-
Sayansi na Dini Mwanzo wa UbishiMnara wa Mlinzi—2005 | Aprili 1
-
-
Sayansi na Dini Mwanzo wa Ubishi
MTAALAMU wa nyota mwenye umri wa miaka 70 alikuwa mahututi kitandani, akisoma kwa shida. Mikononi mwake alikuwa na mswada wa hati yake, uliokuwa tayari kuchapishwa. Iwe alijua au hakujua, kitabu chake kingebadili kabisa maoni ya wanadamu kuhusu ulimwengu. Pia kilianzisha ubishi mkali katika dini za Kikristo, ubishi ambao umeendelea hadi leo hii.
Huyo alikuwa Nicolaus Copernicus, Mkatoliki Mpolandi, katika mwaka wa 1543. Kitabu hicho cha Copernicus (On the Revolutions of the Heavenly Spheres) kilidai kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu wala si dunia. Kupitia kitabu hicho kimoja tu, Copernicus alibadili dhana tata ya kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu na kuanzisha dhana nyingine rahisi lakini yenye kuvutia.
Mwanzoni, haikudhaniwa kwamba suala hilo lingezusha ubishi mkali. Sababu moja ni kwamba Copernicus alitoa hoja zake kwa busara. Isitoshe, Kanisa Katoliki lililokuwa limekubali dhana ya kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu, halikupinga dhana za kisayansi za wakati huo. Hata papa mwenyewe alimhimiza Copernicus achapishe kitabu chake. Hatimaye Copernicus alipochapisha kitabu hicho, mhariri wa kitabu hicho aliyekuwa na wasiwasi aliandika utangulizi wake na kusema kwamba dhana ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu inapatana na hesabu ingawa si lazima iwe kweli kisayansi.
Ubishi Wapamba Moto
Kisha akatokea Galileo Galilei, (1564-1642) Mwitaliano Mkatoliki aliyekuwa mtaalamu wa nyota, mwanahisabati, na mwanafizikia. Akitumia darubini yenye lenzi iliyobuniwa karibuni, Galileo aliona anga vizuri zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Uchunguzi wake ulimsadikisha kwamba Copernicus hakuwa amekosea. Galileo pia aliona madoa kwenye jua, jambo ambalo lilitatanisha dhana nyingine iliyopendwa sana ya kifalsafa na kidini ya kwamba jua haliwezi kubadilika wala kuharibika.
Tofauti na Copernicus, Galileo alisambaza dhana zake kwa ujasiri na bidii. Na alifanya hivyo licha ya chuki kali sana ya kidini kwa sababu kufikia wakati huo Kanisa Katoliki lilipinga waziwazi nadharia ya Copernicus. Kwa hiyo, Galileo alipodai dhana ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu ni sahihi na inapatana na Maandiko, kanisa lilimwona kuwa mzushi.a
Galileo alienda Roma kujitetea lakini hakufaulu. Mwaka wa 1616 kanisa lilimwamuru akome kumuunga mkono Copernicus. Galileo alinyamazishwa kwa muda. Halafu mwaka wa 1632 alichapisha kitabu kingine kilichomuunga mkono Copernicus. Mwaka uliofuata, Baraza la Kuhukumu Wazushi lilimhukumu Galileo kifungo cha maisha. Hata hivyo, kwa sababu ya umri wake, walibadili kifungo hicho wakaamua kumzuia nyumbani.
Watu wengi wanauona ubishi kati ya Galileo na kanisa kuwa ushindi wa sayansi dhidi ya dini na hata Biblia. Hata hivyo, kama tutakavyoona katika makala inayofuata, mkataa huo sahili unapuuza mambo mengi ya hakika.
[Maelezo ya Chini]
a Galileo alikosana na watu wengi kwa sababu ya kejeli na maneno yake yenye kuumiza. Pia, kwa kudai dhana ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu inapatana na Maandiko, alijifanya kuwa ana ujuzi mwingi wa kidini jambo ambalo lilikera kanisa zaidi.
-
-
Sayansi na Biblia—Je, Kweli Zinapingana?Mnara wa Mlinzi—2005 | Aprili 1
-
-
Sayansi na Biblia—Je, Kweli Zinapingana?
DHANA iliyoanzisha ubishi kati ya Galileo na Kanisa Katoliki ilianza zamani kabla ya Copernicus na Galileo kuzaliwa. Dhana ya kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu ilikubaliwa na Wagiriki wa kale na kusambazwa na mwanafalsafa Aristotle (384-322 K.W.K.) na Ptolemy, mtaalamu wa nyota aliyekuwa pia mnajimu (karne ya pili W.K.).a
Dhana ya Aristotle kuhusu ulimwengu ilitegemea maoni ya mwanahisabati na mwanafalsafa Mgiriki, Pythagoras (karne ya sita K.W.K.). Akifuata maoni ya Pythagoras ya kwamba duara na tufe ni maumbo kamili, Aristotle aliamini kwamba mbingu zina matabaka kama ya kitunguu. Kila tabaka lilifanyizwa kwa fuwele, dunia ikiwa katikati kabisa. Nyota zilizunguka kwenye tabaka la juu, chanzo cha nguvu za kimungu. Aristotle aliamini pia kwamba jua na vitu vingine vya angani vilikuwa kamili, havikuwa na doa au kasoro yoyote wala havingeweza kubadilika.
Nadharia ya Aristotle ilitokana na falsafa wala si sayansi. Kwa maoni yake, wazo la kwamba dunia inazunguka halikupatana na akili. Pia alikataa dhana ya kwamba dunia iko katika nafasi tupu na hivyo aliamini kwamba pasipo na nguvu zinazoisukuma daima, ingepunguza mwendo wake na kuacha kuzunguka kwa sababu ya msuguano. Kwa miaka 2,000 hivi watu waliamini nadharia ya Aristotle kwa kuwa ilionekana kuwa inapatana na akili wakati huo. Hata kufikia karne ya 16, mwanafalsafa Mfaransa Jean Bodin, alisema hivi kuhusu nadharia hiyo: “Hakuna mtu mwenye akili au aliye na ujuzi kidogo wa fizikia, anaweza kufikiri kwamba dunia ambayo ni kubwa na nzito . . . , huyumba-yumba . . . huzunguka katika mhimili wake na kulizunguka jua; kwa kuwa dunia ikisogea kidogo tu, majiji na ngome, miji na milima itaporomoka.”
Kanisa Lakubali Nadharia ya Aristotle
Ubishi mwingine kati ya Galileo na kanisa ulitokea katika karne ya 13 na ulihusisha Mkatoliki maarufu, Thomas Aquinas (1225-1274). Aquinas alimheshimu sana Aristotle, hata alimwita Mwanafalsafa Mkuu. Kwa miaka mitano Aquinas alijitahidi sana kupatanisha falsafa ya Aristotle na mafundisho ya kanisa. Katika kitabu chake (Galileo’s Mistake), Wade Rowland aliandika kwamba kufikia wakati wa Galileo, “mchanganyiko wa nadharia ya Aristotle na mafundisho ya Aquinas ulikuwa fundisho la msingi katika Kanisa Katoliki.” Pia, kumbuka kwamba nyakati hizo hakukuwa na tofauti kati ya wanasayansi na wanadini. Dini ndiyo iliyosimamia elimu. Kwa kawaida dini ndiyo iliyoamua masuala ya kidini na ya kisayansi.
Huo ndio uliokuwa mwanzo wa ubishi kati ya kanisa na Galileo. Hata kabla ya kujihusisha na elimu ya nyota, Galileo alikuwa ameandika makala rasmi kuhusu mwendo. Alitilia shaka dhana nyingi za Aristotle. Hata hivyo, Galileo alifikishwa mbele ya Baraza la Kuhukumu Wazushi mwaka wa 1633 kwa sababu ya kusisitiza kuwa nadharia ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu inapatana na Maandiko.
Alipokuwa akijitetea, Galileo alisisitiza kuwa anaamini kabisa kwamba Biblia ni Neno la Mungu lililoongozwa kwa roho. Pia alisema kwamba Maandiko yaliandikwa kwa ajili ya watu wa kawaida na mistari ya Biblia inayozungumzia kuzunguka kwa jua haipaswi kufasiriwa kihalisi. Hata hivyo, hakufanikiwa. Kwa kuwa Galileo alikataa ufasiri wa Maandiko uliotegemea falsafa za Kigiriki, alihukumiwa! Katika mwaka wa 1992 ndipo Kanisa Katoliki lilipokubali rasmi kuwa lilikosea katika kumhukumu Galileo.
Mambo Tunayoweza Kujifunza
Tunaweza kujifunza nini kutokana na matukio hayo? Kwanza kabisa, Galileo hakuipinga Biblia. Badala yake, alitilia shaka mafundisho ya kanisa. Mwandishi mmoja wa mambo ya kidini aliandika: “Inaonekana kwamba jambo tunaloweza kujifunza kutokana na kisa cha Galileo si kwamba Kanisa lilishikamana sana na kweli za Biblia; bali kwamba halikushikamana nazo vya kutosha.” Kwa kuruhusu falsafa ya Kigiriki iathiri mafundisho yake, kanisa lilifuata mapokeo badala ya mafundisho ya Biblia.
Yote hayo yanatukumbusha onyo hili la Biblia: “Mjihadhari: labda kuna mtu ambaye atawachukua ninyi kama windo lake kupitia falsafa na udanganyifu mtupu kulingana na pokeo la wanadamu, kulingana na mambo ya msingi ya ulimwengu na si kulingana na Kristo.”—Wakolosai 2:8.
-