Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w98 10/1 kur. 24-27
  • Nilipata Kitu Bora Kuliko Utajiri

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nilipata Kitu Bora Kuliko Utajiri
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Natatanika Huko Marekani
  • Kuungana na Ndugu na Dada Yangu
  • Familia na Mazishi
  • Kujifunza Kweli
  • Kutafuta Mahali Nilipozaliwa
  • Kutanguliza Kweli
  • Kumkumbuka Muumba Wetu Kutoka Ujanani Kuendelea
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • Nilipata Utajiri wa Kweli Katika Australia
    Amkeni!—1994
  • Kumkaribia Mungu Kulinisaidia Niwezane na Hali
    Amkeni!—1993
  • Utafutaji Wangu Wenye Mafanikio wa Maana ya Uhai
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
w98 10/1 kur. 24-27

Nilipata Kitu Bora Kuliko Utajiri

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA CHARLES MYLTON

Siku moja Baba alisema hivi: “Acheni tumtume Charlie Marekani ambako fedha ni nyingi mno na zapatikana kwa urahisi. Angeweza kupata fedha fulani na kutuletea!”

KWA kweli, watu walifikiri ilikuwa rahisi kuwa tajiri huko Marekani. Waliishi maisha magumu mno katika Ulaya mashariki siku hizo. Wazazi wangu walikuwa na shamba dogo na walifuga ng’ombe wachache na kuku kadhaa. Hatukuwa na umeme wala maji ya mfereji ndani ya nyumba. Lakini, hakuna jirani yeyote aliyekuwa na vitu hivyo.

Nilizaliwa Hoszowczyk Januari 1, 1893, karibu miaka 106 iliyopita. Kijiji chetu kilikuwa huko Galicia, jimbo ambalo wakati huo lilikuwa sehemu ya miliki ya Austria na Hungaria. Sasa Hoszowczyk iko mashariki mwa Poland, karibu na Slovakia na Ukrainia. Majira ya baridi yalikuwa makali sana na theluji ilikuwa yenye kina kirefu. Nilipokuwa na umri wa miaka saba, nilikuwa nikitembea umbali wa nusu kilometa kwenda kwenye kijito na kwa kutumia shoka, nilikuwa nikitoboa shimo kwenye barafu ili nipate maji. Nilikuwa nikipeleka maji hayo nyumbani, naye Mama alikuwa akiyatumia kupikia na kusafishia. Alifua nguo zake kwenye kijito hicho, akitumia vipande vikubwa zaidi vya barafu kama ubao wa kufulia.

Hakukuwa shule huko Hoszowczyk, lakini nilijifunza kuzungumza Kipoland, Kirusi, Kislovakia, na Kiukrainia. Tulilelewa tukiwa washiriki wa kanisa la Othodoksi la Kigiriki, nami nilitumikia nikiwa mvulana wa altare. Lakini hata nikiwa na umri mdogo, nilikasirishwa na makasisi waliosema kwamba hatukupaswa kula nyama Ijumaa ilhali wao wenyewe walikula.

Baadhi ya marafiki zetu walikuwa wamerudi kutoka kazini huko Marekani wakiwa na fedha za kurekebisha upya nyumba zao na kununua vifaa vya ukulima. Hilo ndilo lililomfanya Baba azungumze juu ya kunituma Marekani pamoja na majirani fulani waliokuwa wakipanga safari ya kurudi huko. Huo ulikuwa mwaka wa 1907 nilipokuwa na umri wa miaka 14.

Natatanika Huko Marekani

Punde si punde nilikuwa katika meli, na katika muda wa majuma mawili tulikuwa tumevuka Atlantiki. Wakati huo, ulihitaji kuwa na dola 20, la sivyo ungerudishwa katika nchi yako ya nyumbani. Nilikuwa na kipande kimoja cha fedha kilichokuwa sawa na dola 20, na hivyo nilipata kuwa mmoja wa mamilioni ya watu waliopitia Kisiwa cha Ellis, New York, kilichokuwa kiingilio cha Marekani. Bila shaka, hakukuwa na fedha nyingi mno ambazo zilipatikana kwa urahisi, na haikuwa rahisi kuwa tajiri. Kwa kweli, ilikuwa vigumu sana kuwa tajiri!

Tulipanda garimoshi kwenda Johnstown, Pennsylvania. Watu niliokuwa pamoja nao walikuwa wamefika mahali hapo awali na walijua nyumba ya kupanga ambapo ningeweza kukaa. Nilikaa hapo ili niweze kumtafuta dada yangu mkubwa aliyeishi Jerome, Pennsylvania, mji ambao baadaye nilipata kujua kwamba ulikuwa umbali wa kilometa zipatazo 25 tu. Lakini nilikuwa nikisema Yarome, badala ya Jerome, kwa sababu “J” hutamkwa kama “Y” katika lugha yangu ya asili. Hakuna mtu aliyekuwa amewahi kusikia juu ya Yarome, kwa hiyo nilijipata katika nchi ya kigeni, nikiwa naweza kuzungumza Kiingereza kidogo sana na nikiwa na fedha kidogo.

Nilitafuta kazi kila asubuhi. Kwenye ofisi ya uajiri, watu wawili au watatu tu ndio waliokuwa wakiajiriwa kati ya umati mkubwa uliopiga foleni nje. Kwa hiyo kila siku nilirudi kwenye nyumba ya kupanga ili kujifunza Kiingereza kwa msaada wa vitabu vya kujisaidia kibinafsi. Nyakati nyingine nilipata kazi nisizotarajia, lakini miezi ilipita na fedha zangu zilikuwa karibu kwisha.

Kuungana na Ndugu na Dada Yangu

Siku moja nilipita karibu na baa moja iliyokuwa karibu na kituo cha garimoshi. Chakula kwa kweli kilinukia vizuri! Sandwichi, mikate yenye soseji, na bidhaa nyingine kwenye baa hiyo zingepatikana bila malipo mtu akinunua pombe, ambayo glasi moja kubwa ilinunuliwa kwa senti tano. Ingawa nilikuwa mwenye umri mdogo, mhudumu wa baa alinihurumia, akaniuzia pombe.

Nilipokuwa nikila, wanaume fulani waliingia ndani wakisema: “Harakisheni kunywa pombe yenu! Garimoshi inayoenda Jerome inakuja.”

“Je, unamaanisha Yarome?” nikauliza.

“La, Jerome,” wanaume hao wakasema. Wakati huo ndipo nilipojua mahali dada yangu alipoishi. Kwa kweli, kwenye baa hiyo nilikutana na mtu aliyeishi mtaa mmoja naye! Kwa hiyo, nilinunua tikiti ya garimoshi na hatimaye nikampata dada yangu.

Dada yangu na mume wake walisimamia nyumba ya kupangisha wachimba-migodi ya makaa ya mawe, nami niliishi nao. Waliniajiri kazi ya kuangalia mfereji uliotoa maji kwenye mgodi. Nilipaswa kuita mekanika wakati wowote mfereji huo ulipoacha kufanya kazi. Nililipwa senti 15 kwa siku kwa kazi hiyo. Kisha nikafanya kazi kwenye njia ya reli, mahali pa kutengenezea matofali, na hata nikiwa muuza-bima. Baadaye nilihamia Pittsburgh ambako ndugu yangu Steve alikuwa akiishi. Huko, nilifanya kazi katika vinu vya feleji. Sikuweza kuchuma fedha za kutosha kuweza kupeleka nyumbani.

Familia na Mazishi

Siku moja nilipokuwa nikitembea kwenda kazini, nilimwona mhudumu wa nyumbani mchanga, akisimama mbele ya nyumba alimofanya kazi. Niliwaza, ‘Lo, hakika ni mrembo.’ Majuma matatu baadaye, katika mwaka wa 1917, Helen nami tulioana. Katika miaka kumi iliyofuata, tulipata watoto sita ambao mmoja wao alikufa akiwa bado kitoto kichanga.

Katika 1918 kampuni ya Pittsburgh Railways iliniajiri kuwa dereva wa gari la reli. Karibu na jengo kubwa la kuhifadhia magari hayo ya reli, kulikuwa na mkahawa ambapo mtu angepata kikombe cha kahawa. Ndani, wanaume wawili Wagiriki ambao mkahawa huo ulikuwa wao hawakuonekana wakijali kama uliagiza chochote, mradi tu wangeweza kukuhubiria kutoka katika Biblia. Nilikuwa nikisema: “Je, mwamaanisha ulimwengu wote umekosea na nyinyi wawili tu ndio mnaosema kweli?”

“Chunguza katika Biblia!” walikuwa wakinijibu. Lakini wakati huo, walishindwa kunisadikisha.

Kwa kusikitisha, mpendwa wangu Helen aliugua mwaka wa 1928. Ili watoto wapate kutunzwa vema zaidi, niliwapeleka Jerome wakaishi na dada yangu na mume wake. Kufikia wakati huo walikuwa wamenunua shamba. Niliwatembelea watoto mara kwa mara na kutoa fedha kila mwezi za kulipia chakula chao. Pia niliwapelekea nguo. Kwa kusikitisha, hali ya Helen ilizidi kuwa mbaya, naye akafa Agosti 27, 1930.

Nilijihisi mpweke na hoi. Nilipomwendea kasisi ili kufanya mipango ya mazishi, alisema: “Wewe si mshiriki wa kanisa hili tena. Hujalipa ada zako kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja.”

Nilimweleza kwamba mke wangu alikuwa amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na kwamba nilikuwa nikiwapa watoto wangu fedha zozote za ziada ili waweze kuchanga kwenye kanisa lililokuwa Jerome. Hata hivyo, kabla kasisi huyo hajakubali kushughulikia mazishi hayo, ilinibidi nikope dola 50 ili nilipie fedha ambazo kanisa lilinidai. Kasisi huyo pia alitaka dola 15 zaidi ili aongoze Misa kwenye makao ya dada-mkwe wangu ambapo marafiki na familia walikuwa wamepanga kukusanyika ili kuonyesha heshima zao za mwisho kwa Helen. Singeweza kupata dola hizo 15, lakini kasisi huyo alikubali kuongoza Misa hiyo ikiwa ningempa fedha hizo siku ya kupata mshahara.

Siku ya kupata mshahara ilipofika ilinibidi nitumie fedha hizo kununulia watoto viatu na nguo za shule. Majuma mawili hivi baadaye, huyo kasisi alipanda gari langu la reli. “Bado ninakudai dola 15,” akasema. Kisha aliposhuka kwenye kituo chake cha gari, akanitisha, “Nitaenda kwa msimamizi wako na kumfanya atoe hizo fedha katika mshahara wako.”

Mwishoni mwa siku ya kazi, nilienda kwa msimamizi wangu na kumwambia yale yaliyokuwa yametukia. Hata ingawa alikuwa Mkatoliki, alisema, “Kasisi huyo akija hapa, nitamwambia kinaganaga ninachofikiri juu ya tabia yake mbaya!” Jambo hilo lilinifanya niwaze, ‘Makasisi wanataka tu fedha zetu, lakini hawatufunzi chochote juu ya Biblia.’

Kujifunza Kweli

Mara ile nyingine nilipokuwa katika mkahawa uliosimamiwa na wale Wagiriki wawili, tulizungumzia yaliyotukia kati yangu na kasisi. Tokeo likawa kwamba, nilianza kujifunza pamoja na Wanafunzi wa Biblia, kama vile Mashahidi wa Yehova walivyoitwa wakati huo. Nilikuwa nikisoma Biblia na fasihi ya Biblia usiku kucha. Nilijifunza kwamba Helen hakuwa akiteseka purgatori, kama kasisi alivyokuwa amesema, lakini alikuwa amelala katika kifo. (Ayubu 14:13, 14; Yohana 11:11-14) Kwa kweli, nilikuwa nimepata kitu bora kuliko dhahabu—nilikuwa nimepata kweli!

Majuma kadhaa baadaye, kwenye mkutano wangu wa kwanza na Wanafunzi wa Biblia katika uwanja wa Garden Theatre huko Pittsburgh, niliinua mkono wangu na kusema, “Nimejifunza mambo mengi juu ya Biblia usiku huu kuliko nilivyojifunza katika miaka yangu yote nikiwa kanisani.” Baadaye, walipouliza ni nani aliyetaka kushiriki katika kazi ya kuhubiri siku iliyofuata, niliinua mkono wangu tena.

Kisha, katika Oktoba 4, 1931, nilionyesha wakfu wangu kwa Yehova kwa ubatizo wa maji. Wakati huohuo niliweza kupanga nyumba na kuwarudisha watoto wangu kuishi nami, nikiajiri mtunza-nyumba anisaidie kuwatunza. Licha ya madaraka ya kifamilia, kuanzia Januari 1932 hadi Juni 1933, nilishiriki katika aina fulani ya utumishi wa pekee ulioitwa utumishi wa kusaidia, ambao nilitumia muda wa saa 50 hadi 60 nikizungumza na wengine juu ya Biblia.

Karibu na wakati huo nilianza kumwona mwanamke fulani mchanga, mrembo, aliyeonekana sikuzote kuwa akisafiri katika gari langu la reli kwenda na kurudi kutoka kazini. Tungetazamana katika kioo changu cha kutazamia nyuma. Hivyo ndivyo Mary nami tulivyokutana. Tulichumbiana na kuoana katika Agosti 1936.

Kufikia mwaka wa 1949 cheo changu kikubwa kazini kiliniwezesha kuchagua ratiba ya kazi ambayo ilinisaidia kupainia, kama huduma ya wakati wote inavyoitwa. Jean binti yangu mdogo zaidi alikuwa ameanza kupainia mwaka wa 1945, na tulipainia pamoja. Baadaye, Jean alikutana na Sam Friend, aliyekuwa akitumikia kwenye Betheli, makao makuu ya Mashahidi wa Yehova katika Brooklyn, New York.a Walioana mwaka wa 1952. Niliendelea kupainia katika Pittsburgh na kuongoza mafunzo mengi ya Biblia, wakati mmoja nikiongoza mafunzo ya familia tofauti 14 kila juma. Katika 1958, nilistaafu kutoka katika kazi yangu ya kuendesha gari la reli. Baada ya kustaafu, upainia ulikuwa rahisi, kwa kuwa sikulazimika kufanya kazi ya kimwili kwa muda wa saa nane kwa siku.

Katika 1983, Mary aliugua. Nilijaribu kumtunza kama alivyokuwa amenitunza vizuri sana kwa miaka ipatayo 50. Hatimaye akafa Septemba 14, 1986.

Kutafuta Mahali Nilipozaliwa

Katika 1989, Jean na Sam walienda pamoja nami kwenye mikusanyiko huko Poland. Tulizuru pia eneo nililokulia. Warusi walipomiliki sehemu hiyo ya ulimwengu, walibadili majina ya miji na kuwahamisha watu hadi nchi nyingine. Mmoja wa ndugu zangu alihamishwa hadi Istanbul naye dada yangu akahamishwa hadi Urusi. Nalo jina la kijiji changu halikutambuliwa na wale tuliouliza.

Ndipo nikaitambua milima fulani iliyokuwa mbali. Tulipokaribia nilitambua alama-ardhi nyingine—kilima, barabara panda, kanisa, na daraja juu ya mto. Kwa ghafula, tulishangaa kuona kibao cha barabarani kilichosema “Hoszowczyk”! Muda mfupi uliokuwa umepita, uvutano wa Wakomunisti ulikuwa umeisha, na majina ya awali ya vijiji yalikuwa yamerudishwa.

Nyumba yetu haikuwepo tena, lakini joko lililokuwa likitumiwa kwa upishi wa nje lilikuwepo, sehemu fulani ikiwa imefunikwa kwa ardhi. Kisha nikanyosha kidole kuelekea mti fulani mkubwa na kusema: “Ona mti ule. Niliupanda kabla ya kuondoka kwenda Marekani. Angalia jinsi ambavyo umekua!” Baadaye, tulitembelea eneo la makaburi, tukitafuta majina ya washiriki wa familia, lakini hatukuona yoyote.

Kutanguliza Kweli

Mume wa Jean alipokufa mwaka wa 1993, aliniuliza ikiwa nilitaka yeye aondoke Betheli ili anitunze. Nilimwambia kwamba hilo lingekuwa jambo baya zaidi ambalo angeweza kufanya, na bado ninahisi vivyo hivyo. Niliishi peke yangu hadi nilipofika umri wa miaka 102, lakini wakati huo ikawa lazima nihamie katika makao ya kutunzia wazee-wazee. Bado mimi ni mzee katika Kutaniko la Bellevue huko Pittsburgh, nao ndugu huja na kunipeleka kwenye mikutano katika Jumba la Ufalme Jumapili. Ingawa sasa utendaji wangu wa kuhubiri ni mdogo sana, naendelea kuwa katika orodha ya mapainia dhaifu.

Kwa miaka ambayo imepita, nimefurahia shule za pekee za kuzoeza waangalizi zilizopangwa na Watch Tower Society. Katika Desemba 1997, nilihudhuria vipindi fulani vya Shule ya Huduma ya Ufalme kwa ajili ya wazee wa kutaniko. Na tarehe 11 mwezi wa Aprili uliopita, Jean alinipeleka kwenye Ukumbusho wa kifo cha Kristo, sherehe ambayo nimethamini sana kuishiriki kila mwaka tangu 1931.

Baadhi ya wale ambao nimejifunza nao Biblia sasa wanatumikia wakiwa wazee, wengine ni wamishonari katika Amerika Kusini, nao wengine ni wazakuu, wakitumikia Mungu pamoja na watoto wao. Watatu kati ya watoto wangu—Mary Jane, John, na Jean—na vilevile wengi wa watoto na wajukuu wao wanamtumikia Yehova Mungu kwa uaminifu. Sala yangu ni kwamba siku moja binti yangu mwingine na wajukuu na vitukuu wangu watafanya vivyo hivyo.

Sasa nikiwa na umri wa miaka 105, bado nawatia moyo wote wajifunze Biblia na kuzungumza na wengine juu ya yale ambayo wamejifunza. Ndiyo, nimesadiki kwamba ukikaa karibu na Yehova, hutakata tamaa kamwe. Kisha wewe pia waweza kufurahia kitu bora kuliko utajiri ambao huharibika, yaani kweli ambayo hutuwezesha kuwa na uhusiano wenye thamani pamoja na Mpaji-Uhai wetu Yehova Mungu.

[Maelezo ya Chini]

a Simulizi la maisha ya Sam Friend laonekana katika toleo la Mnara wa Mlinzi la Agosti 1, 1986, ukurasa wa 22-26.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nilipokuwa nikiendesha gari la reli

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kwenye makao ya kutunzia wazee-wazee ninapoishi sasa

[Picha katika ukurasa wa 27]

Kibao cha barabarani tulichoona mwaka wa 1989

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki