Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w99 5/1 kur. 30-31
  • Paulo Ashinda Janga

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Paulo Ashinda Janga
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Avunjikiwa Meli
  • Muujiza Kwenye Kisiwa cha Malta
  • Somo Kwetu
  • “Hakuna Hata Mmoja Wenu Atakayepotea”
    “Kutoa Ushahidi Kamili” Kuhusu Ufalme wa Mungu
  • Meli Inaharibika Katika Kisiwa
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
  • Paulo Apelekwa Roma
    Masomo Unayoweza Kujifunza Katika Biblia
  • Piga Mbiu ya Ufalme wa Yehova kwa Ujasiri!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1999
w99 5/1 kur. 30-31

Walifanya Mapenzi ya Yehova

Paulo Ashinda Janga

PAULO yuko katika hali yenye kukatisha tumaini. Yeye na wengine 275 wamo melini ambayo imekumbwa na Euroakilo—upepo ulio mkali zaidi katika Mediterania. Dhoruba hiyo ni kali sana hivi kwamba jua halionekani mchana, wala nyota hazionekani usiku. Kwa kufaa, abiria wanahofia maisha yao. Hata hivyo, Paulo anawafariji kwa kusimulia jambo alilofunuliwa kimungu kupitia ndoto: “Hakuna nafsi kati yenu itakayopotea, ni mashua tu itakayopotea.”—Matendo 27:14, 20-22.

Usiku wa 14 wa dhoruba hiyo, mabaharia wanafanya uvumbuzi wenye kushtusha—kina cha maji ni pima 20 tu.a Baada ya umbali mfupi, wanapima kina tena. Wakati huu maji yana kina cha pima 15. Nchi kavu iko karibu! Lakini habari hizi njema zadokeza jambo lenye kuamsha fikira. Kwa kuwa wanarushwa huku na huku usiku katika maji yenye kina kifupi, meli inaweza kugonga miamba na kuharibika. Kwa hekima, mabaharia wanatia nanga. Baadhi yao wanataka kuteremsha mashua ndogo na kuipanda, wakihatarisha maisha yao baharini.b Lakini Paulo anawazuia. Anawaambia ofisa-jeshi pamoja na askari-jeshi hivi: “Isipokuwa watu hawa wabaki katika mashua, nyinyi hamwezi kuokolewa.” Ofisa huyo anamsikiliza Paulo, na sasa abiria wote 276 wanangojea mapambazuko kwa wasiwasi.—Matendo 27:27-32.

Avunjikiwa Meli

Asubuhi inayofuata, abiria wa meli hiyo waona ghuba yenye ufuo. Wakiwa na tumaini jipya, mabaharia wakata nanga na kutweka tanga la mbele kwenye upepo. Meli inaanza kuelekea ufukoni—labda kukiwa na kelele za shangwe.— Matendo 27:39, 40.

Hata hivyo, meli inakwama kwa ghafula kwenye fungu la mchanga. Lililo baya hata zaidi, mawimbi makali yapiga tezi, yakiivunja vipande-vipande. Itawabidi abiria wote waondoke melini! (Matendo 27:41) Lakini hilo linatokeza tatizo. Wengi kati ya wale waliomo melini—kutia ndani Paulo—ni wafungwa. Chini ya sheria ya Roma, mlinzi anayemwacha mfungwa wake atoroke lazima apate adhabu iliyokusudiwa mfungwa wake. Kwa mfano, mlinzi mzembe angeuawa ikiwa muuaji kimakusudi angetoroka.

Kwa kuhofia kupatwa na hayo, askari-jeshi wanaazimia kuwaua wafungwa wote. Hata hivyo, ofisa-jeshi, mwenye urafiki na Paulo, aingilia kati. Anaamuru wale wote wanaoweza kuogelea wajitose majini na kuogelea hadi nchi kavu. Wale wasioweza kuogelea lazima washikilie mbao au vifaa vingine kutoka melini. Abiria katika meli hiyo iliyoharibika wajikokota mmoja baada ya mwingine hadi ufukoni. Kupatana na maneno ya Paulo, hakuna mtu hata mmoja anayekufa!—Matendo 27:42-44.

Muujiza Kwenye Kisiwa cha Malta

Kikundi hicho chenye uchovu chapata mahali penye usalama kwenye kisiwa kiitwacho Malta. Wakazi wa kisiwa hicho ni “wenye kusema lugha ya kigeni,” kihalisi “washenzi” (Kigiriki, barʹba·ros).c Lakini watu wa Malta si washenzi. Kinyume chake, Luka, mwandamani msafiri wa Paulo, aripoti kwamba “wa[li]tuonyesha fadhili ya kibinadamu isiyo ya kawaida, kwa maana waliwasha moto na kutupokea sisi sote kwa njia ya kusaidia kwa sababu ya mvua iliyokuwa ikinyesha na kwa sababu ya baridi.” Paulo mwenyewe anajiunga na wenyeji wa Malta kukusanya kuni na kuziweka motoni.—Matendo 28:1-3, New World Translation—With References, kielezi-chini.

Kwa ghafula, nyoka-kipiri ajifungilia kwenye mkono wa Paulo! Wenyeji wa kisiwa hicho wanakata kauli kwamba lazima Paulo awe muuaji kimakusudi. Yaelekea wanafikiri kwamba Mungu huadhibu watenda-dhambi kwa kushambulia sehemu ya mwili wao iliyotumiwa kufanya dhambi. Lakini tazama! Kwa kuwashangaza sana wenyeji hao, Paulo akung’uta nyoka-kipiri huyo ndani ya moto. Kama vile simulizi la Luka, shahidi wa kujionea, lisemavyo, “walikuwa wakitarajia [Paulo] atavimba kwa sababu ya mwasho au kwa ghafula aanguke akiwa mfu.” Wenyeji wa kisiwa wanabadili maoni yao na kuanza kusema kwamba lazima Paulo awe ni mungu.—Matendo 28:3-6.

Paulo akaa Malta kwa miezi mitatu inayofuata, wakati ambapo anamponya baba ya Publio, mkuu wa kisiwa, aliyempokea Paulo kwa ukaribishaji-wageni, naye pia anawaponya wengine wanaougua magonjwa mbalimbali. Kwa kuongezea, Paulo apanda mbegu za kweli, jambo linalotokeza baraka nyingi kwa wakazi wakaribisha-wageni wa Malta.—Matendo 28:7-11.

Somo Kwetu

Paulo alikabili magumu mengi wakati wa huduma yake. (2 Wakorintho 11:23-27) Katika simulizi lililopo juu, yeye alikuwa mfungwa kwa ajili ya habari njema. Kisha, akalazimika kukabili majaribu yasiyotarajiwa: dhoruba kali na baadaye mvunjikomeli. Katika yote hayo, Paulo hakuyumbayumba katika azimio lake la kuwa mhubiri wa habari njema mwenye bidii. Kutokana na mambo yaliyompata, yeye aliandika hivi: “Katika hali zote nimejifunza siri ya jinsi ya kushiba na pia jinsi ya kuwa na njaa, jinsi ya kuwa na wingi na pia jinsi ya kupatwa na uhitaji. Kwa mambo yote ninayo nguvu kwa njia ya yeye anipaye nguvu.”—Wafilipi 4:12, 13.

Azimio letu la kuwa wahudumu wenye bidii wa Mungu wa kweli na lisidhoofishwe kamwe na matatizo ya maisha! Matatizo yasiyotarajiwa yatokeapo, tumtwike Yehova mzigo wetu. (Zaburi 55:22) Kisha, tungojee kwa saburi kuona jinsi anavyotuwezesha kuvumilia jaribu hilo. Wakati huohuo, twaendelea kumtumikia kwa uaminifu, tukiwa na uhakika kwamba yeye anatujali. (1 Wakorintho 10:13; 1 Petro 5:7) Kwa kubaki imara, hata hali iweje, sisi—kama Paulo—twaweza kushinda janga.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa kawaida, pima moja hukadiriwa kuwa dhiraa nne, au meta 1.8 hivi.

b Mashua ndogo ilitumiwa kwenda ufukoni wakati meli ilipotia nanga karibu na pwani. Kwa wazi, mabaharia walikuwa wakijaribu kuokoa maisha yao huku wakipuuza maisha ya wale wasiokuwa na ustadi wa kuendesha meli, ambao wangeachwa nyuma.

c Kichapo Word Origins cha Wilfred Funk chasema: “Wagiriki walidharau lugha nyingine isipokuwa ile yao, na kusema kwamba zilisikika kuwa za ‘kishenzi’ na yeyote aliyezizungumza walimwita barbaros.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki