Je! Vita Haviepukiki?
VITA ni sehemu ya habari yenye kushusha moyo. Bila shaka zile taarifa juu ya ukatili hukuudhi. Lakini labda hizo hukufanya pia utake kujua kwa nini ni lazima silaha zitumiwe ili kusuluhisha mabishano. Je! watu hawatapata kamwe kujifunza kuishi katika amani?
Dawa kwa pigo la vita yaonekana kuwa ngumu zaidi kupatikana kuliko ponyo la UKIMWI. Katika karne ya 20, mataifa mazima-mazima yamekusanywa kwa ajili ya vita, mamilioni ya watu wametumwa vitani, na mamia ya majiji yameharibiwa kabisa. Mwisho wa mauaji hauonekani ukiwa karibu hata kidogo. Biashara yenye faida ya kununua na kuuza silaha huhakikisha kwamba majeshi ya ulimwengu—na wapiganaji wa kuvizia—yataendelea kupigana kwa njia yenye kutia hofu.
Silaha za vita zilipokuwa zenye kudhuru zaidi, idadi za waliojeruhiwa zilipanda sana. Zaidi ya nusu ya wale wanajeshi milioni 65 waliopiga vita katika Vita ya Ulimwengu 1 waliuawa au kujeruhiwa. Miaka 30 hivi baadaye, makombora mawili tu ya atomu yaliua raia Wajapani zaidi ya 150,000. Tangu Vita ya Ulimwengu 2, mapigano yamekuwa sanasana ya mahali-mahali. Hata hivyo, hayo ni yenye kudhuru sana, hasa kwa raia, ambao sasa hufanyiza asilimia 80 ya wale wanaojeruhiwa.
Jambo lililo la kinyume kabisa ni kwamba, uchinjaji huo mwingi umetokea katika enzi ambayo imeona jitihada zisizo na kifani za kuharamisha vita isiwe njia ya kusuluhisha mabishano kati ya mataifa. Ile Vita Baridi ilipoisha hivi karibuni, matumaini yalikuwa mengi kwamba utaratibu wa ulimwengu mpya wenye amani, ungetokea. Hata hivyo, amani ya duniani pote yaendelea kuwa ndoto tu kama vile imekuwa. Kwa nini?
Je! Ni Jambo la Lazima Kibiolojia?
Wanahistoria na wataalamu fulani wa hali za kibinadamu hudai kwamba vita haviepukiki—hata ni vya lazima—kwa sababu tu hivyo ni sehemu ya shindano la kimageuzi la kuendelea kuishi. Akivutwa na kufikiri huko, mchanganuzi mmoja wa kijeshi Friedrich von Bernhardi alitoa hoja katika 1914 kwamba vita hupiganwa “kwa sababu ya maendeleo ya kibiolojia, kijamii na kiadili.” Nadharia hiyo ilikuwa kwamba vita ni njia ya kuondolea mbali watu au mataifa walio dhaifu, huku walio hodari wakiendelea kuwako.
Hoja ya jinsi hiyo isingefariji hata kidogo yale mamilioni ya wajane na mayatima wa vita. Zaidi ya kuwa chukizo la kiadili, kufikiri huko hupuuza maonevu halisi ya vita ya kisasa. Bunduki mimina-risasi haiwapendelei walio hodari, na kombora huwaangamiza watu wenye nguvu pamoja na walio dhaifu.
Akipuuza masomo mazito ya vita ya ulimwengu ya kwanza, Adolf Hitler alikuwa na ndoto juu ya kuanzisha jamii ya kipekee kupitia ushindi wa kijeshi. Katika kitabu chake Mein Kampf (Shindano Langu), aliandika hivi: “Ainabinadamu imepata ukuu zaidi kupitia shindano la milele, nayo huangamia tu katika amani ya milele. . . . Ni lazima wenye nguvu zaidi watawale na wasichangamane na walio dhaifu zaidi.” Lakini, badala ya kuiinua ainabinadamu, Hitler alidhabihu mamilioni ya maisha na kuharibu kontinenti nzima.
Hata hivyo, ikiwa vita si jambo la lazima kibiolojia, ni nini huisukuma ainabinadamu kuelekea hatua ya kujiharibu yenyewe? Ni kani zipi zilazimishazo mataifa yaingie katika “mambo [hayo] ya wakatili”?a Ifuatayo ni orodha ya baadhi ya mambo ya msingi ambayo huzuia jitihada zilizo bora zaidi za wafanya-amani.
Mambo Yasababishayo Vita
Utukuzo wa taifa. Mara nyingi ukichochewa na wanasiasa na majemadari, utukuzo wa taifa ni mojayapo kani zenye nguvu zaidi katika kuendeleza vita. Vita vingi vimeanzishwa ili kulinda “masilahi ya taifa” au kutetea “heshima ya taifa.” Wakati maoni ya ukuu wa nchi yangu yashindapo, yawe yafaa au hayafai, hata shambulio la waziwazi laweza kutetewa kuwa tendo la haki ili kumzuia adui yako asizitumie silaha zake dhidi yako.
Chuki ya kikabila. Vita vingi vya kimkoa huanzishwa kisha kuchochewa na chuki za muda mrefu kati ya jamii za rangi, makabila na lugha mbalimbali. Vile vita vyenye kuhuzunisha vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi iliyokuwa Yugoslavia, katika Liberia, na katika Somalia ni vielelezo vya hivi karibuni.
Ushindani wa kiuchumi na wa kijeshi. Katika kile kipindi kilichoonekana kuwa chenye amani kabla ya Vita ya Ulimwengu 1, kwa kweli serikali za Ulaya zilijenga majeshi makubwa sana. Ujerumani na Uingereza zilihusika katika ushindani wa kujenga manowari. Kwa kuwa kila taifa kuu ambalo hatimaye lilihusika katika mauaji liliamini kwamba vita ingeongeza nguvu zalo na kuleta faida nyingi sana za kiuchumi, hali zilikuwa tayari kwa ajili ya pigano.
Uadui wa kidini. Tofauti za kidini zaweza kutokeza mchanganyiko uwezao kulipuka, hasa zinapotiwa nguvu na migawanyiko ya kirangi. Uhasama wa kidini umekuwa ndio msingi wa mapigano katika Lebanoni na Ailandi Kaskazini, pamoja na vita kati ya India na Pakistan.
Mchochezi wa vita asiyeonekana. Biblia hufunua kwamba “mungu wa dunia hii,” Shetani Ibilisi, ni mtendaji zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote. (2 Wakorintho 4:4) Akiwa amejaa hasira nyingi na akiwa na “wakati mchache tu,” yeye anavuruga hali, kutia na vita, vinavyoiharibu zaidi hali ya dunia yenye ole.—Ufunuo 12:12.
Si rahisi kuondolea mbali mambo hayo ya msingi yasababishayo vita. Zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, Plato alisema kwamba “ni wafu tu ambao wameona mwisho wa vita.” Je! kadirio lake lenye huzuni ni kweli chungu ambayo ni lazima tujifunze kukubali? Au tuna sababu ya kutumaini kwamba siku moja kutakuwa na ulimwengu usio na vita?
[Maelezo ya Chini]
a Ni Napoléon aliyefafanua vita kuwa “mambo ya wakatili.” Akiwa ametumia sehemu kubwa ya maisha yake akiwa mtu mzima katika jeshi na karibu miaka 20 akiwa kamanda mkuu zaidi wa jeshi, alijionea mwenyewe ukatili mbalimbali wa mapigano.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
Cover: John Singer Sargent’s painting Gassed (detail), Imperial War Museum, London
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Instituto Municipal de Historia, Barcelona