Fumbo la Magonjwa
OWMADJI MCHANGA ANAHARA. Hawa, mama yake, ana wasiwasi juu ya kuishiwa maji mwilini; alisikia kwamba huko kijijini mtoto wa binamu yake alikufa majuzi kwa sababu hiyohiyo. Nyanya ya Owmadji, mama-mkwe wa Hawa, anataka kumpeleka Owmadji kwa mganga. “Roho mwovu ndiye anayemfanya mtoto awe mgonjwa,” yeye asema. “Ulikataa kumpa hirizi ya kuvaa ili apate kinga, na sasa matatizo yanaanza!”
HALI hiyo ni ya kawaida katika sehemu nyingi za ulimwengu. Mamia ya mamilioni huamini kwamba roho waovu ndio kisababishi kisichoonekana cha magonjwa. Je, hilo ni kweli?
Kusababisha Fumbo Hilo
Huenda wewe binafsi usiamini kwamba roho wasioonekana husababisha magonjwa. Kwa kweli, huenda usielewe sababu iwezayo kumfanya yeyote afikirie hivyo, kwa kuwa wanasayansi wameonyesha kwamba magonjwa mengi husababishwa na virusi na bakteria. Hata hivyo, kumbuka kwamba wanadamu hawakujua sikuzote juu ya pathojeni hizi ndogo sana. Vitu visivyoonekana kwa macho ya binadamu vilipata kuonekana pale Antonie van Leeuwenhoek alipobuni hadubini katika karne ya 17. Hata hivyo, wanasayansi walianza kuelewa uhusiano kati ya pathojeni na magonjwa kutokana na uvumbuzi mbalimbali wa Louis Pasteur katika karne ya 19.
Kwa kuwa visababishi vya magonjwa havikujulikana kwa kipindi kirefu katika historia ya binadamu, mawazo mengi ya kishirikina yalisitawi, kutia ndani nadharia kwamba magonjwa yote husababishwa na roho waovu. Kichapo The New Encyclopædia Britannica chadokeza njia moja ambayo mawazo hayo yaliweza kusitawi. Chasema kwamba waponyaji wa kale walijaribu kutibu wagonjwa kwa aina mbalimbali za mizizi, majani, na chochote kingine walichoweza kupata. Wakati mwingine, baadhi ya tiba hizo ziliponya. Ndipo mponyaji huyo angechanganya tiba yenye kuponya na taratibu na desturi nyingi za kishirikina, ili kuficha tiba halisi. Hivyo, mponyaji alihakikisha kwamba watu wangelazimika kuendelea kutumia huduma zake. Kwa njia hiyo, tiba ikawa kitu kisichoeleweka kabisa, nao watu wakatiwa moyo kutegemea msaada wa nguvu zinazozidi zile za kibinadamu.
Njia hizi za kitamaduni za kuponya zingalipo katika nchi kadhaa. Wengi husema kwamba magonjwa husababishwa na roho za wazazi wa kale waliokufa. Wengine husema kwamba Mungu hutufanya tuwe wagonjwa na kwamba ugonjwa ni adhabu kwa dhambi zetu. Hata watu wenye elimu wakielewa hali ya kibiolojia ya magonjwa, bado wanaweza kuogopa uvutano wa nguvu zinazozidi zile za kibinadamu.
Wachawi na waponyaji wa kitamaduni hutumia woga huo ili kuwanyonya watu. Basi, twapaswa kuamini nini? Je, inanufaisha kutegemea roho kupata utunzi wa kiafya? Biblia husema nini?