Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 1/15 kur. 25-27
  • Sheria ya Mdomo—Kwa Nini Iliandikwa?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sheria ya Mdomo—Kwa Nini Iliandikwa?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mapokeo Yalitoka Wapi?
  • “Ni Nani Aliyekupa Wewe Mamlaka Hii?”
  • Sheria Matatani—Utatuzi Mpya
  • Kwa Nini Sheria ya Mdomo Iandikwe?
  • Ile Mishnah na Sheria ya Mungu kwa Musa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Biblia—Je! Imepuliziwa na Mungu?
    Je! Ulimwengu Usio na Vita Utakuwako Wakati Wowote?
  • Sheria ya Kabla ya Kristo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Uadilifu Si kwa Mapokeo ya Mdomo
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 1/15 kur. 25-27

Sheria ya Mdomo—Kwa Nini Iliandikwa?

KWA nini Wayahudi wa karne ya kwanza walishindwa kumkubali Yesu kuwa Mesiya? Shahidi mmoja wa kujionea aripoti: “Baada ya [Yesu] kwenda ndani ya hekalu, makuhani wakuu na wanaume wazee wa watu wakamjia alipokuwa akifundisha nao wakasema: ‘Ni kwa mamlaka gani wewe wafanya mambo haya? Na ni nani aliyekupa wewe mamlaka hii?’” (Mathayo 21:23) Kwa maoni yao, Mweza Yote alikuwa amelipa taifa la Wayahudi Torati (Sheria), nayo iliwapa wanaume fulani mamlaka yenye kupewa na Mungu. Je, Yesu alikuwa na mamlaka hayo?

Yesu aliistahi sana Torati na pia wale ambao Torati hiyo iliwapa mamlaka ya kweli. (Mathayo 5:17-20; Luka 5:14; 17:14) Lakini mara nyingi alishutumu wale waliokiuka amri za Mungu. (Mathayo 15:3-9; 23:2-28) Wanaume hao walifuata mapokeo yaliyokuja kuitwa sheria ya mdomo. Yesu alikataa mamlaka ya sheria hiyo. Nao wengi wakakataa kuwa yeye ndiye Mesiya. Waliamini kwamba mtu aliyeunga mkono mapokeo ya wale waliokuwa mamlakani, ndiye tu angeweza kuungwa mkono na Mungu.

Hiyo sheria ya mdomo ilitoka wapi? Wayahudi walikujaje kuiona kuwa yenye mamlaka sawa na ya Sheria iliyorekodiwa katika Maandiko? Na ikiwa ilikusudiwa kuwa mapokeo ya mdomo, kwa nini iliandikwa hatimaye?

Mapokeo Yalitoka Wapi?

Waisraeli waliingia katika uhusiano wa agano pamoja na Yehova Mungu kwenye Mlima Sinai mwaka wa 1513 K.W.K. Kupitia Musa, walipokea sheria za agano hilo. (Kutoka 24:3) Kufuata kanuni hizo kungewawezesha ‘kutakasa nafsi zao kwa kuwa Yehova Mungu wao alikuwa mtakatifu.’ (Mambo ya Walawi 11:44) Chini ya agano la Sheria, ibada ya Yehova ilihusisha dhabihu zilizotolewa na makuhani waliochaguliwa. Kungekuwa na mahali muhimu pa ibada—hatimaye kwenye hekalu katika Yerusalemu.—Kumbukumbu la Torati 12:5-7; 2 Mambo ya Nyakati 6:4-6.

Sheria ya Kimusa iliandaa utaratibu wa jumla wa jinsi ambavyo Israeli likiwa taifa lingemwabudu Yehova. Hata hivyo, habari fulani ndogondogo hazikutajwa waziwazi. Kwa mfano, Sheria ilikataza kufanya kazi siku ya Sabato, lakini haikutofautisha kabisa baina ya kazi na shughuli nyinginezo.—Kutoka 20:10.

Kama Yehova angeliona kuwa ilifaa kufanya hivyo, angeliweza kuandaa kanuni zenye kuonyesha mambo madogo-madogo ambayo yangelitia ndani kila swali lenye kuwazika. Lakini alikuwa amewaumba wanadamu wakiwa na dhamiri, naye aliwaruhusu kuwa na uwezo wa kuchukua hatua ya kwanza ya kumtumikia wakiwa na kadiri fulani ya uhuru ambao uliwezekana ndani ya mfumo wa sheria zake. Sheria iliagiza kesi za kihukumu zishughulikiwe na makuhani, Walawi, na waamuzi. (Kumbukumbu la Torati 17:8-11) Kesi zilipoongezeka, vielelezo fulani viliwekwa, na yaelekea baadhi yavyo vilipitishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Njia za kushughulikia wajibu mbalimbali kwenye hekalu la Yehova zilipitishwa kutoka baba hadi mwana. Kadiri taifa la Israeli lilivyoendelea kuweko, ndivyo mapokeo yalivyozidi kuongezeka.

Hata hivyo, sehemu muhimu zaidi ya ibada ya Israeli iliendelea kuwa Sheria iliyoandikwa ambayo Musa alipewa. Andiko la Kutoka 24:3, 4 lasema: “Musa akaenda akawaambia watu maneno yote ya BWANA, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena BWANA tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya BWANA.” (Italiki ni zetu.) Ilikuwa ni kwa kupatana na sheria hizi zilizoandikwa kwamba Mungu alifanya agano na Waisraeli. (Kutoka 34:27) Kwa kweli, Maandiko hayataji popote pale juu ya kuweko kwa sheria ya mdomo.

“Ni Nani Aliyekupa Wewe Mamlaka Hii?”

Kwa wazi, Sheria ya Kimusa iliwapa makuhani, wazao wa Aroni, mamlaka ya msingi ya kidini na ufundishaji. (Mambo ya Walawi 10:8-11; Kumbukumbu la Torati 24:8; 2 Mambo ya Nyakati 26:16-20; Malaki 2:7) Hata hivyo, kwa karne kadhaa zilizofuata, baadhi ya makuhani hao walikosa uaminifu, wakawa wafisadi. (1 Samweli 2:12-17, 22-29; Yeremia 5:31; Malaki 2:8, 9) Katika enzi ya kutawaliwa na Wagiriki, makuhani wengi waliridhiana kuhusiana na masuala ya kidini. Katika karne ya pili K.W.K., Mafarisayo—kikundi kipya ndani ya Dini ya Kiyahudi ambacho hakikuuamini ukuhani—kilianza kutokeza mapokeo ambayo kwake mtu wa kawaida angejiona kuwa mtakatifu sawa tu na kuhani. Mapokeo hayo yaliwavutia wengi, lakini yalikuwa mambo yasiyokubalika yaliyoongezwa kwenye Sheria.—Kumbukumbu la Torati 4:2; 12:32 (13:1 katika tafsiri za Kiyahudi).

Mafarisayo walikuja kuwa wasomi wapya wa Sheria, wakifanya kazi ambayo walihisi makuhani hawakuwa wakifanya. Kwa kuwa Sheria ya Kimusa haikuwaruhusu kuwa na mamlaka hayo, walitokeza njia mpya za kufasiri Maandiko kupitia vidokezi visivyoeleweka na njia nyinginezo zilizoonekana kuunga mkono maoni yao.a Wakiwa watunzaji na vilevile waendelezaji wakuu wa mapokeo haya, walitokeza msingi mpya wa mamlaka katika Israeli. Kufikia karne ya kwanza W.K., Mafarisayo walikuwa na nguvu nyingi katika Dini ya Kiyahudi.

Walipokusanya mapokeo ya mdomo yaliyokuwepo na kutafuta vidokezi vya Kimaandiko ili waanzishe mapokeo zaidi, yaliyokuwa yao wenyewe, Mafarisayo waliona uhitaji wa kuzidisha mamlaka ya utendaji wao. Dhana mpya kuhusu chanzo cha mapokeo haya ilianzishwa. Marabi walianza kufundisha hivi: “Musa aliipokea Torati katika Sinai, akaipitisha kwa Yoshua, Yoshua akaipitisha kwa wazee, nao wazee wakaipitisha kwa manabii. Nao manabii wakaipitisha kwa wanaume wa kusanyiko kubwa.”—Avot 1:1, Mishnah.

Kwa kusema, “Musa aliipokea Torati,” marabi hawakuwa wakirejezea sheria zilizoandikwa tu, bali pia mapokeo yao yote. Walidai kwamba Mungu alimpa Musa mapokeo hayo—yaliyobuniwa na kuendelezwa na wanadamu—huko Sinai. Nao walifundisha kwamba Mungu hakuwaruhusu wanadamu wafasili Torati, lakini alikuwa amefasili kwa maneno kile ambacho Sheria iliyoandikwa haikutaja. Kulingana nao, Musa alipitisha hiyo sheria ya mdomo kwa vizazi vingi na si kwa makuhani, bali kwa viongozi wengine. Mafarisayo wenyewe walidai kuwa warithi wa asili wa mamlaka hiyo iliyopitishwa kwa kufuatana bila “kuwepo na pengo.”

Sheria Matatani—Utatuzi Mpya

Yesu, ambaye mamlaka aliyopewa na Mungu ilitiliwa shaka na viongozi wa kidini wa Kiyahudi, alikuwa ametabiri juu ya kuharibiwa kwa hekalu. (Mathayo 23:37–24:2) Baada ya Waroma kuharibu hekalu mwaka wa 70 W.K., matakwa ya Sheria ya Kimusa yaliyohusisha dhabihu na utumishi wa kikuhani, hayangeweza tena kutimizwa. Mungu alikuwa ameanzisha agano jipya kwa msingi wa dhabihu ya fidia ya Yesu. (Luka 22:20) Agano la Sheria ya Kimusa lilikuwa limekomeshwa.—Waebrania 8:7-13.

Badala ya kuyaona matukio hayo kuwa uthibitisho wa kwamba Yesu alikuwa Mesiya, Mafarisayo walipata utatuzi mwingine. Walikuwa tayari wamenyakua sehemu kubwa ya mamlaka ya ukuhani. Hekalu likiwa limeharibiwa, wangeweza kuchukua hatua moja zaidi. Chuo cha kirabi cha Yavneh kilikuja kuwa kitovu cha Sanhedrini—mahakama kuu ya Kiyahudi—iliyopangwa upya. Chini ya uongozi wa Yohanan ben Zakkai na Gamaliel wa Pili katika Yavneh, Dini ya Kiyahudi iliundwa upya kabisa. Utumishi kwenye sinagogi, ulioongozwa na marabi, ulichukua mahali pa ibada kwenye hekalu, iliyosimamiwa na makuhani. Sala, hasa zile zilizotolewa Siku ya Kufunika, zilichukua mahali pa dhabihu. Mafarisayo walitoa hoja kwamba sheria ya mdomo iliyopewa Musa katika Sinai ilikuwa tayari imeona mambo hayo kimbele na kufanya maandalizi kwa ajili yake.

Vyuo vya kirabi vilianza kuwa na umashuhuri zaidi. Utaratibu wao mkuu wa masomo ulitia ndani kujadiliana, kukariri, na matumizi ya sheria ya mdomo. Hapo awali, msingi wa sheria ya mdomo ulihusianishwa na ufasiri wa Maandiko—Midrash. Sasa, mapokeo yaliyoongezeka daima ambayo yalikuwa yakikusanyika yalianza kufundishwa na kupangwa kwa utengano. Kila kanuni ya sheria ya mdomo ilisahilishwa ikawa mafungu ya maneno yawezayo kukaririwa kwa urahisi, mara nyingi ikifanywa kuwa melodia.

Kwa Nini Sheria ya Mdomo Iandikwe?

Kuwepo kwa vyuo vingi vya kirabi na kuongezeka kwa kanuni za kirabi kulitokeza tatizo jipya. Msomi wa kirabi Adin Steinsaltz aeleza: “Kila mwalimu alikuwa na njia yake, naye alieleza kanuni zake za mdomo katika mtindo wake wa pekee. . . . Haikutosha tena kufahamu tu mafundisho ya mfunzi wa mtu binafsi, na mwanafunzi alilazimika kufahamu mafundisho ya wasomi wengine . . . Hivyo, wanafunzi walilazimika kukariri mambo mengi mno kwa sababu ya ‘ongezeko kubwa la ghafula la ujuzi.’” Kwa kuzungukwa na habari nyingi zisizo na utaratibu, uwezo wa mwanafunzi wa kukumbuka ulikazwa hadi kufikia hali ya kutoweza kustahimili zaidi.

Katika karne ya pili W.K., uasi wa Wayahudi dhidi ya Roma, ulioongozwa na Bar Kokhba, ulisababisha unyanyasaji mkali wa wasomi warabi. Akiba—aliyekuwa rabi mashuhuri, aliyemwunga mkono Bar Kokhba—na pia wasomi wengi wenye kuongoza waliuawa. Marabi walihofia kwamba unyanyasaji ulioanzishwa upya ungeweza kuhatarisha kule kuwepo hasa kwa sheria ya mdomo. Walikuwa wameamini mapokeo yangepitishwa vizuri zaidi kwa mdomo kutoka bwana-mkubwa hadi mwanafunzi, lakini hali hizi zenye kubadilika zilisababisha kuwepo kwa jitihada zaidi ya kutokeza muundo uliopangwa ili kuhifadhi mafundisho ya watu wenye hekima, yasije yakasahaulika milele.

Katika kipindi fulani cha baadaye cha amani ya kadiri pamoja na Roma, Judah Ha-Nasi, rabi mwenye umashuhuri wa mwishoni mwa karne ya pili na mwanzoni mwa karne ya tatu W.K., alikusanya wasomi wengi na kuhariri mapokeo mengi mno ya mdomo kuwa mfumo uliopangwa ambao ulifanyizwa kwa Sehemu sita, kila moja ikigawanywa zaidi kuwa sehemu nne ndogo zaidi—zote zikawa 63. Maandishi hayo yalikuja kuitwa Mishnah. Ephraim Urbach, bingwa wa sheria ya mdomo, aeleza: “Mishnah . . . ilipewa kibali na mamlaka ambayo hayajapata kupewa kitabu chochote ila Torati yenyewe.” Mesiya alikuwa amekataliwa, hekalu lilikuwa magofu, lakini sheria ya mdomo ilihifadhiwa katika maandishi kwa njia ya Mishnah, enzi mpya katika Dini ya Kiyahudi ilianza.

[Maelezo ya Chini]

a Mtindo huu wa kufasiri Andiko waitwa midrash.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kwa nini Wayahudi wengi walikataa mamlaka ya Yesu?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki