Sauli—Chombo-Kichaguliwa kwa Bwana
SAULI wa Tarso alikuwa mpinzani na mwuaji wa wafuasi wa Kristo. Lakini Bwana alitaka kumtumia kwa kusudi tofauti baadaye. Sauli angekuja kuwa mwakilishi mwenye kutokeza wa kazi ileile aliyokuwa amepinga sana. Yesu alisema: “Mtu huyu [Sauli] ni chombo-kichaguliwa kwangu ili kupeleka jina langu kwa mataifa vilevile kwa wafalme na wana wa Israeli.”—Matendo 9:15.
Maisha ya Sauli akiwa “mtu fidhuli” yalibadilika kabisa alipoonyeshwa rehema na kuwa “chombo-kichaguliwa” kwa Bwana Yesu Kristo. (1 Timotheo 1:12, 13) Nguvu zilizomchochea kushiriki katika kumpiga Stefano kwa mawe na katika mashambulizi mengine dhidi ya wanafunzi wa Yesu sasa zilielekezwa kwa makusudi tofauti kabisa wakati Sauli alipogeuka na kuwa mtume Paulo aliye Mkristo. Kwa wazi Yesu aliona sifa nzuri katika Sauli. Sifa zipi? Sauli alikuwa nani? Malezi yake yalimfanyaje awe mwenye kufaa katika kuendeleza ibada ya kweli? Je, tunaweza kujifunza jambo lolote kutokana naye?
Historia ya Familia ya Sauli
Wakati wa kuuawa kwa Stefano baada tu ya Pentekoste ya 33 W.K., Sauli alikuwa “mwanamume kijana.” Alipokuwa akimwandikia Filemoni karibu mwaka wa 60-61 W.K., alikuwa “mwanamume mwenye umri mkubwa.” (Matendo 7:58; Filemoni 9) Wasomi wanadokeza kwamba, kulingana na njia ya kale ya kuhesabu umri, inaelekea kwamba “kijana” angekuwa na umri wa kati ya miaka 24 na 40, ilhali “mwanamume mwenye umri mkubwa” angekuwa na umri wa kati ya miaka 50 hadi 56. Kwa hiyo huenda Sauli alizaliwa miaka michache tu baada ya kuzaliwa kwa Yesu.
Wakati huo Wayahudi waliishi katika sehemu nyingi za ulimwengu. Ushinde, utumwa, uhamisho, biashara, na uhamaji wa hiari ni baadhi ya mambo yaliyowafanya watawanyike kutoka Yudea. Ingawa familia yake ilikuwa sehemu ya Wayahudi waliotawanyika, Sauli akazia utii wao kwa Sheria, akitaarifu kwamba ‘alitahiriwa siku ya nane, akatokana na ukoo wa familia ya Israeli, wa kabila la Benyamini, Mwebrania aliyezaliwa kutoka kwa Waebrania; kwa habari ya sheria, Farisayo.’ Sauli aliitwa jina lilelile la Kiebrania sawa na mtu mmoja mashuhuri wa kabila lake—mfalme wa kwanza wa Israeli. Sauli wa Tarso akiwa mzaliwa wa Roma pia alikuwa na jina la Kilatini, Paullus.—Wafilipi 3:5; Matendo 13:21; 22:25-29.
Kuzaliwa kwa Sauli akiwa Mroma kulimaanisha kwamba mmoja kati ya wazazi wake wa kiume wa kale alikuwa amepata pendeleo la kuwa raia wa Roma. Jinsi gani? Kuna njia kadhaa. Mbali na kuurithi, uraia ungeweza kupewa watu mmoja-mmoja au vikundi vya watu ama kwa sababu ya wema fulani mahususi, ama kwa sababu ya faida tu za kisiasa, au utumishi fulani wa pekee uliotolewa kwa Serikali. Mtumwa aliyeweza kulipa fedha ili awekwe huru na Mroma, au yule ambaye angewekwa huru na raia Mroma, angekuwa Mroma pia. Vivyo hivyo na askari-mstaafu wa jeshi la Roma. Baada ya muda, wenyeji waliokuwa wakiishi katika koloni za Roma wangeweza kuwa raia. Hata imesemwa kwamba katika nyakati fulani uraia ulinunuliwa kwa pesa nyingi sana. Jinsi ambavyo familia ya Sauli ilipata uraia ni jambo lisilofahamika.
Tunavyojua ni kwamba Sauli alitoka Tarso, jiji na mji mkuu wa mkoa wa Kilikia wa Roma (sasa liko kusini mwa Uturuki). Ingawa jumuiya kubwa ya Wayahudi iliishi katika eneo hilo, maisha ya huko yangeweza kumfanya Sauli afahamu utamaduni wa watu wa Mataifa. Tarso lilikuwa jiji kubwa lenye ufanisi na lililokuwa maarufu likiwa kituo cha elimu ya Kigiriki. Idadi ya watu wa jiji hilo katika karne ya kwanza inakadiriwa kuwa ilikuwa kati ya watu 300,000 na 500,000. Kilikuwa kituo cha kibiashara kwenye barabara kuu kati ya Asia Ndogo, Siria, na Mesopotamia. Ufanisi wa jiji la Tarso ulitokana na biashara na rutuba ya uwanda uliolizingira jiji hilo ambao ulizalisha hasa nafaka, divai, na kitani. Biashara yake yenye kusitawi ilitokeza vitambaa vya singa za mbuzi vilivyotumiwa kutengenezea mahema.
Elimu ya Sauli
Sauli, au Paulo, alijiruzuku kwa njia ya haki na kutegemeza utendaji wake wa kitheokrasi kwa kutengeneza mahema. (Matendo 18:2, 3; 20:34) Kazi ya kutengeneza mahema ilikuwa ya kawaida katika jiji lao la Tarso. Yaelekea kwamba Sauli alipokuwa kijana alifundishwa na baba yake kazi ya kutengeneza mahema.
Hali ya Sauli ya kujua lugha nyingi—hasa umahiri wake katika Kigiriki, iliyokuwa lugha ya kawaida ya Milki ya Roma— ikawa muhimu sana katika kazi yake ya umishonari. (Matendo 21:37–22:2) Wachunguzi wa maandishi yake wanasema kuwa Kigiriki chake ni bora kabisa. Msamiati wake si kama ule wa kikale, na badala yake, unashabihi ule wa Septuagint, tafsiri ya Kigiriki ya Maandiko ya Kiebrania aliyoinukuu au kuifasili mara nyingi. Kwa kufikiria uthibitisho huo, wasomi mbalimbali hukisia kwamba angalau Sauli alipata elimu nzuri ya msingi kwa Kigiriki, labda katika shule ya Kiyahudi. “Katika nyakati za kale, elimu nzuri—na hasa elimu ya Kigiriki—ilihitaji fedha; mara nyingi ilihitaji utegemezo fulani wa kimwili,” asema msomi Martin Hengel. Hivyo, elimu ya Sauli inadokeza kwamba alitoka katika familia mashuhuri.
Yaelekea kwamba alipokuwa na umri wa miaka 13 au chini, Sauli aliendeleza elimu yake huko Yerusalemu, kilometa zipatazo 840 kutoka nyumbani. Alielimishwa penye miguu ya Gamalieli, mwalimu aliyejulikana sana na mwenye kustahiwa sana wa mapokeo ya Mafarisayo. (Matendo 22:3; 23:6) Mtaala huo, unaoweza kulinganishwa na elimu ya chuo kikuu leo, ulimpa fursa ya kuwa mashuhuri katika Dini ya Kiyahudi.a
Atumia Uwezo kwa Njia Bora
Sauli ana aina tatu za malezi kwa sababu ya kuzaliwa katika familia ya Kiyahudi kwenye jiji la Kiroma lililofuata utamaduni wa Kigiriki. Bila shaka malezi yaliyohusisha lugha mbalimbali yalimsaidia kuwa “mambo yote kwa watu wa namna zote.” (1 Wakorintho 9:19-23) Baadaye uraia wake wa Roma ulimwezesha kutetea huduma yake kisheria na kutangaza habari njema kwa mtu mwenye mamlaka ya juu zaidi katika Milki ya Roma. (Matendo 16:37-40; 25:11, 12) Bila shaka, Yesu aliyefufuka alijua malezi ya Sauli, elimu yake na utu wake, akamwambia Anania hivi: “Shika njia yako uende, kwa sababu mtu huyu ni chombo-kichaguliwa kwangu ili kupeleka jina langu kwa mataifa vilevile kwa wafalme na wana wa Israeli. Kwa maana mimi nitamwonyesha wazi ni mambo mengi kama nini ambayo lazima ateseke kwa ajili ya jina langu.” (Matendo 9:13-16) Bidii ya Sauli ilipotumiwa kwa kusudi linalofaa, ilikuwa yenye faida sana katika kueneza ujumbe wa Ufalme katika maeneo ya mbali.
Kwa Yesu kumchagua Sauli kwa ajili ya utume wa pekee lilikuwa tukio lisilo na kifani katika historia ya Ukristo. Na bado, Wakristo wote wa wakati huu wakiwa mmoja-mmoja wana uwezo na sifa mbalimbali zinazoweza kutumiwa kueneza habari njema kwa matokeo. Sauli alipoelewa yale Yesu alimtaka afanye, hakusitasita. Alifanya yote aliyoweza katika kuendeleza masilahi ya Ufalme. Je, ndivyo ulivyo?
[Maelezo ya Chini]
a Kuhusu aina ya elimu aliyopokea Sauli kutoka kwa Gamalieli, ona Mnara wa Mlinzi, wa Julai 15, 1996, ukurasa wa 26–29.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 30]
Usajili na Utoaji wa Vyeti kwa Raia Waroma
Usajili wa watoto halali wa raia wa Roma ulianzishwa na Augusto kwa sheria mbili zilizotungwa mwaka wa 4 na wa 9 W.K. Watoto walihitaji kusajiliwa kabla ya siku 30 baada ya kuzaliwa. Familia zilipaswa kufanya tangazo mbele ya hakimu kwenye ofisi ifaayo ya kuweka rekodi za umma katika mikoa, zikitaarifu kwamba mtoto huyo hakuwa haramu na kwamba alikuwa ni raia wa Roma. Majina ya wazazi, jinsia yake na jina lake, na tarehe aliyozaliwa pia ziliandikwa. Hata kabla ya kuanzishwa kwa sheria hizi, usajili wa raia wote katika manispaa, koloni, na wilaya zote za Roma ulifanywa upya kwa kuhesabu watu baada ya kila miaka mitano.
Hadhi ya mtu ingeweza kuthibitishwa kwa kuchunguza maandishi yake katika hifadhi za nyaraka zilizotunzwa vyema. Nakala halali za maandishi hayo zingeweza kupatikana kwenye mabamba madogo ya mbao yenye kukunjwa. Wasomi wengi wanasema kwamba Paulo alipodai kuwa raia Mroma, huenda aliweza kuonyesha cheti cha kuthibitisha jambo hilo. (Matendo 16:37; 22:25-29; 25:11) Kwa kuwa uraia wa Roma ulionwa kuwa “mtakatifu” na ulimwezesha mtu kuwa na mapendeleo mengi, ughushi wowote wa vyeti hivyo ulikuwa kosa zito. Adhabu kwa sababu ya udanganyifu wowote juu ya hadhi ya mtu ilikuwa kifo.
[Hisani]
Historic Costume in Pictures/Dover Publications, Inc., New York
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 31]
Jina la Kiroma la Sauli
Kila raia wa kiume Mroma alikuwa na angalau majina matatu. Alikuwa na jina la kwanza, jina la familia (lililohusiana na kabila lake, au ukoo), na jina la ziada. Kielelezo kimoja kinachojulikana sana ni Gayo Yulio Kaisari. Biblia haitaji majina kamili ya Kiroma, lakini vichapo visivyo vya kidini husema kwamba Agripa aliitwa Marko Yulio Agripa. Galio aliitwa Lukio Yuniasi Galio. (Matendo 18:12; 25:13) Mifano ya Kimaandiko ya majina mawili ya mwisho kati ya majina matatu ya mtu ni Pontio Pilato (maandishi yaliyoko chini), Sergio Paulo, Klaudio Lisiasi, na Porkio Festo.—Matendo 4:27; 13:7; 23:26; 24:27.
Ni vigumu kuthibitisha kwa uhakika iwapo Paullus lilikuwa jina la kwanza la Sauli au jina la ziada. Ilikuwa kawaida kwa mtu kuongeza jina jingine lisilo rasmi ambalo angeitwa na watu wa familia yake au watu wanaomfahamu. Kama sivyo, jina lisilo la Kiroma kama Sauli lingetumiwa kuwa jina la badala. “[Sauli] halikuwa kamwe jina la Kiroma,” asema msomi mmoja, “lakini linaonekana kwa kufaa kuwa jina la ziada la kienyeji la raia wa Roma.” Katika maeneo yenye lugha nyingi, huenda mtu alichagua jina alilotaka kutumia kati ya majina yake yote kwa kutegemea hali za huko.
[Hisani]
Photograph by Israel Museum, ©Israel Antiquities Authority