Maswali Kutoka kwa Wasomaji
Je, Mariamu aliyekuwa mamake Yesu alikuwa na mimba tayari alipoenda kumtembelea mtu wa ukoo wake Elisabeti?
Ndiyo, ni dhahiri alikuwa na mimba.
Katika Luka sura ya 1, twasoma kwanza juu ya mimba ya Elisabeti, mke wa kuhani Zekaria, aliyemzaa Yohana (Mbatizaji). Elisabeti alipokuwa “katika mwezi wake wa sita malaika Gabrieli” alimtembelea Mariamu ili kumjulisha kwamba yeye angepata mimba na kumzaa “Mwana wa Aliye Juu Zaidi Sana.” (Luka 1:26, 30-33, NW) Lakini Mariamu alipata mimba lini?
Simulizi la Luka laendelea kusimulia kwamba baada ya hapo Mariamu alisafiri kwenda Yuda ili kumtembelea mtu wa ukoo wake Elisabeti aliyekuwa na mimba. Hao wanawake wawili walipokutana, kile kitoto kichanga (Yohana) katika tumbo la uzazi la Elisabeti kiliruka. Elisabeti alirejezea ‘mzao wa tumbo la uzazi la Mariamu,’ naye akamwita Mariamu “mama wa Bwana wangu.” (Luka 1:39-44) Kwa hiyo mkataa wenye kupatana na akili ni kwamba Mariamu alikuwa amepata mimba tayari, kwamba alikuwa na mimba alipoenda kumwona Elisabeti.
Luka 1:56 husema hivi: “Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.” Mstari huo hautoi hesabu sahihi hadi siku barabara katika kalenda. Huo wasema “kadiri ya miezi mitatu,” ambayo ingemfikisha Elisabeti kwenye mwezi wake wa tisa wa mimba.
Baada ya kumsaidia Elisabeti katika sehemu ya mwisho ya mimba yake, Mariamu aliondoka kwenda nyumbani kwake Nazareti. Labda Mariamu alitambua kwamba mara Elisabeti anapomzaa (Yohana), huenda kukawa na wageni wengi, baadhi yao wakiwa watu wa ukoo. Hilo lingeweza kumletea shida au aibu mwanamke kijana asiyeolewa ambaye mwenyewe alikuwa na mimba. Mimba ya Mariamu ilikuwa imeendelea kadiri gani alipoondoka kwenda Nazareti? Kwa kuwa alikuwa pamoja na Elisabeti “kadiri ya miezi mitatu,” labda Mariamu alikuwa mwisho-mwisho wa mwezi wa tatu au mapema katika mwezi wa nne wa mimba yake aliporudi Nazareti.