Je, Mungu Ameamua Tayari Yatakayotupata?
“MATATIZO mengi sana ya kuwazika tu yangeepukwa ikiwa ule usemi ambao mara nyingi hueleweka vibaya wa kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu usingetumiwa kamwe.” Huenda ukataka kujua ni kwa nini, ikiwa umetumia maneno “kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu” au umeyasikia yakitumiwa.
Kulingana na ensaiklopedia ya Kifaransa ya Katoliki Théo iliyo ya karibuni, yafaa tusiyatumie maneno “kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu.” Kitabu kingine chasema hivi: “Leo, yaonekana kwamba [wazo la] kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu si kiini tena cha majadiliano ya kitheolojia, hata kwa Waprotestanti walio wengi.”
Hata hivyo, swali juu ya kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu limesumbua watu wengi muda wote wa historia. Wazo hilo lilikuwa kiini cha ubishi uliosababisha yale Marekebisho ya Kidini na hata katika Kanisa Katoliki, lilikuwa habari ya mazungumzo makali kwa karne nyingi. Ingawa halijadiliwi sana leo, hilo lingali laendelea kuwa tatizo. Ni nani asingetaka kujua kama yatakayompata yalikuwa yameamuriwa kimbele?
Kuamuliwa Kimbele Yatakayompata Mtu—Maana ya Maneno Hayo
Maneno “kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu” humaanisha nini katika makanisa? Dictionnaire de théologie catholique huyaona kuwa “madhumuni ya kimungu ya kuongoza kwenye uhai wa milele, watu fulani waliokusudiwa kwa jina.” Kwa kawaida inafikiriwa kwamba wale waliochaguliwa, “waliokusudiwa kwa jina,” ni wale wanaorejezewa na mtume Paulo katika barua yake kwa Waroma, kwa maneno yafuatayo: “Mungu hufanya kazi kwa mema pamoja na wale wampendao, waitwao kulingana na kusudi lake. Kwa kuwa wale aliowajua kimbele aliamua kimbele pia wapatanishwe na mfano wa Mwana wake . . . Na wale alioamua kimbele yatakayowapata aliwaita pia; na wale aliowaita aliwaona pia kuwa haki; na wale aliowaona kuwa haki aliwatukuza pia.”—Warumi 8:28-30, Revised Standard Version.
Hata kabla ya kuzaliwa kwao, yadhaniwa kwamba watu fulani walichaguliwa na Mungu wakiwa na tazamio la kushiriki utukufu wa Kristo mbinguni. Hilo laongoza kwenye swali hili ambalo limejadiliwa kwa muda mrefu: Je, Mungu huchagua kulingana na mapenzi yake wale ambao yeye ataka kuokoa, au wanadamu wana hiari na daraka katika kujipatia na kudumisha upendeleo wa Mungu?
Augustino, Mwanzilishi wa Wazo la Kuamuliwa Kimbele Yatakayompata Mtu
Ingawa Baba wengine wa Kanisa walikuwa wametangulia kuandika juu ya wazo la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu, kwa ujumla Augustino (354-430 W.K.) huonwa kuwa ndiye aliyewekea makanisa ya Katoliki na Protestanti msingi wa fundisho hilo. Kulingana na Augustino, waadilifu wameamuliwa kimbele na Mungu tangu zamani za kale kupokea baraka za milele. Kwa upande ule mwingine, wasio waadilifu, ingawa hawakuamuliwa kimbele na Mungu yatakayowapata kwa maana halisi ya maneno hayo, wanapaswa kupokea adhabu inayostahili kwa ajili ya dhambi zao, hukumu ya adhabu. Elezo la Augustino liliachia wazo la hiari nafasi ndogo, hivyo likifungulia njia ubishani mwingi.
Warithi wa Augustino
Jadiliano juu ya wazo la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu na wazo la hiari lilitokea kwa ukawaida katika Enzi za Kati, nalo likafikia upeo wakati wa yale Marekebisho ya Kidini. Luther aliona wazo la mtu mmoja-mmoja kuamuliwa kimbele yatakayompata kuwa chaguo la hiari kwa upande wa Mungu, bila kuona Kwake kimbele ustahili au matendo mema ya wakati ujao ya wale waliochaguliwa. Calvin alifikia mkataa ulio tofauti sana kwa wazo lake la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu lenye sehemu mbili: Wengine wanaamuliwa kimbele kupokea wokovu wa milele, na wengine kupokea hukumu ya adhabu ya milele. Hata hivyo, Calvin pia aliona chaguo la Mungu kuwa lenye kulingana na mapenzi yake, na hata kuwa la kifumbo.
Suala la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu na lile swali linalohusiana kwa ukaribu la “neema”—neno litumiwalo na makanisa kuonyesha tendo ambalo kwalo Mungu huokoa na hutangaza watu kuwa waadilifu—lilikuwa kubwa sana hivi kwamba katika 1611 Makao Matakatifu ya Papa ya Kikatoliki yalikataza jambo lolote lisichapishwe juu ya habari hiyo bila kibali yayo. Katika Kanisa Katoliki, mafundisho ya Augustino yaliungwa mkono sana na Wafuasi Wafaransa wa Jansen wa karne ya 17 na ya 18. Wao walitetea Ukristo mgumu na ulio bora sana na hata walikuwa na wafuasi kutoka miongoni mwa jamii ya watu wa koo zilizo bora. Hata hivyo, ubishani juu ya jambo hilo haukupungua. Mfalme Louis 14 aliamuru uharibifu wa makao ya watawa ya Port-Royal, uliokuwa mwanzo wa wazo la Wafuasi wa Jansen.
Katika makanisa ya Marekebisho ya Kidini ya Kiprotestanti, mazungumzo hayo hayakuwa karibu kwisha. Pamoja na wengine hao Warekebishaji wa Kidini, waliofuata Jacobus Arminius, waliamini kwamba mwanadamu ana daraka katika wokovu wake mwenyewe. Baraza la Protestanti la Dordrecht (1618-1619) lilisuluhisha swali hilo kwa muda tu wakati lilipochagua kufuata namna halisi ya imani ya Ukalvini. Kulingana na kitabu L’Aventure de la Réforme—Le monde de Jean Calvin, katika Ujerumani ugomvi huo juu ya wazo la kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu na wazo la hiari lilitokeza kipindi kirefu cha “majaribio yasiyofanikiwa ya kupatanisha, pamoja na kutendwa vibaya, kufungwa gerezani, na kuhamishwa mbali kwa wanatheolojia.”
Wazo la Kuamuliwa Kimbele Yatakayompata Mtu au Wazo la Hiari?
Tangu mwanzo, mawazo haya mawili yenye kupingana kabisa, kuamuliwa kimbele yatakayompata mtu na hiari, yalichochea mabishano makali mengi. Kwa upande wake Augustino alikuwa hawezi kueleza kutopatana huko. Calvin pia aliona jambo hilo kuwa wonyesho wa mapenzi ya enzi kuu ya Mungu na kwa hiyo kuwa jambo lisiloelezeka.
Lakini je, ufunuo wa Biblia wa sifa na utu wa Mungu watusaidia tuelewe maswali hayo kwa wazi zaidi? Makala ifuatayo itachunguza mambo haya kwa urefu.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Calvin
Luther
Jansen
[Hisani]
Picha: Bibliothèque Nationale, Paris