Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • Namna Mtoto Musa Alivyookolewa
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Miriamu, dada yake Musa anaongea na binti ya Farao

      HADITHI YA 28

      Namna Mtoto Musa Alivyookolewa

      TAZAMA mtoto mchanga analia, akakikamata kidole cha mama yule. Huyu ni Musa. Unajua mama huyo mzuri ni nani? Ni binti mfalme wa Misri, binti ya Farao mwenyewe.

      Mama ya Musa alimficha mtoto wake mpaka alipokuwa mwenye umri wa miezi mitatu, kwa sababu hakutaka auawe na Wamisri. Lakini alijua kwamba huenda Musa akaonekana, basi akafanya hivyo ili amwokoe.

      Alichukua kikapu akakitengeneza ili maji yasiingie ndani. Kisha akamweka Musa ndani yake, akakiweka kikapu hicho katika majani marefu kando ya Mto Nailo. Miriamu, dada yake Musa aliambiwa asimame karibu aone itakavyokuwa.

      Mtoto Musa akilia akiwa kwenye kikapu

      Upesi binti Farao akaja kwenye Mto Nailo aoge. Mara moja akaona kikapu katika majani marefu. Akamwita mtumishi wake mmoja, akamwambia: ‘Kaniletee kikapu kile.’ Binti mfalme alipofungua kikapu hicho, lo! aliona mtoto mzuri kama nini! Mtoto Musa alikuwa akilia, naye binti mfalme akamhurumia. Hakutaka amruhusu auawe.

      Miriamu akaja. Unaweza kumwona katika picha hii. Miriamu akamwuliza binti Farao hivi: ‘Niende nikamwite mwanamke Mwisraeli akulelee mtoto huyu?’

      ‘Nenda tafadhali,’ akasema binti mfalme.

      Basi Miriamu akakimbia haraka kwenda kumwambia mama yake. Mama ya Musa alipokuja kwa binti mfalme, binti mfalme akasema: ‘Mchukue mtoto huyu unilelee, nami nitakulipa.’

      Basi mama ya Musa akalea mtoto wake mwenyewe. Baadaye Musa alipokuwa mkubwa kidogo, mama yake alimpeleka kwa binti Farao, aliyemlea kama mwanawe mwenyewe. Hivyo ndivyo Musa alivyokua katika nyumba ya Farao.

      Kutoka 2:1-10.

      Maswali ya Funzo

  • Sababu Musa Alikimbia
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa anakimbia Misri

      HADITHI YA 29

      Sababu Musa Alikimbia

      TAZAMA Musa anakimbia Misri. Unaweza kuwaona wanaume hao wanaomfuata? Unajua kwa nini wanataka kumwua Musa? Ebu tuone kama twaweza kujua.

      Musa alikua katika nyumba ya Farao, mtawala wa Misri. Akawa mwenye akili na mkuu sana. Musa alijua kwamba yeye si Mmisri, bali wazazi wake ni watumwa Waisraeli.

      Siku moja, alipokuwa mwenye miaka 40, Musa alamua kwenda kuona namna watu wake walivyokuwa. Walikuwa wakiteswa sana. Alimwona Mmisri akimpiga mtumwa Mwisraeli. Musa akatazama huku na huku, na alipokosa kumwona mtu yeyote, alimpiga Mmisri mpaka akafa, kisha Musa akaficha mwili wake katika mchanga.

      Kesho yake Musa akatoka tena kuwaona watu wake. Alifikiri angeweza kuwasaidia wasiwe watumwa tena. Lakini aliona wanaume Waisraeli wakipigana, basi akamwambia yule aliyekuwa na kosa hivi: ‘Kwa nini unampiga sana ndugu yako?’

      Mwanamume huyo akasema: ‘Nani aliyekufanya wewe uwe mtawala na hakimu wetu? Je! utaniua mimi kama ulivyomwua yule Mmisri?’

      Musa akaogopa. Alifahamu kwamba watu wamejua alilomtenda yule Mmisri. Hata Farao alisikia habari hizo, naye akawatuma watu wakamwue Musa. Ndiyo sababu Musa alilazimika kukimbia Misri.

      Musa alipoondoka Misri, alikwenda mbali kwenye nchi ya Midiani. Ndiko alikokutana na jamaa ya Yethro, akaoa binti yake mmoja jina lake Sipora. Musa akawa mchungaji wa kondoo za Yethro. Alikaa katika nchi hiyo ya Midiani kwa miaka 40. Sasa akawa mwenye umri wa miaka 80. Ndipo siku moja, Musa alipokuwa akichunga kondoo za Yethro, kulitokea ajabu moja iliyogeuza maisha yote ya Musa. Fungua ukurasa mwingine, tuone ajabu hiyo ni nini.

      Kutoka 2:11-25; Matendo 7:22-29.

      Maswali ya Funzo

  • Mti Mdogo Unaowaka Moto
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa na mti mdogo unaowaka moto

      HADITHI YA 30

      Mti Mdogo Unaowaka Moto

      MUSA alikuwa amekwenda mpaka kwenye Mlima wa Horebu ili atafute majani ya kondoo zake. Akaona mti mdogo ukiwaka moto, lakini haukuteketea!

      ‘Hii ni ajabu,’ Musa akawaza. ‘Nitakaribia zaidi nione vizuri.’ Alipokaribia, sauti ikatoka katika mti huo mdogo ikisema: ‘Usije karibu zaidi. Ondoa viatu vyako, kwa sababu unasimama mahali patakatifu.’ Mungu alikuwa akisema kupitia kwa malaika, hivyo Musa akafunika uso wake.

      Kisha Mungu akasema: ‘Nimeyaona mateso ya watu wangu huko Misri. Basi nitawaokoa, nami nanakutuma wewe ukawatoe watu wangu Misri.’ Yehova alikusudia kuwapeleka watu wake kwenye nchi nzuri ya Kanaani.

      Lakini Musa akasema: ‘Mimi ni mtu tu. Nifanyeje hivyo? Nikienda nao Waisraeli wataniuliza, “Nani aliyekutuma?” Nitasema nini?’

      ‘Utasema hivi,’ Mungu akajibu. ‘“YEHOVA Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakoo amenituma kwenu.”’ Yehova akaongezea: ‘Hilo ndilo jina langu milele.’

      ‘Lakini kama hawaniamini nikisema umenituma, hapo itakuwaje,’ Musa akajibu.

      ‘Nini hicho mkononi mwako?’ Mungu akauliza.

      Musa akajibu: ‘Fimbo.’

      ‘Itupe chini,’ Mungu akasema. Musa alipoitupa chini, fimbo ikawa nyoka. Kisha Yehova akamwonyesha Musa muujiza mwingine. Akasema: ‘Ingiza mkono wako katika vazi lako.’ Musa akaingiza, na alipoutoa mkono wake, ulikuwa mweupe kama theluji! Mkono huo ulikuwa kama umepatwa na ugonjwa mbaya unaoitwa ukoma. Kisha Yehova akampa Musa uwezo wa kufanya mwujiza wa tatu. Halafu akamwambia hivi: ‘Utakapofanya miujiza hii Waisraeli wataamini kwamba nimekutuma.’

      Baada ya hayo Musa akaenda nyumbani na kumwambia Yethro hivi: ‘Tafadhali uniruhusu nirudi kwa watu wangu huko Misri nione wa hali gani.’ Basi Yethro akamwambia Musa, kwa heri, naye Musa akaanza safari ya kurudi Misri.

      Kutoka 3:1-22; 4:1-20.

      Maswali ya Funzo

  • Musa na Haruni Wanamwona Farao
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa na Haruni wakiwa mbele ya Farao

      HADITHI YA 31

      Musa na Haruni Wanamwona Farao

      MUSA aliporudi Misri, akamwambia Haruni ndugu yake habari ya miujiza yote. Musa na Haruni walipowaonyesha Waisraeli miujiza hiyo, watu wote wakaamini kwamba Yehova alikuwa nao.

      Kisha Musa na Haruni wakaenda kumwona Farao. Wakamwambia: ‘Yehova Mungu wa Israeli anasema, “Waruhusu watu wangu waende mwendo wa siku tatu, wakaniabudu jangwani.”’ Lakini Farao akajibu hivi: ‘Mimi simwamini Yehova. Na sitawaruhusu Waisraeli waende.’

      Farao alikasirika, kwa sababu watu walitaka wapewe ruhusa ya kwenda kumwabudu Yehova. Basi akawalazimisha wafanye kazi ngumu hata zaidi. Waisraeli wakamlaumu Musa kwa sababu waliteswa vibaya sana, naye Musa akahuzunika. Lakini Yehova akamwambia asisumbuke. ‘Nitamfanya Farao aruhusu watu wangu waende,’ Yehova akasema.

      Nyoka ya Haruni inakula nyoka wengine

      Musa na Haruni wakaenda kumwona Farao tena. Wakati huu walifanya mwujiza. Haruni akaitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka mkubwa. Lakini watu wenye akili wa Farao pia wakazitupa fimbo zao chini, nyoka wakatokea. Lakini, ebu tazama! Nyoka wa Haruni anakula wale nyoka wa watu wenye akili. Hata hivyo Farao hataki kuwaruhusu Waisraeli waende.

      Basi wakati wa Yehova ukafika wa kuonyesha yeye ana uwezo kuliko Farao. Unajua alivyofanya? Ni kwa kuleta mapigo 10 au taabu kubwa, juu ya Misri.

      Baada ya mapigo mengi kidogo, Farao akaagiza Musa aitwe, na kusema: ‘Lizuie pigo, nami nitawapa ruhusa Waisraeli waende.’ Lakini pigo hilo lilipozuiwa, Farao aligeuza nia yake. Hakuwaruhusu watu waende. Lakini, mwishowe, baada ya pigo la 10, Farao alifukuza Waisraeli.

      Je! Unajua mapigo hayo 10 yalikuwa gani? Fungua ukurasa unaofuata tuone.

      Kutoka 4:27-31; 5:1-23; 6:1-13, 26-30; 7:1-13.

      Maswali ya Funzo

  • Mapigo 10
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Mto Naili wabadilika na kuwa damu, pigo la kwanza

      HADITHI YA 32

      Mapigo 10

      TAZAMA picha hizi. Kila moja inaonyesha pigo ambalo Yehova alileta juu ya Misri. Katika picha ya kwanza unaweza kumwona Haruni akiupiga Mto Nailo kwa fimbo yake. Alipoupiga, maji ya mto yakawa damu. Samaki wakafa, nao mto ukaanza kunuka vibaya.

      Farao anawafukuza vyura kitandani mwake, pigo la pili

      Kisha, Yehova akafanya vyura watoke katika Mto Nailo. Walikuwa mahali pote—katika majiko ya kuokea mikate, vikaangio, katika vitanda vya watu—mahali pote. Vyura hao walipokufa Wamisri waliwakusanya wengi sana, na nchi ikanuka vibaya.

      Halafu Haruni akaipiga ardhi kwa fimbo yake, nayo mavumbi yakawa chawa. Hao ni wadudu wadogo wanaouma. Chawa walikuwa pigo la tatu juu ya nchi ya Misri.

      Mwanamke anaumwa na chawa, pigo la tatu

      Mapigo mengine yaliumiza Wamisri peke yao, si Waisraeli. Pigo la nne lilikuwa mainzi wakubwa waliojaa katika nyumba za Wamisri wote. Pigo la tano lilikuwa juu ya wanyama. Ng’ombe na kondoo na mbuzi wengi wa Wamisri wakafa.

      Kisha, Musa na Haruni wakachukua majivu na kuyatupa angani. Yakawa vidonda vibaya juu ya watu na wanyama. Hilo lilikuwa pigo la sita.

      Baada ya hapo Musa akainua mkono wake kuelekea angani, naye Yehova akapeleka ngurumo na mvua ya mawe. Ilikuwa mvua ya mawe iliyo mbaya zaidi kuipiga Misri.

      Pigo la nane lilikuwa kundi la nzige. Nzige hao wengi sana hawakuwa wameonekana kabla ya hapo wala baadaye. Walikula kila kitu ambacho mvua ya mawe haikuharibu.

      Wamisri wanajaribu kukimbia mainzi, pigo la nne
      Wanyama wa Waisraeli wanakufa, pigo la tano

      Pigo la tisa lilikuwa giza. Kwa muda wa siku tatu giza zito liliifunika nchi, lakini Waisraeli wakawa na nuru katika makao yao.

      Mwishowe Mungu akawaambia watu wake wapake damu ya mwana-mbuzi au mwana-kondoo juu ya milango yao. Kisha malaika wa Mungu akapita juu ya Misri. Malaika huyo alipoiona damu, hakuua mtu ye yote katika nyumba hiyo. Lakini katika nyumba zote ambazo damu haikupakwa juu ya milango, malaika wa Mungu aliua wazaliwa wa kwanza wa wanadamu na wa wanyama. Hilo lilikuwa pigo la 10.

      Baada ya pigo hilo, Farao akawaambia Waisraeli waondoke. Watu wa Mungu wote walikuwa tayari kwenda, na usiku uo huo wakaanza kutoka Misri.

      Kutoka sura ya 7 hadi 12.

      Maswali ya Funzo

  • Kuvuka Bahari Nyekundu (ya Shamu)
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa atenganisha Bahari Nyekundu kwa nguvu za Mungu

      HADITHI YA 33

      Kuvuka Bahari Nyekundu (ya Shamu)

      TAZAMA tukio hili! Yule ni Musa akiwa na fimbo imenyoshwa juu ya Bahari Nyekundu. Wale walio pamoja naye salama upande mwingine ni Waisraeli. Lakini Farao na jeshi lake lote wanazama katika bahari. Na tuone ilivyokuwa.

      Kama tulivyojifunza, Farao aliwaambia Waisraeli waondoke Misri Mungu alipokwisha kuleta pigo la 10 juu ya Wamisri. Wanaume Waisraeli karibu 600,000 wakaondoka, pia wanawake na watoto wengi. Pia, hesabu kubwa ya watu wengine, waliokuwa wamemwamini Yehova, wakaondoka pamoja na Waisraeli. Wote walichukua kondoo na mbuzi na ng’ombe zao wakaenda nazo.

      Kabla ya kuondoka, Waisraeli waliwaomba Wamisri wawape mavazi na vitu vya dhahabu na fedha. Wamisri hao waliogopa sana, kwa sababu ya lile pigo la mwisho lililowapata. Basi wakawapa Waisraeli kila kitu walichowaomba.

      Baada ya siku chache Waisraeli wakafika kwenye Bahari Nyekundu. Wakapumzika huko. Wakati huo, Farao na watu wake walianza kuhuzunika kwa vile wamewafukuza Waisraeli. ‘Tumeacha watumwa wetu wakaenda!’ wakasema.

      Hivyo Farao akabadili tena nia yake. Upesi akatayarisha gari lake la vita na jeshi lake. Kisha akaanza kuwafuatia Waisraeli akiwa na magari ya pekee 600, pia magari mengine yote ya Misri.

      Waisraeli walipomwona Farao na jeshi lake wakiwafuata, waliogopa sana. Hakukuwa na njia ya kukimbilia. Ile Bahari Nyekundu ilikuwa upande wao mmoja na Wamisri upande mwingine. Lakini Yehova aliweka wingu kati ya watu wake na Wamisri. Hivyo Wamisri hawakuweza kuwaona Waisraeli wawashambulie.

      Kisha Yehova akamwambia Musa anyoshe fimbo yake juu ya Bahari Nyekundu. Alipoinyosha, Yehova akafanya upepo wenye nguvu wa mashariki uvume. Yale maji ya bahari yalitengana, yakasimama pande mbili.

      Ndipo Waisraeli wakaanza kutembea katika bahari katika nchi kavu. Ilichukua saa nyingi ili mamilioni ya watu pamoja na wanyama wao wapite salama katika bahari kwenda upande mwingine. Mwishowe Wamisri waliweza kuwaona Waisraeli tena. Watumwa wao walikuwa wakikimbia! Basi wakaingia haraka katika bahari wakiwafuata.

      Walipoingia, Mungu alifanya magurudumu ya magari yao yatoke. Wamisri wakaanza kuogopa na kupaza sauti hivi: ‘Yehova anawapigania Waisraeli. Na tuondoke huku!’ Lakini walikuwa wamechelewa.

      Wakati huo ndipo Yehova alipomwambia Musa anyoshe fimbo yake juu ya Bahari Nyekundu, kama ulivyoona katika picha. Musa alipofanya hivyo, zile kuta zilianza kurudi na kuwafunika Wamisri na magari yao. Jeshi lote lilikuwa limewafuata Waisraeli katika bahari. Hakuna hata mmoja wa Wamisri hao aliyeokoka!

      Maji ya Bahari Nyekundu yanarudi na kuwafunika Farao na magari ya Wamisri

      Lo! watu wote wa Mungu walifurahi kwa vile walivyookoka! Wanaume wakaimba wimbo wa kumshukuru Yehova, wakisema: ‘Yehova amepata ushindi mtukufu. Amewatupa farasi na wanaowapanda baharini.’ Miriamu dada ya Musa akachukua matari yake, nao wanawake wote wakamfuata wakiwa na matari yao. Na walipokuwa wakicheza kwa furaha, waliimba wimbo ule ule walioimba wanaume wakisema: ‘Yehova amepata ushindi mtukufu. Amewatupa farasi na wanaowapanda baharini.’

      Kutoka sura ya 12 mpaka 15.

      Maswali ya Funzo

  • Aina Mpya ya Chakula
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Mama Mwisraeli na mwanaye wakiokota mana

      HADITHI YA 34

      Aina Mpya ya Chakula 34

      UNAJUA watu wanaokota nini chini? Ni cheupe, na chembamba na chenye kupasuka vipande vyembamba. Ni chakula.

      Umekuwa karibu mwezi mmoja tu tangu Waisraeli waondoke Misri. Wamo jangwani. Humo chakula kidogo kinamea, watu wanalia, wakisema: ‘Afadhali Yehova angetuua huko Misri. Tulikula huko kila chakula tulichotaka.’

      Basi Yehova asema: ‘Nitatelemsha chakula kutoka angani.’ Ndivyo Yehova anafanya. Kesho yake Waisraeli wanapoona chakula hicho cheupe kilichoanguka, wanaulizana hivi: ‘Ni nini hiki?’

      Musa anajibu: ‘Ndicho chakula ambacho Yehova amewapa mle.’ Watu wanakiita MANA. Utamu wake ni kama keki (mkate) nyembamba zenye asali.

      ‘Kila mtu aokote anachoweza kula,’ Musa anawaambia watu. Basi kila asubuhi wanaokota hivyo. Jua linapokuwa kali, ile mana iliyoachwa chini inayeyuka.

      Pia Musa anasema: ‘Mtu asiweke mana ikae mpaka kesho.’ Lakini watu wengine hawasikii. Unajua inavyokuwa? Kesho yake ile mana waliyoweka inajaa wadudu, inaanza kunuka vibaya!

      Waisraeli wakiokota mana

      Walakini kuna siku moja katika juma ambayo Yehova anawaambia watu wakusanye mana nyingi mara mbili. Siku hiyo ni ya sita. Yehova anawaambia waweke akiba ya kesho, kwa sababu hataangusha mana yoyote siku ya saba. Wanapoweka akiba ya siku ya saba, haijai wadudu wala kunuka! Huo ni mwujiza mwingine.

      Miaka yote ambayo Waisraeli walikuwa jangwani Yehova aliwalisha mana.

      Kutoka 16:1-36; Hesabu 11:7-9; Yoshua 5:10-12.

      Maswali ya Funzo

  • Yehova Anatoa Sheria Zake 35
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa akipokea sheria za Mungu katika Mlima Sinai

      HADITHI YA 35

      Yehova Anatoa Sheria Zake 35

      KARIBU miezi miwili baada ya Waisraeli kuondoka Misri, wanakuja kwenye Mlima Sinai unaoitwa pia Horebu. Ni pale pale ambapo Yehova alisema na Musa katika mti mdogo uliowaka moto. Watu wanapiga kambi hapa na kukaa kidogo.

      Watu wanapongojea chini, Musa apanda mlima. Katika mlima, Yehova anamwambia Musa kwamba Yeye anataka Waisraeli wamtii na kuwa watu Wake wa pekee. Musa anaposhuka, anawaambia Waisraeli maneno ya Yehova. Watu hao wanasema kwamba watamtii Yehova, kwa sababu wanataka kuwa watu wake.

      Sasa Yehova anafanya mwujiza. Anafanya kilele cha mlima kitoke moshi, na kufanyiza ngurumo yenye sauti kubwa. Pia anawaambia watu hivi: ‘Mimi ni Yehova Mungu wenu niliyewatoa Misri.’ Kisha anawaamuru hivi: ‘Usiabudu miungu mingine isipokuwa mimi.’

      Mungu anawapa Waisraeli amri nyingine tisa, au sheria. Watu wanaogopa sana. Wanamwambia Musa hivi: ‘Wewe sema na sisi, kwa sababu Mungu akisema na sisi huenda tukafa.’

      Baadaye Yehova anamwambia Musa hivi: ‘Njoo kwangu mlimani. Nitakupa mabamba mawili ya mawe ambapo nimeandika sheria ninazotaka watu washike.’ Tena Musa anapanda mlimani. Anakaa huko muda wa siku 40 mchana na usiku.

      Mungu ana sheria nyingi nyingi za kuwapa watu. Musa anaziandika sheria hizo. Pia Mungu anampa Musa mabamba mawili ya mawe. Juu ya hayo, Mungu mwenyewe ameandika sheria 10 alizowaambia watu wote. Zinaitwa Amri Kumi.

      Amri Kumi ni sheria za maana. Hata sheria nyingine nyingi ambazo Mungu anawapa Waisraeli ni za maana. Moja ya hizo sheria ni hii: ‘Inakupasa umpende Yehova Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote, kwa nafsi yako yote na nguvu zako zote.’ Nyingine ni hii: ‘Inakupasa umpende jirani yako kama unavyojipenda.’ Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, alisema kwamba hizo ndizo sheria mbili zilizo kubwa kuliko zote ambazo Yehova aliwapa watu wake Waisraeli. Baadaye tutajifunza mambo mengi juu ya Mwana wa Mungu na mafundisho yake.

      Kutoka 19:1-25; 20:1-21; 24:12-18; 31:18; Kumbukumbu la Torati 6:4-6; Mambo ya Walawi 19:18; Mathayo 22:36-40.

      Maswali ya Funzo

  • Ndama ya Dhahabu 36
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Waisraeli wakiimba, wakicheza dansi, na kuabudu ndama ya dhahabu

      HADITHI YA 36

      Ndama ya Dhahabu 36

      MAMA WEE! Sasa watu wanafanya nini? Wanaabudu ndama! Kwa nini wanafanya hivyo?

      Musa anapokawia mlimani, watu wasema hivi: ‘Hatujui yaliyompata Musa. Basi na tufanye mungu atutoe katika nchi hii.’

      ‘Vema,’ Haruni ndugu yake Musa asema. ‘Vueni pete zenu za dhahabu masikioni mniletee.’ Haruni anaziyeyusha na kufanya ndama ya dhahabu. Kisha watu wasema hivi: ‘Huyu ni Mungu wetu, aliyetutoa katika Misri!’ Halafu Waisraeli wanafanya karamu kubwa, na kuiabudu ndama hiyo ya dhahabu.

      Yehova anapoona hayo, anakasirika sana. Anamwambia Musa hivi: ‘Fanya haraka ushuke. Watu wanafanya vibaya sana. Wamesahau sheria zangu nao wanaabudu ndama ya dhahabu.’

      Musa anavunja mabamba mawili ya mawe yaliyokuwa yameandikwa Amri Kumi

      Musa anashuka haraka mlimani. Anapokaribia, anaona hivi. Watu wanaimba na kucheza wakizunguka ndama ya dhahabu! Musa anakasirika sana hata anayatupa chini mabamba mawili ya mawe yenye kuandikwa sheria, nayo yanavunjika-vunjika. Kisha anachukua ndama ya dhahabu na kuiyeyusha kabisa. Halafu anaisaga kuwa unga.

      Watu wamefanya jambo baya sana. Musa anawaambia wanaume kati yao wachukue panga zao. ‘Wale watu wabaya walioiabudu ndama ya dhahabu lazima wafe,’ Musa anasema. Basi wanaume hao wanawaua watu 3,000! Inatupasa tumwabudu Yehova pekee kuliko miungu ya uongo, sivyo?

      Kutoka 32:1-35.

      Maswali ya Funzo

  • Hema ya Ibada
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Maskani au hema la mkutano lililotumiwa na Waisraeli

      HADITHI YA 37

      Hema ya Ibada

      UNAJUA jengo hili? Ni hema ya pekee ya kuabudia Yehova. Watu walimaliza kuijenga mwaka mmoja baada ya kuondoka Misri. Unajua aliyetoa wazo la kuijenga?

      Ni Yehova. Musa alipokuwa katika Mlima Sinai, Yehova alimwambia namna ya kuijenga. Alimwambia ijengwe ili iwe vyepesi kubomolewa. Kwa njia hiyo sehemu zake zingeweza kuchukuliwa mahali pengine, na kuunganishwa tena. Basi Waisraeli walipokuwa wakihama hapa na pale jangwani, walichukua hema hiyo.

      Ukitazama ndani ya chumba kidogo mwishoni mwa hema, unaweza kuona sanduku, au kasha. Hilo laitwa sanduku la agano. Kila upande ulikuwa na malaika au kerubi mmoja wa dhahabu. Tena Mungu aliziandika Amri Kumi juu ya mabamba mawili ya mawe, kwa sababu Musa alikuwa ameyavunja yale ya kwanza. Na mawe hayo yalitunzwa ndani ya sanduku la agano. Pia, mtungi wa mana ulitunzwa ndani yake. Unakumbuka mana ni nini?

      Yehova anachagua Haruni ndugu yake Musa awe kuhani mkuu. Anawaongoza watu wamwabudu Yehova. Na wanawe ni makuhani pia.

      Sasa kitazame chumba kikubwa zaidi cha hema hiyo. Ni kikubwa mara mbili kuliko kile chumba kidogo. Unaliona lile sanduku au kasha dogo, na moshi kidogo ukipanda kutoka ndani yake? Ndiyo madhabahu ambapo makuhani wanachoma uvumba. Halafu kuna kinara cha taa chenye taa saba. Na kitu cha tatu chumbani ni meza. Mikate 12 inatunzwa juu yake.

      Bakuli la maji na madhabahu

      Uani mwa hema mna bakuli kubwa, au birika, iliyojaa maji. Makuhani wanaitumia kwa kuogea. Pia kuna madhabahu kubwa. Hapo ndipo wanyama wafu wanapochomwa wawe toleo kwa Yehova. Hema iko katikati ya kambi, na Waisraeli wanakaa katika hema zao kuizunguka.

      Kutoka 25:8-40; 26:1-37; 27:1-8; 28:1; 30:1-10, 17-21; 34:1, 2; Waebrania 9:1-5.

      Maswali ya Funzo

  • Wapelelezi 12
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Yoshua na Kalebu na wapelelezi wengine wakimwonyesha Musa matunda kutoka nchi ya Kanaani

      HADITHI YA 38

      Wapelelezi 12

      TAZAMA matunda ambayo wanaume hawa wanabeba. Tazama kichala kile cha zabibu kilivyo kikubwa. Kinataka wanaume wawili wakibebe kwa mti. Zitazame tini na yale makomamanga. Matunda hayo mazuri yalitoka wapi? Nchi ya Kanaani. Kumbuka, wakati mmoja Ibrahimu, Isaka na Yakobo walikaa Kanaani. Lakini kwa sababu kulikuwako njaa kuu, Yakobo na jamaa yake, walihama wakaenda Misri. Sasa, miaka kama 216 baadaye, Musa anawarudisha Waisraeli Kanaani. Wamefika mahali panapoitwa Kadeshi huko jangwani.

      Watu wabaya wanakaa Kanaani. Basi Musa anawatuma wapelelezi 12, akiwaambia: ‘Nendeni mkaone ni watu wangapi wanaokaa huko, na wana nguvu gani. Mjue kama udongo unafaa mimea. Mhakikishe kurudisha matunda fulani.’

      Wapelelezi hao wanaporudi Kadeshi, wanamwambia Musa hivi: ‘Ni nchi nzuri kweli kweli.’ Na kama ushuhuda wa hayo, wanamwonyesha Musa matunda fulani. Lakini wapelelezi 10 wanasema hivi: ‘Watu wanaokaa huko ni wakubwa na wenye nguvu sana. Tutauawa tukijaribu kuichukua nchi hiyo.’

      Waisraeli wanaogopa kwa kusikia hayo. ‘Afadhali tungefia Misri au hata humu jangwani,’ wanasema. ‘Tutauawa vitani, wake zetu na watoto watatekwa nyara. Na tuchague kiongozi mpya mahali pa Musa, turudi Misri!’

      Lakini wapelelezi wawili wanamtumaini Yehova, wanajaribu kuwatuliza watu. Ni Yoshua na Kalebu. Wanasema: ‘Msiogope. Yehova yuko pamoja na sisi. Itakuwa rahisi kuichukua nchi hiyo.’ Lakini watu hawasikii. Hata wanataka kuwaua Yoshua na Kalebu. Hilo lamkasirisha Yehova sana, anamwambia Musa hivi: ‘Hakuna yeyote kati ya watu hao kuanzia wale wenye miaka 20 na zaidi watakaoingia Kanaani. Wamekwisha kuiona miujiza niliyofanya huko Misri na jangwani, lakini bado hawanitumaini. Basi watatanga-tanga jangwani muda wa miaka 40 mpaka mtu wa mwisho afe. Yoshua (Yosua) na Kalebu peke yao wataingia Kanaani.’

      Hesabu 13:1-33; 14:1-38.

      Maswali ya Funzo

  • Fimbo ya Haruni Inamea Maua
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa akiwa ameshika fimbo ya Haruni iliyomea maua

      HADITHI YA 39

      Fimbo ya Haruni Inamea Maua

      YATAZAME maua na lozi hizo zilizoiva zikimea katika fimbo hiyo. Hiyo ni fimbo ya Haruni. Maua na matunda hayo yalimea katika fimbo ya Haruni usiku mmoja tu! Ebu tuone sababu yake.

      Waisraeli wamekuwa wakitanga-tanga jangwani kwa muda fulani sasa. Wengine kati ya watu hawataki Musa awe kiongozi, wala Haruni kuwa kuhani mkuu. Kora anafikiri hivyo, pia Dathani, Abiramu na viongozi wa watu 250. Wote hao wanakuja kumwambia Musa hivi: ‘Kwa nini wewe unajiweka juu ya wengine wetu?’

      Musa anamwambia Kora na wafuasi wake hivi: ‘Kesho asubuhi mchukue makoleo ya moto mweke uvumba ndani yake. Ndipo mje kwenye hema ya Yehova. Tutaona ni nani ambaye Yehova atachagua.’

      Kesho yake Kora na wafuasi wake 250 wanafika kwenye hema. Wengine wengi wanafuata ili wawaunge mkono wanaume hao. Yehova anakasirika sana. ‘Ondokeni kwenye hema za watu hao wabaya,’ Musa anasema. ‘Msishike mali yao.’ Watu wanasikiliza, na kuondoka kwenye hema za Kora, Dathani na Abiramu.

      Kisha Musa anasema hivi: ‘Kwa hili mtajua ni nani ambaye Yehova amechagua. Ardhi itafunguka na kuwameza watu hawa wabaya.’

      Mara Musa anapomaliza kusema, ardhi inafunguka. Hema ya Kora na mali yake na Dathani na Abiramu na wale walio pamoja nao wanazama, nayo ardhi inawafunika. Watu wanaposikia kilio cha hao wanaotumbukia katika ardhi, wanapiga kelele hivi: ‘Kimbieni! Ardhi isitumeze sisi pia!’

      Kora na wafuasi wake 250 bado wako karibu na hema. Basi Yehova anapeleka moto, na wote wanateketezwa. Kisha Yehova anamwambia Eleazari mwana wa Haruni achukue makoleo ya moto ya watu hao waliokufa ayafanye yawe kifuniko chembamba cha madhabahu.

      Yehova anataka wafahamu sana kwamba Haruni na wanawe ndio amechagua wawe makuhani. Basi anamwambia Musa hivi: ‘Mwambie kiongozi wa kila kabila la Israeli alete fimbo yake. Kisha weka kila moja ya fimbo hizo katika hema mbele ya sanduku la agano. Ile fimbo ya mtu niliyemchagua awe kuhani itamea maua.’

      Musa anapotazama kesho yake, lo! fimbo ya Haruni imemea maua hayo na lozi zilizoiva! Basi unaona sasa kwa nini Yehova alifanya fimbo ya Haruni imee maua?

      Hesabu 16:1-49; 17:1-11; 26:10.

      Maswali ya Funzo

  • Musa Anaupiga Mwamba
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Musa na Haruni wanadai kuwa wametoa maji kwenye mwamba

      HADITHI YA 40

      Musa Anaupiga Mwamba

      MWAKA baada ya mwaka unapita—miaka 10, miaka 20, miaka 30, miaka 39! Waisraeli wangali jangwani. Lakini miaka hiyo yote Yehova anawaangalia watu wake. Anawalisha mana. Anawaongoza mchana kwa nguzo ya wingu, na usiku kwa nguzo ya moto. Na wakati wa miaka yote hiyo mavazi yao hayamaliziki na miguu haipati vidonda.

      Sasa ndio mwezi wa kwanza wa mwaka wa 40 tangu waondoke Misri. Tena Waisraeli wanapiga kambi katika Kadeshi. Hapo ndipo walipokuwa wakati wapelelezi 12 walipotumwa kwenda kwenye nchi ya Kanaani karibu miaka 40 iliyopita. Miriamu dada yake Musa anakufa katika Kadeshi. Na kama zamani, matata yanatokea hapa.

      Watu hawawezi kupata maji. Hivyo wanamlilia Musa hivi: ‘Afadhali tungekufa. Kwa nini ukatutoa Misri kuja mahali hapa pabaya pasipomea kitu? Hakuna nafaka, hakuna tini, hakuna zabibu, hakuna komamanga. Wala hakuna maji ya kunywa.’

      Musa na Haruni wanapokwenda kwenye hema wakasali, Yehova anamwambia Musa hivi: ‘Wakusanye watu. Kisha mbele yao wote useme na mwamba ule. Maji mengi yatatoka watu na wanyama wao wote wanywe.’ Basi Musa anakusanya watu, na kusema: ‘Sikilizeni, ninyi msiomtumaini Mungu! Je! Haruni na mimi tuwatolee maji katika mwamba huu?’ Kisha Musa anaupiga mwamba huo mara mbili kwa fimbo, maji mengi yatiririka katika mwamba huo. Kuna maji mengi ya kunywa watu wote na wanyama.

      Lakini Yehova anawakasirikia Musa na Haruni. Unajua kwa nini? Kwa sababu Musa na Haruni walisema kwamba wao watatoa maji katika mwamba. Lakini Yehova ndiye aliyetoa. Na kwa vile Musa na Haruni hawakusema kweli hiyo, Yehova anasema kwamba atawaadhibu. ‘Hamtawaingiza watu wangu Kanaani,’ anasema.

      Upesi Waisraeli wanaondoka Kadeshi. Baada ya kitambo kidogo wanafika kwenye Mlima Hori. Huko ndiko Haruni alikufa juu ya kilele cha mlima. Anakufa akiwa mwenye miaka 123. Waisraeli wanahuzunika sana, na watu wote wanamlilia Haruni muda wa siku 30. E·le·aʹzari mwanawe anakuwa kuhani mkuu wa pili wa taifa la Israeli.

      Hesabu 20:1-13, 22-29; Kumbukumbu la Torati 29:5.

      Maswali ya Funzo

  • Nyoka wa Shaba
    Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia
    • Waisraeli walioumwa na nyoka, wanamtazama nyoka wa Musa aliyefanyizwa kwa shaba

      HADITHI YA 41

      Nyoka wa Shaba

      JE! HUYO anaonekana kama nyoka wa kweli aliyezungushwa juu ya mti? Hapana. Nyoka huyo amefanyizwa kwa shaba. Yehova alimwambia Musa amweke juu ya mti ili watu wamtazame waishi. Lakini nyoka wengine chini ni wa kweli. Wamewauma watu na kuwafanya wagonjwa. Unajua kwa nini?

      Ni kwa sababu Waisraeli wamempinga Mungu na Musa. Wanalaumu hivi: ‘Kwa nini ulitutoa Misri ili tufe huku jangwani? Hakuna chakula wala maji huku. Tumechoka kula mana hii.’

      Lakini mana hiyo ni chakula kizuri. Yehova amewapa mana hiyo kwa mwujiza. Na kwa mwujiza amewapa maji pia lakini watu hawamshukuru Mungu kwa vile alivyowaangalia. Basi Yehova anawapeleka nyoka hao wenye sumu ili awaadhibu Waisraeli. Nyoka hao wanawauma, na wengi wao wanakufa.

      Mwishowe watu wanamwendea Musa na kusema: ‘Tumefanya dhambi, kwa sababu tumepinga Yehova na wewe. Basi mwombe Yehova awaondoe nyoka hawa.’

      Musa anaombea watu. Naye Yehova anamwambia Musa afanyize nyoka huyu wa shaba. Anamwambia amweke juu ya mti, ili mtu anayeumwa amtazame. Musa anafanya kama anavyoambiwa na Mungu. Watu walioumwa wanamtazama nyoka wa shaba wanapona.

      Kuna jambo la kujifunza kutokana na hayo. Sote tuko kama Waisraeli hao walioumwa na nyoka hao. Sote tuko katika hali ya kufa. Ebu tazama huku na huku, utaona kwamba watu wanazeeka, wanakuwa wagonjwa, na kufa. Ni kwa sababu yule mwanamume na mwanamke wa kwanza, Adamu na Hawa walijitenga na Yehova, na sote ni watoto wao. Lakini Yehova amefanya njia ili tuweze kuishi milele.

      Musa na nyoka wa shaba

      Yehova alimtuma Mwanawe, Yesu Kristo, duniani. Yesu aliwekwa juu ya mti, kwa sababu watu wengi walidhani alikuwa mbaya. Lakini Yehova alimtoa Yesu atuokoe. Tukimtazama, tukimfuata, ndipo twaweza kuwa na uzima wa milele. Lakini tutajifunza zaidi juu ya hilo baadaye.

      Hesabu 21:4-9; Yohana 3:14, 15.

      Maswali ya Funzo

Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
Toka
Ingia
  • Kiswahili
  • Shiriki
  • Mapendezi
  • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
  • Masharti ya Utumiaji
  • Sera ya Faragha
  • Mpangilio wa Faragha
  • JW.ORG
  • Ingia
Shiriki