Krismasi (Noël) Ilianza Zamani Sana
Si kwamba tu sasa inaenea ulimwenguni pote; vilevile ilianza zamani za kale sana
UNASUKUMWA huku na huku na kundi la watu ambalo limejaa katika duka. Kwa mara ya mia tano katika majuma ya karibuni wasikia kwenye vikuza sauti mdundo wa sauti za namna fulani ya wimbo wa Krismasi. Sauti yake inapatana vizuri sana na sauti ya fedha zikiingia katika masanduku ya kuwekea fedha dukani. Baba Krismasi yuko pale amevaa mavazi yake mekundu na ndevu nyeupe, akitoa zawadi kwa watoto ambao wamepanga mstari ili wakalie mapajani pake. Ishara za “Merry Christmas” zilizotapakaa zimeandikwa katika Kiingereza, walakini namna ya sauti zinazokuzunguka ni ya lugha ya kigeni. Unashangaa uko wapi.
Uko Japan, nchi ambayo idadi yake ya dini za Kikristo zikiunganishwa ni ndogo zaidi ya moja kwa mia. Tangu Vita ya Pili ya Ulimwengu Krismasi imekuwa sherehe kubwa humo.
Hivi karibuni, Wabudha wa Japan walisherehekea Krismasi kwa kupamba jengo lenye orofa 53 katika Tokyo kwa mianga yenye rangi ikiangaza namna ya mfano wa bikira Mariamu.
Juu ya Japan, gazeti la Newsweek lilitaja hivi wakati fulani uliopita:
“Sasa Krismasi ndiyo sikukuu kubwa kupita zote mwakani. . . . Siku za mwisho za Desemba zinapita katika mfululizo wa karamu nyumbani, maafisini, viwandani, na katika vilabu vya usiku, na kuliacha taifa likiwa na uchovu mkubwa sana wakati wa kuanza mwaka mpya.”
Miti ya Krismasi mingi mno kama msitu inapamba maduka. Kadi (vipande vya karatasi) za Krismasi zinaonyeshwa. Mababa Krismasi wako kila mahali, wengi wao wakiwa wanawake. Msimamizi mmoja wa duka alisema hivi: “Tumepata kuona kwamba wanawake wanapata kutumainiwa na watoto zaidi, sana sana wale wadogo.” Vile-vile wana sifa kwa washerehekeaji wenye kutumia fedha nyingi zaidi, kwa maana akina Mama Krismasi wasichana wenye sura nzuri wako mikahawani nao akina Mama Krismasi walio uchi wako vilabuni vya usiku.
HONG KONG, SINGAPORE, KOREA KUSINI, HAWAII, AFRIKA
Katika Hong Kong 90 kwa mia ya Wachina si Wakristo, walakini kufikia katikati ya Oktoba wilaya za biashara zinapambwa kwa mapambo ya Krismasi na kujawa na wanunuzi. Wanaume wanene, wenye ndevu nyeupe, wenye kuvaa suti nyekundu wako kila mahali, wakiwa wameshika watoto mapajani pao na kutoa zawadi. Maduka ya Wakomunisti ndiyo ya kwanza kuuza bidhaa za Krismasi.
Katika Singapore, miezi miwili kabla ya Krismasi ishara kubwa madukani zatangaza “Merry Christmas and Happy New Year!” (“Krismasi Yenye Shangwe na Mwaka Mpya Wenye Furaha!”) Michoro yamwonyesha Baba Krismasi na kuzaliwa kwa Yesu. Mababa Krismasi walio hai wakiwa wamevalia mavazi mekundu wanagawia watoto peremende.
Krismasi ni mojawapo ya sikukuu kubwa zaidi katika Korea ya Kusini, kwa wasioamini na vilevile kwa 14 kwa mia ya idadi ya watu wanaodai kuwa Wakristo. Vilabu vya usiku vinajaa usiku unaotangulia Krismasi, walakini karamu za jamaa ndizo za kawaida zaidi. Wanunuzi wanajaa kwenye maduka ili kununua zawadi. Mababa Krismasi wapo, na vilevile miti ya Krismasi.
Katika Hawaii Wabudha wanapelekeana zawadi za Krismasi, wanapamba nyumba zao kwa ajili ya sikukuu hiyo na kufanya karamu za jamaa.
Waafrika wengi katika Kenya huiona Krismasi kuwa wakati wa kusherehekea. Siku ya Krismasi wanasherehekea, wanakunywa pombe, wanapelekeana zawadi na kucheza ngoma. Wanajifanya kana kwamba wako na wazimu kwa kupiga na kucheza ngoma usiku kucha. Nyingi za nyumba zao zina miti ya Krismasi iliyopambwa kwa maua. Mahali pa misunobari ya kawaida wanatumia migomba ya ndizi au miti ambayo wakati wote ni ya kijani kibichi kama vile mierezi.
KRISMASI ILIYOFANYWA KUWA YA KIBIASHARA YAFIKA KWENYE NCHI ZA KIKOMUNISTI NA KIYAHUDI
Msafiri mmoja alisema hivi aliporudi nchini United States:
“Hivi karibuni tulipokuwa tukipitia sehemu za faragha za Kremlin, kiongozi wetu alionyesha kwa kidole jumba la michezo la kisasa la Bolshio na kusema, ‘Pale ndipo tunapoweka mwerezi mkubwa na kufanyia sherehe zetu za Krismasi za kila mwaka, tofauti peke yake ikiwa kwamba tunaifanya Januari 7, nanyi Desemba 25’ Katika Berlin ya Mashariki wakati wa Desemba iliyopita, nilishangaa kuona katika sehemu za watu wote miti mikubwa sana ya Krismasi iliyopambwa?’
Kwa ujumla Wayahudi wanamkataa Yesu Kristo, walakini wengi wao wanapamba sehemu zao za biashara kwa mapambo ya Krismasi, wanajiunga katika karamu za maafisini na kutuma kadi za salamu za sikukuu. Kwa habari ya Hanukkah (sikukuu ya Wayahudi ya siku nane inayoanzia Desemba 25), Rabi Morris Kertzer anasema hivi katika kitabu chake What Is a Jew?:
“Wayahudi Waamerika wamegeuza sherehe hii ndogo kuwa kubwa sana sana kwa sababu mila zake za kitamaduni zinafanana sana na sherehe za Krismasi ambazo hufanywa wakati ule ule. . . Katika kuiga hali iliyopo kwa ujumla katika Desemba, Hanukkah sasa inasherehekewa kwa kupelekeana zawadi na wote vijana kwa wazee, na nyumba zinapambwa kimaridadi kwa ishara za Hanukkah.”
Msimamizi wa hapo zamani wa chama cha Umoja wa Makundi ya Kiebrania ya Amerika aliuliza hivi: “Je! si Krismasi imekuwa sikukuu ya ulimwenguni pote inayosherehekewa na wote?” Baada ya kutaja namna Wayahudi wanavyovutwa kwenye sherehe za kutoa zawadi na kufanya karamu za Krismasi kwa shangwe, alisema hivi:
“Kama ningalikuwa mhudumu Mkristo mahali pa mwalimu Myahudi, hakuna jambo ambalo ningalisikitikia zaidi, na kuchukia kabisa, kama kugeuzwa huku kunakofanywa kwa wingi sana na maelfu ya Wakristo, na Wayahudi fulani, pamoja na wengi wasioamini dini ya Kiyahudi au Ukristo, . . . Kwa siku takatifu kama hiyo kuwa sikukuu ya kipagani, isiyo na maana yo yote ya kiroho.”
KRISMASI 1LIANZA ZAMANI ZA KALE ZAIDI
“Mrudisheni Kristo katika Krismasi!” Hiki ndicho kilio kinachosikiwa mara nyingi na wengi ambao kwa unyofu wanataka kumheshimu Kristo Yesu wakati wa kusherehekea siku ya kila mwaka ya kuzaliwa kwake. Wao wanakosa kufahamu kwamba Kristo Yesu hakuwa katika Krismasi hata kidogo. Kanisa la Puritan la Uingereza si kwamba tu lilipuza Krismasi; vilevile lilishtaki watu walioasi ambao walithubutu kuisherehekea kisiri! Wakati wa mapema wa New England kusherehekea Krismasi kulikatazwa na sheria kwa sababu Wapuritani walikasirishwa na vyanzo visivyo vya Kikristo vya mila na mapokeo yake.
Warumi na Wagiriki wa kale pamoja walisherehekea kuzaliwa kwa jua lisiloshindwa Desemba 25. Sherehe hiyo inarudi nyuma mpaka Babeli. Nimrodi alifanywa kuwa mungu-jua. Alipouawa na adui zake, alifananishwa na gogo, na alipozaliwa tena alifananishwa na mti wenye majani mabichi. Baada ya kueleza hayo, kitabu cha Dakt. Alexander Hislop The Two Babylons kinasema hivi:
“Sasa Gogo la Yule ni mwili uliokufa wa Nimrodi, aliyefanywa kuwa mungu-jua, walakini aliyeuawa na adui zake; mti wa Krismasi ni Nimrodi—mungu aliyeuawa ambaye amepata kuwa hai tena.”
Gogo hilo la Yule lilikuwa likichomwa katika usiku wa Desemba 24; kufikia asubuhi iliyofuata mahali pake palikuwa pamechukuliwa na mti wenye majani mabichi. Dakt. Hislop anaonyesha chanzo cha kipagani cha mila nyingine za wakati wa Krismasi—mishumaa, kufanya karamu, bakuli zenye mvinyo, kupelekeana zawadi na nyinginezo.—kur. 91-103.
Yesu hakuzaliwa Desemba 25, bali wakati wa vuli wakati wachungaji walipokuwa pamoja na makundi yao mashambani. Zaidi ya hayo, Wakristo hawakuwa wakisherehekea kuzaliwa kwake, bali waliamriwa wawe wakiadhimisha kifo chake kwa Chakula cha Bwana cha Jioni, ambacho alianzisha yeye mwenyewe usiku wa kusalitiwa kwake. “Fanyeni hivi,” akasema, “kwa ukumbusho wangu.”—Luka 22:19, 20.
Krismasi haihusiani hata kidogo na Kristo. Inajaa ibada ya mashetani. Hakuna wo wote wa uhakika huu utakaoimaliza. Inafanikiwa na kuenea pote kwa sababu ni ya kibiashara. Mababa Krismasi na Watakatifu Nickolas wengi zaidi na zaidi wanakuwa “Mtakatifu Nipe.”