Jinsi Vita na Ukatili Vinavyotuathiri Sisi Sote
“Tangu Vita vya Pili vya Dunia, idadi ya jeuri imeongezeka zaidi ulimwenguni, hivi kwamba mtu mmoja kati ya watu wanne wanaoishi duniani leo anaishi katika maeneo yaliyoathiriwa na vita.”
Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed, Januari 26, 2023.
Vita na jeuri vinaweza kuanza ghafla katika maeneo ambayo sasa yana amani. Hata wale ambao wanaishi katika maeneo ambayo hayajapatwa na vita huathiriwa pia. Na madhara yanayotokana na vita yanaweza kudumu kwa muda mrefu hata baada ya vita hivyo kwisha. Fikiria mifano ifuatayo:
Upungufu wa chakula. Kulingana na Shirika la Chakula Duniani, “vita ndio chanzo kikuu cha njaa. Watu wengi ambao hawana chakula cha kutosha wanaishi katika maeneo yaliyo na vita.”
Matatizo ya afya ya kimwili na ya kiakili. Uwezekano wa vita kutokea unaweza kuwasababishia watu mkazo na mahangaiko mengi sana. Wale wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na vita hawakabili tu hatari za kimwili bali pia, wanakabili hatari ya kupatwa na matatizo ya afya ya akili. Na inasikitisha kwamba mara nyingi wanashindwa kupata huduma za kitiba wanazohitaji.
Vita vinasababisha watu wakimbie makao yao. Kulingana na Shirika la Wakimbizi Ulimwenguni, kufikia Septemba 2023, zaidi ya watu milioni 114 ulimwenguni pote wamelazimika kuyakimbia makao yao. Sababu kuu ya janga hilo ni vita na ukatili.
Hali ngumu ya kiuchumi. Kwa kawaida, watu hukabili hali ngumu ya kiuchumi, kama vile kupanda kwa bei za bidhaa kwa sababu ya vita. Huenda watu wakateseka kwa sababu serikali inatumia pesa nyingi kwa ajili ya kugharimia vita, hata pesa ambazo kwa kawaida zingetumiwa kugharimia huduma za kiafya na elimu. Na baada ya vita kwisha, gharama kubwa hutumiwa kujenga upya majengo yaliyoharibiwa wakati wa vita.
Uharibifu wa mazingira. Watu huteseka wakati eneo wanaloishi linapoharibiwa kimakusudi. Uchafuzi wa maji, hewa, na udongo unaweza kusababisha matatizo ya kiafya ya muda mrefu, na mabomu yaliyofichwa na kusahauliwa ardhini yanaweza kusababisha madhara kwa muda mrefu hata baada ya vita kwisha.
Bila shaka, vita husababisha uharibifu na gharama kubwa sana.