Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 12/15 kur. 4-8
  • Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Fungu la Kupeana Zawadi
  • Asili ya Krismasi
  • Kuifahamu Krismasi Kindani Kupitia Maandiko
  • Krismasi—Kwa Nini Inapendwa Sana Katika Japani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Je! Ni Lazima Wewe Usherehekee Krismasi?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Ni Nini Kilichoipata Krismasi ya Kidesturi?
    Amkeni!—1993
  • Mizizi ya Krismasi ya Kisasa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 12/15 kur. 4-8

Krismasi—Mbona Husherehekewa Hata Mashariki?

KUNA imani ya zamani katika Mashariki inayotukumbusha Baba Krismasi. Hiyo ni imani ya Wakorea katika mungu aitwaye Chowangshin, na baadhi ya Wachina na Wajapani wana imani kama hiyo.

Chowangshin alionwa kuwa mungu aliyesimamia mambo ya jikoni, mungu wa moto aliyehusiana na ibada ya kale ya moto ya Wakorea. (Zamani za kale, Wakorea walibeba kwa uangalifu makaa yenye kuwaka, wakihakikisha kwamba hayakuzimika.) Iliaminika kwamba mungu huyo alichunguza mwenendo wa washiriki wa familia kwa mwaka mmoja, kisha akapaa mbinguni kupitia meko na dohani ya jikoni.

Inadhaniwa kwamba Chowangshin alipiga ripoti kwa mfalme wa mbinguni tarehe 23 mwezi-luna wa Desemba. Alitarajiwa kurudi mwishoni mwa mwaka kupitia dohani na meko, akileta zawadi na adhabu kulingana na mwenendo wa kila mmoja. Siku aliporudi, washiriki wa familia walipaswa kuwasha mishumaa jikoni na penginepo katika nyumba. Picha za mungu huyo wa jikoni zinafanana na Baba Krismasi kwa njia nyingine—alionyeshwa akiwa na nguo nyekundu! Ilikuwa ni desturi kwa binti-mkwe kushona soksi nyekundu kulingana na utamaduni wa Wakorea, na kumpa mama-mkwe wake mwanzoni mwa majira ya baridi kali. Alifanya hivyo ili kuonyesha kwamba alitaka mama-mkwe aishi muda mrefu, kwa kuwa siku zinakuwa ndefu zaidi baada ya tarehe hiyo.

Je, huoni ufanani fulani kati ya mambo ambayo tayari yametajwa na Krismasi? Kuna hadithi na desturi zinazofanana: dohani, mishumaa, kupeana zawadi, soksi, mzee mwenye nguo nyekundu, na tarehe. Hata hivyo, si mambo hayo yenye kufanana pekee ambayo yamefanya Krismasi ikubaliwe kwa urahisi nchini Korea. Imani katika Chowangshin ilikuwa karibu kutoweka kabisa wakati Krismasi ilipoanza kusherehekewa nchini Korea. Kwa kweli, leo Wakorea wengi hawajui kwamba imani kama hiyo ilikuwako.

Hata hivyo, jambo hilo laonyesha jinsi desturi zinazohusiana na mwanzo wa baridi kali na mwisho wa mwaka zilivyoenea kwa njia mbalimbali ulimwenguni kote. Katika karne ya nne W.K., kanisa mashuhuri katika Milki ya Roma lilibadili jina la Saturnalia, msherehekeo wa kipagani wa Roma wa kuzaliwa kwa mungu-jua, na kuufanya sehemu ya Krismasi. Sherehe ya Krismasi ilifufua tu desturi za Korea zikiwa na jina tofauti. Jambo hilo liliwezekanaje?

Fungu la Kupeana Zawadi

Desturi ya kutoa zawadi haikutoweka kamwe. Kwa muda mrefu, Wakorea wamefurahia kupeana zawadi. Hiyo ikawa sababu moja iliyofanya sherehe ya Krismasi ipendwe sana Korea.

Baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, wanajeshi wa Marekani nchini Korea, ambao walitaka kuimarisha uhusiano wao na watu, walikutana makanisani ili kuwapa zawadi na misaada. Walifanya hivyo hasa Siku ya Krismasi. Watoto wengi walienda makanisani kwa sababu ya udadisi tu, na huko wakapewa zawadi za chokoleti kwa mara ya kwanza. Kama uwezavyo kuona, wengi wao walikuwa wakitazamia kwa hamu Krismasi iliyofuata.

Kwa watoto kama hao, Baba Krismasi alikuwa mwanajeshi Mmarekani aliyevaa kofia nyekundu. Andiko la Mithali 19:6 lasema: “Na kila mtu ni rafiki yake atoaye tunu.” Naam, kupeana zawadi kukawa na matokeo mazuri. Lakini kama uwezavyo kuona kutokana na mstari huo, zawadi kama hizo si uhakikisho wa urafiki wenye kudumu. Hata nchini Korea, watu wengi walienda kanisa walipokuwa wadogo ili kula chokoleti tu. Lakini hawakusahau Krismasi. Pamoja na ukuzi wa haraka wa uchumi wa Korea, biashara pia ilikua, na kupeana zawadi wakati wa Krismasi kukawa njia rahisi ya kuongeza uuzaji wa bidhaa. Biashara zilitumia Krismasi vibaya ili kuongeza faida.

Mambo hayo yanakupa ufahamu wa kindani kuhusu Krismasi katika nchi za Mashariki leo. Bidhaa nyingi hutengenezwa zikikusudiwa kuuzwa wakati wa zile shamrashamra za Krismasi. Mipango ya matangazo ya bidhaa huanza katikati ya msimu wa kiangazi. Uuzaji hufikia upeo mwishoni mwa mwaka, kutokana na ununuzi wa zawadi za Krismasi, kadi, na rekodi za muziki. Kwani matangazo ya bidhaa yanaweza kufanya kijana wa kawaida ahuzunike ikiwa yeye anakaa nyumbani asipokee zawadi zozote katika Mkesha wa Krismasi!

Siku ya Krismasi ikaribiapo, watu hujazana madukani jijini Seoul wakinunua zawadi, na hivyo ndivyo inavyokuwa katika majiji mengine ya Mashariki. Kuna msongamano wa magari. Wateja humiminika kwenye hoteli, maeneo ya biashara, mikahawa, na klabu za usiku. Sherehe zenye kelele za ulevi—kuimba kwa sauti kubwa—huweza kusikika. Katika Mkesha wa Krismasi, hata wanaume na wanawake walevi huonekana wakitembea kwenye barabara zilizojaa takataka.

Hivyo ndivyo Krismasi inavyokuwa. Krismasi katika nchi za Mashariki haisherehekewi tu na wale wanaodai kuwa Wakristo peke yao. Ni wazi kwamba nchini Korea kama kwingineko, biashara ndizo hunufaika zaidi kutokana na sikukuu hiyo ya Jumuiya ya Wakristo. Je, ni biashara pekee inayofanya Krismasi kuwa tofauti kabisa na roho ya Kristo? Wakristo wa kweli wapaswa kuchunguza zaidi suala hili zito linalohusika.

Asili ya Krismasi

Mnyama mkali ambaye amefungiwa kizimbani katika bustani ya wanyama bado ni mnyama mkali. Na lingekuwa kosa kubwa sana kuamini kwamba mnyama huyo amekuwa mpole kwa sababu amekuwa kizimbani kwa muda na aonekana kufurahi pamoja na watoto wake. Huenda ukawa umesikia ripoti juu ya kushambuliwa kwa wafanyakazi wa bustani za wanyama.

Kwa njia fulani tunaweza kulinganisha mnyama huyo na sherehe ya Krismasi. Mwanzoni sherehe hiyo ilikuwa “mnyama” ambaye hakuwa sehemu ya Ukristo. Chini ya kichwa kidogo “Relation to the Roman Saturnalia” (Uhusiano na Saturnalia ya Roma), kichapo The Christian Encyclopedia (cha Kikorea)a chasema hivi kuhusu Krismasi:

“Sikukuu za kipagani za Saturnalia na Brumalia zilikuwa zimetia mizizi sana katika desturi zilizopendwa hivi kwamba uvutano wa Kikristo haungeweza kuzitangua. Jambo la kwamba maliki Konstantino alitambua Jumapili (siku ya Phœbus na Mithras na vilevile Siku ya Bwana) . . . huenda lilifanya Wakristo wa karne ya nne waone kwamba inafaa kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na siku ya kuzaliwa kwa jua kwa wakati mmoja. Msherehekeo huo wa kipagani wenye kelele nyingi na kujifurahisha ulipendwa sana hivi kwamba Wakristo walifurahi kupata sababu ya kuendelea kuusherehekea bila kubadili hali yake au jinsi ulivyosherehekewa.”

Je, unafikiri kwamba jambo kama hilo lingeweza kutukia bila upinzani wowote? Ensaiklopedia hiyohiyo yasema: “Wahubiri Wakristo wa Magharibi na wa Mashariki ya Karibu walipinga jinsi siku ya kuzaliwa kwa Kristo ilivyosherehekewa isivyofaa, huku Wakristo wa Mesopotamia wakiwashutumu ndugu zao wa Magharibi kuwa waabudu sanamu na waabudu jua kwa kukubali msherehekeo huo wa kipagani uwe wa Kikristo.” Ni kweli kwamba kulikuwa na makosa fulani tangu mwanzo. “Hata hivyo, msherehekeo huo ulikubaliwa haraka, hatimaye ukawa imara sana hivi kwamba hata yale marekebisho ya Kiprotestanti ya karne ya kumi na sita hayakuweza kuuondoa,” ensaiklopedia hiyo yasema.

Ndiyo, msherehekeo wa mungu-jua, ambao haukuwa sehemu ya Ukristo wa kweli, ukakubaliwa katika kanisa mashuhuri wakati huo. Ukapewa jina tofauti—lakini sifa zake za kipagani zikabaki vilevile. Nao ukachangia kuingiza upagani katika makanisa yanayodai kuwa ya Kikristo, na pia kuchafua hali ya kiroho ya watu mmoja-mmoja. Historia yathibitisha kwamba Jumuiya ya Wakristo ilipokua, mtazamo wa awali wa “penda adui zako” ulibadilika ukawa vita vyenye jeuri na kushuka kwa maadili.

Baada ya muda, ikawa wazi kwamba licha ya jina lake bandia, Krismasi ilidhihirisha asili yake ya kipagani kwa kuwa yenye kelele za ulevi, kunywa kupita kiasi, kujifurahisha, kucheza dansi, kupeana zawadi, na kupamba nyumba kwa matawi ya miti ya kijani kibichi. Ili kufikia lengo kuu la kibiashara—kuuza zaidi—Krismasi imetumiwa kujinufaisha kwa kila njia iwezekanayo. Vyombo vya habari huisifu; umma nao huifurahia sana. Duka moja katika eneo la biashara la Seoul, ambalo huuza chupi pekee, lilizungumziwa kwenye habari za televisheni kwa kuonyesha kwenye madirisha yake mti wa Krismasi ukiwa umepambwa kwa chupi pekee. Shamrashamra za Krismasi zilikuwa dhahiri, lakini hakukuwepo ishara yoyote ya kumkaribisha Kristo.

Kuifahamu Krismasi Kindani Kupitia Maandiko

Tunajifunza nini kutokana na historia hiyo juu ya asili na ukuzi wa Krismasi? Shati au blauzi isipofungwa vifungo vizuri kuanzia juu, njia pekee ya kurekebisha hali hiyo ni kuanza tena. Sivyo? Licha ya ukweli huo, wengine hutoa hoja kwamba Krismasi imekubaliwa na Jumuiya ya Wakristo japo asili yake ni ibada ya jua. Hivyo wao huona kwamba sikukuu hiyo imetakaswa kuwa siku ya kuzaliwa kwa Kristo ikiwa na maana tofauti.

Tunaweza kujifunza somo lenye thamani kutokana na tukio la kihistoria lililotokea katika nchi ya Yuda ya kale. Katika mwaka wa 612 K.W.K., Wayudea walianzisha ibada ya kipagani ya jua katika hekalu la Yerusalemu. Je, ibada hiyo ya sanamu ilikuwa imetakaswa kwa kuwa ilifanyiwa mahali palipotengwa kwa ajili ya ibada safi ya Yehova Mungu? Mwandishi wa Biblia, Ezekieli aliandika hivi kuhusu ibada ya jua iliyokuwa ikifanywa kwenye hekalu la Yerusalemu: “Tazama, mlangoni pa hekalu la BWANA, kati ya ukumbi na madhabahu, walikuwako watu kama ishirini na watano, . . . nyuso zao zimeelekea upande wa mashariki, nao wanaliabudu jua, kwa kuuelekea upande wa mashariki. Basi, akaniambia, Umeyaona haya, Ee mwanadamu? Je! ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda, wayafanye machukizo wanayoyafanya hapa? kwa maana wameijaza nchi hii udhalimu, tena wamerejea nyuma ili kunikasirisha; na, tazama, wanaliweka tawi puani.”—Ezekieli 8:16, 17.

Naam, badala ya kutakaswa, aina hiyo ya ibada ilihatarisha hekalu lote. Mazoea hayo yalienea kote katika Yuda na kusababisha kuenea kwa jeuri na kushuka kwa maadili katika nchi hiyo. Ndivyo hali ilivyo katika Jumuiya ya Wakristo, ambako mazoea ambayo asili yake ni ibada ya jua ya Saturnalia hudhihirika wazi wakati wa Krismasi. Jambo la maana ni kwamba miaka kadhaa baada ya Ezekieli kupata ono hilo, Yerusalemu lilihukumiwa na Mungu—likaharibiwa na Wababiloni.—2 Mambo ya Nyakati 36:15-20.

Huenda ikawa ulichekeshwa na maelezo ya yule msomi kutoka Korea kumhusu Yesu, ambayo yalisimuliwa katika makala iliyotangulia. Lakini ukweli ni kwamba alikuwa na sababu nzuri ya kutoa maelezo kama hayo kwa kuwa yeye hakuwa na ujuzi sahihi kumhusu Kristo. Ufafanuzi huo waweza kufanya watu ambao husherehekea Krismasi wafikiri kwa uzito. Kwa nini? Kwa sababu Krismasi haionyeshi Kristo kwa usahihi. Bila shaka, Krismasi huficha vile alivyo sasa. Yesu si mtoto mchanga katika hori.

Biblia hukazia tena na tena kwamba Yesu sasa ni Mesiya, Mfalme mwenye nguvu wa Ufalme wa kimbingu wa Mungu. (Ufunuo 11:15) Yeye yu tayari kukomesha umaskini na taabu ambazo watu fulani huzikumbuka wakati wa msimu wa Krismasi wanapotoa michango kwa mashirika ya kutoa misaada.

Kwa wazi, Krismasi haijanufaisha nchi za Jumuiya ya Wakristo wala nchi nyinginezo, kutia ndani zile za Mashariki. Badala yake, imekengeusha watu wasizingatie ule ujumbe wa kweli wa Kikristo juu ya Ufalme wa Mungu na mwisho wa mfumo mwovu wa sasa. (Mathayo 24:14) Twakuomba uulize Mashahidi wa Yehova wakueleze jinsi mwisho huo utakavyokuja. Nawe waweza kujifunza kwao kuhusu baraka zenye kudumu ambazo baadaye zitakuwepo duniani, chini ya mwelekezo wa Ufalme wa Mungu na Mfalme anayetawala, Yesu Kristo.—Ufunuo 21:3, 4.

[Maelezo ya Chini]

a Kinachotegemea kichapo The New Schaff-Herzog Encyclopedia of Religious Knowledge.

[Blabu katika ukurasa wa 6]

Krismasi ilisaidia kuingiza upagani katika makanisa yanayodai kuwa ya Kikristo

[Picha katika ukurasa wa 5]

Watoto wengi walienda makanisani kwa sababu ya udadisi tu na kupokea zawadi za chokoleti. Kisha kutazamia kwa hamu Krismasi iliyofuata

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mkesha wa Krismasi katika eneo la biashara la Seoul, Korea

[Picha katika ukurasa wa 8]

Kristo si mtoto mchanga tena bali ni Mfalme mwenye nguvu wa Ufalme wa Mungu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki