Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g99 3/8 kur. 19-20
  • Wasemavyo Wataalamu Kuhusu Matibabu Bila Damu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wasemavyo Wataalamu Kuhusu Matibabu Bila Damu
  • Amkeni!—1999
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Vibadala Visivyo na Damu
  • Mashahidi wa Yehova Wawakilishwa
  • Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
    Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
  • Kuokoa Uhai kwa Damu—Jinsi Gani?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Kutia Damu Mishipani—Je, Kutaendelea?
    Amkeni!—2006
  • Maswali ya Funzo la Kijitabu Mashahidi wa Yehova na Suala la Damu
    Huduma Yetu ya Ufalme—1988
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1999
g99 3/8 kur. 19-20

Wasemavyo Wataalamu Kuhusu Matibabu Bila Damu

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NORWAY

“HATA ikiwa nitasahau kila kitu katika mkutano huu, sitasahau kibanda chenu.” Ndivyo alivyosema daktari mmoja aliyehudhuria Mkutano wa 25 wa shirika la International Society of Blood Transfusion, uliofanywa Oslo, Norway, majira ya kiangazi kilichopita (Juni 27 hadi Julai 2, 1998). Alikuwa amezuru tu kibanda cha habari ambacho Mashahidi wa Yehova walikuwa nacho wakiwa waonyeshaji walioidhinishwa.a

Madaktari zaidi ya 1,700 kutoka nchi 83 walihudhuria mkutano huo. Wajumbe wengi waliwakilisha benki za damu, lakini pia kulikuwako wanabiolojia wa damu, madaktari-wapasuaji, na madaktari-nusukaputi. Wataalamu hawa walishiriki habari gani kwenye mkutano huu wa maana? Mashahidi wa Yehova walionyesha nini kwenye maonyesho yao, na walipata itikio gani kutoka kwa wajumbe?

Vibadala Visivyo na Damu

Baadhi ya habari zilizozungumziwa zilikuwa kutia damu mishipani, kupima damu, na vibadala vya kitiba kwa damu ya binadamu. Dakt. C. V. Prowse, wa shirika la Scottish National Blood Transfusion Service, alizungumzia kuhusu “Vibadala kwa Damu ya Kibinadamu na Uwezo wa Damu.” Alitaja vitu fulani vya (kisanisia) vinavyochochea ukuzi vyenye uwezo wa kuongeza viwango vya chembe za damu kwa kuchochea mwili utokeze chembe hizi. Kwa kielelezo, erythropoietin hutokezwa na mafigo na huchochea utokezwaji wa chembe nyekundu za damu. Lakini sasa hizi zaweza kutokezwa katika maabara. Dakt. Prowse alisema kwamba “erythropoietin ya kisanisia imethibitishwa hasa kuwa tiba ya namna mbalimbali za ugonjwa wa kupungukiwa na damu.”

Kitu fulani kinachofanana na hicho kimebuniwa kuchochea mwili utokeze vigandisha-damu. Dakt. Prowse alisema: “Hivi karibuni zaidi wanasayansi wamegundua vitu vinavyochochea ukuzi wa vigandisha-damu katika uwanja huu wa kitaalamu. Dawa ya Interleukin 11 tayari imeidhinishwa kwa sababu ya matokeo yake katika kuongeza idadi ya vigandisha damu . . . , na inaonekana kwamba thrombopoietin na mwenzi wake, rh-PEG-MGDF, karibuni zitaidhinishwa.”

Dakt. Prowse alitaja pia mambo fulani ya kisanisia yanayochangia ugandishaji (protini za plazima) na ambayo yamesaidia watu wenye ugonjwa wa damu kutoganda: “Vitu vya kisanisia vinavyofanana na idadi fulani ya protini za plazima, vimeidhinishwa na katika visa fulani vimethibitishwa kuwa tiba inayopendelewa kwa sababu ya mahangaiko kuhusu ambukizo la vitu vinavyotolewa kwenye plazima.” Dakt. Prowse aliongezea kwamba “idadi fulani ya vitu vinginevyo vya kugandisha sasa vinabuniwa ili vitokezwe.”

N. S. Faithfull, anayehusika na shirika la dawa, alitoa hotuba kuhusu misombo ya perfluorocarbon (PFC). Aina fulani za perfluorocarbon zaweza kusafirisha oksijeni katika mfumo wa mzunguko wa damu. Kemikali za kwanza kutengenezwa kutokana na zile za zamani hazikuthibitika kuwa zenye kutosheleza kama damu “bandia.” Je, maendeleo yamefanywa? Faith­full alisema: “Kwa miaka michache iliyopita, maendeleo zaidi ya tekinolojia ya PFC na majaribio ambayo yamethibitishwa na madaktari yamefanywa kwa kutumia [aina mbili] za emalshani ya PFC.” Alitoa ripoti ya mojawapo ya majaribio hayo yaliyohusisha wagonjwa 256 waliokuwa wakifanyiwa upasuaji wa mifupa, wa uzazi, au wa mfumo wa mkojo—hatua ambazo mara nyingi huhusisha kupoteza damu nyingi. Matokeo yamekuwa gani? “Data kutoka uchunguzi wa aina zote mbili ilionyesha kwamba Kihema cha Oksijeni kilikuwa bora kuliko damu katika kutengua—dalili hizi [dalili huonyesha uhitaji wa kutiwa damu mishipani] na kwamba dalili hizo zilitenguliwa kwa muda mrefu zaidi kuliko kutenguliwa kulikosababishwa na damu inayofanana.”

Mkutano huo ulipashwa habari kwamba ukubwa wa visehemu vya PFC katika emalshani hizo “ni mdogo sana . . . , karibu mara 40 kwa udogo kuliko kipenyo cha RBC [chembe nyekundu ya damu]. Ukubwa huu unawezesha visehemu vya PFC kuvuka mishipa ya damu ambayo haina chembe nyekundu za damu zinazotiririka.” Jambo hili ni lenye manufaa hakika iwapo tishu fulani zisizo na damu zinaharibika.

Tabibu mmoja Mwingereza alikazia uhitaji wa kutumia damu kidogo wakati wa upasuaji. Alitoa himizo hili kwa sababu ya ukosefu wa damu na kwa sababu ya hatari zinazohusishwa na utiaji damu mishipani. Ili kutolea kielezi cha jambo linaloweza kufanywa ili kupunguza matumizi ya damu, alitaja daktari-mpasuaji mmoja aliyetumia damu kwa asilimia 10 tu ya upasuaji wa nyonga aliofanya. Madaktari-wapasuaji fulani katika hospitali hiyohiyo walitumia damu kwa kiwango cha asilimia 70 ya upasuaji wa nyonga waliofanya.

Mashahidi wa Yehova Wawakilishwa

Habari kuhusu vibadala vingi vya namna hiyo na njia zinazotumiwa ilipatikana kwenye kibanda cha Mashahidi wa Yehova. Kibandiko kimoja kilionyesha kwamba ulimwenguni pote, vitivo vya kitiba 120 sasa vinatoa dawa isiyo na damu, na wakachapisha taarifa zilizofupishwa kutoka kwenye makala za kitiba takriban 1,000. Habari ilitolewa kuhusu njia mbalimbali za kuepuka utiaji damu mishipani—mbinu ambazo zaweza kutumiwa kabla ya upasuaji, wakati wa upasuaji, na baada ya upasuaji.

Itikio lilikuwa nzuri sana. Wakati wa mkutano huo Mashahidi waliokuwa kwenye kibanda hicho walizungumza na madaktari takriban 480—ambao wengi wao walirudi ili kupata habari zaidi, hata wakaja pamoja na wafanyakazi wenzao. Profesa wa unusukaputi na upasuaji kutoka California alisema hivi: “Inapendeza sana.” Profesa mmoja kutoka Ujerumani alisema: “Ninaweza kutumia habari hii kufundisha wanafunzi wangu.” Daktari aliyewakilisha benki kubwa zaidi ya damu nchini China alisema: “Tunahi­taji sana habari hii kwa sababu ya upungufu wa damu.”

Siku ambayo alipokea taarifa iliyochapishwa, msimamizi wa benki ya damu wa hospitali ya Norway alirudi na kusema: “Je, naweza kupata mbili au tatu zaidi? Nitawapatia madaktari-­wapasuaji na madaktari-nusukaputi na kuwaambia watumie mbinu hizi ili kupunguza au ­kuepuka matumizi ya damu kuhusiana na upasuaji.” Daktari mwingine alisema: “Hiki ndicho kibanda chenye kuvutia zaidi kwenye mkutano huu.”

Mashahidi wa Yehova wamekuwa watendaji tufeni pote katika kuwasaidia watu wapate madaktari wanaoweza na watakaotibu wagonjwa bila kuwatia damu mishipani. Pia Mashahidi wametoa habari za karibuni kuhusu vibadala vya damu vinavyoweza kutumiwa badala ya kutia damu mishipani. Kwenye mkutano huo, mamia ya madaktari, kutia ndani madaktari-wapasuaji, na wafanyakazi wa kitiba wengineo kutoka nchi nyingi, walivutiwa na habari hiyo. Jambo hili lapaswa kuwaathiri ifaavyo watu hawa wanapojaribu kutumia mbinu na vibadala vingi ambavyo hufanya kutiwa damu mishipani kusiwe kwa lazima.

[Maelezo ya Chini]

a Kwa sababu za kidini, Mashahidi wa Yehova hawakubali kutiwa damu mishipani, na badala yake huomba matibabu yasiyohusisha damu. (Matendo 15:28, 29) Kwa habari kuhusu kiini cha habari hii na kwa nini kuwe na kukubali sababu kuhusu jambo hili, ona broshua Damu Yaweza Kuokoaje Uhai Wako?, iliyochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki