Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 9/1 kur. 19-21
  • Jihadhari na Majivuno

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Jihadhari na Majivuno
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Matokeo Katika Mahusiano
  • Majivuno Hutokana na Udhaifu
  • “Lakini Ni Kweli!”
  • Yahitajika ili Kutimiza Mambo?
  • Mafaa ya Kuwa Mwenye Kiasi
  • Usiache Uwezo Wako Uwe Udhaifu Wako
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Kusitawisha Kiasi cha Kikristo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
  • Kiasi cha Kikristo Ni Uthibitisho wa Hekima
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1984
  • Unaweza Kudumisha Sifa ya Kiasi Unapojaribiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Funzo)—2017
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 9/1 kur. 19-21

Jihadhari na Majivuno

WATU wengi leo huona majivuno kuwa sifa njema. Ni jambo la kawaida kwa watu kujionyesha juu ya sifa zao bora, stadi zao, na juu ya mambo waliyotimiza. Watu fulani waamini kwamba ni lazima mtu ajivune ili afanikiwe. Wengine waamini kwamba majivuno huwafanya wajistahi zaidi. Gazeti Time laonelea hivi: “Sifa ya kiasi, ingawa haijapotea, imeanza kuonekana kuwa jambo la kikale.” Mwandikaji Jody Gaylin aeleza: “Kwa ubaya, kujivuna bila kuona haya . . . ndilo jambo lipendwalo zaidi. Mazungumzo pamoja na rafiki mmoja au mtu unayemfahamu huandamana na jambo jingine jipya: kujitangaza.”

Watu wanaoigwa katika mambo mbalimbali wameweka kielelezo cha majisifu. Huenda ikawa umeyasikia maneno ya bingwa wa zamani wa ndondi: “Haikutukia tu kwamba nikawa mtu mkuu zaidi ulimwenguni katika wakati huu wa historia.” Maneno ya mshiriki mmoja wa beni ya muziki iliyoitwa Beatles yajulikana sana: “Sisi ni maarufu kuliko Yesu Kristo sasa.” Ingawa watu fulani waliyaona maneno hayo kuwa yalisemwa bila makusudi mabaya, wengine waliwaona watu walioyasema kuwa watu wa kuigwa wafaao kufuatwa.

Kuenea sana kwa majivuno kwatokeza suali hili: Je, yafaa mtu ajigambe juu ya mali zake na uwezo wake? Bila shaka ni jambo la kawaida kwa mtu mmoja kujivunia matimizo yake na hata kuwaeleza marafiki wa karibu na watu wa ukoo. Lakini vipi juu ya wale wanaofuata ule msemo, “Kama una kitu, kionyeshe waziwazi”? Na zaidi, vipi juu ya wale ambao ingawa hawajivuni waziwazi, wanahakikisha kwa werevu kwamba wengine wamejua juu ya uwezo wao na matimizo yao? Je, kujitangaza hivyo kwafaa, au hata ni lazima, kama wengine wapendekezavyo?

Matokeo Katika Mahusiano

Fikiria matokeo ya majivuno ya watu wengine kwako. Kwa kielelezo, unaitikiaje kwa taarifa hizi zinazofuata?

“Vitabu ambavyo sijaandika ni bora kuliko vitabu vilivyoandikwa na wengine.”—Mtunga-vitabu aliye maarufu sana.

“Kama ningalikuwako wakati wa uumbaji, ningalitoa madokezo fulani mazuri juu ya kupangwa kuzuri zaidi kwa ulimwengu wote mzima.”—Mfalme mmoja wa enzi za kati.

“Hakuna Mungu kwa sababu, kama angekuwapo, singeamini yupo kama Yeye hangekuwa mimi.”—Mwanafalsafa wa karne ya 19.

Je, watu hao mmoja-mmoja wakuvutia kwa maelezo yao? Je, wafikiri ungefurahia kukaa pamoja nao? Yaelekea sivyo. Kwa kawaida, kujivuna—kwa uzuri au hata kwa mzaha—huwafanya wengine wawe na mikazo, waudhike, labda wakuonee wivu. Mtunga-zaburi Asafu alipatwa na matokeo hayo, naye aliungama hivi: “Naliwaonea wivu wenye kujivuna.” (Zaburi 73:3) Hakika, hakuna mmoja wetu anayetaka kufanya marafiki wetu na washiriki wetu wahisi vibaya! Wakorintho wa Kwanza 13:4 yasema hivi: “Upendo . . . hautakabari.” Upendo wa kimungu pamoja na kujali hisia za wengine kutatufanya tujiepushe na hali ya kuonyesha zile tunazoona kuwa stadi zetu na mali zetu.

Mtu anapojidhibiti na kusema bila majivuno, yeye huwafanya wengine wastarehe na kujihisi vizuri. Huo ni uwezo wenye thamani sana. Labda mkuu wa serikali Mwingereza Bwana Chesterfield alikuwa na jambo hilo akilini alipomshauri mwana wake: “Uwe mwenye hekima kuliko watu wengine ukiweza; lakini usiwaambie uko hivyo.”

Watu hawana vipawa vilevile. Jambo lililo rahisi kwa mtu mmoja huwa gumu kwa mwingine. Upendo utamfanya mtu ashughulike na wengine wasio na uwezo kama wake kwa huruma. Yaelekea kwamba yule mtu mwingine ana vipawa katika mambo mengine. Mtume Paulo alituambia: “Kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomwagia kila mtu kiasi cha imani.”—Warumi 12:3.

Majivuno Hutokana na Udhaifu

Ingawa watu fulani waweza kuepuka watu wenye kujigamba, wakijihisi kuwa wa hali ya chini, wengine huitikia kwa njia tofauti. Wao huamua kwamba watu wenye majivuno hawana usalama. Mwandikaji Frank Trippett aeleza kwa nini mtu ajitangazaye, kwa kinyume, hushusha staha yake kwa maoni ya wengine: “Kila mtu ajua moyoni mwake kwamba mara nyingi majivuno huwa wonyesho wa udhaifu fulani mbalimbali wa kusikitisha.” Kwa kuwa wengi huona waziwazi kupitia kujifanya huko, je, si jambo la hekima zaidi kuepuka kujisifu bure?

“Lakini Ni Kweli!”

Wengine hujaribu kutetea kujitukuza kwao kwa njia hiyo. Wao huhisi kwamba kwa sababu wao kwa kweli wana vipawa katika mambo fulani, kujifanya kana kwamba huna vipawa hivyo kungekuwa unafiki.

Lakini, je, majivuno yao ni ya kweli? Kujipima mwenyewe huelekea kukutegemea. Ile tuhisiyo kuwa sifa bora ndani yetu wenyewe yaweza kuwa ya kawaida kwa wengine. Jambo la kwamba mtu ahisi ni lazima ajigambe laweza hata kumaanisha kwamba kumbe yeye hata hana uwezo —wa kujisimamia mwenyewe bila kujitangaza. Biblia yakariri mwelekeo wa kibinadamu wa kujidanganya ionyapo hivi: “Anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”—1 Wakorintho 10:12.

Hata kama mtu ana kipawa kisicho cha kawaida katika jambo fulani, je, hiyo hufanya ifae kujisifu? La, kwa sababu kujisifu hutukuza wanadamu, hali vipawa vyovyote tuwezavyo kuwa navyo vimetoka kwa Mungu. Ni yeye anayepaswa kupokea utukufu. Kwa nini tusifiwe kwa kitu tulichozaliwa nacho? (1 Wakorintho 4:7) Isitoshe, kama vile tuna sifa zilizo bora, pia tuna udhaifu mbalimbali. Je, unyoofu wamaanisha kwamba tuvute fikira za wengine kwa makosa yetu na mapungufu yetu? Watu wachache tu wenye majivuno wanafikiria hivyo. Huenda ikawa kwamba Mfalme Herode Agripa 1 kwa kweli alikuwa msemaji mwenye kipawa. Lakini kukosa kwake kiasi kulitokeza kifo chake kibaya. Tukio hilo baya laonyesha jinsi majivuno yamchukizavyo Mungu, na vilevile jinsi wanadamu wengi hawayapendi.—Matendo 12:21-23.

Vipawa na sifa bora kwa kawaida huja kujulikana bila kujitangaza kusikofaa. Wengine watambuapo na kumpongeza mtu kwa sifa zake na matimizo yake, hiyo hufaa sana yule anayepongezwa. Mithali 27:2 chasema hivi kwa hekima: “Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe; mtu mgeni wala si midomo yako wewe.”

Yahitajika ili Kutimiza Mambo?

Watu fulani huhisi kwamba kujitukuza kwenye uhakika kunahitajika ili kutimiza mambo katika jamii yenye ushindani mwingi. Wao wana wasiwasi kwamba wasiposema na kutangaza uwezo wao, hawatatambuliwa na kuthaminiwa. Maelezo haya yanayotoka katika gazeti Vogue yaonyesha vema hali hiyo: “Zamani tulifundishwa kwamba kiasi ni sifa njema, sasa twajifunza kwamba unyamavu waweza kukuzuia.”

Kwa watu wanaotaka kufanya maendeleo kwa viwango vya ulimwengu huu, huenda hilo likawa hangaiko la haki. Lakini hali ya Mkristo ni tofauti. Yeye ajua kwamba Mungu hujali na kutumia uwezo mbalimbali wa watu wenyenyekevu, si watu wenye kiburi. Kwa hiyo, Mkristo hana haja ya kutumia mbinu za kujisifu. Ni kweli kwamba mtu mwenye kujitumaini kupita kiasi aweza kupata umashuhuri wa muda mfupi kwa kuwa mwenye kudai au kushurutisha mambo sana. Lakini baada ya muda yeye hufichuliwa na kunyenyekezwa, hata kuaibishwa. Ni kama vile Yesu Kristo alivyosema: “Ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”—Mathayo 23:12; Mithali 8:13; Luka 9:48.

Mafaa ya Kuwa Mwenye Kiasi

Ralph Waldo Emerson aliandika hivi: “Kila mtu ninayekutana naye ni bora zaidi kwa njia fulani. Kwa njia hiyo, najifunza kwake.” Elezo lake lapatana na onyo lenye pumzi ya kimungu la mtume Paulo kwamba Wakristo ‘wasitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.’ (Wafilipi 2:3) Maoni hayo yenye kiasi humfanya mtu awe katika hali ya kujifunza kutoka kwa wengine.

Kwa hiyo jihadhari sifa zako bora zisije zikawa udhaifu wako. Usikengeuke kutoka kwa uwezo wako mbalimbali na matimizo yako kwa maneno yenye majivuno. Ongezea maadili yako sifa ya kiasi. Kwa kweli hiyo ndiyo sifa ambayo hutukuza staha ya mtu mbele ya wengine. Hiyo husaidia mtu awe na mahusiano mazuri zaidi pamoja na wanadamu wenzake na kuleta ukubali wa Yehova Mungu.—Mika 6:8; 2 Wakorintho 10:18.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki