Je, Ibilisi Hutufanya Tuwe Wagonjwa?
MAGONJWA HAYAKUPASWA KUWEPO KAMWE. Mungu alituumba tuishi milele tukiwa na afya kamili. Shetani, kiumbe wa roho, ndiye aliyeiletea familia ya binadamu magonjwa, maumivu, na kifo alipowashawishi wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, wafanye dhambi.—MWANZO 3:1-5, 17-19; WAROMA 5:12.
JE, HILO lamaanisha kwamba magonjwa yote ni matokeo ya moja kwa moja yasababishwayo na viumbe wa roho? Kama ilivyotajwa katika makala iliyotangulia, wengi leo hufikiri hivyo. Nyanya ya Owmadji mchanga alifikiri hivyo. Lakini je, kuhara kwa Owmadji—ugonjwa ambao mara nyingine huua watoto wachanga katika nchi za joto—kulisababishwa na roho wasioonekana?
Fungu la Shetani
Biblia hujibu swali hilo vizuri kabisa. Kwanza, inaonyesha kwamba roho za wazazi wetu wa kale waliokufa haziwezi kuathiri walio hai. Watu wanapokufa, “hawajui neno lo lote.” Hawana roho zinazoendelea kuishi baada ya kifo. Wamelala kaburini, ambamo “hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima.” (Mhubiri 9:5, 10) Wafu hawawezi kwa vyovyote kufanya walio hai wawe wagonjwa!
Hata hivyo, Biblia hufunua kwamba roho waovu wako. Mwasi wa kwanza katika ulimwengu wote alikuwa kiumbe wa roho ambaye sasa anaitwa Shetani. Wengine walijiunga naye nao wakaja kuitwa roho waovu. Je, Shetani na roho waovu waweza kusababisha magonjwa? Imetukia hivyo. Baadhi ya miujiza ya Yesu ya uponyaji ilihusisha kufukuza roho waovu. (Luka 9:37-43; 13:10-16) Hata hivyo, mengi ya maponyo aliyofanya Yesu yalihusisha magonjwa yasiyosababishwa moja kwa moja na roho waovu. (Mathayo 12:15; 14:14; 19:2) Vivyo hivyo leo, kwa kawaida magonjwa husababishwa na mambo ya asili wala si nguvu zinazozidi zile za kibinadamu.
Namna gani uchawi? Andiko la Mithali 18:10 latuhakikishia: “Jina la BWANA ni ngome imara; mwenye haki huikimbilia, akawa salama.” Andiko la Yakobo 4:7 lasema: “Mpingeni Ibilisi, naye atawakimbia.” Naam, Mungu aweza kuwakinga waaminifu wake dhidi ya uchawi na nguvu nyingine zozote zisizo za kawaida. Hiyo ni maana moja ya maneno haya ya Yesu: “Kweli itawaweka nyinyi huru.”—Yohana 8:32.
‘Namna gani Yobu?’ huenda wengine wakauliza. ‘Je, roho mwovu siye aliyemfanya mgonjwa?’ Ndiyo, Biblia yasema kwamba ugonjwa wa Yobu ulisababishwa na Shetani. Lakini kisa cha Yobu kilikuwa cha pekee. Kwa muda mrefu, Yobu alilindwa na Mungu ili asishambuliwe moja kwa moja na roho waovu. Kisha Shetani akamsai Yehova ampige Yobu, na kwa kuwa masuala makubwa yalihusika katika kisa hiki, Yehova akaondoa kwa sehemu kinga yake kwa mwabudu wake.
Hata hivyo, Mungu aliweka mipaka. Alipomruhusu Shetani amtese Yobu, Shetani angeweza kumfanya Yobu awe mgonjwa kwa muda fulani, lakini hangeweza kumwua. (Ayubu 2:5, 6) Hatimaye, kuteseka kwa Yobu kukaisha, naye Yehova akamthawabisha sana kwa uaminifu-maadili wake. (Ayubu 42:10-17) Kanuni zilizothibitishwa na uaminifu-maadili wa Yobu ziliandikwa katika Biblia zamani sana nazo ni dhahiri kwa wote. Hakuna haja ya kisa kingine kama hicho cha kupimia kanuni.
Shetani Hufanyaje Kazi?
Katika takriban kila kisa, uhusiano pekee kati ya Shetani na magonjwa ya kibinadamu ni uhakika wa kwamba Shetani alishawishi wenzi wa kwanza wa kibinadamu, nao wakafanya dhambi. Yeye na roho waovu wake hawasababishi kila ugonjwa moja kwa moja. Hata hivyo, Shetani aweza kutushawishi tufanye maamuzi yasiyo ya busara na kuridhiana imani yetu, jambo liwezalo kudhuru afya yetu. Yeye hakuwaroga, kuwaua, wala kuwashambulia Adamu na Hawa kwa ugonjwa. Alimshawishi Hawa asimtii Mungu, naye Adamu akafanya vivyo hivyo. Baadhi ya matokeo yakawa magonjwa na kifo.—Waroma 5:19.
Wakati mmoja, nabii asiye mwaminifu aitwaye Balaamu alikodiwa na mfalme wa Moabu ili alilaani taifa la Israeli, ambalo lilitisha Moabu kwa kupiga kambi kwenye mipaka yake. Balaamu alijaribu kulaani Israeli, lakini akashindwa kwa sababu taifa hilo lilikingwa na Yehova. Kisha Wamoabi wakaanza kuwashawishi Waisraeli washiriki katika ibada ya sanamu na ukosefu wa adili katika ngono. Mbinu hiyo ikafanikiwa, nao Waisraeli wakapoteza kinga ya Yehova.—Hesabu 22:5, 6, 12, 35; 24:10; 25:1-9; Ufunuo 2:14.
Twaweza kujifunza jambo muhimu kutokana na tukio hilo la kale. Msaada wa kimungu huwakinga waabudu waaminifu wa Mungu dhidi ya mashambulio ya moja kwa moja ya roho waovu. Hata hivyo, huenda Shetani akajaribu kushawishi watu mmoja-mmoja waridhiane imani yao. Huenda akawashawishi wafanye mambo yasiyofaa kiadili. Au, kama simba angurumaye, huenda akajaribu kuwaogopesha watende kwa njia inayowaondolea kinga ya Mungu. (1 Petro 5:8) Hiyo ndiyo sababu mtume Paulo humwita Shetani “yule aliye na uwezo wa kusababisha kifo.”—Waebrania 2:14.
Nyanya ya Owmadji alijaribu kumshawishi Hawa azuie magonjwa kwa kutumia hirizi na makago. Ni nini kingelitokea kama Hawa angelikubali? Angelionyesha kutokuwa na imani kamili katika Yehova Mungu, naye hangeliweza tena kutumainia kinga yake.—Kutoka 20:5; Mathayo 4:10; 1 Wakorintho 10:21.
Shetani alijaribu kumshawishi Yobu pia. Hakutosheka na kumpokonya familia yake, mali, na afya yake. Mke wa Yobu pia alimtolea shauri baya sana aliposema: “Umkufuru Mungu, ukafe.” (Ayubu 2:9) Kisha akatembelewa na “rafiki” watatu waliojaribu kwa pamoja kumsadikisha kwamba yeye ndiye wa kulaumiwa kwa ugonjwa wake. (Ayubu 19:1-3) Kwa njia hiyo, Shetani alijaribu kutumia hali dhaifu ya Yobu ili amvunje moyo na kutilia shaka tumaini lake katika uadilifu wa Yehova. Hata hivyo, Yobu aliendelea kumtegemea Yehova akiwa tumaini lake la pekee.—Linganisha Zaburi 55:22.
Tunapokuwa wagonjwa, sisi pia twaweza kuvunjika moyo. Katika hali kama hiyo, Shetani hujaribu kwa haraka kutufanya tutende kwa njia itakayofanya turidhiane imani yetu. Hivyo, tunapopatwa na ugonjwa, ni muhimu kukumbuka kwamba yaelekea sababu ya msingi inayofanya tuteseke ni kutokamilika tulikorithi, wala si nguvu fulani zisizo za kawaida. Kumbuka, Isaka mwaminifu alipata kuwa kipofu miaka mingi kabla hajafa. (Mwanzo 27:1) Sababu ilikuwa uzee wala si roho waovu. Raheli alikufa akizaa, si kwa sababu ya Shetani, bali udhaifu wa kibinadamu. (Mwanzo 35:17-19) Hatimaye, waaminifu wote wa kale wakafa—si kwa sababu ya kurogwa au laana bali kwa sababu ya kutokamilika kulikorithiwa.
Ni mtego kuwaza kwamba roho wasioonekana wanahusika moja kwa moja na kila ugonjwa unaotushika. Huenda hilo likatufanya tuogope roho hao isivyofaa. Kisha, tunapokuwa wagonjwa, huenda tukashawishika kujaribu kuwatuliza roho waovu badala ya kujitenga nao kabisa. Ikiwa Shetani aweza kutuogopesha tugeukie mazoea ya uwasiliani-roho, hilo lingekuwa kumwacha Mungu wa kweli, Yehova. (2 Wakorintho 6:15) Twapaswa kuongozwa na hofu yenye staha kwa Mungu, wala si hofu ya kishirikina kwa Mpinzani wake.—Ufunuo 14:7.
Owmadji mchanga tayari ana kinga nzuri zaidi iwezekanayo dhidi ya roho waovu. Kulingana na mtume Paulo, Mungu humwona kuwa ‘mtakatifu’ kwa sababu mama yake ni mwamini, naye aweza kusali ili Mungu awe pamoja na binti yake kupitia roho takatifu. (1 Wakorintho 7:14) Akiwa na ujuzi huo sahihi, Hawa aliweza kutafutia Owmadji matibabu yafaayo badala ya kutegemea hirizi.
Visababishi Mbalimbali vya Magonjwa
Watu walio wengi hawaamini katika viumbe wa roho. Wanaposhikwa na ugonjwa, wao huenda kwa daktari—ikiwa wanaweza. Bila shaka, mgonjwa aweza kwenda kwa daktari na bado asipone. Madaktari hawawezi kufanya miujiza. Lakini watu wengi wenye ushirikina, wanaoweza kuponywa, huenda kwa daktari wakiwa wamechelewa mno. Wao hujaribu njia za uwasiliani-roho za kuponya, na zinaposhindwa, wao huenda kwa daktari ikiwa hatua ya mwisho. Wengi hufa isivyo lazima.
Wengine hufa mapema kwa sababu ya kutojua. Hawatambui dalili nao hawajui wachukue hatua gani ili wazuie magonjwa. Ujuzi husaidia kuzuia kuteseka kusiko kwa lazima. Yafaa izingatiwe kwamba akina mama wanaojua kusoma na kuandika hufiwa na wototo wachache zaidi kutokana na magonjwa kuliko akina mama wasiojua kusoma na kuandika. Naam, kutokuwa na ujuzi kwaweza kusababisha kifo.
Uzembe ni kisababishi kingine cha magonjwa. Kwa mfano, wengi hupatwa na magonjwa kwa sababu wao huruhusu wadudu watambae juu ya chakula kabla ya kukila au kwa sababu wale wanaokitayarisha hawanawi mikono kwanza. Ni hatari pia kulala bila chandarua cha kujikinga na mbu katika maeneo ambapo ugonjwa wa malaria umeenea.a Kuhusu afya, mara nyingi ni kweli kwamba “usipoziba ufa utajenga ukuta.”
Mtindo-maisha usio wa busara umefanya mamilioni wengi washikwe na magonjwa na kufa mapema. Afya ya wengi imeharibiwa na ulevi, ukosefu wa adili katika ngono, matumizi mabaya ya dawa, na kutumia tumbaku. Mtu akijiingiza katika maovu hayo kisha ashikwe na ugonjwa, je, ni kwa sababu mtu fulani alimroga au roho fulani alimshambulia? La. Yeye ndiye wa kulaumiwa kwa ugonjwa wake. Kuwalaumu roho kungekuwa kukataa kuwajibika mwenyewe kwa mtindo-maisha usio wa busara.
Bila shaka, hatuwezi kudhibiti mambo mengine. Kwa mfano, tunaweza kukosa kinga dhidi ya vijiumbe-maradhi au uchafuzi wenye kusababisha magonjwa. Hivyo ndivyo ilivyotukia kwa Owmadji. Mama yake hakujua kilichosababisha kuhara huko. Watoto wake hawawi wagonjwa mara nyingi kama watoto wengine kwa sababu yeye huweka nyumba na ua wake ukiwa safi, naye sikuzote hunawa mikono kabla ya kutayarisha chakula. Lakini watoto wote hushikwa na ugonjwa mara kwa mara. Kuhara kwaweza kusababishwa na maambukizo 25 tofauti-tofauti ya vijiumbe-hai. Yaelekea hakuna atakayepata kujua kuhara kwa Owmadji kulisababishwa na kijiumbe-hai kipi.
Suluhisho la Muda Mrefu
Magonjwa hayasababishwi na Mungu. “Mungu hawezi kujaribiwa na mambo maovu wala yeye mwenyewe hamjaribu yeyote.” (Yakobo 1:13) Mmoja wa waabudu wake akishikwa na ugonjwa, Yehova humtegemeza kiroho. “BWANA atamtegemeza alipo mgonjwa kitandani. Katika ugonjwa wake umemtandikia.” (Zaburi 41:3) Naam, Mungu ni mwenye huruma. Yeye hutaka kutusaidia, wala si kutudhuru.
Kwa kweli, Yehova ana suluhisho la muda mrefu la magonjwa—kifo na ufufuo wa Yesu. Kupitia dhabihu ya fidia ya Yesu, wenye mioyo minyofu wanakombolewa kutoka katika hali yao ya dhambi nao hatimaye watapata afya kamili na uhai udumuo milele katika dunia paradiso. (Mathayo 5:5; Yohana 3:16) Miujiza ya Yesu ilionyesha kimbele ponyo la kweli ambalo Ufalme wa Mungu utaleta. Mungu pia atamwondoa Shetani na roho waovu wake. (Waroma 16:20) Kwa kweli, Yehova ameweka akibani mambo ya ajabu kwa ajili ya wale wanaodhihirisha imani katika yeye. Twahitaji tu kuwa na subira na kuvumilia.
Kwa sasa, Mungu hutoa hekima yenye kutumika na mwelekezo wa kiroho kupitia Biblia na udugu wa ulimwenguni pote wa waabudu waaminifu. Yeye hutuonyesha jinsi ya kuepuka maovu yasababishayo matatizo ya afya. Naye hutupa rafiki za kweli watakaotusaidia matatizo yakitokea.
Mfikirie Yobu tena. Ikiwa angeenda kwa mganga, hilo lingekuwa jambo baya kama nini! Kufanya hivyo kungemwondolea kinga ya Mungu, naye hangepata baraka zozote zilizomngojea baada ya kujaribiwa vikali. Mungu hakumsahau Yobu, naye hatatusahau. “Nyinyi mmesikia juu ya uvumilivu wa Yobu na mmeona tokeo alilotoa Yehova,” asema mwanafunzi Yakobo. (Yakobo 5:11) Tusipokata tamaa, sisi pia tutapokea baraka za ajabu katika wakati wa Mungu uliowekwa.
Ilikuwaje kwa Owmadji mchanga? Mama yake alikumbuka makala fulani katika Amkeni!, gazeti-jenzi la Mnara wa Mlinzi, juu ya tiba ya kurudisha maji mwilini kwa kunywa mchanganyiko wa maji, chumvi, na sukari.b Alifuata maagizo yaliyotolewa na kumtayarishia Owmadji mchanganyiko huo ili anywe. Sasa msichana huyo mchanga ni mzima na mwenye afya.
[Maelezo ya Chini]
a Takriban watu nusu bilioni huambukizwa malaria. Takriban watu milioni mbili hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa huo, hasa barani Afrika.
b Ona Amkeni! la Februari 8, 1987, ukurasa wa 21-23, “Kinywaji Chenye Chumvi Kinachookoa Uhai!”
[Picha katika ukurasa wa 7]
Yehova amepanga kuwe na suluhisho la kudumu la tatizo la ugonjwa