Kwa Nini Tumwamini Yesu Kristo?
“HATA watu wengi wasio Wakristo huamini kuwa Yeye alikuwa mwalimu mkuu mwenye hekima. Yeye kwa hakika alikuwa mmoja wa watu mashuhuri zaidi waliopata kuishi.” (The World Book Encyclopedia) “Yeye” ni nani? Yesu Kristo, mwanzilishi wa Ukristo.
Ingawa hivyo, licha ya mambo ambayo ensaiklopedia hiyo husema, kwa mamia ya mamilioni ya watu katika Mashariki na kwingineko, Yesu Kristo ni mtu asiyejulikana, yeye ni jina tu wanalokumbuka kutokana na vitabu vya shule za upili. Hata katika makanisa ya Jumuiya ya Wakristo, mna wanatheolojia na makasisi ambao husema kwamba hatumjui Yesu kikweli nao hutilia shaka uhalisi wa masimulizi manne yaliyopo hadi leo (zile Gospeli) katika Biblia kuhusu maisha yake.
Je, yawezekana kuwa waandishi wa Gospeli walibuni masimulizi ya maisha ya Yesu? Sivyo hata kidogo! Mwanahistoria anayejulikana sana, Will Durant, aliandika hivi baada ya kuchanganua masimulizi hayo: “Kwamba wanaume wachache wa kikawaida wangeweza katika kizazi kimoja kubuni mtu mwenye nguvu na mwenye uvutano mwingi kadiri hiyo, mwenye elimu ya maadili ya hali ya juu kadiri hiyo na njozi yenye kuchochea kadiri hiyo ya udugu wa kibinadamu, ungekuwa muujiza wenye kustaajabisha mno zaidi ya wowote ulioandikwa katika Gospeli. Baada ya Uchambuzi wa Hali ya Juu Zaidi kuwapo kwa muda wa karne mbili, maelezo yanayohusu maisha, tabia, na mafundisho ya Kristo, yanabaki yakiwa yenye kufahamika wazi vya kutosha, na ndiyo sehemu yenye kusisimua zaidi katika historia ya watu wa Magharibi.”
Ingawa hivyo, kuna watu wanaompuuza Yesu Kristo wakisema hafai kuzingatiwa kwa sababu ya mambo ambayo wale wanaodai kuwa wafuasi wake wamefanya. ‘Waliangusha bomu la atomu juu ya Nagasaki,’ watu fulani nchini Japani wangesema. ‘Na kulikuwa Wakristo wengi zaidi jijini Nagasaki kuliko katika majiji mengi nchini Japani.’ Lakini je, unaweza kumlaumu tabibu kwa kuugua kwa mgonjwa ikiwa mgonjwa akosa kufuata maagizo ya daktari? Watu wengi zaidi wanaodai kuwa Wakristo wamepuuza kwa muda mrefu maagizo ya Yesu ya kushinda matatizo ya wanadamu. Ingawa hivyo, Yesu alitoa utatuzi wa matatizo yetu ya kila siku na vilevile wa taabu za mwanadamu ulimwenguni pote. Hiyo ndiyo sababu twakualika usome makala inayofuata na ujionee mwenyewe yeye alikuwa mtu wa aina gani.