Sababu Inayowafanya Wawe Wajeuri
KITOTO kichanga sana cha majuma 27, kilizaliwa kabla ya wakati wake, huko Denver, Colorado, Marekani. Mvulana huyo alisalimika, na baada ya miezi mitatu hospitalini, alirudishwa nyumbani kwa wazazi wake. Majuma matatu baadaye, kijana huyo alikuwa tena hospitalini. Kwa nini? Alikuwa amepatwa na dhara kubwa kwenye ubongo kwa sababu ya kutikiswa kijeuri na baba yake. Baba yake hangeweza kuvumilia kulialia kwa mtoto huyo mchanga. Mvulana huyo mchanga akawa kipofu na asiyejiweza. Tiba ya kisasa ilikuwa imemwokoa kutokana na vurugu ya wakati wa kuzaliwa kwake, lakini haingeweza kumwokoa kutokana na ujeuri wa baba yake.
Watoto wengi sana hutendwa vibaya, kupigwapigwa, au kuuawa katika mojawapo ya mahali penye ujeuri mkubwa zaidi duniani—nyumbani! Watu fulani hukadiria kwamba watoto wapatao 5,000 kila mwaka hufa kifo kinachosababishwa na wazazi wao katika Marekani pekee! Wenye kuhasiriwa si watoto peke yao. Kulingana na gazeti World Health, “kutendwa vibaya kwa mke ndicho kisababishi kikubwa zaidi cha madhara kati ya wanawake waliofikia umri wa kuwa na watoto” katika Marekani. Vipi nchi nyinginezo? “Wanawake wapatao thuluthi moja kufikia zaidi ya nusu ya idadi ya wanawake waliofanyiwa uchunguzi katika nchi zinazoendelea, waripoti kwamba wao hupigwa na wenzi wao.” Ndiyo, ujeuri umefanyiza uharibifu mkubwa sana, na hasa nyumbani.
Waume wengi na wake hujaribu kutatua kutoelewana kwao kwa kuwa wajeuri. Katika nchi fulani, wazazi na walimu huwa wajeuri dhidi ya watoto kama njia ya kuondolea mbali hasira yao. Ili kujifurahisha, watu wakandamizao wengine hupenda kuwachokoza walio dhaifu, na kuwatendea ujeuri. Kwa nini watu huwa wajeuri hivyo?
Sababu Inayowafanya Watu Kuwa Wajeuri
Watu fulani hudai kwamba wanadamu ni wajeuri kiasili. Ijapokuwa uhalifu wa kijeuri kwa ujumla umepungua katika Marekani, huo umeongezeka kati ya vijana. Tena kumekuwa na ongezeko la upendezi wa ujeuri. Ile mifumo mitatu mikubwa ya usambazaji wa habari za televisheni, imeongeza idadi ya habari za uhalifu mara mbili na kuongeza mara tatu ripoti za mauaji. Ndiyo, uhalifu ni biashara yenye faida kubwa. “Hatuukubali uhalifu tu,” akasema Karl Menninger daktari wa magonjwa ya akili, “tunaufanya uwe habari motomoto katika magazeti yetu. Thuluthi moja au robo ya programu zetu za televisheni huutumia kuwafurahisha watoto wetu. Eti twauruhusu tu! La, rafiki zangu, twaupenda.”
Uchunguzi wa kisayansi wa hivi majuzi wadokeza kwamba biolojia ya ubongo na mazingira yetu yamechangia sana hali ya kibinadamu ya kutaka kufanya ugomvi. “Kauli tunayoanza kukata sote ni kwamba mazingira mabaya ambamo watoto wengi zaidi hujipata kwayo, kwa kweli yanasababisha mweneo mkubwa wa ujeuri,” asema Dakt. Markus J. Kruesi wa Chuo Kikuu cha Illinois, Taasisi ya Uchunguzi wa Uhalifu wa Vijana. “Matukio ya kimazingira yanafanyiza sana mabadiliko ya chembe fulani za ubongo ambazo hufanya watu watende haraka-haraka bila kutafakari.” Mambo kama vile “kuporomoka kwa muundo wa familia, kuongezeka kwa jamaa za mzazi mmoja, ufukara usiokuwa na mwisho, na utumizi mbaya sana wa dawa za kulevya, yanaweza kuubadili utendaji wa ubongo ukiufanya uwe katika hali ya kutaka kufanya ugomvi—tokeo ambalo wakati mmoja lilifikiriwa kuwa lisilowezekana,” chasema kitabu Inside the Brain.
Mabadiliko katika ubongo, yadaiwa, hutia ndani kushuka kwa kiwango cha serotonin, kemikali fulani ya ubongo ambayo yafikiriwa huzuia hali ya kutaka kufanya ugomvi. Uchunguzi wafunua kwamba kileo chaweza kupunguza serotonin katika ubongo, hivyo ikitokeza msingi wa kisayansi wa uhusiano kati ya hali ya kutaka kufanya ugomvi na utumizi mbaya wa kileo.
Jambo jingine bado lahusika katika kuongezeka kwa ujeuri leo. “Kumbuka,” chatutahadharisha kitabu cha unabii chenye kutumainika, Biblia, kwamba, “kutakuwa nyakati ngumu katika siku za mwisho. Watu watakuwa wenye ubinafsi, wenye pupa, wenye kujigamba, wenye kichwa kikubwa . . . wao watakuwa wasio na fadhili, wasio na huruma, wachongezi, wajeuri, na wakali; wao watachukia yaliyo mema; wao watakuwa wenye hila, bila hadhari, na wenye kujaa majivuno . . . Jitenge kabisa na watu wa jinsi hiyo.” (2 Timotheo 3:1-5, Today’s English Version) Ndiyo, ujeuri tunaouona leo ni utimizo wa unabii wa Biblia juu ya “siku za mwisho.”
Jambo jingine hufanya wakati huu hasa kuwa wenye jeuri. “Ole wa dunia na wa bahari,” yasema Biblia, “kwa sababu Ibilisi ameteremka kwenu, akiwa na hasira kubwa, akijua ana kipindi kifupi cha wakati.” (Ufunuo 12:12) Ibilisi na majeshi yake ya roho waovu wametupwa kutoka mbinguni na sasa wanaelekezea wanadamu makusudio yao maovu. Akiwa “mtawala wa mamlaka ya hewa,” Ibilisi huongoza kwa hila ile “roho ambayo sasa hutenda katika wana wa kutotii,” akifanya dunia iwe mahali panapozidi kuwa na ujeuri.—Waefeso 2:2.
Basi, twaweza kukabilianaje na “hewa” yenye ujeuri ya ulimwengu huu? Na twaweza kutatuaje kutoelewana bila kuwa wajeuri?
[Blabu katika ukurasa wa 3]
Watoto wengi sana hutendwa vibaya, kupigwapigwa, au kuuawa katika mojawapo ya mahali penye ujeuri mkubwa zaidi duniani—nyumbani!yy