Jerome—Mtangulizi Mwenye Kubishaniwa Katika Utafsiri wa Biblia
APRILI 8, 1546, Baraza la Trent lilitoa agizo kwamba Vulgate ya Kilatini “imeidhinishwa na Kanisa [Katoliki] . . . na kwamba yeyote asithubutu kuikataa kwa kisingizio chochote kile.” Ingawa Vulgate ilikamilishwa miaka elfu moja mapema, tafsiri hiyo na vilevile mtafsiri wake, Jerome, alikuwa kitovu cha ubishi kwa muda mrefu. Jerome alikuwa nani? Kwa nini yeye na tafsiri yake ya Biblia vilisababisha ubishi? Maandishi yake yanaathirije kazi ya kutafsiri Biblia leo?
Asitawi Kuwa Msomi
Jina la Kilatini la Jerome lilikuwa Eusebius Hieronymus. Alizaliwa karibu mwaka wa 346 W.K. katika mji ulioitwa Stridon, katika mkoa wa Roma wa Dalmatia, karibu na mpaka wa kisasa kati ya Italia na Slovenia.a Wazazi wake walikuwa na utajiri wa kadiri, naye alijua ubora wa pesa akiwa mchanga, akasomea mjini Roma alikofundishwa na mwanasarufi maarufu aitwaye Donatus. Jerome alithibitika kuwa mwanafunzi mwenye kipawa katika sarufi, ufasaha wa kusema, na falsafa. Wakati huo alianza kujifunza Kigiriki pia.
Baada ya kuondoka Roma mwaka wa 366 W.K., Jerome alizurura huku na huku, na hatimaye akaenda Aquileia, nchini Italia, ambako alijulishwa juu ya dhana inayohusu maisha ya kujinyima raha. Kwa kuvutiwa na maoni haya ya kujinyima sana, yeye na kikundi cha marafiki wake walitumia miaka kadhaa iliyofuata wakijizoeza njia ya maisha ya kujinyima raha.
Mnamo mwaka wa 373 W.K., mvurugo fulani usiojulikana ulikivunja kikundi hicho. Akiwa amevunjika moyo, Jerome alifunga safari ndefu kuelekea upande wa mashariki ng’ambo ya Bithinia, Galatia, na Kilikia na hatimaye akafika Antiokia ya Siria.
Hiyo safari ndefu iliharibu afya yake. Akiwa ameishiwa nguvu kabisa na afya yake imeharibika, Jerome karibu afe kutokana na homa. “Aha! laiti Bwana Yesu Kristo angenisafirisha kwa ghafula hadi kwako,” akasema, akimwandikia rafiki yake. “Mwili wangu dhaifu, ambao ni dhaifu hata niwapo mwenye afya, umeharibika kabisa.”
Punde si punde, Jerome akakabili tatizo jingine—la kiroho—kana kwamba ugonjwa, upweke, na pambano katika akili zake havikutosha. Katika ndoto alijiona “akiburutwa kuelekea kiti cha hukumu” cha Mungu. Alipoombwa ajitambulishe, Jerome akajibu: “Mimi ni Mkristo.” Lakini yule aliyekuwa msimamizi akajibu vikali hivi: “Wewe wasema uwongo, wewe ni mfuasi wa Cicero na wala si mfuasi wa Kristo.”
Hadi kufikia wakati huo tamaa ya Jerome ya kupata elimu ilikazia hasa kujifunza maandishi bora ya kipagani badala ya kukazia Neno la Mungu. “Niliteswa,” akasema, “na moto wa dhamiri.” Akitumaini kurekebisha mambo, Jerome aliapa ndotoni hivi: “Bwana, ikiwa kwa vyovyote nitamiliki tena vitabu vya kilimwengu, au nikivisoma tena kwa vyovyote, basi nitakuwa nimekukana Wewe.”
Baadaye, Jerome alibisha kwamba hakuwajibika kutimiza kiapo alichoapa akiwa ndotoni. Hata hivyo alijitolea kutimiza kiapo chake—angalau kwa kufuata kanuni ya kiapo hicho. Hivyo, Jerome akaondoka Antiokia, akajitenga na kukaa huko Chalcis, jiji lililoko katika jangwa la Siria. Akiwa anaishi maisha ya utawa, alivama sana katika kujifunza Biblia na fasihi za kitheolojia. Jerome akasema: “Nilivisoma vitabu vya Mungu kwa bidii kubwa zaidi kuliko ile niliyokuwa nayo nilipovisoma vitabu vya wanadamu.” Pia, alijifunza lahaja ya Kisiria ya mahali hapo na kuanza kujifunza Kiebrania kwa msaada wa Myahudi aliyegeuza imani akawa Mkristo.
Utume wa Papa
Baada ya miaka mitano hivi ya maisha ya utawa, Jerome alirudi Antiokia ili kuendeleza masomo yake. Hata hivyo, alipowasili huko, alikuta kanisa limegawanyika sana. Kwa kweli, alipokuwa angali jangwani, Jerome alimsihi Papa Damasus ampe ushauri, akisema: “Kanisa limegawanyika katika vikundi vitatu, na kila kimoja cha vikundi hivi kina hamu ya kunifanya nikiunge mkono.”
Baada ya muda, Jerome akaamua kujiunga na Paulinus, mmoja wa wanaume watatu aliyedai cheo cha askofu wa Antiokia. Jerome alikubali Paulinus amfanye kasisi kwa masharti mawili. Kwanza, alitaka awe huru kufuatilia tamaa zake za maisha ya utawa. Na pili, alisisitiza juu ya kutokuwa na majukumu yoyote ya kikuhani ya kuhudumia kanisa fulani hususa.
Mnamo mwaka wa 381 W.K., Jerome aliandamana na Paulinus kwenye Baraza la Konstantinopo na baada ya hapo wakaenda naye hadi Roma. Upesi Papa Damasus akatambua stadi za Jerome za usomi na lugha. Katika kipindi cha mwaka mmoja Jerome akapewa cheo chenye fahari kuu cha kuwa katibu muhtasi wa Damasus.
Akiwa katibu, Jerome hakuepuka ubishi. Kwa vyovyote, yaonekana alichochea ubishi huo. Kwa kielelezo, aliendelea kuishi maisha ya kujinyima raha akiwa ndani ya makao yenye anasa ya papa. Na zaidi, kwa kuendeleza maisha yake sahili na kushutumu vikali makasisi kwa kujiingiza mno katika mambo ya kilimwengu, Jerome akawa na maadui wengi.
Hata hivyo, licha ya wale waliomkashifu, Jerome alipokea utegemezo kamili wa Papa Damasus. Papa huyo alikuwa na sababu nzuri za kumtia moyo Jerome aendelee na uchunguzi wa Biblia. Wakati huo, kulikuwa na tafsiri nyingi za Biblia katika Kilatini zilizokuwa zikitumiwa. Nyingi ya hizo zilikuwa zimetafsiriwa bila uangalifu, nazo zilikuwa na makosa yenye kuonekana wazi. Hangaiko jingine alilokuwa nalo Damasus ni kwamba lugha ilikuwa ikiitenganisha milki ya Mashariki na ya Magharibi ya kanisa. Ni wachache waliokijua Kilatini upande wa Mashariki; na wachache hata zaidi upande wa Magharibi walikijua Kigiriki.
Hivyo basi, Papa Damasus alihangaikia sana kuwa na tafsiri ya Kilatini iliyosahihishwa ya Gospeli. Damasus alitaka tafsiri ambayo ingedhihirisha Kigiriki cha asili kwa usahihi, na bado iwe yenye ufasaha na kueleweka vizuri katika Kilatini. Jerome alikuwa mmoja wa wasomi wachache ambao wangetokeza tafsiri kama hiyo. Kwa vile alikuwa na ufasaha wa Kigiriki, Kilatini, na Kisiria na pia ujuzi wa kadiri wa Kiebrania, Jerome alistahili sana kupewa kazi hiyo. Basi Damasus alipompa utume, Jerome akaanza mradi ambao ungechukua zaidi ya miaka 20 iliyofuata ya maisha yake.
Ubishi Waongezeka
Ijapokuwa alizitafsiri Gospeli kwa haraka mno, Jerome alionyesha ustadi wa kisomi ulio wazi. Kwa kuzilinganisha hati zote za Kigiriki zilizopatikana wakati huo, alifanya masahihisho ya kimtindo na kimaana pia katika maandishi ya Kilatini, ili kuyafanya yapatane kwa ukaribu zaidi na maandishi ya Kigiriki.
Tafsiri ya Jerome ya zile Gospeli nne ilipokewa vyema kwa ujumla, kama zilivyopokelewa Zaburi alizofanyia marekebisho kwa Kilatini, marekebisho ambayo yalitegemea maandishi ya Kigiriki ya Septuagint. Hata hivyo, bado kulikuweko waliomchambua. “Viumbe fulani wa kudharauliwa,” akaandika Jerome, “walinishambulia kimakusudi kwa kudai kwamba nilijitahidi kusahihisha mafungu katika gospeli, kinyume cha amri ya wahenga na maoni ya ulimwengu wote.” Shutuma za hadharani kama hizo ziliongezeka baada ya kifo cha Papa Damasus katika mwaka wa 384 W.K. Kwa sababu uhusiano kati ya Jerome na papa mpya haukuwa mzuri, aliamua kuondoka Roma. Kwa mara nyingine tena, Jerome akaelekea mashariki.
Asitawi Kuwa Msomi wa Kiebrania
Katika mwaka wa 386 W.K., Jerome alikaa Bethlehemu, ambako aliishi muda wote uliobaki wa maisha yake. Aliandamana na kikundi kidogo cha wafuasi waaminifu-washikamanifu kwake, miongoni mwao akiwa Paula, mwanamke tajiri wa uzawa wa kiungwana kutoka Roma. Paula alikuwa ameikubali njia ya maisha ya kujinyima raha likiwa tokeo la mahubiri ya Jerome. Kwa kutumia pesa ambazo Paula alitoa, kao la watawa likajengwa chini ya mwelekezo wa Jerome. Hapo Jerome akafuatilia kazi yake ya kisomi, akamaliza kazi iliyo kubwa zaidi katika maisha yake.
Kuishi Palestina kulimpa Jerome fursa ya kuboresha uelewevu wa lugha ya Kiebrania. Aliwalipa wafunzi kadhaa Wayahudi ili wamsaidie kuyaelewa mambo magumu zaidi ya lugha hiyo. Hata hivyo, haikuwa rahisi ajapokuwa na mfunzi. Kuhusu mwalimu mmoja, Baraninas wa Tiberio, Jerome alisema: “Ilinitaabisha na kunigharimu sana kumshawishi Baraninas anifundishe usiku.” Ni kwa nini walijifunza usiku? Kwa sababu Baraninas aliyaogopa maoni ya jamii ya Wayahudi juu ya ushirikiano wake na “Mkristo”!
Katika siku ya Jerome, mara nyingi Wayahudi waliwadhihaki Wasio Wayahudi ambao walisema Kiebrania kwa sababu ya kushindwa kwao kutamka sauti za kooni vizuri. Na bado baada ya juhudi nyingi, Jerome akawa stadi wa sauti hizo. Pia, Jerome alitohoa maneno mengi sana ya Kiebrania kwa Kilatini. Hatua hii ilimsaidia kuyakumbuka maneno hayo na pia ilihifadhi matamshi ya Kiebrania cha wakati huo.
Ubishi Mkubwa Zaidi wa Jerome
Haijulikani Papa Damasus alitaka Jerome atafsiri kiasi gani cha Biblia. Lakini hakuna shaka juu ya jinsi Jerome alivyoliona jambo hilo. Jerome alimakinika sana na kujitolea. Tamaa yake kubwa ilikuwa kutokeza kifaa ambacho kingekuwa “msaada kwa Kanisa, kinachofaa vizazi vya baadaye.” Hivyo akaazimia kutokeza tafsiri iliyosahihishwa ya Biblia nzima ya Kilatini.
Ili kutafsiri Maandiko ya Kiebrania, Jerome alinuia kuitumia Septuagint ikiwa msingi wa tafsiri yake. Wengi waliiona tafsiri hiyo ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania, ambayo ilitafsiriwa mara ya kwanza katika karne ya tatu K.W.K., kuwa ilipuliziwa moja kwa moja na Mungu. Kwa hiyo, Septuagint ilienezwa sana miongoni mwa Wakristo waliosema Kigiriki wakati huo.
Hata hivyo, Jerome alipoendelea na kazi yake, alipata mambo yasiyopatana kati ya hati za Kigiriki, ambayo ni sawa na yale aliyopata katika hati za Kilatini. Jerome akavunjika moyo zaidi. Hatimaye, akakata kauli kwamba ili kutokeza tafsiri inayoweza kutumainiwa, lazima apuuze hati za Kigiriki, Septuagint ikiwa miongoni mwao, na aende moja kwa moja kwa maandishi-awali ya Kiebrania.
Uamuzi huo ulisababisha upinzani mkali. Baadhi ya watu wakamwita Jerome mpotoshaji wa maandiko, mwenye kumkufuru Mungu na mwenye kuacha mapokeo ya kanisa kwa kupendelea Wayahudi. Hata Augustine—mwanatheolojia mkuu wa kanisa wakati huo—alimsihi sana Jerome ayarudie maandishi ya Septuagint, akisema: “Ikiwa tafsiri yako itaanza kusomwa na wote katika makanisa mengi, hilo litakuwa jambo la kuhuzunisha sana kwa sababu, wakati wa kusoma Andiko, lazima tofauti zitatokea baina ya Makanisa ya Kilatini na Makanisa ya Kigiriki.”
Naam, hofu ya Augustine ilikuwa kwamba huenda kanisa lingegawanyika ikiwa makanisa ya Magharibi yangetumia maandishi ya Kilatini ya Jerome—yanayotegemea maandishi ya Kiebrania—huku makanisa ya Kigiriki ya Mashariki yakiwa yangali yanatumia tafsiri ya Septuagint.b Kwa kuongezea, Augustine alitoa maoni yenye mashaka juu ya kuiacha Septuagint kwa kupendelea tafsiri ambayo ni Jerome pekee angeweza kuitetea.
Jerome aliwajibuje wapinzani wote hao? Kama ilivyo kawaida yake, Jerome aliwapuuza wachambuzi wake. Aliendelea kutafsiri moja kwa moja kutoka kwa Kiebrania, na kufikia mwaka wa 405 W.K., akawa ameimaliza Biblia yake ya Kilatini. Miaka mingi baadaye tafsiri yake ikapewa jina Vulgate, linalorejezea tafsiri iliyopokewa na wengi (hilo neno la Kilatini vulgatus likimaanisha “kawaida, kinachopendwa na wengi”).
Matimizo ya Kudumu
Tafsiri ya Maandiko ya Kiebrania ya Jerome ilikuwa zaidi ya kuyarekebisha tu maandishi yaliyokuwepo. Hiyo ilibadili mtindo wa kujifunza na kutafsiri Biblia wa vizazi vya baadaye. “Hiyo Vulgate,” akasema mwanahistoria Will Durant, “bado ndiyo utimizo mkuu na wenye kuvutia zaidi wa kifasihi wa karne ya nne.”
Ingawa Jerome alikuwa mtu mwenye kejeli na mgomvi, alifaulu akiwa peke yake kuurudisha tena uchunguzi wa Biblia hadi kwenye maandishi yaliyopuliziwa ya Kiebrania. Alichunguza kwa makini na kulinganisha hati za kale za Biblia za Kiebrania na Kigiriki ambazo hatuwezi kuzipata leo. Pia, maandishi yake yalitangulia yale ya Wamasora Wayahudi. Hivyo, Vulgate ni marejeo yenye mafaa sana ya kulinganishia tafsiri nyingine za maandishi ya Biblia.
Bila kupuuza tabia ya Jerome yenye kupita kiasi au maoni yake ya kidini, wapendao Neno la Mungu waweza kuthamini juhudi zenye bidii za huyu mtangulizi mwenye kubishaniwa katika utafsiri wa Biblia. Na ni kweli, Jerome alifikia mradi wake—alitokeza kitu “kinachofaa vizazi vya baadaye.”
[Maelezo ya Chini]
a Si wanahistoria wote hukubaliana juu ya tarehe na utaratibu wa matukio katika maisha ya Jerome.
b Kama ilivyotokea baadaye, tafsiri ya Jerome ikawa Biblia ya msingi kwa Jumuiya ya Wakristo ya Magharibi, ilhali Septuagint yaendelea kutumiwa katika Jumuiya ya Wakristo ya Mashariki hadi leo.
[Picha katika ukurasa wa 28]
Sanamu ya Jerome mjini Bethlehemu
Picha zimeandaliwa na]
Garo Nalbandian
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 26]
Juu kushoto, hati ya Kiebrania: Courtesy of the Shrine of the Book, Israel Museum, Jerusalem; Chini kushoto, hati ya Kisiria: Reproduced by kind Permission of The Trustees of the Chester Beatty Library, Dublin; Juu katikati, hati ya Kigiriki: Courtesy of Israel Antiquities Authority