Je! Ushindani Ndio Ufunguo wa Kufanikiwa?
“KUSHINDA siyo mambo yote, ndilo jambo pekee.” Leo wengi huishi kupatana na maneno hayo, ambayo mara nyingi husemwa kuwa yalitajwa na kocha wa kandanda ya Amerika, Vince Lombardi. Sasa, nchi zilizokuwa za Kikomunisti hapo awali zimejiunga katika kusifu mashindano. Kuanzisha ushindani katika shughuli zazo za biashara kunasemwa kuwa ndilo jambo linalohitajiwa ili kupata utajiri. Katika Mashariki wazazi wengi huwashindanisha watoto wao dhidi ya wengine na kuwapeleka kwenye shule zinazowafundisha kipawa cha kupita mitihani ya mchujo. Wazazi wenye kushughulikia sana jambo hilo wanasadiki kwamba kuingia shule mashuhuri ndio ufunguo wa ufanisi wa wakati ujao.
Wengi huamini kwa uthabiti kwamba ushindani ndio ufunguo wa kufanikiwa. Kulingana na imani yao, wanadamu wamefanya maendeleo kwa kushindana wao kwa wao. “Kushindana ili kupata cheo cha juu zaidi ndicho chanzo cha nguvu za kampuni za Japani,” wakasema asilimia 65.9 ya wakubwa wa kampuni kuu zilizochunguzwa na Muungano wa Mashirika ya Kiuchumi ya Japani. Na yaonekana kampuni za Japani zimekuwa zikifanikiwa kwa muda fulani. Hata hivyo, je, ushindani ndio ufunguo wa kufanikiwa kwelikweli?
Je! Huthawabisha Kikweli?
Watu ambao hushindana dhidi ya wengine huonyesha mtazamo wenye ubinafsi, wa kujitanguliza. Wao hufurahi wengine wanapopatwa na hasara, wakiwazia kwamba hilo litafanya matokeo yao yawe mazuri. Wao waweza kutumia mbinu zenye kudhuru wengine kwa faida zao binafsi. Ufuatiaji huo wa kufanikiwa kupitia ushindani utaongoza kwenye nini? Yasuo, aliyejishughulisha sana katika shindano la kuwa mashuhuri katika kampuni yake, akumbuka mwendo wake wa zamani na asema hivi: “Nikiwa nimejaa roho ya ushindani na fikira za kufikia cheo cha juu zaidi, nilijilinganisha na wengine na kujihisi kuwa bora zaidi. Watu hao walipowekwa katika cheo cha juu kuliko yangu, nilikuwa nikinung’unika na kulalamika kila siku juu ya uongozi wa wafanyakazi wa kampuni hiyo. Sikuwa na marafiki wa kweli.”
Roho ya ushindani yaweza kuongoza kwenye kifo cha mapema. Jinsi gani? Gazeti la Japani Mainichi Daily News lahusianisha karoshi, au kifo kutokana na kufanya kazi nyingi mno, na mwenendo wa aina ya A. Aina ya A yasimulia namna ya mwenendo inayokabiliana na mkazo kwa kukazia mno matumizi mazuri ya wakati, ushindani, na uhasama. Wastadi wa maradhi ya moyo kutoka Amerika, Friedman na Rosenman wahusianisha mwenendo wa aina ya A na ugonjwa wa moyo. Ndiyo, roho ya ushindani yaweza kusababisha kifo.
Ushindani kazini waweza kuongoza kwenye matatizo mengine ya kimwili na ya kiakili pia. Kielelezo kimoja ni Keinosuke, aliyekuwa mwuza-bidhaa mashuhuri wa mojayapo kampuni kuu za kuuza magari katika Japani. Aliweka rekodi ya kuuza jumla ya magari 1,250. Picha yake iliwekwa fremu na kuangikwa katika chumba kilichotumiwa na baraza la wakurugenzi kwenye makao makuu ya kampuni hiyo. Ingawa alikirihi kutumia wafanyakazi wenzake kuwa njia ya kupata vyeo vya juu zaidi, kampuni hiyo ilimsukuma ashindane. Likiwa tokeo, katika mwaka mmoja alipatwa na vidonda vya tumbo na vya mbuti. Mwaka uo huo, wakubwa 15 katika kampuni alimofanyia kazi walilazwa hospitalini, na mmoja akajiua.
Nyumbani, ule mtazamo wa kujitahidi kuwa na vitu vingi vya kimwili kama majirani huwasukuma watu wafanye wonyesho wa kujivunia njia yao ya maisha katika ushindani usiokoma kamwe. (1 Yohana 2:16) Hilo hunufaisha ubiashara pekee, kutia fedha mikononi mwa wafanya-biashara wa dunia.—Linganisha Ufunuo 18:11.
Ingawa kutaka kupita wengine na roho ya ushindani yaweza kutokeza kazi ya ustadi, si ajabu kwamba Mfalme Sulemani alionelea hivi: “Tena nikafikiri amali zote, na kila kazi ya ustadi, ya kwamba inatoka katika mtu kupingana [kushindana, New World Translation] na mwenzake. Hayo nayo ni ubatili na kujilisha upepo.” (Mhubiri 4:4) Kwa hiyo twaweza kudumishaje amani ya akili ingawa tunaishi katika jamii yenye ushindani? Ili kupata jibu, acheni kwanza tuone ni wapi wazo la ushindani lilianzia.