Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w98 1/15 kur. 19-22
  • Kupanga Kimbele kwa Ajili ya Wapendwa Wetu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kupanga Kimbele kwa Ajili ya Wapendwa Wetu
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kwa Nini Ufikirie Kifo?
  • Unyakuzi wa Mali
  • “Hao Wawili Watakuwa Mwili Mmoja”
  • Desturi za Maziko
  • Kuchukua Hatua za Kisheria
  • Kuzungumza Mambo Pamoja na Familia
  • Hami Familia Yako
  • Maoni ya Mkristo Kuhusu Desturi za Mazishi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Jinsi Familia Yako Inavyoweza Kuwa na Furaha
    Biblia Inatufundisha Nini?
  • Faida Zenye Kudumu Kutokana na Kuifuata Biblia Kama Jamaa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1975
  • Kufanikisha Maisha ya Jamaa
    Unaweza Kuishi Milele Katika Paradiso Duniani
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
w98 1/15 kur. 19-22

Kupanga Kimbele kwa Ajili ya Wapendwa Wetu

KISA chenye kusikitisha cha Annie kilitokea hivi karibuni katika gazeti fulani la habari la Kiafrika. Mume wa Annie alikuwa mfanya-biashara. Alikufa mwaka wa 1995, akiacha magari 15; akaunti kadhaa za benki; dola (za Kimarekani) zipatazo 4,000 pesa taslimu; duka; baa; na nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala. Alichokosa kuacha ni wasia.

Yaripotiwa kwamba ndugu-mkwe wa Annie alikamata hiyo mali na fedha na kuwalazimisha yeye na watoto wake sita kuondoka katika nyumba yao. Wakiwa fukara, Annie na watoto wake sasa huishi na ndugu yake. Wanne kati ya watoto wake wamelazimika kuacha shule, kwa kuwa hakuna fedha za karo au za yunifomu.

Annie alipeleka ombi kwenye mahakama kuu, ambayo iliamua kwamba apasa kurudishiwa baadhi ya mali, kutia na gari moja. Lakini hakuna kitu chochote kilichorudishwa. Lazima aende mahakamani tena ili kujaribu kupata agizo la kumlazimisha ndugu-mkwe wake akubaliane na uamuzi wa mahakama kuu.

Kwa Nini Ufikirie Kifo?

Kisa cha Annie chatoa kielelezi juu ya yale ambayo huenda yakatokea kichwa cha familia ashindwapo kupanga kwa ajili ya uwezekano wa kifo chake. Wakati wa kufa, wanadamu wote ‘huwaachia wengine mali zao.’ (Zaburi 49:10) Zaidi ya hayo, wafu hawana mamlaka juu ya yale ambayo mali zao hufanyiwa. (Mhubiri 9:5, 10) Ili awe na mamlaka juu ya yale yatukiayo kwa mali yake, lazima mtu apange mambo kabla ya kifo.

Ingawa sisi sote twajua kwamba huenda tukafa bila kutarajia, watu wengi hukosa kufanya maandalizi ya mapema kwa ajili ya wapendwa wao wanaobaki hai. Ingawa mazungumzo yetu yatakaziwa vikundi fulani vya kitamaduni katika Afrika, matatizo kama hayo yako katika sehemu nyingine za ulimwengu.

Kama wewe wachukua hatua kuhusiana na matumizi ya mali yako iwapo kifo kingetokea ni jambo la kibinafsi. (Wagalatia 6:5) Hata hivyo, huenda mtu akauliza, ‘Kwa nini wakati ambapo mtu yuko hai awatunze sana na kushughulikia mke na watoto wake lakini asiwafanyie maandalizi yoyote kwa hali yao njema iwapo angekufa?’ Sababu kuu ni kwamba walio wengi kati yetu hawapendi kufikiria uwezekano wa kwamba huenda tukafa, sembuse kupanga kwa ajili ya kifo. Kwa hakika, hatuwezi kujua kimbele siku ya kufa kwetu, kama vile Biblia isemavyo: “Kwa kuwa hamjui uhai wenu utakuwa nini kesho. Kwa maana nyinyi ni ukungu unaotokea kwa muda kidogo na kisha kutoweka.”—Yakobo 4:14.

Kupanga kwa ajili ya uwezekano wa kifo ni jambo la busara. Pia kwaonyesha hangaiko lenye upendo kwa wabakio hai. Ikiwa hatutapanga mambo yetu, wengine watafanya hivyo. Labda watu ambao hatujapata kuwajua watafanya maamuzi kuhusu mali zetu na mipango ya maziko. Chini ya hali za namna hiyo katika nchi fulani, Serikali huamua ni nani atakayepata fedha zetu na mali yetu. Katika sehemu nyingine, jamaa huamua, na mara nyingi maamuzi hayo huandamana na kubishana-bishana ambako huendeleza nia ya kudhuru wengine ndani ya familia. Isitoshe, huenda yale yaamuliwayo yatofautiane kabisa na yale ambayo tungetaka.

Unyakuzi wa Mali

Mjane huteseka zaidi mume wake afapo. Mbali na huzuni ya kumpoteza mwenzi wake, mara nyingi yeye huwa mhasiriwa wa unyakuzi wa mali. Jambo hilo lilifafanuliwa mapema katika kisa cha Annie. Sehemu ya sababu ya unyakuzi wa mali yahusiana na jinsi ambavyo wake huenda wakaonwa kuwa. Katika tamaduni fulani mke wa mtu haonwi kuwa sehemu ya familia yake. Katika maana fulani yeye ni mgeni ambaye huenda akarudia familia yake wakati wowote au kuolewa tena katika familia nyingine. Tofauti na hilo, yawaziwa kwamba, ndugu, dada, na wazazi wa mtu hawatamwacha kamwe. Akifa, familia yake huamini kwamba mali iliyokuwa yake ni yao, bali si ya mke na watoto wake.

Waume ambao hawawafunulii wake zao siri huendeleza kufikiri kwa namna hiyo. Mike alizungumza mambo yake ya kibiashara na ndugu zake tu. Walijua raslimali zake zilikuwa nini, lakini mke wake alijua machache sana. Alipokufa, ndugu zake walimjia na kudai malipo ambayo mume wake alikuwa akitarajia. Hata hakujua juu ya malipo hayo. Ndipo, wakakamata mashine zake za fotokopi na za chapa ambazo mume wake alikuwa amemnunulia. Mwishowe, ndugu za mume wake walirithi nyumba na kila kitu kilichokuwa ndani yake. Mjane huyo na binti yake mchanga walilazimishwa kuondoka, wakichukua mavazi yao tu.

“Hao Wawili Watakuwa Mwili Mmoja”

Waume Wakristo huwapenda wake zao na kuwaona kuwa wenye kustahili kutumainiwa. Wanaume hao huzingatia shauri hili la Kimaandiko: “Waume wapaswa kuwa wakiwapenda wake zao kama miili yao wenyewe.” Wanaume hao pia hukubaliana na taarifa hii iliyopuliziwa kimungu: “Mwanamume ataacha baba yake na mama yake naye atashikamana na mke wake, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.”—Waefeso 5:28, 31.

Waume wenye kumhofu Mungu pia hukubaliana na mtume Mkristo Paulo, aliyeandika hivi: “Hakika ikiwa yeyote hawaandalii kitu wale walio wake mwenyewe, na hasa kwa ajili ya wale walio washiriki wa nyumbani mwake, ameikana imani naye ni mbaya zaidi kuliko mtu asiye na imani.” (1 Timotheo 5:8) Kwa kupatana na kanuni hiyo, ikiwa mume Mkristo angepanga kwenda safari ndefu, angehakikisha kwamba familia yake ingeshughulikiwa wakati ambapo yuko mbali. Vivyo hivyo, je, si jambo la akili kwamba angefanya maandalizi kwa ajili ya mke na watoto wake iwapo angekufa? Kujitayarisha kwa ajili ya huzuni kubwa isiyotarajiwa ni jambo la busara na pia la upendo.

Desturi za Maziko

Kwa waume Wakristo kuna upande mwingine wa jambo hilo wa kufikiriwa. Kuongeza huzuni ya mjane juu ya kumpoteza mwenzi wake, mali, na labda hata watoto wake, jamii nyingine humshurutisha atekeleze sherehe za kuomboleza za kidesturi. Gazeti la habari la The Guardian la Nigeria laomboleza kwamba katika maeneo fulani, pokeo humtaka mjane alale usingizi pamoja na maiti ya mume wake katika chumba kilekile chenye giza. Katika sehemu nyingine, wajane hawaruhusiwi kuondoka nyumbani kwa kipindi cha maombolezo cha miezi ipatayo sita. Wakati huo, hawapaswi kuoga, na hata kuosha mikono yao kabla ya au baada ya milo kwakatazwa.

Desturi hizo hutokeza matatizo, hasa kwa wajane Wakristo. Tamaa yao ya kumpendeza Mungu huwasukuma kuepuka desturi ambazo hazipatani na mafundisho ya Biblia. (2 Wakorintho 6:14, 17) Hata hivyo, kwa sababu ya kutokubaliana na desturi hizo, huenda mjane akapatwa na mnyanyaso. Huenda hata ikambidi akimbie ili aokoe uhai wake.

Kuchukua Hatua za Kisheria

Kwa hekima Biblia husema hivi: “Mawazo [“mipango,” NW] ya mwenye bidii huuelekea utajiri tu.” (Mithali 21:5) Kichwa cha familia aweza kufanya mipango gani? Katika jamii zilizo nyingi yawezekana kuandika wasia au kutayarisha hati ambayo yataarifu jinsi mali ya mtu ipaswavyo kugawanywa iwapo angekufa. Huenda ukatia ndani mambo madogo-madogo juu ya mipango ya maziko. Huenda hiyo hati pia ikaeleza kimahususi yale ambayo mwenzi wa ndoa apaswa kufanya (au kutofanya) kuhusiana na desturi za maziko na za maombolezo.

Mwanamke aitwaye Leah alifiwa na mume wake mwaka wa 1992. Yeye asema hivi: “Nina watoto watano—wasichana wanne na mvulana mmoja. Mume wangu alikuwa mgonjwa kwa muda fulani kabla hajafa. Lakini hata kabla ya kuwa mgonjwa, aliandika wasia akisema kwamba alitaka mimi na watoto wake turithi mali zake zote. Hizo zilitia ndani fedha za bima, shamba la kulima, wanyama wa shambani, na nyumba. Alitia sahihi huo wasia na kunipa. . . . Baada ya kifo cha mume wangu, jamaa walitaka fungu fulani la urithi wake. Niliwatajia kwamba mume wangu alikuwa amenunua hilo shamba la kulima kwa fedha zake mwenyewe na kwamba hawakuwa na haki ya kudai kitu chochote. Walipoona wasia ulioandikwa, waliukubali.”

Kuzungumza Mambo Pamoja na Familia

Huenda matatizo yakatokea mtu asiposema na familia yake juu ya itikadi zake na matakwa yake. Fikiria kisa cha mwanamume mmoja ambaye jamaa zake walisisitiza kwamba maziko yake yafanyike kijijini kupatana na desturi ya mahali hapo. Mjane wake na watoto wake walilazimishwa kuacha mwili wake na jamaa zake maisha yao yalipotishwa. Yeye aomboleza hivi: “Ikiwa mume wangu angalimwambia hata mmoja wa wajomba zake au binamu zake jinsi alivyotaka azikwe, familia haingalisisitiza kufanya mazoea yao ya kidesturi ya maziko.”

Katika jamii fulani makubaliano ya mdomo lazima yafuatwe kama vile ambavyo hati iliyoandikwa hufuatwa. Hali iko hivyo katika sehemu fulani za Swaziland, ambako watu wengi wana itikadi ambazo huendeleza utaratibu mbalimbali wa maziko na wa maombolezo. Akijua hilo, mwanamume Mkristo aitwaye Isaac alifanya mkutano na jamaa zake, ambao hawakuwa Mashahidi wa Yehova, na kuzungumzia yale aliyotaka yafanywe baada ya kifo chake. Aliwaambia ni nani angerithi mali mahususi za kimwili, na kuwaeleza waziwazi jinsi ambavyo maziko yake yalipasa kuongozwa. Baada ya yeye kufa, mambo yalitendeka kulingana na matakwa yake. Isaac alifanyiwa maziko ya Kikristo, na mke wake akatunzwa vema.

Hami Familia Yako

Utakachofanya ili uhami familia yako kifo chako kikitukia ni jambo la kibinafsi, lakini Mkristo aitwaye Edward asema hivi: “Nina bima ya maisha ya kunufaisha washiriki wanane wa familia yangu. Mke wangu ameweka sahihi kwenye akaunti yangu ya benki. Kwa hiyo nikifa, yeye aweza kupata fedha katika hiyo akaunti. . . . Nina wasia wa kunufaisha familia yangu. Nikifa, chochote kile niachacho kitakuwa cha mke wangu na watoto wangu. Niliandika wasia wangu miaka mitano iliyopita. Ulitayarishwa na mwanasheria, na mke wangu na mwanangu wana nakala. Katika wasia wangu, nilieleza kimahususi kwamba jamaa zangu hawapaswi kuhusishwa katika maziko yangu. Mimi ni mali ya tengenezo la Yehova. Kwa hiyo hata ikiwa Shahidi mmoja au wawili tu ndio wapatikana kuongoza maziko yangu, hao watatosha. Nimezungumzia hilo pamoja na washiriki wa jamaa yangu.”

Katika maana fulani, kufanya mipango ya namna hiyo ni zawadi kwa familia yako. Bila shaka, kupanga kwa ajili ya uwezekano wa kifo si kama zawadi ya chokoleti au shada la maua. Lakini, kwaonyesha upendo wako. Kwathibitisha kwamba wataka ‘kuwaandalia kitu washiriki wa nyumba yako’ hata wakati ambapo hauko nao tena.

[Sanduku katika ukurasa wa 21]

Yesu Alifanya Uandalizi kwa Ajili ya Mama Yake

“Kando ya mti wa mateso wa Yesu, palikuwa pamesimama mama yake na dada ya mama yake; Maria mke wa Klopasi, na Maria Magdalene. Kwa hiyo Yesu, kwa kuona mama yake na mwanafunzi ambaye yeye alimpenda wamesimama kando, akamwambia mama yake: ‘Mwanamke, ona! Mwana wako!’ Halafu akamwambia huyo mwanafunzi: ‘Ona! Mama yako!’ Na tangu saa hiyo na kuendelea huyo mwanafunzi [Yohana] akampeleka nyumbani kwake mwenyewe.”—Yohana 19:25-27.

[Picha katika ukurasa wa 22]

Kwa ufikirio Wakristo wengi huchukua hatua za kisheria ili kuhami familia zao

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki