Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w05 4/1 kur. 3-4
  • Sayansi na Dini Mwanzo wa Ubishi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sayansi na Dini Mwanzo wa Ubishi
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ubishi Wapamba Moto
  • Galileo
    Amkeni!—2015
  • “Hata Hivyo Imo Katika Mwendo!”
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1991
  • Mtu Aliyeonyesha Kwamba Dunia Huzunguka
    Amkeni!—2005
  • Mgogoro Kati ya Galileo na Kanisa
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2005
w05 4/1 kur. 3-4

Sayansi na Dini Mwanzo wa Ubishi

MTAALAMU wa nyota mwenye umri wa miaka 70 alikuwa mahututi kitandani, akisoma kwa shida. Mikononi mwake alikuwa na mswada wa hati yake, uliokuwa tayari kuchapishwa. Iwe alijua au hakujua, kitabu chake kingebadili kabisa maoni ya wanadamu kuhusu ulimwengu. Pia kilianzisha ubishi mkali katika dini za Kikristo, ubishi ambao umeendelea hadi leo hii.

Huyo alikuwa Nicolaus Copernicus, Mkatoliki Mpolandi, katika mwaka wa 1543. Kitabu hicho cha Copernicus (On the Revolutions of the Heavenly Spheres) kilidai kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu wala si dunia. Kupitia kitabu hicho kimoja tu, Copernicus alibadili dhana tata ya kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu na kuanzisha dhana nyingine rahisi lakini yenye kuvutia.

Mwanzoni, haikudhaniwa kwamba suala hilo lingezusha ubishi mkali. Sababu moja ni kwamba Copernicus alitoa hoja zake kwa busara. Isitoshe, Kanisa Katoliki lililokuwa limekubali dhana ya kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu, halikupinga dhana za kisayansi za wakati huo. Hata papa mwenyewe alimhimiza Copernicus achapishe kitabu chake. Hatimaye Copernicus alipochapisha kitabu hicho, mhariri wa kitabu hicho aliyekuwa na wasiwasi aliandika utangulizi wake na kusema kwamba dhana ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu inapatana na hesabu ingawa si lazima iwe kweli kisayansi.

Ubishi Wapamba Moto

Kisha akatokea Galileo Galilei, (1564-1642) Mwitaliano Mkatoliki aliyekuwa mtaalamu wa nyota, mwanahisabati, na mwanafizikia. Akitumia darubini yenye lenzi iliyobuniwa karibuni, Galileo aliona anga vizuri zaidi kuliko mtu mwingine yeyote. Uchunguzi wake ulimsadikisha kwamba Copernicus hakuwa amekosea. Galileo pia aliona madoa kwenye jua, jambo ambalo lilitatanisha dhana nyingine iliyopendwa sana ya kifalsafa na kidini ya kwamba jua haliwezi kubadilika wala kuharibika.

Tofauti na Copernicus, Galileo alisambaza dhana zake kwa ujasiri na bidii. Na alifanya hivyo licha ya chuki kali sana ya kidini kwa sababu kufikia wakati huo Kanisa Katoliki lilipinga waziwazi nadharia ya Copernicus. Kwa hiyo, Galileo alipodai dhana ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu ni sahihi na inapatana na Maandiko, kanisa lilimwona kuwa mzushi.a

Galileo alienda Roma kujitetea lakini hakufaulu. Mwaka wa 1616 kanisa lilimwamuru akome kumuunga mkono Copernicus. Galileo alinyamazishwa kwa muda. Halafu mwaka wa 1632 alichapisha kitabu kingine kilichomuunga mkono Copernicus. Mwaka uliofuata, Baraza la Kuhukumu Wazushi lilimhukumu Galileo kifungo cha maisha. Hata hivyo, kwa sababu ya umri wake, walibadili kifungo hicho wakaamua kumzuia nyumbani.

Watu wengi wanauona ubishi kati ya Galileo na kanisa kuwa ushindi wa sayansi dhidi ya dini na hata Biblia. Hata hivyo, kama tutakavyoona katika makala inayofuata, mkataa huo sahili unapuuza mambo mengi ya hakika.

[Maelezo ya Chini]

a Galileo alikosana na watu wengi kwa sababu ya kejeli na maneno yake yenye kuumiza. Pia, kwa kudai dhana ya kwamba jua ndilo kitovu cha ulimwengu inapatana na Maandiko, alijifanya kuwa ana ujuzi mwingi wa kidini jambo ambalo lilikera kanisa zaidi.

[Picha katika ukurasa wa 3]

Copernicus

[Hisani]

Taken from Giordano Bruno and Galilei (German edition)

[Picha katika ukurasa wa 3]

Galileo ajitetea mbele ya Baraza la Roma la Kuhukumu Wazushi

[Hisani]

From the book The Historian’s History of the World, Vol. IX, 1904

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Background: Chart depicting Copernicus’ concept of the solar system

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki