Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w97 1/1 kur. 30-31
  • Kumtafutia Isaka Mke

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kumtafutia Isaka Mke
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Utume Mgumu
  • Masomo Kwetu Sisi
  • Rebeka alitaka kumfurahisha Yehova
    Wafundishe Watoto Wako
  • Rebeka Alikuwa Tayari Kumpendeza Yehova
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2010
  • Ndoa Ambayo Inanufaisha Mamilioni Wanaoishi Sasa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1989
  • “Mimi Niko Tayari Kwenda”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2016
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
w97 1/1 kur. 30-31

Walifanya Mapenzi ya Yehova

Kumtafutia Isaka Mke

YULE mwanamume mzee-mzee aliyeketi kando ya kisima alikuwa amechoka sana. Yeye na watumishi wake pamoja na ngamia zao kumi walikuwa wamesafiri njia yote kutoka ujirani wa Beer-sheba hadi kaskazini mwa Mesopotamia—umbali wa kilometa zaidi ya 800.a Sasa kwa kuwa walikuwa wamefika mwisho wa safari yao, msafiri huyo aliyekuwa amechoka alitua ili kufikiria utume wake mgumu. Mwanamume huyo alikuwa nani, na kwa nini alikuwa amefanya safari hii iliyohitaji bidii nyingi?

Mwanamume huyo alikuwa mtumishi wa Abrahamu, “mzee wa nyumba yake.” (Mwanzo 24:2) Ingawa hakutajwa jina katika simulizi hili, yaonekana huyo alikuwa Eliezeri, ambaye wakati mmoja Abrahamu alimrejezea kuwa ‘mtu aliyezaliwa nyumbani mwake’ na aliyesema juu yake kuwa angekuwa ‘mrithi wake.’ (Mwanzo 15:2, 3) Bila shaka, huo ulikuwa wakati ambapo Abrahamu na Sara hawakuwa na mtoto. Sasa mwana wao, Isaka, alikuwa na umri wa miaka 40, na ingawa Eliezeri hakuwa tena mrithi mkuu wa Abrahamu, bado alikuwa mtumishi wake. Kwa hiyo alitii Abrahamu alipoomba jambo gumu lifanywe. Hilo lilikuwa nini?

Utume Mgumu

Katika siku ya Abrahamu ndoa haikuathiri familia fulani tu bali iliathiri pia kabila zima, au jumuiya ya mzee wa ukoo. Kwa hiyo, lilikuwa jambo la kidesturi kwa wazazi kuwachagulia watoto wao wenzi. Hata hivyo, katika kumtafutia mwana wake Isaka mke, Abrahamu alikabili hali ya kutatanisha. Mazoea yasiyomcha Mungu ya Wakanaani wa mahali hapo yalifanya kumwoa mmoja wao kuwa jambo lisilowezekana kabisa. (Kumbukumbu la Torati 18:9-12) Na ingawa lilikuwa jambo la kidesturi kwa mwanamume kumwoa mtu wa kabila lake mwenyewe, watu wa ukoo wa Abrahamu waliishi mamia ya kilometa kutoka hapo kaskazini mwa Mesopotamia. Hakuweza kumwacha tu Isaka ahamie huko, kwa kuwa Yehova alikuwa amemwahidi Abrahamu hivi: “Nitawapa uzao wako nchi hii,” nchi ya Kanaani. (Mwanzo 24:7, italiki ni zetu.) Kwa sababu hiyo, Abrahamu alimwambia Eliezeri: “Enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.”—Mwanzo 24:4.

Alipoimaliza hiyo safari ndefu, Eliezeri alipumzika kando ya kisima huku akitafakari juu ya utume wake. Aling’amua kwamba punde tu wanawake wangekuja kisimani ili kuchota ugavi wa usiku wa maji. Kwa hiyo alimwomba sana Yehova hivi: “Yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.”—Mwanzo 24:14.

Alipokuwa angali anasali, mwanamke kijana mwenye kuvutia aitwaye Rebeka akakaribia. “Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe,” Eliezeri akamwambia. Rebeka akafanya hivyo, kisha akasema: “Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa.” Hilo lilikuwa toleo lenye ukarimu, kwa kuwa ngamia mwenye kiu aweza kunywa maji yanayofikia lita 95 katika muda wa dakika kumi tu! Kama ngamia za Eliezeri walikuwa wenye kiu hivyo au la, ni lazima Rebeka awe alijua kwamba utumishi aliojitolea kufanya ungekuwa wa kujitahidi. Kwa kweli, “akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote.”—Mwanzo 24:15-20.

Akihisi mwelekezo wa Yehova, Eliezeri alimpa Rebeka pete ya puani ya dhahabu na vikuku viwili vya dhahabu, vyenye thamani ya karibu dola 1,400 katika thamani za leo. Rebeka alipomwambia kwamba alikuwa mjukuu wa kike wa Nahori, nduguye Abrahamu, Eliezeri alitoa sala ya kumshukuru Mungu. “BWANA akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu,” akasema. (Mwanzo 24:22-27) Eliezeri aliletwa hadi kwa familia ya Rebeka. Hatimaye, Rebeka akawa mkewe Isaka, naye akawa na pendeleo la kuwa mzazi wa kale wa Mesiya, Yesu.

Masomo Kwetu Sisi

Yehova alibariki jitihada yenye sala ya Eliezeri ya kumtafutia Isaka mwenzi mwenye kumhofu Mungu. Lakini, kumbuka kwamba ndoa ya Isaka ilihusiana moja kwa moja na kusudi la Mungu la kutokeza mbegu kupitia Abrahamu. Kwa hiyo simulizi hili halipaswi kutufanya tukate kauli kwamba kila mtu anayesali ili kupata mwenzi atapewa mmoja kimuujiza. Hata hivyo, tukishikamana na kanuni za Yehova, atatupa sisi nguvu za kuvumilia magumu yanayotokana na hali yoyote ile maishani—ndoa au useja.—1 Wakorintho 7:8, 9, 28; linganisha Wafilipi 4:11-13.

Eliezeri alihitaji kujitahidi sana ili kufanya mambo kwa njia ya Yehova. Sisi pia huenda tukaona kwamba kujipatanisha na viwango vya Yehova si jambo rahisi sikuzote. Kwa kielelezo, huenda isiwe rahisi kupata kazi ya kuajiriwa ambayo haikomeshi utendaji wa kitheokrasi, kupata mwenzi mwenye kumhofu Mungu, kupata washiriki wenye kujenga, kupata vitumbuizo visivyoshusha heshima. (Mathayo 6:33; 1 Wakorintho 7:39; 15:33; Waefeso 4:17-19) Hata hivyo, Yehova aweza kuwategemeza wale wanaokataa kuacha kanuni za Biblia. Biblia huahidi hivi: “Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako.”—Mithali 3:5, 6.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa kufikiria mwendo wa wastani wa ngamia, huenda ikawa ilichukua siku zaidi ya 25 kumaliza hiyo safari.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki