Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w95 3/1 kur. 20-23
  • Maimonidi—Yule Mtu Aliyefafanua Upya Dini ya Kiyahudi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Maimonidi—Yule Mtu Aliyefafanua Upya Dini ya Kiyahudi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Maimonidi Alikuwa Nani?
  • Aliandika Nini?
  • Alifundisha Nini?
  • Dini ya Kiyahudi na Itikadi Nyinginezo Ziliathiriwaje?
  • Dini ya Kiyahudi—Jitihada ya Kutafuta Mungu Kupitia Andiko na Pokeo
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Ni Nani Astahiliye Kuitwa Rabi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Naḥmanides—Je, Alikanusa Ukristo?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Wayahudi, Wakristo, na Lile Tumaini la Kimesiya
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
w95 3/1 kur. 20-23

Maimonidi—Yule Mtu Aliyefafanua Upya Dini ya Kiyahudi

“TANGU Musa hadi Musa, hakukuwa na yeyote aliyekuwa kama Musa.” Wayahudi wengi watatambua msemo huu wa kifumbo kuwa maneno ya kumsifu Musa Ben Maimoni wa karne ya 12 aliyekuwa mwanafalsafa wa Kiyahudi, mratibu, na mfafanuzi wa Talmud na Maandiko—ambaye pia aitwa Maimonidi na Rambam.a Leo, watu wengi hawamjui Maimonidi, lakini maandishi yake yalikuwa na uvutano mkubwa sana kwa fikira za Kiyahudi, Kiislamu, na za kikanisa za siku zake. Kwa kufuatisha sheria kabisa, yeye alifafanua upya Dini ya Kiyahudi. Maimonidi alikuwa nani, na kwa nini Wayahudi wengi humwona kama “Musa wa pili”?

Maimonidi Alikuwa Nani?

Maimonidi alizaliwa Córdoba, Hispania, katika 1135. Baba yake, Maimoni, aliyemwandalia mengi ya mafundisho yake ya kidini ya awali, alikuwa msomi aliyejulikana sana aliyetoka katika familia iliyoheshimiwa ya kirabi. Waalmohadi waliposhinda Córdoba katika 1148, Wayahudi walikabili chaguo la ama kusilimu ama kutoroka. Hilo lilianzisha kipindi kirefu cha kutangatanga kwa familia ya Maimonidi. Katika 1160 waliishi Fez, Moroko, ambako alipokea masomo ya kuwa tabibu. Katika 1165 familia yake ililazimika kutorokea Palestina.

Hata hivyo, hali katika Israeli haikuwa nzuri. Jumuiya ndogo ya Kiyahudi ilikabili hatari kutokana na vikosi vya Wakrusedi wa Jumuiya ya Wakristo na vilevile vikosi vya Waislamu. Baada ya kipindi kipunguacho miezi sita katika hilo “Bara Takatifu,” Maimonidi na familia yake walipata himaya katika Fustat, Jiji la Kale la Cairo, Misri. Hapa ndipo vipawa vya Maimonidi vilipotambuliwa wazi. Katika 1177 akaja kuwa kiongozi wa jumuiya ya Wayahudi, na katika 1185 aliwekwa kuwa tabibu katika makao ya Saladin, aliyekuwa kiongozi maarufu wa Waislamu. Maimonidi aliendelea na vyeo hivyo mpaka kifo chake katika 1204. Ustadi wake wa kitiba ulijulikana sana hivi kwamba unasemwa kutoka mbali kama Uingereza, Mfalme Richard Mjasiri alijaribu kumchukua Maimonidi kuwa tabibu wake binafsi.

Aliandika Nini?

Maimonidi alikuwa mwandikaji sana. Alipokuwa akitoroka mnyanyaso wa Waislamu, akiwa mafichoni na akiwa mkimbizi, yeye alikusanya sehemu kubwa ya kitabu chake cha kwanza kikuu, Commentary on the Mishnah.b Kikiwa kimeandikwa katika Kiarabu, kinaelewesha wazi mengi ya mawazo na misemo katika Mishnah, nyakati nyingine kikikengeuka na kueleza falsafa ya Maimonidi juu ya Dini ya Kiyahudi. Katika sehemu inayofafanua masimulizi ya Sanhedrin, Maimonidi alifanyiza kanuni 13 za msingi za imani ya Kiyahudi. Dini ya Kiyahudi haijapata kufafanua kanuni rasmi za kufuatwa. Sasa, Kanuni 13 za Imani za Maimonidi zikawa kiolezo cha kuigwa cha mfululizo wa kanuni za Kiyahudi zinazofanyizwa.—Ona sanduku, ukurasa 23.

Maimonidi alitaka kufafanua mfuatano mzuri wa mambo yote, yawe ya kimwili au kiroho. Alikataa imani bila uthibitisho, akidai maelezo kwa kila kitu kwa msingi wa kile alichoona kuwa uthibitisho mzuri na wa akili. Mwelekeo huo wa asili yake ulimwongoza aandike kitabu chake kikuu—Mishneh Torah.c

Katika siku za Maimonidi Wayahudi waliona “Torati,” au “Sheria,” kuwa hazitumiki tu kwa maneno yaliyoandikwa na Musa bali zatumika vilevile kwa mafasiri yote ya kirabi juu ya Sheria katika karne zilizokuwa zimepita. Mawazo hayo yaliandikwa katika Talmud na katika maelfu ya maamuzi ya kirabi na maandishi kuhusu Talmud. Maimonidi alitambua kwamba ukubwa wenyewe tu na mvurugo wa habari hizi zote ulimfanya Myahudi wa kawaida asiweze kufanya maamuzi yaliyohusu maisha yake ya kila siku. Wengi hawakuwa katika hali ya kuweza kujifunza katika maisha yao yote fasihi yote ya kirabi, sehemu kubwa ikiandikwa katika Kiaramu kilichokuwa kigumu. Suluhisho la Maimonidi lilikuwa ni kuhariri habari hizi, akionyesha maamuzi yatumikayo, na kuzipanga upya katika mfumo mmoja ulio na utaratibu mzuri wa vitabu 14, vilivyogawanywa kulingana na mada ya habari. Alikiandika kwa ustadi katika Kiebrania chenye kueleweka vizuri.

Mishneh Torah kilikuwa kiongozi chenye kutumika sana hivi kwamba baadhi ya viongozi wa Kiyahudi waliogopa kwamba kingechukua mahali pa Talmud kabisa. Na bado, hata wapinzani walikiri usomi wa hali ya juu wa kitabu hicho. Kanuni hii iliyopangwa vizuri kwa utaratibu ilikuwa utimizo mkubwa sana, ukiupa nguvu mpya mfumo wa Dini ya Kiyahudi ambao mtu wa kawaida hangeweza kutumia wala kuelewa.

Kisha, Maimonidi alianza kuandika kitabu kingine kikubwa—The Guide for the Perplexed. Kwa sababu ya kutafsiriwa kwa vitabu vya kale vya Kigiriki hadi Kiarabu, Wayahudi wengi walikuwa wanaanza kufahamu Aristoto na wanafalsafa wengine. Wengine walishangaa, wakipata ugumu wa kupatanisha maana halisi ya misemo ya Kibiblia na falsafa. Katika The Guide for the Perplexed, Maimonidi, ambaye alivutiwa sana na Aristoto, alijaribu kueleza jambo kuu la Biblia na la Dini ya Kiyahudi kwa njia ambayo lilipatana na mawazo na akili ya kifalsafa.—Linganisha 1 Wakorintho 2:1-5, 11-16.

Kwa kuongezea vitabu hivi vikuu na maandishi mengine ya kidini, Maimonidi aliandika akiwa na mamlaka katika nyanja za tiba na astronomia. Upande mwingine wa maandishi yake mengi haupaswi kupuuzwa. Encyclopaedia Judaica yaeleza hivi: “Barua za Maimonidi zaonyesha nzi mpya ya uandikaji wa barua. Ni yeye aliye mwandikaji-barua wa kwanza wa Kiyahudi ambaye barua zake zimehifadhiwa sana. . . . Barua zake zilivutia akili na moyo wa wasomaji wazo, naye alibadili mtindo wake wa kuandika ili ziwafae.”

Alifundisha Nini?

Katika zile Kanuni 13 za Imani, Maimonidi aliandaa muhtasari wa wazi wa itikadi, baadhi yazo zikitegemea Maandiko. Hata hivyo, kanuni za saba na tisa zapinga ukuu wa imani ya Kimaandiko inayotegemea Yesu akiwa Mesiya.d Kwa kufikiria yale mafundisho ya uasi-imani ya Jumuiya ya Wakristo, kama vile Utatu, na ule unafiki wa wazi unaoonyeshwa na mmwagiko wa damu katika zile Krusedi, haishangazi kwamba Maimonidi hakusema zaidi juu ya suala la Umesiya wa Yesu.—Mathayo 7:21-23; 2 Petro 2:1, 2.

Maimonidi aandika: “Je, kwaweza kuwa kikwazo kikubwa zaidi kuliko [Ukristo]? Manabii wote walisema juu ya Mesiya akiwa mkombozi wa Israeli na mwokovu walo . . . [Kwa kutofautisha, Ukristo] ulisababisha Wayahudi wauawe kwa upanga, mabaki yao kutawanywa na kunyenyekezwa, Torati kubadilishwa, na wengi wa ulimwengu kukosea na kutumikia mungu fulani badala ya Bwana.”—Mishneh Torah, “Sheria za Wafalme na Vita Vyao,” sura ya 11.

Na bado, kwa staha yote aliyoonyeshwa, Wayahudi wengi hupendelea kumpuuza Maimonidi katika masuala fulani aliyosema waziwazi. Kwa sababu ya uvutano uliokuwa ukiendelea kuwa mkubwa wa Dini ya Kiyahudi ya kifumbo (Kabbalah), unajimu ulikuwa ukiendelea kupendwa zaidi miongoni mwa Wayahudi. Maimonidi aliandika hivi: “Yeyote anayejihusisha na unajimu na anapanga safari zake kwa kutegemea wakati uliowekwa na wale wachunguzao mbingu apaswa kuchapwa viboko . . . Mambo hayo yote ni ya uongo na udanganyifu . . . Yeyote aaminiye mambo haya . . . ni mjinga tu asiye na akili.”—Mishneh Torah, “Sheria za Ibada-Sanamu,” sura ya 11; linganisha Mambo ya Walawi 19:26; Kumbukumbu la Torati 18:9-13.

Maimonidi pia alichambua sana zoea jingine: “[Marabi] walijiwekea kiasi cha fedha cha kudai watu mmoja-mmoja na jumuiya na kufanya watu wafikiri, kwa ujinga kabisa, kwamba hilo ni takwa na lafaa . . . Hayo yote ni makosa. Hakuna hata neno moja, ama katika Torati ama katika misemo ya wahenga [wa Kitalmud], ya kuunga mkono itikadi hiyo.” (Commentary on the Mishnah, Avot 4:5) Akiwa tofauti na marabi hao, Maimonidi alifanya kazi kwa bidii ili kujitegemeza akiwa tabibu, akikataa katakata malipo kwa ajili ya utumishi wake wa kidini.—Linganisha 2 Wakorintho 2:17; 1 Wathesalonike 2:9.

Dini ya Kiyahudi na Itikadi Nyinginezo Ziliathiriwaje?

Profesa Yeshaiahu Leibowitz wa Chuo Kikuu cha Hebrew, Jerusalem, alisema: “Maimonidi ndiye mtu mwenye uvutano zaidi katika historia ya Dini ya Kiyahudi, tangu enzi za Wazee wa Ukoo na Manabii hadi enzi ya sasa.” Encyclopaedia Judaica yasema hivi: “Uvutano wa Maimonidi kwenye maendeleo ya wakati ujao ya Dini ya Kiyahudi hauwezi kukadirika. . . . C. Tchernowitz . . . hata afikia hatua ya kusema kwamba kama si Maimonidi Dini ya Kiyahudi ingekuwa imevunjika katika madhehebu na itikadi tofauti-tofauti . . . Ulikuwa ni utimizo wake mkubwa kuunganisha maoni mbalimbali.”

Kwa kupanga upya mawazo ya Kiyahudi ili kupatana na mawazo na akili yake, Maimonidi alifafanua upya Dini ya Kiyahudi. Wanachuo pamoja na umati wa watu walipata ufafanuzi huu mpya kuwa wenye kutumika na wenye kuvutia. Hata wapinzani wake hatimaye walikubali mfikio wa Maimonidi. Ingawa maandishi yake yalikusudiwa kuwaweka huru Wayahudi kutokana na uhitaji wa kutegemea maelezo mengi mno, upesi maelezo marefu yaliandikwa kuhusu vitabu vyake.

Encyclopaedia Judaica yaeleza hivi: “Maimonidi alikuwa . . . mwanafalsafa mashuhuri zaidi wa Kiyahudi wa Enzi za Kati na kitabu chake Guide of the Perplexed ndicho kitabu cha kifalsafa kilicho muhimu zaidi kilichoandikwa na Myahudi yeyote.” Ingawa kiliandikwa katika Kiarabu, The Guide for the Perplexed kilitafsiriwa katika Kiebrania Maimonidi alipokuwa angali hai na baadaye kidogo kikatafsiriwa katika Kilatini, jambo lililofanya kipatikane kotekote Ulaya. Matokeo yalikuwa kwamba mkusanyo wa kipekee wa Maimonidi wa falsafa za Aristoto pamoja na mawazo ya Kiyahudi upesi ulipenya katika fikira za Jumuiya ya Wakristo. Wasomi wa Jumuiya ya Wakristo wa enzi hiyo, kama vile Albertus Magnus na Thomas Aquinas, mara nyingi hurejezea maoni ya Maimonidi. Wasomi wa Kiislamu pia walivutiwa. Maandishi ya kifalsafa ya Maimonidi baadaye yalivutia wanafalsafa wa Kiyahudi, kama vile Baruch Spinoza, kuachana kabisa na Dini ya Kiyahudi ya kawaida.

Maimonidi aweza kuonwa kuwa mtu mwenye Mvuvumko aliyeishi kabla ya ule Mvuvumko. Kusisitiza kwake kwamba imani ipatane na kusababu kungali kanuni nzuri. Kanuni hiyo ilimfanya aseme kwa bidii dhidi ya ushirikina wa kidini. Na bado, kielelezo kibaya cha Jumuiya ya Wakristo na uvutano wa kifalsafa wa Aristoto ulimzuia asifikie maamuzi yapatanayo kabisa na kweli ya Biblia. Ingawa si wote waweza kukubali maelezo yaliyoandikwa katika kaburi la Maimonidi—“Tangu Musa hadi Musa, hakukuwa na yeyote aliye kama Musa”—ni lazima ikubaliwe kwamba yeye alifafanua upya mwendo na mfanyizo wa Dini ya Kiyahudi.

[Maelezo ya chinis]

a “Rambam” ni mfanyizo wa herufi za kwanza za Kiebrania, jina lililofanyizwa kwa herufi za kwanza za maneno “Rabi Musa Ben Maimoni.”

b Mishnah ni mkusanyo wa maelezo ya kirabi, kinachotegemea kile ambacho Wayahudi walikiona kuwa sheria ya mdomo. Kiliandikwa katika mwisho-mwisho wa karne ya pili na mapema katika karne ya tatu W.K., kikifanyiza mwanzo wa Talmud. Kwa habari zaidi ona broshua Je! Ulimwengu Usio na Vita Utakuwako Wakati Wowote? ukurasa 10, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

c Jina Mishneh Torah ni neno la Kiebrania litokalo katika Kumbukumbu la Torati 17:18, yaani, nakala, au rudio, la Sheria.

d Kwa habari zaidi kuhusu uthibitisho wa Yesu akiwa Mesiya aliyeahidiwa, ona broshua Je! Ulimwengu Usio na Vita Utakuwako Wakati Wowote? kurasa 24-30, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

[Sanduku katika ukurasa wa 23]

KANUNI 13 ZA IMANI ZA MAIMONIDIe

1. Mungu ndiye Muumba na Mtawala wa vitu vyote. Ni yeye peke yake amefanyiza, na afanyiza, na atafanyiza vitu vyote.

2. Mungu ni mmoja. Hakuna umoja wowote ambao unafanana na Wake kwa njia yoyote.

3. Mungu hana mwili. Mawazo ya maumbo ya mwili hayatumiki Kwake.

4. Mungu ni mwanzo na wa mwisho.

5. Inafaa kusali kwa Mungu peke yake. Mtu asisali kwa mtu yeyote au kitu chochote.

6. Maneno yote ya manabii ni kweli.

7. Unabii wa Musa ni kweli kabisa. Yeye alikuwa mkuu wa manabii wote, wa kabla yake na wa baada yake.

8. Torati yote ambayo sasa tunayo ndiyo ile aliyopewa Musa.

9. Torati haitabadilishwa, na hakuna nyingine itakayoletwa na Mungu.

10. Mungu ajua matendo na mawazo yote ya binadamu.

11. Mungu huthawabisha wote wanaoshika amri Zake, naye huadhibu wale wanaomkosea Yeye.

12. Mesiya atakuja.

13. Wafu watarudishwa kwenye uhai.

[Maelezo ya Chini]

e Maimonidi alifafanua kanuni hizi katika kitabu chake Commentary on the Mishnah, (Sanhedrin 10:1). Baadaye Dini ya Kiyahudi ilizichukua kuwa kanuni rasmi. Maandiko haya ya juu yamefupishwa kutoka jinsi yanavyofanana katika kitabu cha Kiyahudi cha sala.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 21]

Jewish Division / The New York Public Library / Astor, Lenox, and Tilden Foundations

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki