Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w98 9/1 kur. 30-31
  • Paulo Atoa Ushahidi kwa Ujasiri Mbele ya Waheshimiwa

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Paulo Atoa Ushahidi kwa Ujasiri Mbele ya Waheshimiwa
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kujitetea kwa Paulo kwa Ujasiri
  • Somo Kwetu
  • Wasaidie Wengine Wakubali Ujumbe wa Ufalme
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2003
  • “Ninakata Rufaa kwa Kaisari!”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • “Neno la Yehova Likazidi Kukua”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Piga Mbiu ya Ufalme wa Yehova kwa Ujasiri!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
w98 9/1 kur. 30-31

Walifanya Mapenzi ya Yehova

Paulo Atoa Ushahidi kwa Ujasiri Mbele ya Waheshimiwa

TOFAUTI kati ya hao wanaume wawili ilikuwa yenye kutokeza sana. Mmoja alivaa taji ilhali yule mwingine alikuwa na minyororo. Mmoja alikuwa mfalme; yule mwingine alikuwa mfungwa. Baada ya miaka miwili gerezani, mtume Paulo sasa alisimama mbele ya Herode Agripa wa Pili, mtawala wa Wayahudi. Mfalme na Bernike mwandamani wake, walikuwa wamekuja “kwa wonyesho mwingi wenye fahari za madaha na kuingia ndani ya chumba cha baraza pamoja na makamanda wa kijeshi na vilevile wanaume waheshimiwa katika jiji.” (Matendo 25:23) Kitabu kimoja cha marejezo chasema: “Yamkini kulikuwapo watu maelfu kadhaa.”

Festo, gavana aliyekuwa tu ametoka kuwekwa rasmi, alikuwa amepanga kuwe na mkutano. Feliksi, gavana aliyekuwa amemtangulia alikuwa ameridhika kumwacha Paulo ateseke gerezani. Lakini Festo alishuku uhalali wa mashtaka dhidi ya Paulo. Kwani, Paulo alisisitiza sana kutokuwa na hatia hivi kwamba, alikuwa ametaka kuwasilisha kesi yake kwa Kaisari! Kesi ya Paulo ilichochea udadisi wa Mfalme Agripa. “Mimi mwenyewe ningependezwa pia na kumsikia huyo mtu,” akasema. Festo alifanya mipango upesi, yaelekea akiwaza juu ya maoni ambayo mfalme angekuwa nayo kumhusu mfungwa huyo wa pekee.—Matendo 24:27–25:22.

Siku iliyofuata, Paulo alijikuta amesimama mbele ya umati mkubwa wa waheshimiwa. “Najihesabu mwenyewe kuwa mwenye furaha kwamba ni mbele yako napaswa kujitetea siku hii,” akamwambia Agripa, “hasa kwa kuwa wewe ni mtaalamu katika desturi zote na vilevile mabishano miongoni mwa Wayahudi. Kwa hiyo nakuomba unisikie kwa subira.”—Matendo 26:2, 3.

Kujitetea kwa Paulo kwa Ujasiri

Kwanza, Paulo alimwambia Agripa juu ya maisha yake ya wakati uliopita akiwa mnyanyasaji wa Wakristo. “Nilijaribu kuwalazimisha wakane imani yao,” akasema. “Nilifikia hatua ya kuwanyanyasa hata katika majiji ya nje.” Paulo aliendelea kusimulia jinsi alivyopata ono lenye kushtusha ambamo Yesu aliyefufuliwa alimwuliza: “Kwa nini unaninyanyasa mimi? Kufuliza kupiga teke dhidi ya michokoo hufanya iwe vigumu kwako.”a—Matendo 26:4-14.

Kisha Yesu akampa Sauli utume wa kutoa ushahidi kwa watu wa mataifa yote juu ya “mambo ambayo umeona na pia mambo nitakayokufanya uyaone kwa habari yangu.” Paulo alisimulia kwamba alijitahidi sana kutimiza mgawo wake. Hata hivyo, “kwa sababu ya mambo haya,” akamwambia Agripa, “Wayahudi walinikamata katika hekalu na kujaribu kuniua kikatili.” Akitaka kuchochea itikio lenye huruma kwa kutaja kupendezwa kwa Agripa na Dini ya Kiyahudi, Paulo alikazia kwamba utoaji wake wa ushahidi ulihusisha “[kutosema] lolote ila mambo ambayo Manabii na vilevile Musa walitaarifu yalipaswa yatukie” kuhusu kifo na ufufuo wa Mesiya.—Matendo 26:15-23.

Festo akakatiza kwa kusema kwa mkazo: “Kusoma kwingi kunakusukuma kuingia katika kichaa!” Paulo akamjibu: “Mimi sishikwi na kichaa, Ewe Mtukuzwa Festo, bali ninatamka semi za kweli na za utimamu wa akili.” Kisha Paulo akasema hivi kumhusu Agripa: “Mfalme ambaye ninasema naye kwa uhuru wa usemi ajua vema juu ya mambo haya; kwa maana nimeshawishika kwamba hakuna hata moja kati ya mambo haya liponyokalo kujulikana naye, kwa maana jambo hili halijafanywa pembeni.”—Matendo 26:24-26.

Kisha Paulo akasema na Agripa moja kwa moja. “Je, wewe, Mfalme Agripa, wawaamini Manabii?” Bila shaka swali hili lilimtia Agripa wasiwasi. Kwa vyovyote, alikuwa na sifa aliyopaswa kudumisha, na kukubaliana na Paulo kungekuwa kukubaliana na kile Festo alichokiita “kichaa.” Labda akifahamu kusitasita kwa Agripa, Paulo alijibu swali lake mwenyewe. “Najua waamini,” akasema. Sasa Agripa akazungumza, lakini bila kukanusha wala kukubali hayo. “Kwa muda mfupi,” akamwambia Paulo, “ungenishawishi niwe Mkristo.”—Matendo 26:27, 28.

Kwa ustadi Paulo alitumia taarifa ya Agripa ya kukwepa ili kutoa hoja yenye nguvu. “Kama ingekuwa kwa muda mfupi au kwa muda mrefu,” akasema, “mimi ningeweza kutaka kwa Mungu kwamba iwe si wewe tu bali pia wote wanisikiao leo wangepata kuwa watu wa namna niliyo mimi, isipokuwa vifungo hivi.”—Matendo 26:29.

Agripa na Festo hawakumpata Paulo na jambo lolote la kustahili kifo au kifungo. Hata hivyo ombi lake la kuwasilisha kesi yake kwa Kaisari halingeweza kubatilishwa. Hiyo ndiyo sababu Agripa alimwambia Festo hivi: “Mtu huyu angaliweza kufunguliwa kama hakuwa amekata rufani kwa Kaisari.”—Matendo 26:30-32.

Somo Kwetu

Njia ya Paulo ya kutoa ushahidi mbele ya waheshimiwa hutuandalia kielelezo chenye kutokeza. Alipozungumza na Mfalme Agripa, Paulo alitumia busara. Bila shaka alifahamu kashfa iliyowahusu Agripa na Bernike. Uhusiano wao ulikuwa wa maharimu, kwa kuwa Bernike alikuwa kwa kweli dadake Agripa. Lakini wakati huo Paulo hakuchagua kuzungumzia maadili. Badala yake, alikazia hoja ambazo yeye na Agripa walikubaliana kwa ujumla. Zaidi ya hayo, ingawa Paulo alifunzwa na Gamalieli, Farisayo mwenye elimu, yeye alikiri kwamba Agripa alikuwa stadi wa desturi za Wayahudi. (Matendo 22:3) Licha ya maadili ya kibinafsi ya Agripa, Paulo alizungumza naye kwa staha kwa sababu Agripa alikuwa na wadhifa wenye mamlaka.—Waroma 13:7.

Tunapotoa ushahidi kwa ujasiri juu ya yale tunayoamini, si mradi wetu kufichua au kushutumu, mazoea yasiyo safi ya wasikilizaji wetu. Badala yake, ili kufanya iwe rahisi kwao kukubali kweli, twapaswa kukazia sehemu zifaazo za habari njema, tukikazia matumaini yetu sote kwa ujumla. Tunapozungumza na wale wenye umri mkubwa zaidi au walio katika mamlaka, twapaswa kutambua wadhifa wao. (Mambo ya Walawi 19:32) Kwa njia hiyo, twaweza kumwiga Paulo, aliyesema: “Nimekuwa mambo yote kwa watu wa namna zote, ili nipate kwa vyovyote kuokoa wengine.”—1 Wakorintho 9:22.

[Maelezo ya Chini]

a Usemi “kupiga teke dhidi ya michokoo” hufafanua kitendo cha fahali ambaye hujiumiza anapopiga teke fimbo yenye ncha kali ambayo imenuiwa kuendesha na kuongoza mnyama. Vivyo hivyo, kwa kuwanyanyasa Wakristo, Sauli angejidhuru mwenyewe tu, kwa kuwa alikuwa akipigana na watu waliokuwa na utegemezo wa Mungu.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki