Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w96 9/15 kur. 22-24
  • Je, kwa Kweli Wahitaji Kuomba Radhi?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je, kwa Kweli Wahitaji Kuomba Radhi?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Upendo Hutupa Wajibu wa Kuomba Radhi
  • “Jifungeni Unyenyekevu”
  • Kuomba Radhi Humaanisha Mengi Katika Ndoa
  • Zoea Ustadi wa Kuomba Radhi
  • Kwa Nini Niombe Msamaha?
    Vijana Huuliza
  • Jinsi ya Kuomba Msamaha
    Amkeni!—2015
  • Kuomba Msamaha—Ni Njia Bora ya Kufanya Amani
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
  • Kwa Nini Ni Vigumu Sana Kuomba Msamaha?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2002
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
w96 9/15 kur. 22-24

Je, kwa Kweli Wahitaji Kuomba Radhi?

‘MIMI siombi radhi kamwe,’ akaandika George Bernard Shaw. ‘Lililofanywa limefanywa,’ huenda wengine wakasema.

Huenda sisi wenyewe husita kukubali kosa tukihofia kupoteza hali ya kujistahi. Huenda ikawa twajitetea kwamba mtu yule mwingine ndiye ana tatizo. Au huenda tukanuia kuomba radhi lakini twaahirisha mpaka tufikiripo kwamba jambo hilo hatimaye limesahauliwa.

Hivyo basi, je, kuomba radhi ni kwa lazima? Je, kwa kweli huko kwaweza kutimiza chochote?

Upendo Hutupa Wajibu wa Kuomba Radhi

Upendo wa kidugu ni alama ya kutambulisha ya wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Yeye alisema: “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:35) Maandiko huwasihi sana Wakristo ‘wajitahidi kupendana kwa moyo.’ (1 Petro 1:22) Upendo mwingi hutupa wajibu wa kuomba radhi. Kwa nini? Kwa sababu kutokamilika kwa kibinadamu husababisha kwa njia isiyoepukika hisia zilizoumizwa, ambazo huzuia upendo ikiwa hisia hizo hazipozwi.

Kwa kielelezo, kwa sababu ya kutofautiana kibinafsi na mtu fulani katika kutaniko la Kikristo, huenda tukapendelea kutozungumza naye. Ikiwa tumesababisha udhia, uhusiano wenye upendo waweza kurejeshwaje? Katika visa vilivyo vingi, kwa kuomba radhi kisha kujitahidi kuzungumza kwa njia yenye uchangamfu. Twawiwa upendo na waamini wenzetu, na tusemapo kwamba twasikitika kwa kusababisha udhia, twapunguza kiasi fulani cha deni hiyo.—Warumi 13:8.

Ili kutoa kielezi: Mari Carmen na Paqui ni wanawake wawili Wakristo waliokuwa na urafiki wa muda mrefu. Hata hivyo, kwa sababu Mari Carmen aliamini porojo fulani yenye kudhuru, urafiki wake na Paqui ukapoa. Bila kueleza chochote, alimwepuka Paqui kabisa. Karibu mwaka mmoja baadaye, Mari Carmen alipata kujua kwamba ile porojo haikuwa ya kweli. Aliitikiaje? Upendo ulimsukuma amwendee Paqui na kumweleza kwa unyenyekevu majuto yake makuu kwa kuenenda vibaya hivyo. Wote wawili wakaanza kulia sana, nao wamekuwa marafiki imara tangu wakati huo.

Ingawa huenda tusihisi kuwa tumefanya kosa lolote, kuomba radhi kwaweza kusuluhisha kutoelewana. Manuel akumbuka hivi: “Miaka mingi iliyopita mke wangu nami tuliishi katika nyumba ya mmoja wa dada zetu wa kiroho wakati alipokuwa amelazwa hospitalini. Tulijitahidi vilivyo kumsaidia yeye na watoto wake wakati wa ugonjwa wake. Lakini baada ya yeye kurudi nyumbani, alilalamika kwa rafiki kwamba hatukuwa tumeshughulikia gharama za nyumbani ifaavyo.

“Tulimtembelea na kueleza kwamba kwa sababu ya ujana na ukosefu wetu wa uzoefu, hatukuwa tumeshughulikia mambo jinsi ambavyo angefanya. Mara moja akaitikia kwa kusema kwamba yeye ndiye aliyetuwia na kwamba alikuwa mwenye shukrani sana kwa yote tuliyokuwa tumemfanyia. Tatizo lilisuluhishwa. Jambo hilo lililoonwa lilinifundisha umuhimu wa kuomba msamaha kwa unyenyekevu kutoelewana kutokeapo.”

Yehova alibariki wenzi hao wa ndoa kwa ajili ya kuonyesha upendo na ‘kufuatia mambo ya amani.’ (Warumi 14:19) Upendo pia huhusisha ufahamu wa hisia za wengine. Petro atushauri tuonyeshe “Hisia-mwenzi.” (1 Petro 3:8, NW) Ikiwa tuna hisia-mwenzi, tunaelekea zaidi kutambua maumivu ambayo tumesababisha kwa neno au tendo lisilofikiriwa nasi tutasukumwa kuomba radhi.

“Jifungeni Unyenyekevu”

Hata wazee Wakristo waaminifu huenda mara kwa mara wakawa na mabishano makali. (Linganisha Matendo 15:37-39.) Hizo ni pindi ambapo kuomba radhi kungenufaisha sana. Lakini ni nini kitakachosaidia mzee au Mkristo mwingine yeyote aonaye ugumu kuomba radhi?

Unyenyekevu ndio ufunguo. Mtume Petro alishauri hivi: “Jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana.” (1 Petro 5:5) Ingawa ni kweli kwamba katika mabishano yaliyo mengi watu wote wawili huwa na lawama, Mkristo aliye na unyenyekevu hujishughulisha na mapungufu yake mwenyewe na yu tayari kuyakubali.—Mithali 6:1-5.

Yule aombwaye radhi apaswa kukubali kwa njia ya unyenyekevu. Kwa kutoa kielezi, acheni tuseme kwamba wanaume wawili wanaohitaji kuwasiliana wamesimama kwenye vilele vya milima miwili tofauti. Mazungumzo ng’ambo ya ule ufa mkubwa uwatenganishao hayawezekani. Hata hivyo, mmoja wao ashukapo hadi kwenye bonde lililo chini na yule mwingine kufuata kielelezo chake, wao waweza kuwasiliana kwa urahisi. Vivyo hivyo, ikiwa Wakristo wawili wanahitaji kusuluhisha tatizo kati yao, kila mmoja wao na akutane kwa unyenyekevu na yule mwingine kwenye bonde, kitamathali, na kuomba radhi ifaavyo.—1 Petro 5:6.

Kuomba Radhi Humaanisha Mengi Katika Ndoa

Ndoa ya watu wawili wasio wakamilifu huandaa kwa njia isiyoepukika, fursa za kuomba radhi. Na ikiwa mume na mke wote pamoja wana hisia-mwenzi, itawasukuma waombe radhi ikitukia kwamba wamenena au kutenda kwa njia isiyo na ufikirio. Mithali 12:18 huonyesha hivi: “Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga; bali ulimi wa mwenye haki ni afya.” ‘Kuchoma kwa upanga bila kufikiri’ hakuwezi kufunduliwa, lakini kwaweza kupozwa kwa kuomba radhi kutoka moyoni. Bila shaka, hilo hutaka ufahamu na jitihada yenye kuendelea.

Akisema juu ya ndoa yake, Susana asema hivi: “Jack* nami tumeoana kwa miaka 24, lakini bado twajifunza mambo mapya juu ya mmoja na mwenzake. Kwa kuhuzunisha, wakati fulani uliopita, tulitengana na kuishi mbalimbali kwa majuma machache. Hata hivyo, tulisikiliza shauri la Kimaandiko kutoka kwa wazee na tukaungana tena. Sasa twatambua kwamba kwa kuwa tuna nyutu zilizo tofauti sana, yamkini mahitilafiano yatokee. Hayo yatokeapo, twaomba radhi upesi na kujaribu sana kwelikweli kuelewa maoni ya yule mtu mwingine. Nafurahi kusema kwamba ndoa yetu imefanya maendeleo sana.” Jack aongezea hivi: “Pia tumejifunza kutambua zile nyakati tuelekeapo kukasirika. Nyakati hizo twatendeana kwa uangalifu zaidi.”—Mithali 16:23.

Je, uombe radhi ikiwa wafikiri huna kosa? Hisia nzito zinapohusika, ni vigumu kuona ifaavyo mahali kosa lilipo. Lakini jambo la maana ni kuwa na amani katika ndoa. Mfikirie Abigaili, mwanamke Mwisraeli ambaye mume wake alimdhulumu Daudi. Ingawa hangeweza kulaumiwa kwa sababu ya upumbavu wa mume wake, aliomba radhi. “Nakuomba ulisamehe kosa lake mjakazi wako,” akasihi. Daudi aliitikia kwa kumtendea kwa ufikirio, na akikiri kwa unyenyekevu kwamba ikiwa haingalikuwa kwa sababu yake, angalimwaga damu isiyo na hatia.—1 Samweli 25:24-28, 32-35.

Vivyo hivyo, mwanamke Mkristo aitwaye June, aliyekuwa ameolewa kwa miaka 45, ahisi kwamba ndoa yenye mafanikio huhitaji nia ya kuwa wa kwanza kuomba radhi. Yeye asema hivi: “Mimi hujiambia kwamba ndoa yetu ni ya maana zaidi kuliko hisia zangu nikiwa mtu. Kwa hiyo niombapo radhi, nahisi kwamba naichangia ndoa.” Mwanamume mzee-mzee aitwaye Jim ataarifu hivi: “Mimi humwomba mke wangu radhi hata kwa mambo madogo-madogo. Tangu afanyiwe upasuaji mkubwa, yeye huudhika kwa urahisi. Kwa hiyo kwa ukawaida mimi humzungushia mkono wangu na kusema, ‘Pole, Mpenzi. Sikukusudia kukuudhi.’ Sawa na mmea unaotiwa maji, yeye husisimuka mara moja.”

Ikiwa tumemuumiza mtu tumpendaye zaidi, kuomba radhi haraka kuna matokeo sana. Milagros akubali kutoka moyoni, akisema hivi: “Mimi nina hali ya ukosefu wa kujitumaini, na neno kali kutoka kwa mume wangu hunifadhaisha. Lakini aombapo radhi, nahisi vizuri zaidi mara moja.” Kwa kufaa, Maandiko hutuambia sisi hivi: “Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; ni tamu nafsini, na afya mifupani.”—Mithali 16:24.

Zoea Ustadi wa Kuomba Radhi

Tukifanya zoea la kuomba radhi ihitajiwapo, yamkini tutaona kwamba watu wataitikia vizuri. Na huenda wao wenyewe wataomba radhi. Tushukupo kwamba tumemuudhi mtu, kwa nini tusifanye iwe desturi kuomba radhi badala ya kutumia wakati mwingi na jitihada nyingi ili kuepuka kukubali kosa? Huenda ulimwengu ukahisi kwamba kuomba radhi ni ishara ya udhaifu, lakini kwa kweli kunatoa uthibitisho wa ukomavu wa Kikristo. Bila shaka, hatungependa kuwa sawa na wale wanaokubali makosa fulani na bado wanapunguza daraka lao. Kwa kielelezo, je, sisi husema wakati wowote kwamba tunasikitika bila kumaanisha hilo? Ikiwa twachelewa na kuomba radhi sana, je, twanuia kufanyia maendeleo kuwahi kwetu?

Kwa hiyo, basi, je, kwa kweli twahitaji kuomba radhi? Ndiyo, twahitaji. Twawiwa na sisi wenyewe na wengine kufanya hivyo. Kuomba radhi kwaweza kusaidia kuondoa maumivu yasababishwayo na hali ya kutokamilika, na kwaweza kupoza mahusiano yenye shida. Kila wakati tuombapo radhi twapata somo la unyenyekevu na twazoezwa kuwa wenye kujali zaidi hisia za wengine. Likiwa tokeo, waamini wenzetu, wenzi wa ndoa, na wengine watatuona kuwa wale wastahilio shauku yao na kutumainiwa nao. Tutakuwa na amani ya akilini, na Yehova Mungu atatubariki.

[Maelezo ya Chini]

a Si majina yao halisi.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Kuomba radhi kwa moyo mweupe huendeleza upendo wa Kikristo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki