Talmud Ni Nini?
“Bila shaka Talmud ni mojawapo ya kazi za kifasihi ambayo ni yenye kutokeza zaidi.” —The Universal Jewish Encyclopedia.
“[Talmud ni] mojawapo ya utimizo mkubwa wa kiakili wa jamii ya kibinadamu, hati yenye kuhitaji umakini sana, iliyo muhimu sana na ngumu sana kueleweka hivi kwamba, imewashughulisha watu wenye akili zilizo bora zaidi kwa milenia moja na nusu.”—Jacob Neusner, msomi na mtungaji-vitabu Myahudi.
“Talmud ni nguzo kuu [ya Dini ya Kiyahudi] inayotegemeza muundo wote wa kiroho na wa kiakili wa maisha ya Kiyahudi.”—Adin Steinsaltz, msomi na rabi wa Talmud.
BILA shaka Talmud imekuwa na uvutano mkubwa juu ya Wayahudi kwa karne nyingi. Hata hivyo, tofauti na sifa ambazo zimetajwa hapo juu, Talmud imevunjiwa sifa na kuitwa “fasihi isiyoeleweka na yenye kutatanisha.” Imeshutumiwa kuwa kazi yenye kufuru ya Ibilisi. Kwa agizo la papa, ilichujwa tena na tena, ikatwaliwa, na hata zilizo nyingi zaidi zikachomwa katika nyanja za umma za Ulaya.
Ni kazi gani hiyo ambayo imechochea ubishi mwingi hivyo? Ni nini kifanyacho Talmud iwe ya pekee miongoni mwa maandishi ya Kiyahudi? Kwa nini iliandikwa? Nayo imekuwaje na athari kama hiyo juu ya Dini ya Kiyahudi? Je, ina maana yoyote kwa ulimwengu usio wa Kiyahudi?
Wakati wa miaka 150 baada ya kuharibiwa kwa hekalu huko Yerusalemu katika mwaka wa 70 W.K., vyuo vya marabi wenye hekima kotekote Israeli walitafuta kwa hima kupata msingi mpya wa kudumisha mazoea ya Kiyahudi. Walizijadili na kuziunganisha sehemu mbalimbali za sheria yao ya mdomo. Wakijenga juu ya msingi huo, waliweka mipaka na matakwa mapya kuhusu Dini ya Kiyahudi, wakitoa mwelekezo juu ya utakatifu wa maisha ya kila siku bila hekalu. Muundo huo mpya wa kiroho ulionyeshwa katika Mishnah (mkusanyo wa mapokeo ya Kiyahudi), iliyotungwa na Judah ha-Nasi kufikia mwanzoni mwa karne ya tatu W.K.a
Hiyo Mishnah ilikuwa kamili, bila kuhitaji kujitetea kuwa halali kwa msingi wa marejezo ya Biblia. Njia yake ya kujadili na hata mtindo wa Kiebrania chake, ulikuwa wa pekee, tofauti na ule wa maandishi ya Biblia. Maamuzi ya marabi yaliyonukuliwa katika Mishnah yangeathiri maisha ya kila siku ya Wayahudi kila mahali. Kwa kweli, Jacob Neusner aeleza hivi: “Mishnah iliandalia Israeli katiba. . . . Ilihitaji watu wakubaliane nayo na waishi kulingana na sheria zake.”
Lakini namna gani ikiwa wengine walishuku kama mamlaka ya hao watu wenye hekima ambao walinukuliwa katika Mishnah, yalikuwa sawa na Maandiko yaliyofunuliwa? Marabi wangelazimika kuonyesha kwamba, mafundisho ya Tannaim (walimu wa sheria ya mdomo) yapatikanayo katika Mishnah, yalipatana kikamilifu na Maandiko ya Kiebrania. Ufafanuzi zaidi ukawa jambo la lazima. Walihisi uhitaji wa kueleza na kutetea uhalali wa Mishnah na kuthibitisha kwamba ilitokana na Sheria aliyopewa Musa katika Sinai. Hao marabi walilazimika kuthibitisha kwamba sheria ya mdomo na iliyoandikwa, ina roho moja na kusudi moja. Basi badala ya kuwa ndiyo kauli ya mwisho juu ya Dini ya Kiyahudi, Mishnah ilipata kuwa msingi mpya wa mazungumzo na mjadala wa kidini.
Kufanyizwa kwa Talmud
Marabi waliokubali mwito huo mpya walijulikana kuwa Amoraim—“wafasiri,” au “waelezaji,” wa Mishnah. Kila chuo kilitegemea rabi mmoja mashuhuri. Wasomi na wanafunzi wachache walifanya mijadala mwaka wote. Lakini vipindi vilivyokuwa vya maana zaidi vilifanywa mara mbili kwa mwaka, wakati wa miezi ya Adari na Eluli, wakati ambapo kazi ya ukulima haikuwa nyingi, na watu mamia au hata maelfu zaidi wangehudhuria.
Adin Steinsaltz aeleza hivi: “Mkuu wa chuo alisimamia mijadala hiyo, akiwa amekalia kiti au mikeka ya pekee. Katika safu za mbele kuelekeana naye, paliketi wasomi, kutia na washiriki au wanafunzi wake wenye kutokeza, na wasomi wengineo wote waliketi nyuma yao. . . . Utaratibu wa kuketi ulitegemea mpangilio wa vyeo uliofanywa kwa uangalifu [kulingana na umaana wake].” Sehemu fulani ya Mishnah ingekaririwa. Kisha sehemu hiyo ingelinganishwa na habari nyingine yenye kufanana nayo au ya ziada ambayo ilikusanywa na Tannaim, lakini isiyotiwa katika Mishnah. Utaratibu wa kuchanganua ungeanza. Maswali yalizushwa, na vipingamizi kuchanganuliwa ili kupata upatano wa ndani kati ya mafundisho hayo. Maandishi ya kuthibitisha kutoka katika Maandiko ya Kiebrania yalitafutwa ili kuunga mkono mafundisho ya kirabi.
Ijapokuwa mijadala hiyo ilipangwa vizuri, ilikuwa mikali, nyakati nyingine ikiwa yenye fujo. Mwenye hekima mmoja aliyenukuliwa katika Talmud, alisema juu ya maneno yaliyoruka kama “cheche za moto” kutoka vinywani mwa marabi wakati wa mjadala. (Hullin 137b, Talmud ya Babilonia) Steinsaltz asema hivi kuhusu jinsi mjadala ulivyofanywa: “Mkuu wa chuo, au mwenye hekima aliyekuwa akitoa hotuba, angetoa fasiri yake juu ya matatizo. Mara nyingi, wasomi waliomsikiliza wangemshambulia kwa maswali yaliyotegemea vyanzo vingine, maoni ya waelezaji wengine, au mikataa yao wenyewe ya kiakili. Nyakati nyingine mjadala ulikuwa mfupi na uliohusu tu jibu dhahiri na lenye kuthibitisha kwa swali mahususi. Katika visa vingine, wasomi wengine wangetoa utatuzi-badala mbalimbali, na mjadala wa kiwango kikubwa ungefuatia.” Wahudhuriaji wote walikuwa huru kushiriki. Masuala yaliyobainishwa kwenye vipindi hivyo yangewasilishwa kwa vyuo vingine ili wasomi wengine wayapitie.
Hata hivyo, vipindi hivyo havikuwa tu vya mijadala ya kisheria isiyo na mwisho. Mambo ya kisheria yanayohusu sheria na kanuni za maisha ya kidini ya Kiyahudi huitwa Halakah. Neno hilo latokana na neno la msingi la Kiebrania “-enda” na huonyesha ‘jinsi mtu apaswavyo kujiendesha.’ Mambo mengine yote—masimulizi juu ya marabi na watu katika Biblia, semi zenye hekima, dhana za itikadi na falsafa—huitwa Haggadah, kutokana na neno la msingi la Kiebrania “kuambia.” Maneno Halakah na Haggadah yalichanganywa wakati wa mjadala wa kirabi.
Katika kitabu chake kiitwacho The World of the Talmud, Morris Adler aeleza hivi: “Mwalimu mwenye akili angekatisha bishano la kisheria lililo refu na gumu kwa habari isiyolemea sana na yenye kujenga zaidi. . . . Hivyo, twaona hekaya na historia, sayansi na elimu ya mila na desturi za wakati huo, ufafanuzi na wasifu wa Biblia, hotuba na theolojia zikiwa zimechanganywa kuwa kile ambacho, kwa mtu asiyejua jinsi vyuo vilivyofanya mambo, kingeonekana kuwa mchanganyiko wa data ambayo haijapangwa.” Kwa wasomi katika hivyo vyuo, kuacha kote huko kwa kitambo mambo yaliyokuwa yakijadiliwa kulikuwa na kusudi fulani na kulihusiana na hoja iliyokuwa ikijadiliwa. Halakah na Haggadah yalikuwa mawe ya kujengea jengo jipya lililokuwa likijengwa katika vyuo vya marabi.
Kufanyizwa kwa Talmud Mbili
Hatimaye, kitovu kikuu cha kirabi huko Palestina, kilihamishwa hadi Tiberiasi. Vyuo vingine vya maana vilianzishwa katika Sepphoris, Kaisaria, na Lida. Lakini hali ya kiuchumi iliyokuwa ikidhoofika, misuko-suko ya daima ya kisiasa, na hatimaye mkazo na mnyanyaso kutoka kwa Ukristo wenye kuasi imani ulitokeza kuhama kwa kiwango kikubwa hadi kwenye kitovu kingine chenye idadi kubwa ya Wayahudi, kilichokuwa Mashariki—Babilonia.
Kwa karne nyingi, wanafunzi walikuwa wametoka kwa wingi huko Babilonia kwenda Palestina ili kujifunza chini ya marabi wakubwa kwenye vyuo. Mmoja wa wanafunzi hao alikuwa Abba ben Ibo, ambaye pia aliitwa Abba Arika—Abba yule mrefu—lakini baadaye alijulikana tu kuwa Rab. Alirudi Babilonia wapata mwaka wa 219 W.K., baada ya kujifunza chini ya Judah ha-Nasi, na kurudi huko kulitia alama wakati wa badiliko la maana kuhusu umuhimu wa kiroho wa jumuiya ya Wayahudi wa Babilonia. Rab alianzisha chuo fulani katika Sura, eneo lililokuwa na Wayahudi wengi lakini wasomi wachache. Sifa yake iliwavuta wanafunzi wa kawaida 1,200 kwenye chuo chake, kukiwa na maelfu zaidi waliohudhuria wakati wa miezi ya Wayahudi ya Adari na Eluli. Samuel, mtu mashuhuri aliyeishi wakati mmoja na Rab, alianzisha chuo katika Nehardea. Vyuo vingine vya muhimu vilianzishwa katika Pumbeditha na Mehoza.
Sasa hakukuwa na uhitaji wa kusafiri hadi Palestina, kwa kuwa mtu angeweza kujifunza chini ya wasomi wakuu katika Babilonia. Kufanyizwa kwa Mishnah ikiwa maandishi yaliyochanganywa na mengine kulitayarisha njia ya kuwa na vyuo vya Babilonia vilivyojitegemea kabisa. Ijapokuwa mitindo na njia tofauti za kujifunza sasa zilisitawi katika Palestina na Babilonia, kuwasiliana mara nyingi na kubadilishana walimu kulihifadhi muungano wa vyuo hivyo.
Mwishoni mwa karne ya nne na mwanzoni mwa karne ya tano W.K., hali ilipata kuwa ngumu hasa kwa Wayahudi waliokuwa katika Palestina. Vizuizi vingi mno na mnyanyaso chini ya mamlaka iliyokuwa ikiibuka ya Jumuiya ya Wakristo yenye kuasi imani lilitokeza kuchukuliwa kwa hatua ya mwisho ya kubatilisha Sanhedrini na wadhifa wa Nasi (mwanzilishi), wapata mwaka wa 425 W.K. Kwa hiyo Wafasiri wa Palestina walianza kuunganisha pamoja mihtasari ya mijadala ya vyuo kuwa kazi yenye upatano ili wahakikishe kuhifadhiwa kwake. Kazi hiyo iliyotungwa kwa haraka mwishoni mwa karne ya nne W.K., ilipata kujulikana kuwa Talmud ya Palestina.b
Huku vyuo vilivyokuwa Palestina vikipungua, Wafasiri wa Babilonia walikuwa wakifikia upeo wa uwezo wao mbalimbali. Abaye na Raba waliendeleza mjadala tata na wenye hila uliopata kuwa bishano ambalo baadaye, lilipata kuwa kigezo cha mchanganuo wa Talmud. Kisha, Ashi, mkuu wa chuo katika Sura (371-427 W.K.), akaanza kukusanya na kuhariri mihtasari ya mijadala. Kulingana na Steinsaltz, alifanya hivyo “akiogopa kwamba, habari nyingi sana za mdomo zilizokosa mpango, zilikuwa hatarini mwa kutoweka kabisa.”
Habari hiyo nyingi mno haingeweza kupangwa na mwanamume mmoja au hata kizazi kimoja. Kipindi cha Wafasiri katika Babilonia kiliisha katika karne ya tano W.K., lakini kazi ya mwisho ya kuhariri Talmud ya Babilonia iliendelezwa hadi karne ya sita W.K. na kikundi kilichoitwa Saboraim, neno la Kiaramu linalomaanisha “waelezaji,” au “wenye maoni.” Wahariri hao wa mwisho waliunda na kuandika mamia ya mihtasari mbalimbali na kuifanya Talmud ya Babilonia iliyo kamili, wakiipa mtindo na muundo wa maandishi ulioifanya kuwa tofauti na maandishi mengine yote ya Kiyahudi.
Talmud Ilitimiza Nini?
Marabi wa Talmud walikusudia kuthibitisha kwamba Mishnah na Maandiko ya Kiebrania yalikuwa na chanzo kilekile. Kwa nini? Jacob Neusner aeleza hivi: “Suala lililotajwa wazi lilikuwa yale Mishnah iliyotimiza. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, mamlaka ya mwenye hekima mwenyewe ndiyo iliyohusika.” Ili kuimarisha mamlaka hiyo, kila mstari wa Mishnah, nyakati nyingine kila neno, lilichunguzwa, likapingwa, likaelezwa, na kupatanishwa katika mtindo fulani. Neusner asema kwamba kwa njia hiyo, marabi “waligeuza lengo la Mishnah.” Ingawa Mishnah yenyewe ilitungwa ikiwa kazi iliyo kamili, sasa ilikuwa imegawanyika. Wakati hayo yalipofanyika, Mishnah ilitungwa na kufanyizwa upya.
Kitabu hicho kipya—Talmud—kilitimiza kusudi la marabi. Walitoa sheria juu ya kuchanganua, na kwa hiyo kikafundisha watu kufikiri kama marabi. Marabi waliamini kwamba njia yao ya kujifunza na kuchanganua, ilidhihirisha akili ya Mungu. Kule kujifunza Talmud kwenyewe kukawa ndilo lengo, namna ya ibada—utumizi wa akili wakidhani kwamba walikuwa wakimwiga Mungu. Kwa karne nyingi baadaye, Talmud yenyewe ingechanganuliwa kwa njia hiyohiyo. Matokeo yakiwa nini? Mwanahistoria Cecil Roth aandika hivi: “Talmud . . . iliwapa [Wayahudi] sifa yenye kuonekana iliyowatofautisha na watu wengine, na vilevile nguvu yao yenye kutokeza ya ukinzani na ya ushikamano. Njia yake ya kujadili mambo na kusababu, ilinoa akili zao, na kuwapa . . . umakini wa kiakili. . . . Talmud ilimpa Myahudi wa Enzi za Kati aliyenyanyaswa, ulimwengu mwingine ambamo angeweza kutorokea . . . Ilimpa nchi ya kuzaliwa ambayo angeweza kubeba nchi yake ilipopotea.”
Kwa kuwafundisha wengine kufikiri kwa marabi, bila shaka Talmud imekuwa na nguvu. Lakini swali kwa wote—Wayahudi na wasio Wayahudi—ni hili, Je, kwa kweli Talmud hudhihirisha akili ya Mungu?—1 Wakorintho 2:11-16.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi kuhusu kusitawi na yaliyomo katika Mishnah, ona makala “Ile Mishnah na Sheria ya Mungu kwa Musa” katika Mnara wa Mlinzi la Novemba 15, 1997.
b Talmud ya Palestina yajulikana sana kuwa Talmud ya Yerusalemu. Hata hivyo, neno hilo limetumiwa kimakosa, kwa kuwa Wayahudi hawakuruhusiwa kuingia Yerusalemu wakati wa kipindi cha Wafasiri.
[Sanduku katika ukurasa wa 31]
Zile Talmud Mbili—Je, Zalinganaje?
Neno la Kiebrania “Talmud” humaanisha “kuchunguza” au “kujifunza.” Wafasiri wa Palestina na wa Babilonia walikuwa wamekusudia kuichunguza, au kuichanganua, Mishnah. Talmud zote mbili (ya Palestina na ya Babilonia) hufanya hivyo, lakini zalinganaje? Jacob Neusner aandika hivi: “Talmud ya kwanza huchanganua uthibitisho, ya pili huchunguza kauli; ya kwanza hubaki katika mambo yaliyochunguzwa, ile ya pili haifanyi hivyo kabisa.”
Uhariri wenye umakini na mkamilifu zaidi wa Talmud ya Babilonia, uliifanya iwe kubwa zaidi na pia, yenye kina na yenye kupenya zaidi katika mtindo wake wa wazo na mchanganuo. Neno “Talmud” litajwapo, kwa kawaida humaanisha Talmud ya Babilonia. Hiyo ndiyo Talmud ambayo imechunguzwa na kuelezwa zaidi katika karne zote. Kwa maoni ya Neusner, Talmud ya Palestina “iliandikwa na mtu mwenye uhodari,” nayo Talmud ya Babilonia “iliandikwa na mtu mwenye kipaji.”