Je, Wewe Ni Mwenye Kutazamia Mema au Mwenye Kutazamia Mabaya?
“ZILIKUWA ndizo nyakati bora zaidi, zilikuwa ndizo nyakati mbaya zaidi, . . . zilikuwa nyakati za ongezeko la matumaini, zilikuwa nyakati za kukata tumaini, tulitazamia kila kitu, hatukutazamia chochote.” Hayo maneno ya ufunguzi ya kichapo kilicho kazi bora ya Charles Dickens kiitwacho A Tale of Two Cities, chatofautisha kwa ustadi jinsi matukio yawezavyo kuathiri kufikiri kwetu, hisia zetu, na mtazamo wetu.
Miji miwili iliyorejezewa ilikuwa London na Paris wakati wa msukosuko wa Mapinduzi ya Ufaransa. Kwa raia walioonewa wa Ufaransa ya karne ya 18, haki za kibinadamu zilizotangazwa na hayo mapinduzi kwa kweli zilikuwa “nyakati za ongezeko la matumaini.” Lakini kwa wale wa mfumo wa kisiasa na kijamii wa kabla ya mapinduzi au mfumo wa kisiasa uliokuwa ukiondoka, zilikuwa “nyakati za kukata tumaini,” zilizoongoza kwenye kifo na uharibifu.
Kutazamia mema au kutazamia mabaya? Yote hayo yalitegemea upande uliokuwako. Na bado yategemea hilo.
Wakati wa Kujichunguza
Je, wewe ni mwenye kutazamia mema? Je, waona upande wenye kupendeza wa maisha, sikuzote ukitazamia yaliyo bora zaidi? Au wewe huwa na mwelekeo wa kutazamia mabaya, ukiwa na mtazamo hasi juu ya matarajio yako, ukitumainia yaliyo bora lakini wakati uleule ukitarajia yaliyo mabaya zaidi?
Miaka 60 iliyopita James Branch Cabell, mwandishi wa riwaya Mmarekani, alitoa muhtasari wa hizo falsafa mbili zenye kuhitilafiana, hivi: “Mwenye kutazamia mema hutangaza kwamba twaishi katika jamii ya kibinadamu iliyo bora kabisa iwezayo kupatikana; na mwenye kutazamia mabaya huhofu kwamba hilo ni kweli.” Ikiwa wahisi kwamba maoni hayo ni ya kudharau mambo, chunguza ubaya na uzuri wa pande tatu tu za ulimwengu wa leo kama zionyeshwavyo chini. Kisha chunguza maitikio yako, na ujiulize, ‘Je, mimi ni mwenye kutazamia mema au mwenye kutazamia mabaya?’
Amani Yenye Kudumu: Waweza kutaja maeneo mangapi yenye taabu ulimwenguni? Ireland, iliyokuwa Yugoslavia, Mashariki ya Kati, Burundi, Rwanda—hayo yaingia upesi akilini. Je, mapambano hayo na mengine yaweza kupata kutatuliwa ili kuhakikisha kwamba kuna amani yenye kudumu ya tufeni pote? Je, ulimwengu waelekea kupata amani?
Uthabiti wa Kiuchumi: Zikitarajia muungano wa kifedha kufikia mwaka wa 1999, nchi za Muungano wa Ulaya zinakabili kwa uzito matatizo ya infleshoni na mikopo kutoka kwa umma. Kwingineko, ufisadi humomonyoa muundo wa kiuchumi wa mataifa mengi ya Amerika na ya Afrika, ambako infleshoni huwekelea mzigo wenye kulemea ambao karibu hauwezi kuchukulika na matatizo ya kikabila hutenganisha bado. Je, uthabiti wa kiuchumi wa ulimwengu uko mbele tu?
Ukosefu wa Kazi ya Kuajiriwa: Katika uchaguzi wa kitaifa wa mwaka wa 1997, makanisa ya Uingereza yaliungana ili kuhimiza vyama vyote vya kisiasa viweke kwanza kabisa katika ajenda zao kazi za kuajiriwa kwa ajili ya watu wote. Lakini karibu asilimia 30 ya wafanyakazi wote ulimwenguni wakiwa hawana kazi au hawana kazi ya kutosha, je, kwaweza kuwepo kazi ya kuajiriwa kwa ajili ya watu wote, yenye kudumu—hasa kwa ajili ya vijana?
Jinsi ilivyo rahisi kutazamia mabaya! Hata hivyo kuna msingi wa kutazamia mema, nasi twakualika uchunguze jinsi iwezekanavyo kusitawisha mtazamo wa kutarajia mema.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Mapinduzi ya Ufaransa
[Hisani]
Kutoka katika kitabu Pictorial History of the World