Je, Krismasi Imempoteza Kristo?
“Sijaweza kamwe kukubaliana na zile shamrashamra za msimu wa Krismasi. Kwangu zimeonekana kuwa tofauti sana na maisha na mafundisho ya Yesu.”—Mohandas K. Gandhi.
WATU wengi wangempinga Gandhi kabisa. ‘Ati nini,’ huenda wakauliza, ‘je, kwa kweli mwanasiasa Mhindu angeweza kujua lolote juu ya sikukuu ya Kikristo?’ Hata hivyo, lazima ikubaliwe kwamba Krismasi imeenea ulimwenguni pote, ikipenya aina zote za tamaduni. Kila Desemba, sikukuu hiyo huonekana kuwa imeathiri tamaduni zote.
Kwa kielelezo, watu wa Asia wapatao milioni 145 husherehekea Krismasi, watu milioni 40 zaidi ya idadi ya miaka kumi iliyopita. Na ikiwa kwa kutumia neno “shamrashamra” Gandhi alimaanisha upande usio wa kidini wa Krismasi ya kisasa, ununuaji vitu wenye kichaa ambao sisi sote huuona, ni vigumu kukana kwamba upande huo wa sherehe hiyo mara nyingi huwa wenye kutokeza zaidi. Gazeti Asiaweek lataarifu hivi: “Krismasi katika Asia—kuanzia zile taa za kusherehekea katika Hong Kong hadi ile mivinje mikubwa ya Krismasi kwenye sebule za hoteli katika Beijing kufikia hori iliyoko mjini Singapore—hasa ni pindi isiyo ya kidini, (pindi ya biashara).”
Je, sherehe ya siku hizi ya Krismasi imekosa kumhusisha Kristo? Kirasmi, Desemba 25 imeadhimishwa tangu karne ya nne W.K., wakati Kanisa Katoliki lilipoiteua siku hiyo iwe ya kuadhimisha kidini kuzaliwa kwa Yesu. Lakini kulingana na kura ya maoni ya juzi katika Marekani, asilimia 33 pekee ya waliotoa maoni yao ndio walioonelea kuwa kuzaliwa kwa Kristo ndilo jambo la maana sana kuhusu Krismasi.
Wewe waonaje? Je, wakati fulani unahisi kuwa katika kule kutangaza bidhaa kusikokoma, kulazimishwa kununua zawadi, kupamba mivinje, kupanga na kushiriki karamu, kupeleka kadi za Krismasi—Yesu kwa njia fulani amesahauliwa?
Wengi wanaonelea kwamba njia moja ya kumshirikisha Kristo tena katika Krismasi ni kupitia kuonyesha Mandhari ya Kuzaliwa kwake, au hori. Yaelekea umeona vikusanyiko hivi vya mifano, vikiwakilisha kitoto kichanga Yesu kikiwa horini kimezungukwa na Maria, Yosefu, wachungaji, “wanaume watatu wenye hekima,” ama “wafalme watatu,” wanyama kadhaa wa kufugwa, na watazamaji fulani. Mara nyingi inafikiriwa kuwa hori hizi huwakumbusha watu maana halisi ya Krismasi. Kulingana na U.S. Catholic, “hori hutokeza taswira inayoeleweka zaidi kuliko vile gospeli yoyote ile ingefanya, hata ingawa hiyo pia hukazia wazo la kwamba masimulizi haya si ya kihistoria.”
Ingawa hivyo, ni jinsi gani Mandhari ya Kuzaliwa kwa Yesu ingedokeza kwamba masimulizi ya Gospeli katika Biblia si ya kihistoria? Naam, lazima ikubaliwe kwamba mifano midogo ya kuchongwa iliyopakwa rangi kwa umaridadi huongeza hisia changamfu za hekaya au hadithi iliyotungwa kuhusu kuzaliwa kwa Kristo. Mandhari ya Kuzaliwa kwa Yesu, ambayo mtawa fulani katika karne ya 13 aliifanya kupendwa na wengi, hapo awali ilikuwa jambo lisilo na mapambo mengi. Siku hizi, kama tu mambo mengine mengi sana yanayoshirikishwa na sikukuu hii, Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu zimegeuzwa kuwa biashara kubwa. Katika Naples, nchini Italia, maduka mengi huuza sanamu za Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu, ama presepi, mwaka mzima. Baadhi ya sanamu zinazopendwa zaidi huwakilisha, si watu kutoka masimulizi ya Gospeli, bali watu maarufu wa siku hizi, kama vile Princess Diana, Mama Teresa, na msanii wa nguo Gianni Versace. Kwingineko, presepi hufanyizwa kwa chokoleti, tambi, na hata kauri pia. Basi unaweza kuona ni kwa nini ni vigumu kuelewa historia kupitia maonyesho kama haya.
Ni jinsi gani, basi, hizo Mandhari za Kuzaliwa kwa Yesu zingeweza kutokeza “taswira inayoeleweka zaidi kuliko vile gospeli yoyote ile ingefanya”? Je, masimulizi ya Gospeli si ya kihistoria kwelikweli? Hata watilia-shaka walio sugu lazima wakubali kwamba Yesu alikuwa mtu halisi, aliyekuwepo kikweli. Hivyo ni lazima wakati fulani alikuwa mtoto halisi, aliyezaliwa mahali hususa. Lazima kuwe na njia bora zaidi ya kupata taswira inayoeleweka zaidi ya matukio yanayohusiana na kuzaliwa kwake kuliko tu kukodolea macho Mandhari ya Kuzaliwa kwake!
Kwa hakika, ipo. Wanahistoria wawili waliandika masimulizi mbalimbali ya kuzaliwa kwa Yesu. Ikiwa pengine unaona kwamba Kristo husahauliwa hasa wakati wa Krismasi, kwa nini usiyachunguze masimulizi haya wewe mwenyewe? Humo utapata, si hekaya ama ngano bandia, bali masimulizi yenye kuvutia sana—masimulizi halisi ya kuzaliwa kwa Kristo.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Mpaka kwenye ukurasa wa 3-6, 8, na 9: Fifty Years of Soviet Art