendelea vilevile muda wote wa enzi zilizopita. Kwa hiyo, iwe takwimu nyinginezo zaonyesha ongezeko katika namna fulani za utendaji wa kijiolojia au mwingineo au la, dunia haijawa yenye utendaji wenye nguvu nyingi zaidi isiyodhibitika katika nyakati za karibuni.
Basi, ni nini sababu ya ongezeko katika matukio na uharibifu wa misiba ya asili ambayo sisi husoma juu yayo? Ikiwa kani za asili si zenye kulaumika, yaonekana kwamba lawama laendea wanadamu. Na, kwa kweli, wenye mamlaka wametambua kwamba utendaji mbalimbali wa kibinadamu umefanya mazingira yetu yaelekee zaidi kuwa na misiba ya asili na pia yaweze kupatwa nayo kwa urahisi. Katika mataifa yanayositawi, uhitaji wenye kuongezeka wa chakula hulazimu wakulima wapande chakula kingi kupita kiasi katika mashamba waliyo nayo au kujitwalia shamba kwa kufyeka misitu ambayo ni muhimu. Hilo huongoza kwenye mmomonyoko mbaya sana wa udongo. Idadi ya watu yenye kuongezeka huharakisha pia ukuzi wa mitaa michafu-michafu na mitaa ya hali ya chini iliyojengwa kishaghalabaghala katika maeneo yasiyo salama. Hata katika mataifa yaliyositawi zaidi, watu, kama wale mamilioni wanaoishi kando ya Ufa la San Andreas katika Kalifornia, wamejihatarisha yajapokuwa maonyo ya wazi. Katika hali za jinsi hiyo, tukio lisilo la kawaida—dhoruba, furiko, au tetemeko la dunia—litukiapo, je, tokeo lenye kuleta msiba laweza kweli kuitwa “la asili”?
Kielelezo halisi ni ile hali ya ukame katika Sahel ya Afrika. Kwa kawaida sisi hufikiria ukame kuwa ukosefu wa mvua au maji, unaoongoza kwenye njaa kali, kufa-njaa, na kifo. Lakini je! ile njaa kali sana na kufa-njaa kwingi katika eneo hilo husababishwa tu na ukosefu wa maji? Kitabu Nature on the Rampage chasema hivi: “Ithibati iliyokusanywa na mashirika ya kisayansi na yanayotoa msaada yaonyesha kwamba njaa kali ya leo haiendelei sanasana kwa sababu ya ukame wenye kuendelea muda mrefu kama vile [iendeleavyo] kwa sababu ya matumizi mabaya yenye kuendelea kwa muda mrefu ya nyenzo za bara na ya maji. . . . Hali yenye kuendelea ya Sahel kuwa jangwa ni tukio lenye kusababishwa na binadamu sana-sana.” Gazeti la habari la Afrika Kusini, The Natal Witness, laonelea hivi: “Njaa kali haihusu ukosefu wa chakula; inahusu ukosefu wa uwezo wa kupata chakula. Yaani, inahusu umaskini.”
Ayo hayo yaweza kusemwa juu ya sehemu kubwa ya uharibifu unaotokana na maafa mengineyo makuu. Uchunguzi mbalimbali umeonyesha kwamba mataifa yaliyo maskini zaidi hupatwa na viwango vya vifo vya juu zaidi sana kutokana na misiba ya asili kuliko mataifa tajiri zaidi ya ulimwengu. Kwa kielelezo, kulingana na uchunguzi mmoja, tangu 1960 hadi 1981, Japani ilikuwa na matetemeko ya dunia 43 pamoja na misiba mingineyo na watu 2,700 walikufa, hiyo ikiwa wastani wa vifo 63 kwa kila msiba. Katika kipindi icho hicho, Peru ilikuwa na misiba 31 kukiwa na vifo 91,000, au vifo 2,900 kwa kila msiba. Kwa nini tofauti hiyo? Huenda ikawa kani za asili zilisababisha msiba wa asili, lakini ni utendaji mbalimbali wa kibinadamu wa—kijamii, kiuchumi, kisiasa—ambao ni lazima uwe ndio kisababishi cha tofauti kubwa katika vifo na uharibifu wa mali uliotokea.
Ni Nini Masuluhisho?
Wanasayansi na wastadi wamejaribu kwa miaka kadhaa kubuni njia za kukabiliana na misiba ya asili. Wao hupenya ndani sana katika dunia ili kujaribu kuelewa jinsi matetemeko ya dunia na milipuko ya volkano inavyotukia. Kwa satelaiti za angani wao hutazama miendo ya halihewa ili kufuatisha vijia vya tufani na vimbunga au kutabiri mafuriko na ukame. Utafiti wote huo umewapa habari ambayo wao watumaini utawawezesha kupunguza athari za kani hizo za asili.
Je! jitihada hizo zimekuwa na matokeo mazuri? Kuhusu hatua hizo za tekinolojia ya hali ya juu, zilizo ghali, shirika moja la kuchunguza mazingira ya asili laonelea hivi: “[Hatua] hizo zina mahali pazo pafaapo. Lakini zikitumia kiasi kisichofaa cha fedha na juhudi—zikitumika zikiwa udhuru wa kupuuza hali za hatari zilizomo katika jamii fulani ambazo hufanya misiba iwe mibaya zaidi—basi zaweza kusababisha madhara zaidi kuliko mema.” Kwa kielelezo, ingawa yafaa kujua kwamba delta ya mwambao wa Bangladesh huwa na tisho la daima la kupatwa na mafuriko na mawimbi makubwa mno, ujuzi huo hauzuii mamilioni ya Wabangladeshi wasilazimike kuishi huko. Tokeo ni misiba ya mara kwa mara yenye idadi za vifo vinavyofikia jumla ya mamia ya maelfu.
Kwa wazi, habari juu ya namna mambo hutukia yaweza kufaa kufikia hatua fulani tu. Jambo jingine linalohitajiwa ni uwezo wa kupunguza misongo inayowalazimu watu kuishi katika maeneo yaliyo hatarini au kuishi katika njia zinazoharibu mazingira. Yaani, kuundwa upya kwa mfumo wa kijamii, kiuchumi, na kisiasa ambao twaishi chini yao kungehitajiwa ili kupunguza madhara yanayofanywa na matukio ya asili. Ni nani awezaye kutimiza kazi hiyo ngumu? Ni Yule tu awezaye kudhibiti hata kani zisababishazo misiba ya asili.
Matendo ya Mungu Yaliyo Mbele
Yehova Mungu hatashughulika na ishara tu bali atafikia kiini cha huzuni ya kibinadamu. Atamaliza pupa na mifumo ya kisiasa, ya kibiashara, na ya kidini yenye uonevu ambayo ‘imemtawala mwanadamu kwa kumwumiza.’ (Mhubiri 8:9, NW) Yeyote anayefahamu Biblia hatashindwa kuona kwamba kotekote katika kurasa zayo mna unabii mwingi sana unaoelekezea wakati Mungu atakapochukua hatua ya kuondolea dunia uovu na kuteseka na kurejeza paradiso ya kidunia yenye amani na uadilifu.—Zaburi 37:9-11, 29; Isaya 13:9; 65:17, 20-25; Yeremia 25:31-33; 2 Petro 3:7; Ufunuo 11:18.
Kwa kweli, hilo ndilo Yesu Kristo aliwafundisha wafuasi wake wote waombe, yaani, “Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.” (Mathayo 6:9, 10) Ufalme wa Kimesiya utaondoa na kuchukua mahali pa utawala wote wa kibinadamu, kama vile nabii Danieli alivyotabiri: “Katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.”—Danieli 2:44.
Ufalme wa Mungu utatimiza nini ambacho mataifa ya leo hayawezi kutimiza? Biblia huandaa mmweko wenye kusisimua wa yale yatakayokuja. Badala ya hali ambazo zimeonyeshwa kwenye kurasa hizi, kama vile njaa kali na umaskini, “[kutakuwa] wingi wa nafaka katika ardhi juu ya milima,” na “mti wa kondeni utazaa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, nao watakuwa salama katika nchi yao.” (Zaburi 72:16; Ezekieli 34:27) Kuhusu mazingira ya asili, Biblia hutuambia hivi: “Jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. . . . Maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani. Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi kiu itakuwa chemchemi za maji.” (Isaya 35:1, 6, 7) Na vita havitakuwapo tena.—Zaburi 46:9.
Jinsi ambavyo Yehova Mungu atakavyotimiza yote hayo, na jinsi atakavyoshughulika na kani za asili hivi kwamba hazitakuwa tena kisababishi cha madhara yoyote, Biblia haisemi. Hata hivyo, jambo la hakika ni kwamba wote waishio chini ya serikali hiyo yenye uadilifu “hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA [Yehova, NW], na watoto wao pamoja nao.”—Isaya 65:23.
Katika kurasa za gazeti hili, na pia katika vichapo vingine vya Watch Tower Society, Mashahidi wa Yehova wameonyesha mara kwa mara kwamba Ufalme wa Mungu ulisimamishwa mbinguni katika mwaka wa 1914. Chini ya mwelekezo wa Ufalme huo, ushahidi wa tufeni pote umetolewa kwa karibu miaka 80, na leo tuko ukingoni mwa “mbingu mpya na nchi [dunia, NW] mpya” zilizoahidiwa. Ainabinadamu itawekwa huru si kutoka tu katika uharibifu uletwao na misiba ya asili bali pia kutoka katika maumivu na kuteseka kote ambako kumekuwa kukikumba wanadamu kwa muda wa miaka elfu sita iliyopita. Kuhusu wakati huo yaweza kwelikweli kusemwa, “mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”—2 Petro 3:13; Ufunuo 21:4.
Lakini, namna gani sasa? Je! Mungu amekuwa akitenda kwa niaba ya wale walio katika msononeko kwa sababu ya hali za asili au nyinginezo? Kwa hakika amefanya hivyo lakini si lazima iwe kwa njia ambayo watu walio wengi huenda wakatazamia.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Utendaji mbalimbali wa kibinadamu umefanya mazingira yetu yaelekee zaidi kuwa na misiba ya asili
[Hisani]
Laif/Sipa Press
Chamussy/Sipa Press
Wesley Bocxe/Sipa Press
Jose Nicolas/Sipa Press