-
Kuingia Katika Ulimwengu Usio na Huruma!Amkeni!—2003 | Desemba 22
-
-
Kuingia Katika Ulimwengu Usio na Huruma!
MTOTO huzaliwa katika ulimwengu wenye ukatili, usio na huruma, na uliojaa matatizo. Ingawa mtoto hawezi kueleza hisia zake, wanasayansi fulani wanaamini kwamba mtoto hujua kinachoendelea hata kabla hajazaliwa.
Kitabu The Secret Life of the Unborn Child kinasema: “Sasa tunajua kwamba mtoto aliye tumboni ni mwanadamu anayetambua mambo na anayetenda, ambaye huanza kuwa na hisia katika mwezi wake wa sita tumboni (na labda hata mapema zaidi).” Ingawa mtoto hawezi kukumbuka, wanasayansi fulani wanadhani kwamba maisha yake ya baadaye yanaweza kuathiriwa na hali ngumu zinazokuwepo wakati wa kujifungua.
Matatizo huendelea baada ya kuzaliwa. Anapotoka nje ya tumbo la mama yake, mtoto haendelei kupata chakula na oksijeni kupitia kiunga-mwana kilichounganishwa na kitovu chake. Anahitaji kuanza kupumua na kula ili aendelee kuishi. Anahitaji mtu wa kumlisha na kumwandalia mahitaji mengine.
Mtoto anahitaji pia kukua kiakili, kihisia, na kiroho. Kwa hiyo, mtu fulani anahitaji kumlea. Ni nani anayeweza kumtunza vizuri? Mtoto anahitaji nini kutoka kwa wazazi wake? Mahitaji hayo yanaweza kutoshelezwaje? Makala zinazofuata zitajibu maswali hayo.
-
-
Kile Ambacho Watoto WanahitajiAmkeni!—2003 | Desemba 22
-
-
Kile Ambacho Watoto Wanahitaji
TANGU mtoto anapozaliwa, anahitaji kutunzwa kwa wororo. Anahitaji kupapaswa kwa wororo na kukumbatiwa. Madaktari fulani wanaamini kwamba saa 12 za kwanza za maisha yake ni muhimu sana. Wanasema kwamba mara tu baada ya kuzaliwa, kile ambacho mama na mtoto wanahitaji na wanataka sana ni “kupapasana, kukumbatiana, kutazamana na kusikilizana, bali si kulala wala kula.”a
Kwa kawaida wazazi humshika, humpakata, humpapasa, na kumkumbatia mtoto wao. Naye mtoto huanza kuwa na uhusiano wa karibu na wazazi wake na huitikia wanapomjali. Uhusiano huo ni wenye nguvu sana hivi kwamba wazazi hujitoa mhanga kumtunza mtoto lolote liwalo.
Kwa upande mwingine, mtoto anaweza kudhoofika na kufa wazazi wasipomjali. Hivyo, madaktari fulani husema kwamba mtoto anapaswa kuletwa kwa mama yake mara tu anapozaliwa. Wanapendekeza kwamba anapaswa kuwa na mama yake angalau dakika 30 mpaka 60 za kwanza kabisa za maisha yake.
Ingawa watu fulani husisitiza kwamba mama na mtoto wake wawe pamoja mara tu baada ya kuzaliwa, jambo hilo haliwi rahisi katika hospitali nyingine. Mara nyingi watoto hutenganishwa na mama zao kwa sababu inahofiwa kwamba watoto wataambukizwa magonjwa. Hata hivyo, uthibitisho unaonyesha kwamba mtoto anapokuwa na mama yake haielekei ataambukizwa ugonjwa hatari. Kwa hiyo, hospitali nyingi zaidi zinawaruhusu akina mama kuwa na watoto wao kwa muda mrefu zaidi baada ya kuzaliwa.
Kuhangaikia Uhusiano Wako na Mtoto
Akina mama fulani hawavutiwi na watoto wao wanapowatazama kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, wanajiuliza, ‘Je, nitampenda mtoto wangu?’ Ni kweli kwamba si mama wote wanaowapenda watoto wao mara tu wanapowaona. Lakini hakuna haja ya kuwa na wasiwasi.
Hata mama asipovutiwa na mtoto wake mara moja, anaweza kuvutiwa naye baadaye. Mama mmoja mwenye uzoefu anasema: “Uhusiano wako pamoja na mtoto wako hauathiriwi unapomtazama baada ya kujifungua.” Hata hivyo, ikiwa wewe ni mjamzito na una wasiwasi kuhusu uhusiano wako wa baadaye pamoja na mtoto wako, itafaa uzungumze na daktari wako mapema. Mweleze unataka kuwa na mtoto wako wakati gani na kwa muda gani.
“Tafadhali Ongea Nami!”
Inaonekana kuna wakati ambapo huwa rahisi kwa watoto kujifunza mambo fulani. Baada ya muda inakuwa vigumu kujifunza mambo hayo tena kwa urahisi. Kwa mfano, mtoto mchanga hujifunza lugha moja au zaidi kwa urahisi. Lakini anapofikia umri wa miaka mitano hivi, inakuwa vigumu kujifunza lugha.
Inakuwa vigumu hata zaidi kwa mtoto kujifunza lugha fulani anapofikia umri wa miaka 12 mpaka 14. Kulingana na daktari wa mfumo wa neva wa watoto, Peter Huttenlocher, wakati huo “ukubwa na idadi ya viunganishi vya neva katika sehemu za ubongo zinazoshughulikia lugha hupungua.” Basi, miaka michache ya kwanza maishani ni muhimu katika kujifunza lugha!
Watoto huwezaje kuzungumza, jambo ambalo ni muhimu sana katika ukuzi wa akili yao? Hasa kwa kuongea na wazazi. Watoto huchochewa hasa na sauti za watu. Barry Arons wa Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts anasema, “mtoto . . . huiga sauti ya mama yake.” Hata hivyo, watoto hawaigi sauti zote. Arons anasema kwamba mtoto “haigi kelele za kitanda chake zinazosikika wakati uleule mama yake anapozungumza.”
Wazazi katika sehemu mbalimbali huzungumza na watoto wao kwa njia moja. Mzazi anapozungumza kwa upendo, mpigo wa moyo wa mtoto huongezeka. Inaaminika kwamba jambo hilo humsaidia mtoto kuhusianisha vitu na majina yake. Ni kana kwamba mtoto anasema: “Tafadhali ongea nami!”
“Tafadhali Nitazameni!”
Imegunduliwa kwamba katika mwaka wa kwanza au baadaye, mtoto huwa na uhusiano wa karibu na mtu anayemlea, hasa mama yake. Mtoto anapokuwa na uhusiano huo mzuri, anapatana na watu wengine kuliko watoto ambao hawana uhusiano mzuri na wazazi wao. Uhusiano huo unapaswa kusitawishwa kabla mtoto hajafikia umri wa miaka mitatu.
Ni nini kinachoweza kutukia mtoto anapopuuzwa wakati huo ambapo akili yake inaweza kuathiriwa kwa urahisi? Martha Farrell Erickson aliyewachunguza akina mama 267 na watoto wao kwa miaka zaidi ya 20, anasema: “Mtoto anapopuuzwa, pole kwa pole yeye hukosa uchangamfu na hatimaye anashindwa kuchangamana na wengine au kujifunza mambo mengine.”
Akielezea maoni yake kuhusu matokeo mabaya ya kumpuuza mtoto, Dakt. Bruce Perry, wa Hospitali ya Watoto ya Texas anasema: “Kama ningeombwa nichague kati ya kumvunja mtoto wa miezi 6 mifupa yake yote au kumpuuza kwa miezi miwili, ningesema afadhali avunjwe mifupa yake yote.” Kwa nini? Perry anaonelea kwamba “mifupa inaweza kupona, lakini mtoto akipuuzwa kwa miezi miwili, akili yake itachanganyikiwa daima.” Watu fulani hudai kwamba madhara hayo yanaweza kutibiwa. Hata hivyo, uchunguzi wa kisayansi unaonyesha kwamba malezi yafaayo ni muhimu kwa akili ya mtoto.
Kitabu Infants kinasema, “kwa ujumla [watoto] hutaka kupenda na kupendwa.” Mtoto anapolia, mara nyingi anawasihi wazazi wake hivi: “Tafadhali nitazameni!” Inafaa wazazi wamshughulikie kwa njia ya upendo. Kwa njia hiyo mtoto ataanza kujua kwamba anaweza kuwaeleza wengine mahitaji yake. Atajifunza kuchangamana na wengine.
‘Si Nitamharibu Mtoto?’
Huenda ukajiuliza, ‘Nikimhangaikia mtoto kila anapolia, si nitamharibu?’ Labda. Watu wana maoni tofauti kuhusu jambo hilo. Kwa kuwa kila mtoto ni tofauti, wazazi wanapaswa kuamua njia nzuri ya kumlea. Hata hivyo, uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba mtoto aliyezaliwa hivi karibuni akiwa na njaa, maumivu, au akikasirika, homoni za mfadhaiko hutokezwa mwilini. Yeye huonyesha mfadhaiko wake kwa kulia. Inasemekana kwamba mzazi anapoitikia na kumhangaikia mtoto, anaanza kusaidia ubongo wake kutokeza chembe zitakazomsaidia kujua jinsi ya kujituliza. Pia kulingana na Dakt. Megan Gunnar, mtoto anayehangaikiwa anapolia, hutokeza homoni chache za mfadhaiko za cortisol. Hata anapokasirika, yeye hujituliza haraka.
Erickson anasema: “Watoto wanaohangaikiwa haraka na kwa ukawaida wanapolia, hasa katika miezi 6 hadi 8 ya kwanza, hawalii sana kama wale wanaopuuzwa.” Pia ni muhimu kuitikia kwa njia mbalimbali. Ukiitikia kwa njia moja kila wakati, kama vile kwa kumlisha au kumpakata, ataharibika. Wakati mwingine inatosha kuongea tu anapolia. Au kumsogelea na kuzungumza polepole sikioni mwake kunaweza kusaidia. Kwa upande mwingine, kupapasa mgongo au tumbo lake kunaweza kusaidia pia.
“Kazi ya mtoto ni kulia tu.” Huo ni msemo wa Mashariki. Kulia ndiyo njia ya mtoto ya kueleza anachotaka. Ungehisije ikiwa ungepuuzwa kila unapoomba kitu fulani? Basi, mtoto ambaye anahitaji kutunzwa atahisije akipuuzwa kila anapolia? Lakini ni nani anayepaswa kumshughulikia?
Ni Nani Anayepaswa Kumtunza Mtoto?
Sensa ya hivi karibuni nchini Marekani, ilionyesha kwamba asilimia 54 ya watoto hutunzwa kwa kadiri fulani na watu ambao si wazazi wao tangu wanapozaliwa mpaka wanapofikia darasa la tatu. Katika familia nyingi wazazi wote hufanya kazi ili kupata riziki. Hata hivyo, akina mama wengi hupewa likizo ya kujifungua, ikiwezekana, ili kuwatunza watoto wao kwa majuma au miezi kadhaa. Lakini ni nani atakayemlea mtoto baadaye?
Ni wazi kwamba hakuna sheria kali kuhusu jambo hilo. Hata hivyo, ni vizuri kukumbuka kwamba mtoto anahitaji msaada wakati huo muhimu. Wazazi wote wawili wanahitaji kufikiria jambo hilo kwa uzito. Wanapofanya uamuzi wanapaswa kufikiria njia mbalimbali za kushughulikia hali hiyo.
Dakt. Joseph Zanga, wa Chuo cha Marekani cha Tiba ya Watoto, anasema: “Imeonekana kwamba hata kuwaacha watoto watunzwe na walezi bora zaidi hakuwezi kuchukua mahali pa mama na baba.” Wataalamu fulani wamesema kwamba watoto wanaopelekwa kwenye vituo vya utunzaji hawawi na walezi wao kwa muda wa kutosha.
Kwa kuwa wanatambua mahitaji ya watoto wao, akina mama fulani wanaofanya kazi wameamua kuacha kazi ili kuwa na watoto wao badala ya kuwaachia wengine wawatunze. Mwanamke mmoja alisema: “Nimepata uradhi ambao naamini singepata kwa kufanya kazi nyingine yoyote.” Bila shaka, matatizo ya kiuchumi hayawezi kuwaruhusu akina mama wote wafanye hivyo. Wazazi wengi wanalazimika kuwapeleka watoto wao kwenye vituo vya utunzaji, hivyo wao hufanya jitihada nyingi ili kuwa pamoja na watoto na kuwahakikishia upendo wao. Pia, wazazi wengi wasio na mwenzi ambao wanafanya kazi hulazimika kuwapeleka watoto wao kwenye vituo hivyo na hujitahidi sana kuwalea, nao wanapata matokeo mazuri.
Kulea watoto kunaweza kufurahisha, hata kusisimua. Lakini ni kazi ngumu. Unawezaje kufaulu?
[Maelezo ya Chini]
a Katika mfululizo huu, Amkeni! linaelezea maoni ya wataalamu maarufu wa utunzaji wa watoto kwani habari hizi zinaweza kuwasaidia na kuwaelimisha wazazi. Lakini tunapaswa kuelewa kwamba maoni hayo yanaweza kubadilika baada ya muda fulani, tofauti na kanuni za Biblia ambazo Amkeni! huunga mkono kwa ukamili.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 6]
Watoto Wanyamavu
Madaktari fulani huko Japan wanasema kwamba idadi ya watoto ambao hawalii au kutabasamu imeongezeka. Daktari wa watoto, Satoshi Yanagisawa, anawaita watoto wanyamavu. Kwa nini watoto huacha kuonyesha hisia zao? Madaktari fulani wanaamini kwamba hali hiyo hutokea kwa sababu watoto wanapuuzwa na wazazi wao. Nadharia moja inasema kwamba mtoto anapopuuzwa mara nyingi au kueleweka vibaya anapolia, hatimaye anaacha kuonyesha hisia zake.
Kulingana na Dakt. Bruce Perry, daktari mkuu wa akili kwenye Hospitali ya Watoto ya Texas, mtoto anapopuuzwa wakati anapohitaji msaada, sehemu ya ubongo inayomchochea kuwa mwenye huruma huenda isisitawi. Anapopuuzwa kabisa anaweza kushindwa kuonyesha huruma katika maisha yake yote. Dakt. Perry anaamini kwamba huenda hali hiyo ikamfanya mtoto awe mzoefu wa dawa za kulevya na mjeuri anapobalehe.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Uhusiano kati ya mzazi na mtoto huimarika wanapowasiliana
-
-
Kuwaandalia Watoto Mahitaji YaoAmkeni!—2003 | Desemba 22
-
-
Kuwaandalia Watoto Mahitaji Yao
KWA kweli, watoto wanahitaji uangalifu mwingi, na inaonekana wengi hawapati mahitaji yao. Hali ya vijana wengi leo huthibitisha jambo hilo. Mtafiti mmoja aliyenukuliwa katika gazeti The Globe and Mail la Toronto, Kanada, alisema: “Vijana wetu wamejitenga sana na familia zao na hivyo wamekosa uzoefu na hekima.”
Tatizo limetokea wapi? Je, inawezekana tatizo limesababishwa kwa kadiri fulani na kukosa kuona umuhimu wa kuwapa watoto uangalifu? Mwanasaikolojia anayewasaidia wanawake wanaochuma mapato ya chini kujua jinsi ya kuwatunza watoto wao anasema: “Sote tunahitaji kujifunza kuwa wazazi. Na tunapaswa kutambua kwamba tutapata thawabu kubwa sana baadaye tukitumia wakati na watoto wetu sasa.”
Hata watoto wanahitaji kufundishwa kwa ukawaida. Si mara mojamoja tu bali kwa ukawaida, naam, siku nzima. Kutumia wakati pamoja na watoto tangu wakiwa wachanga ni muhimu kwa ukuzi wao.
Wazazi Wanahitaji Kujitayarisha
Wazazi wanahitaji kujitayarisha kabla mtoto hajazaliwa ili watimize wajibu wao mzito. Wanaweza kujifunza kutokana na kanuni ambayo Yesu Kristo alitoa kuhusu umuhimu wa kupangia mambo. Alisema: “Ni nani kati yenu anayetaka kujenga mnara ambaye haketi kwanza na kuhesabu gharama?” (Luka 14:28) Kulea watoto, ambako mara nyingi huitwa mradi wa miaka 20, ni kazi ngumu zaidi kuliko kujenga mnara. Kwa hiyo ili ufanikiwe kumlea mtoto, unahitaji kuupangia mradi huo.
Kwanza, ni muhimu wazazi wajitayarishe kiakili na kiroho. Uchunguzi uliohusisha wanawake 2,000 wajawazito huko Ujerumani ulionyesha kwamba watoto wa akina mama waliotaka kuwa na familia walikuwa na hali nzuri, kihisia na kimwili, kuliko watoto wa akina mama ambao hawakutaka kuwa na watoto. Kwa upande mwingine, mchunguzi mmoja alikadiria kwamba kuna uwezekano wa asilimia 237 kwamba mwanamke aliye katika ndoa yenye matatizo atapata mtoto aliye na matatizo ya kihisia na kimwili kuliko mwanamke aliye katika ndoa isiyo na matatizo.
Basi, ni wazi kwamba akina baba wanachangia sana ukuzi wa mtoto. Dakt. Thomas Verny alisema: “Baba anayempiga na kumpuuza mke wake mjamzito anasababisha hatari kubwa ya kihisia na kimwili kwa mtoto.” Ama kwa hakika, inasemekana kwamba zawadi bora zaidi ambayo mtoto anaweza kupata ni kuwa na baba anayempenda mama yake.
Homoni zinazosababishwa na wasiwasi na mfadhaiko, ambazo hutokezwa katika damu ya mama, zinaweza kumwathiri mtoto akiwa tumboni. Hata hivyo, inadhaniwa kwamba mtoto huwa hatarini mama anapofadhaika sana au kuwa na wasiwasi kwa muda mrefu kuliko anapovunjika moyo au kupatwa na matatizo mara kwa mara. Jambo muhimu zaidi ni jinsi mama anavyohisi kumhusu mtoto wake aliye tumboni.a
Vipi ikiwa u mjamzito na mume wako hakusaidii ama hutaki kuwa na mtoto? Si ajabu kwamba hali fulani zinaweza kumfanya mwanamke ashuke moyo anapokuwa mjamzito. Lakini, sikuzote kumbuka kwamba mtoto wako hana makosa. Basi, unawezaje kuendelea kuwa mtulivu licha ya hali hizo ngumu?
Mamilioni ya watu wamesaidiwa na mwongozo wa hekima unaopatikana katika Neno la Mungu, Biblia. Inasema: “Katika kila jambo kwa sala na dua pamoja na kutoa shukrani maombi yenu na yajulishwe Mungu; na amani ya Mungu yenye ubora unaozidi fikira zote itailinda mioyo yenu na nguvu zenu za akili kwa njia ya Kristo Yesu.” Maneno hayo yanaweza kukusaidia kufuata shauri hili: “Msihangaike juu ya kitu chochote.” (Wafilipi 4:6, 7) Utapata msaada kutoka kwa Muumba anayekujali.—1 Petro 5:7.
Ni Jambo la Kawaida
Akina mama fulani vijana huhuzunika na kuhisi uchovu majuma machache ya kwanza baada ya kupata mtoto. Hata wanawake ambao walitaka sana kuwa na mtoto wanaweza kusononeka. Hilo ni jambo la kawaida. Hiyo ni kwa sababu viwango vya homoni hubadilika-badilika akina mama wanapojifungua. Pia wanawake wanapojifungua kwa mara ya kwanza, wanakuwa na majukumu mbalimbali kama vile kumlisha mtoto, kumbadilisha nepi na kumtunza kila wakati.
Mama mmoja alihisi kwamba mtoto wake analia ili kumkasirisha tu. Si ajabu kwamba mtaalamu wa masuala ya kulea watoto huko Japan alisema: “Akina mama wote hupata mfadhaiko unaotokana na kulea watoto.” Kulingana na mtaalamu huyo, “ni muhimu mama asijitenge kamwe.”
Hata mama akishuka moyo wakati fulani, anaweza kumlinda mtoto wake asiathiriwe na hisia zake zinazobadilika-badilika. Gazeti Time linasema: “Akina mama waliojitahidi kuwatunza watoto wao na kucheza nao licha ya kushuka moyo, waliwasaidia watoto wao kuwa wachangamfu.”b
Jinsi Baba Anavyoweza Kusaidia
Baba anaweza kumsaidia na kumtegemeza mtoto wake. Mtoto anapolia usiku wa manane, mara nyingi baba anaweza kumshughulikia mtoto ili mwenzi wake alale. Biblia inasema: “Ninyi waume, mwishi vizuri pamoja na wake zenu.”—1 Petro 3:7, Verbum Bible.
Yesu Kristo aliwawekea waume mfano bora. Hata alikufa kwa ajili ya wafuasi wake. (Waefeso 5:28-30; 1 Petro 2:21-24) Hivyo, waume wanaojinyima starehe ili kuwatunza watoto wao wanamwiga Kristo. Ama kweli, kulea watoto ni mradi ambao wazazi wote wawili wanapaswa kushiriki.
Ushirikiano
Yoichiro, baba wa msichana wa miaka miwili anasema: “Mimi na mke wangu tumejadiliana kinaganaga jinsi tunavyopaswa kumlea binti yetu. Kila wakati tatizo linapotokea tunajadiliana jinsi ya kulitatua.” Yoichiro anatambua kwamba mke wake anahitaji kupumzika, hivyo yeye huandamana na binti yake katika shughuli mbalimbali.
Zamani, familia zilipokuwa kubwa na zenye umoja, watoto wakubwa na watu wa ukoo waliwasaidia wazazi kuwatunza watoto. Hivyo, mfanyakazi katika Kituo cha Utunzaji wa Watoto huko Kawasaki, Japan, anasema: “Mara nyingi, akina mama hufaidika wanapozungumza na wengine kuhusu jambo hilo. Akina mama wengi wameweza kukabiliana na matatizo waliposaidiwa.”
Gazeti Parents linasema kwamba wazazi “wanahitaji watu wanaoweza kuzungumza nao kuhusu mahangaiko yao.” Watazungumza na nani? Akina mama na baba waliopata mtoto wa kwanza wanaweza kufaidika wakiwa tayari kukubali maoni na kuwasikiliza wazazi wao wenyewe au wakwe zao. Babu na nyanya wanapaswa kutambua kwamba wenzi hao vijana wana haki ya kujiamulia mambo.c
Wazazi vijana wanaweza pia kupata msaada kutoka kwa waamini wenzao. Unaweza kupata watu wenye uzoefu wa miaka mingi katika kulea watoto ambao wako tayari kukusikiliza katika kutaniko la Mashahidi wa Yehova la kwenu. Wanaweza kukupa madokezo yanayofaa. Hata unaweza kuzungumza na “wanawake wenye umri mkubwa,” kama vile Biblia inavyowaita wanawake ambao wamefuata kanuni za Kikristo kwa muda mrefu ambao wako tayari kuwasaidia wanawake vijana.—Tito 2:3-5.
Bila shaka, wazazi wanapaswa kuamua maoni watakayofuata. Yoichiro anasema: “Kila mtu alitushauri.” Mke wake, Takako, anakiri hivi: “Mwanzoni, sikufurahia madokezo ya watu wengine kwa sababu nilihisi wananichambua kwa kuwa sina ujuzi wa kulea watoto.” Hata hivyo, kwa kujifunza kutoka kwa wengine, waume na wake wengi wamesaidiwa kuwa na maoni yanayofaa kuhusu jinsi wanavyoweza kuwatunza watoto wao.
Msaada Bora
Hata ikiwa hakuna mtu aliye tayari kukusaidia, kuna mtu mwenye kutegemeka anayeweza kukuimarisha. Huyo ni Yehova Mungu, aliyetuumba, ambaye macho yake yanaweza kuona hata “kiini-tete” cha watu wote duniani. (Zaburi 139:16) Wakati mmoja Yehova aliwaambia hivi watu wake wa zamani, kama ilivyoandikwa katika Neno lake Biblia: “Je, mke anaweza kumsahau mtoto wake anayenyonya hivi kwamba asimhurumie mwana wa tumbo lake? Hata hawa wanawake wanaweza kusahau, lakini mimi mwenyewe sitakusahau wewe.”—Isaya 49:15; Zaburi 27:10.
Yehova hawasahau wazazi. Amewaandalia maagizo mazuri ya kulea watoto katika Biblia. Kwa mfano, miaka 3,500 hivi iliyopita, Musa nabii wa Mungu aliandika hivi: “Lazima umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa nafsi yako yote na kwa nguvu zako zote.” Kisha Musa akasema: “Maneno haya [kutia ndani shauri la kumpenda na kumtumikia Yehova] ninayokuamuru leo lazima yawe moyoni mwako; nawe uyakazie kwa mwana wako na kuyasema unapoketi katika nyumba yako na unapotembea barabarani na unapolala na unapoamka.”—Kumbukumbu la Torati 6:5-7.
Unafikiri wazo kuu ni nini katika agizo hilo la Neno la Mungu? Ni kwamba unapaswa kuwafundisha watoto wako kila siku kwa ukawaida. Haitoshi tu kuwa na watoto wako mara mojamoja. Kwa kuwa mawasiliano mazuri hutokea bila kupangwa, unahitaji kutenga wakati ili uwe na watoto wako kwa ukawaida. Kufanya hivyo kutakuwezesha kutii amri hii ya Biblia: “Mlee mvulana kulingana na njia inayomfaa.”—Methali 22:6.
Kuwazoeza watoto wako inavyofaa kunatia ndani kuwasomea kwa sauti. Biblia inasema kwamba mwanafunzi wa karne ya kwanza Timotheo, ‘aliyajua maandishi matakatifu tangu utoto mchanga.’ Kwa hiyo, mama yake, Eunike, na nyanya yake Loisi walimsomea kwa sauti alipokuwa angali mtoto. (2 Timotheo 1:5; 3:14, 15) Ni vizuri kuanza kufanya hivyo mara tu unapoanza kuongea na mtoto wako. Lakini utasoma nini, na unawezaje kumfundisha mtoto?
Mtoto wako anapaswa kusikia ukisoma Biblia. Inaonekana Timotheo alisomewa Biblia. Pia kuna vitabu vingine vyenye picha za kupendeza vinavyoweza kumsaidia mtoto kuijua Biblia. Vitabu hivyo humsaidia mtoto kuwazia mambo ambayo Biblia inafundisha. Kwa mfano, kuna Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia na Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi. Vitabu hivyo vimewasaidia mamilioni ya watoto kuingiza mafundisho ya Biblia akilini na moyoni.
Kama Biblia inavyosema, “wana [na mabinti] ni urithi kutoka kwa Yehova; uzao wa tumbo ni thawabu.” (Zaburi 127:3) Muumba wako amekupa “urithi,” mtoto mzuri, anayeweza kukuchangamsha na kukufurahisha. Kulea watoto, hasa wamsifu Muumba wao, ni kazi yenye kufurahisha!
[Maelezo ya Chini]
a Mbali na homoni za mfadhaiko, nikotini, kileo, na dawa nyingine za kulevya zinaweza pia kumwathiri mtoto sana. Akina mama wajawazito wanapaswa kujiepusha kabisa na vitu vyovyote hatari. Isitoshe, ni muhimu kumwuliza daktari kuhusu jinsi dawa zinavyoweza kumwathiri mtoto aliye tumboni.
b Iwapo mama ana huzuni nyingi sana, amevunjika moyo, havutiwi na mtoto wake, na hapendezwi na chochote, huenda anaugua ugonjwa wa kushuka moyo baada ya kujifungua. Ikiwa ndivyo, anapaswa kumwona daktari. Tafadhali ona matoleo ya Amkeni! ya Julai 22, 2002, ukurasa 19-23 na Juni 8, 2003, ukurasa wa 21-23.
c Tafadhali soma makala “Babu na Nyanya—Shangwe Yao, Magumu Yao,” katika toleo la Amkeni! la Machi 22, 1999.
[Picha katika ukurasa wa 8]
Maoni ya mama kuhusu mtoto wake aliye tumboni ni muhimu sana
[Picha katika ukurasa wa 9]
Ingawa mama aliyejifungua karibuni anaweza kuwa na hisia zinazobadilika- badilika, bado anaweza kumsaidia mtoto wake ahisi anapendwa na yuko salama
[Picha katika ukurasa wa 10]
Akina baba wana daraka la kusaidia kuwatunza watoto
-