Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w97 4/15 kur. 19-22
  • Naḥmanides—Je, Alikanusa Ukristo?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Naḥmanides—Je, Alikanusa Ukristo?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ni Nini Kilichochochea Huo Mjadala?
  • Kwa Nini Naḥmanides Alichaguliwa?
  • Naḥmanides Dhidi ya Pablo Christiani
  • Kweli Yaweza Kupatikana Wapi?
  • Dini ya Kiyahudi—Jitihada ya Kutafuta Mungu Kupitia Andiko na Pokeo
    Jitihada ya Ainabinadamu ya Kutafuta Mungu
  • Talmud Ni Nini?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Maimonidi—Yule Mtu Aliyefafanua Upya Dini ya Kiyahudi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Je! Pengo Laweza Kuzibwa?
    Amkeni!—1992
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
w97 4/15 kur. 19-22

Naḥmanides—Je, Alikanusa Ukristo?

ENZI za Kati. Zakumbusha nini? Krusedi? Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi? Mateso? Ijapokuwa hakikuwa kipindi chenye kushirikishwa kwa kawaida na mazungumzo ya kidini ya wazi wazi, wakati huo, katika mwaka wa 1263, mojawapo ya mijadala ya kipekee zaidi ya Wayahudi na Wakristo katika historia ya Ulaya ulitokea. Nani walihusika? Ni masuala gani yaliyozushwa? Mjadala huo waweza kutusaidiaje leo kutambua dini ya kweli?

Ni Nini Kilichochochea Huo Mjadala?

Katika Enzi zote za Kati, Kanisa Katoliki ya Kiroma lilijitokeza lenyewe kuwa dini ya kweli. Hata hivyo, Wayahudi walikuwa hawajaacha kamwe dai lao la kuwa watu waliochaguliwa wa Mungu. Kushindwa kwa kanisa kusadikisha Wayahudi juu ya uhitaji wa kugeuza imani kuliongoza kwenye kuvunjika moyo na mara nyingi kwenye jeuri na mnyanyaso. Wakati wa hizo Krusedi makumi ya maelfu ya Wayahudi walichinjwa au wakachomwa mtini walipopewa chaguo kati ya ubatizo au kifo. Katika nchi nyingi kupinga watu wa Kiyahudi kulikoendeshwa na kanisa kulikuwa kumeenea.

Hata hivyo, mtazamo tofauti, ulienea katika Hispania ya Kikatoliki ya karne za 12 na 13. Wayahudi waliruhusiwa uhuru wa kidini—maadamu hawakushambulia imani ya Kikristo—na hata walipewa nyadhifa muhimu katika ua wa mfalme. Lakini baada ya karibu karne moja ya upendeleo huo, makasisi wa Dominika walichukua hatua za kupunguza uvutano wa Kiyahudi katika jamii na kugeuza Wayahudi wawe Wakatoliki. Mfalme James wa Kwanza wa Aragon alisongwa na Wadominika kupanga kuwe na mjadala rasmi, ili kuthibitisha hali duni ya dini ya Kiyahudi na uhitaji wa Wayahudi wote kugeuza imani.

Huo haukuwa mjadala wa kwanza wa Wayahudi na Wakristo. Katika mwaka wa 1240, mjadala rasmi ulifanywa Paris, Ufaransa. Kusudi lao kubwa lilikuwa kutia jaribuni Talmud, kitabu kitakatifu kwa Wayahudi. Hata hivyo, washiriki Wayahudi waliruhusiwa uhuru mdogo wa kusema. Baada ya kanisa kujulisha rasmi ushindi walo katika mjadala huo, nakala za Talmud zilichomwa kwa wingi katika nyanja za umma.

Lakini mtazamo wenye ustahimilivu zaidi wa Mfalme James wa Kwanza wa Aragon haukuruhusu kuwe na jaribu bandia kama hilo. Waking’amua hivyo, Wadominika walijaribu mfikio tofauti. Kama Hyam Maccoby alivyoeleza katika kitabu chake Judaism on Trial, waliwaalika Wayahudi kwa mjadala “wakijifanya kuwa wenye heshima na ushawishi, badala ya kuwa wenye shutumu la hadharani kama walivyofanya huko Paris.” Wadominika waliweka rasmi Pablo Christiani, Myahudi aliyegeuza imani kuwa Mkatoliki na aliyekuwa amekuwa kasisi Mdominika, awe mwakilishi wao mkuu. Kwa kutumia ujuzi wa Pablo Christiani juu ya maandishi ya Talmud na ya kirabi, Wadominika walihisi uhakika wa kwamba wangeweza kuthibitisha kesi yao.

Kwa Nini Naḥmanides Alichaguliwa?

Ni mtu mmoja tu katika Hispania aliyefikia kiwango cha kiroho kuweza kuwakilisha Wayahudi katika huo mjadala—Moses ben Naḥman, au Naḥmanides.a Naḥmanides aliyezaliwa kama mwaka wa 1194 katika jiji la Gerona, alikuwa amejitambulisha mwenyewe kuwa msomi wa Kibiblia na Talmud katika utineja wake. Kufikia umri wa miaka 30, alikuwa ameandika maelezo juu ya sehemu kubwa ya Talmud, na upesi baadaye alikuwa msemaji mkubwa katika kuamua ubishi juu ya maandishi ya Maimonides yaliyotisha kugawanya jamii ya Wayahudi.b Naḥmanides anafikiriwa kuwa msomi wa mambo ya Kiyahudi na ya Talmud aliye mkuu zaidi katika kizazi chake na labda ni wa pili kwa Maimonides tu katika uvutano wake juu ya Dini ya Kiyahudi katika kipindi hicho.

Naḥmanides alikuwa na uvutano mkubwa juu ya jamii ya Kiyahudi katika Catalonia, na hata Mfalme James wa Kwanza alishauriana naye juu ya mambo ya Serikali. Uwezo wake wa kufikiri kwa makini ulistahiwa na Myahudi na Asiye Myahudi kwa kiwango kilekile. Wadominika waling’amua kwamba ili kuaibisha Wayahudi kwa kufanikiwa, yeye, akiwa rabi wao mkuu zaidi, angepaswa kuwa ndiye wa kufanya mjadala.

Naḥmanides hakutaka kukubali huo mjadala, kwa kung’amua kwamba Wadominika hawakunuia kuwa wasio na upendeleo. Alikuwa ajibu maswali lakini hangeweza kuuliza swali lolote. Hata hivyo, alikubali ombi la mfalme, akiuliza kwamba apewe ruhusa kusema kwa uhuru katika kuitikia kwake. Mfalme James wa Kwanza alikubali jambo hilo. Huko kukubaliwa kusema kwa uhuru wa kadiri fulani kulikuwa hakujatokea hapo mbele na hakungetokea tena katika Enzi zote za Kati, kukiwa uthibitisho dhahiri kwamba huyo mfalme alimstahi sana Naḥmanides. Naḥmanides bado alikuwa na wasiwasi. Ikiwa angefikiriwa kuwa mwenye kupinga sana katika huo mjadala, kungekuwa matokeo yenye kuleta msiba kwake na kwa jamii ya Wayahudi. Jeuri ingeweza kutokea wakati wowote.

Naḥmanides Dhidi ya Pablo Christiani

Kikao kikuu cha majadiliano kilikuwa jumba la mfalme katika Barcelona. Vikao vinne vilifanywa—Julai 20, 23, 26, na 27, 1263. Mfalme alisimamia binafsi kila kikao, kilichohudhuriwa pia na wadhamu mbalimbali wa Kanisa na Serikali, na vilevile Wayahudi wa jamii ya eneo hilo.

Kanisa lilikuwa na uhakika juu ya matokeo ya huo mjadala. Katika simulizi lao rasmi, Wadominika walitaarifu kwamba kusudi la huo mjadala lilikuwa ‘si ili kwamba imani ibishaniwe kana kwamba ilikuwa jambo la kutilia shaka, bali kuharibu makosa ya Wayahudi na kuondosha imani yenye uhakika ya Wayahudi wengi.’

Ijapokuwa alikuwa na umri wa karibu miaka 70, Naḥmanides alionyesha uwezo wake wa kufikiri wenye ufahamu kwa kutafuta kuyafanya hayo mazungumzo yawe juu ya mambo ya msingi tu. Alianza kwa kusema hivi: “Mabishano ya [wakati uliopita] kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi yalihusisha pande nyingi za desturi za kidini ambazo kanuni ya msingi ya imani haizitegemei. Hata hivyo, katika ua huu wa mfalme, napenda kujadili tu juu ya mambo ambayo juu yayo ubishi wote wategemea.” Ndipo ilikubaliwa kwamba mambo ya kujadiliwa yahusu tu kama Mesiya alikuwa amekuja, na kama alikuwa Mungu au mwanadamu, na kama ni Wayahudi au Wakristo walio na sheria ya kweli.

Katika bishano lake la ufunguzi, Pablo Christiani alijulisha wazi kwamba angethibitisha kutoka kwa Talmud kwamba Mesiya alikuwa tayari amekuja. Naḥmanides alijibu vikali kwamba ikiwa hilo lilikuwa kweli, kwa nini marabi waliokubali Talmud hawakukubali Yesu? Badala ya kukazia mabishano yake kusababu kwa Kimaandiko kuliko wazi, Christiani alirejezea tena na tena mafungu ya maneno ya kirabi yasiyo dhahiri ili kuthibitisha mabishano yake. Hatua kwa hatua Naḥmanides alikanusha hayo kwa kuonyesha kwamba yalikuwa yakinukuliwa nje ya muktadha. Lilikuwa jambo la akili kwamba Naḥmanides angeweza kujipatia mwenyewe sifa ya kuwa hodari zaidi katika kujadili maandishi hayo ambayo alikuwa ametoa maisha yake yote kujifunza. Hata Christiani aliporejezea Andiko, kubishana kwake kulikazia mambo yaliyokanushika kwa urahisi.

Ijapokuwa alikubaliwa kujibu maswali tu, Naḥmanides aliweza kutoa mabishano yenye nguvu yaliyoonyesha ni kwa nini msimamo wa Kanisa Katoliki ulikuwa usiokubalika kwa Wayahudi na watu wengine wenye kusababu. Kwa habari ya fundisho la Utatu, alijulisha wazi hivi: “Akili ya Myahudi yeyote au mtu yeyote haitamruhusu kuamini kwamba Muumba wa mbingu na dunia . . . angeweza kuzaliwa na mwanamke Myahudi . . . na baadaye apeanwe kwa adui zake, ambao . . . walimwua.” Naḥmanides alisema kwa usahihi hivi: “Mnachoamini—na ndicho msingi wa imani yenu—hakiwezi kukubalika na akili yenye busara.”

Akikazia kutopatana ambako hadi leo hii kumezuia Wayahudi wengi hata kuwazia uwezekano wa Yesu kuwa ndiye Mesiya, Naḥmanides alitilia mkazo hatia ya damu yenye kupita kiasi ya kanisa. Alisema hivi: “Nabii ataarifu kwamba katika wakati wa Mesiya, . . . watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe. Kutoka siku za huyo Mnazareti hadi sasa, ulimwengu mzima umejaa jeuri na wizi wa kutumia nguvu. [Kwa hakika], Wakristo humwaga damu nyingi zaidi kuliko yale mataifa mengine yote, na wao pia huishi maisha yasiyo ya adili. Lingekuwa jambo gumu kama nini kwako, bwana wangu mfalme, na hawa waheshimiwa wako kama hawangejifunza . . . vita tena kamwe!”—Isaya 2:4.

Baada ya kipindi cha nne, mfalme alisimamisha huo mjadala. Alimwambia Naḥmanides hivi: “Sijapata kuona kamwe mtu aliye na makosa akijadili vizuri kama vile ulivyofanya.” Kwa utimizo wa ahadi yake, yenye kumhakikishia Naḥmanides uhuru wa kusema na kinga, Mfalme James wa Kwanza, wa Aragon alimrudisha nyumbani, pamoja na zawadi ya dinari 300. Kwa kuombwa na askofu wa Gerona, Naḥmanides alifanya rekodi iliyoandikwa ya huo mjadala.

Huku akitangaza ushindi wa kukata maneno, Wadominika bila shaka walikasirika. Baadaye walimshtaki Naḥmanides kuwa alisema makufuru dhidi ya kanisa wakitumia maandishi yake juu ya huo mjadala kuwa ithibati. Kwa kutotosheka na kutendewa kwa upendeleo kwa Naḥmanides na mfalme, Wadominika walikata rufani kwa Papa Clement wa Nne. Ajapokuwa na umri uzidio miaka 70, Naḥmanides alifukuzwa Hispania.c

Kweli Yaweza Kupatikana Wapi?

Je, bishano la upande wowote ule lilisaidia kutambulisha dini ya kweli? Ingawa kila upande ulikazia makosa ya upande ule mwingine, hakuna upande uliotokeza ujumbe wa kweli ulio dhahiri. Kile Naḥmanides alikanusha kwa ustadi hivyo si Ukristo wa kweli bali, badala ya hivyo, alikanusha mafundisho yaliyotungwa na wanadamu, kama vile lile fundisho la Utatu, lililobuniwa na Jumuiya ya Wakristo katika karne za baada ya Yesu. Tabia isiyo ya adili na umwagikaji wa damu usiozuiwa wa Jumuiya ya Wakristo, mambo ambayo Naḥmanides alikazia kwa ujasiri hivyo, pia ni mambo ya historia iliyorekodiwa yasiyoweza kubishaniwa.

Si vigumu kufahamu ni kwa nini, chini ya hali hizo, Naḥmanides na Wayahudi wengine walikosa kuvutiwa na mabishano yaliyopendelea Ukristo. Kwa kuongezea, mabishano ya Pablo Christiani yalitegemea si kusababu kuliko wazi kutoka kwa Maandiko ya Kiebrania, bali maandishi ya kirabi yaliyotumiwa vibaya.

Kihalisi, Naḥmanides hakukanusha Ukristo wa kweli. Kufikia wakati wake nuru ya kweli ya mafundisho ya Yesu na ithibati za Umesiya wake zilikuwa zimekuwa zisizo dhahiri kwa kuwakilishwa isivyo kweli. Kutokea kwa mafundisho kama hayo ya uasi-imani kwa hakika kulitabiriwa na Yesu na mitume.—Mathayo 7:21-23; 13:24-30, 37-43; 1 Timotheo 4:1-3; 2 Petro 2:1, 2.

Hata hivyo, dini ya kweli inatambulika kwa wazi leo. Yesu alisema hivi kuhusu wafuasi wake wa kweli: “Kwa matunda yao mtawatambua. . . . Hivyohivyo kila mti mwema hutokeza matunda bora, lakini kila mti uliooza hutokeza matunda yasiyofaa kitu.” (Mathayo 7:16, 17) Tunakualika kufanya utambuzi huo. Acha Mashahidi wa Yehova wakusaidie kufanya uchunguzi usiopendelea wa ithibati za Kimaandiko. Hivyo, utajifunza maana ya kweli ya ahadi za Mungu zinazohusiana na Mesiya na utawala wake.

[Maelezo ya Chini]

a Wayahudi wengi humrejezea Naḥmanides kuwa “Ramban,” mfanyizo wa herufi za kwanza za Kiebrania uliofanyizwa kwa herufi za kwanza za maneno “Rabbi Moses Ben Naḥman.”

b Ona makala “Maimonides—Yule Mtu Aliyefafanua Upya Dini ya Kiyahudi” katika Mnara wa Mlinzi la Machi 1, 1995, ukurasa wa 20-23.

c Katika 1267, Naḥmanides aliwasili nchi iitwayo sasa Israeli. Miaka yake ya mwisho ilijawa na mambo yaliyotimizwa. Aliimarisha tena kuwapo kwa Wayahudi na kitovu cha kujifunza katika Jerusalem. Alimaliza pia maelezo juu ya Torati, vitabu vitano vya kwanza vya Biblia, na akawa kiongozi wa kiroho wa jamii ya Kiyahudi katika mwambao wa kaskazini mwa Acre, alipofia katika 1270.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Naḥmanides alijadili kesi yake Barcelona

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

Vielezi kwenye ukurasa wa 19-20: Vilitokezwa upya kutokana na Illustrirte Pracht - Bibel/Heilige Schrift des Alten und Neuen Testaments, nach der deutschen Uebersetzung D. Martin Luther’s

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki