JINSI MICHANGO YAKO INAVYOTUMIWA
Mikakati ya Kutunza Mazingira Inayowanufaisha Ndugu Zetu na Sayari Pia
APRILI 1, 2025
Tukiwa Mashahidi wa Yehova, tunajua kwamba Yehova Mungu atachukua hatua hivi karibuni ili kurekebisha uharibifu ambao wanadamu wameisababishia dunia. (Ufunuo 11:18) Hata hivyo, kwa sasa tunafanya yote tuwezayo ili kuitunza dunia. Kwa mfano, katika majengo yetu, tumeweka mikakati inayohakikisha mazingira yanatunzwa.
Isitoshe, katika miradi mipya, tunahakikisha mikakati hiyo inafuatwa ili kupunguza athari mbaya kwa mazingira. Ni miradi gani ya kutunza mazingira ambayo tumetekeleza? Na miradi hii imetusaidiaje kutumia michango kwa njia nzuri zaidi?
Kupunguza Joto Katika Jumba la Kusanyiko
Hapo awali, Jumba la Kusanyiko la Matola nchini Msumbiji, lilikuwa limejengwa bila kuta za kando na lilikuwa limeezekwa paa la mabati. Paa hilo lilifyonza joto jingi kutoka kwenye jua na kulifanya Jumba hilo la Kusanyiko liwe na joto kali. Ndugu mmoja alisema hivi: “Joto hilo lilitufanya tutokwe na jasho sana! Mwishoni mwa programu, akina ndugu walitoka nje haraka ili kupunga hewa na kupoa kidogo.” Tungefanya nini ili kuwaandalia ndugu zetu Jumba zuri zaidi la Kusanyiko ambalo lingewasaidia kukazia fikira programu na kunufaika kikamili?
Tuliamua kutatua tatizo hilo katika njia ambayo ingetunza mazingira. Tuliweka feni zinazosukumwa na upepo na tukaweka kizio cha kupunguza joto chini ya paa. Kizio hicho kinapunguza kiwango cha joto kinachopitishwa na paa kuingia kwenye jengo, na feni hizo huhakikisha kuna mzunguko wa hewa baridi ndani ya jengo. Feni hizo hazitumii umeme bali zinatumia upepo na mzunguko wa asili wa hewa ili kuondoa hewa yenye joto inayokusanyika ndani ya jengo. Feni hizo zinagharimu takriban dola 50 kila moja.a
Feni zinazosukumwa na upepo katika Jumba la Kusanyiko la Matola
Suluhisho hilo limefanya kuwe na hewa safi ndani ya Jumba hilo la Kusanyiko. Kwa kuwa sasa kuna mzunguko mzuri wa hewa, jengo hilo haliwi na unyevu na kuvu nyingi kama zamani. Pia, kiwango cha kaboni dioksidi kinapungua na kunakuwa na mzunguko wa kutosha wa oksijeni. Hivyo, wahudhuriaji wanakuwa macho na wanastarehe zaidi. Ndugu aliyenukuliwa awali anasema: “Sasa hatutoki nje haraka kama tulivyokuwa tukifanya hapo awali mara tu programu ilipoisha. Badala yake, tunabaki ndani ya Jumba la Kusanyiko wakati wa kipindi cha mapumziko na tunafurahia mazungumzo pamoja na marafiki. Paa hili jipya linatufanya tuhisi kama tumeketi chini ya kivuli cha mti mkubwa!”
Sasa ndugu zetu wanafurahia zaidi programu za kusanyiko
Kutumia Nishati ya Jua
Katika mengi ya majengo yetu ulimwenguni pote, tumeweka mifumo ya kutokeza umeme kutokana na miale ya jua. Mifumo hiyo inatumia paneli ambazo zinanasa miale ya jua na kutokeza umeme. Hivyo, hatutegemei sana umeme unaotokana na vyanzo vinavyochafua mazingira. Tunapotumia nishati ya jua tunapunguza uchafuzi wa mazingira na inatusaidia kuokoa michango iliyotolewa.
Mwaka wa 2022, ofisi ya tawi ya Slovenia iliwekewa mfumo huo wa kutokeza umeme kutokana na miale ya jua na unatokeza asilimia 30 ya nishati inayotumiwa na ofisi hiyo. Mfumo huo unapotokeza nishati inayozidi mahitaji ya ofisi ya tawi, nishati hiyo husambazwa ili itumiwe na wakaaji wa eneo hilo. Mfumo huo uligharimu dola 360,000. Hata hivyo, kwa kuwa gharama ya umeme ya ofisi hiyo imepungua, pesa ambazo tutakuwa tumeokoa ndani ya miaka minne kwa kutumia mfumo huo zitakuwa nyingi zaidi kuliko pesa tulizotumia kuununua.
Ofisi ya tawi ya Slovenia
Mwaka wa 2024, tuliweka pia paneli za jua na betri kubwa katika ofisi ya tawi ya Sri Lanka. Mradi huo uligharimu dola milioni 3 hivi na unatoa asilimia 70 ya mahitaji ya umeme ya ofisi hiyo ya tawi. Kufikia mwaka wa tatu tangu mfumo huo ulipowekwa, pesa tutakazokuwa tumeokoa kwa kutumia mfumo huo zitakuwa nyingi zaidi kuliko pesa tulizotumia kuununua. Mwaka huohuo, pia tuliweka mfumo huo kwenye ofisi ya tawi ya Uholanzi. Uligharimu dola milioni 1.1 na unatoa asilimia 35 ya mahitaji ya umeme ya ofisi hiyo ya tawi. Mfumo huo utakuwa umelipia gharama zake baada ya miaka tisa.
Ofisi ya tawi ya Uholanzi
Isitoshe, tumeweka mifumo hiyo katika ofisi kadhaa za utafsiri nchini Mexico, kama vile katika ofisi ya utafsiri ya Tarahumara (ya Kati) iliyo katika jimbo la Chihuahua. Katika eneo ambalo ofisi hiyo ipo, kiwango cha joto hushuka hadi kufikia nyuzi 0 Selsiasi katika majira ya baridi. Na katika majira ya joto, nyakati nyingine kiwango cha joto hupanda hadi kufikia nyuzi 40 Selsiasi! Licha ya hali hizo, akina ndugu hawakuwa wakitumia mifumo ya kupasha au kupoza joto kwa sababu umeme ulikuwa ghali. Ndugu anayeitwa Jonathan anayefanya kazi katika ofisi hiyo ya utafsiri anasema hivi: “Tulitumia blanketi na mavazi mazito katika majira ya baridi, na katika majira ya joto tulifungua madirisha.”
Mwaka wa 2024, mfumo wa kutokeza umeme kutokana na miale ya jua uliwekwa kwenye ofisi hiyo ya utafsiri. Mfumo huo uligharimu dola 21,480. Baada ya miaka mitano mfumo huo utakuwa umelipia gharama hizo. Sasa ndugu zetu wanaweza kutumia mifumo ya kupasha au kupoza joto kwa ukawaida. Jonathan anasema: “Sasa tunafurahia zaidi mgawo wetu na tunafanya kazi vizuri zaidi. Pia, tunafurahi tunapoona michango ikitumiwa kwa njia nzuri zaidi na inayotunza mazingira.”
Sasa timu ya utafsiri ya Tarahumara (ya Kati) inafanya kazi katika mazingira yenye kustarehesha zaidi
Kuhifadhi Maji ya Mvua
Barani Afrika, baadhi ya Majumba ya Ufalme hayana vyanzo vinavyotegemeka vya maji. Kwa sababu hiyo, akina ndugu wanalazimika kubeba maji kwa kilomita kadhaa na kuyaleta kwenye Jumba la Ufalme. Katika Majumba mengine, akina ndugu hununua maji yanayosambazwa na malori. Lakini maji hayo ni bei ghali na njia hii ya kupata maji haitunzi mazingira.
Ili kuwawezesha ndugu hawa kupata maji, tuliweka mifereji ya kukusanya maji kutoka kwenye paa na matangi makubwa ya kuhifadhi maji katika Majumba mengi ya Ufalme barani Afrika. Kabla ya kuweka vifaa hivyo katika Majumba la Ufalme, akina ndugu huchunguza hali ya hewa ya eneo hilo ili wajue njia bora zaidi ya kuhifadhi maji. Gharama ya kuweka vifaa hivyo inaweza kuwa kati ya dola 600 hadi 3,000. Hata hivyo, vifaa hivi hupunguza gharama ya uendeshaji wa Majumba ya Ufalme kwa sababu akina ndugu hawahitaji kulipia tena gharama za maji.
Tangi la maji katika Jumba la Ufalme la Phuthaditjhaba, Afrika Kusini
Mifumo hii ya kukusanya na kuhifadhi maji imewanufaisha ndugu zetu. Dada Noemia kutoka Msumbiji anasema: “Hapo awali, tulisafiri umbali mrefu ili kupata maji. Tungefika kwenye Jumba la Ufalme tukiwa tumechoka sana. Na kwa sababu hatungepata maji ya kutosha, ilikuwa vigumu kudumisha usafi. Sasa kila mmoja wetu anaweza kunawa mikono na tunafika kwenye Jumba la Ufalme tukiwa hatujachoka sana na hilo linatusaidia kufurahia mikutano. Asanteni sana!”
Dada akiwa na mwanaye wakitumia maji ya mvua yaliyohifadhiwa kwenye tangi la maji nchini Afrika Kusini
Tunapata wapi pesa za kugharimia miradi hiyo? Ni kupitia michango inayotolewa kwa ajili ya kazi ya ulimwenguni pote. Sehemu kubwa ya michango hiyo hutolewa kupitia njia mbalimbali zinazopatikana kwenye tovuti ya donate.jw.org. Asanteni sana kwa ukarimu wenu!
a Pesa zote zinazorejelewa katika makala hii ni dola za Marekani.