-
Utumwa Uovu UnaoendeleaAmkeni!—2002 | Juni 22
-
-
Utumwa Uovu Unaoendelea
JE, UTUMWA ulikwisha? Watu wengi wangependa kufikiri hivyo. Neno utumwa huleta mawazo yenye kuogopesha, ya ukatili na uonevu. Hata hivyo, wengi huonelea kwamba mambo hayo yalitukia zamani tu. Kwa mfano, wengine hufikiria juu ya meli za mbao kuukuu zilizowasafirisha watumwa katika karne zilizopita, huku zikiwa zimejaa kabisa watu wenye hofu waliosongamana katika uchafu mwingi.
Ni kweli kwamba siku hizi hakuna meli za kuwasafirisha watumwa, na mikataba ya kimataifa imepiga marufuku utumwa wa aina hiyo. Hata hivyo, utumwa haujakwisha. Shirika la Kimataifa Linalopinga Utumwa, ambalo linatetea haki za binadamu, linakadiria kwamba watu milioni 200 bado ni watumwa kwa njia fulani. Wanafanya kazi katika mazingira ambayo huenda ni mabaya zaidi kuliko yale ya watumwa wa karne zilizopita. Kwa kweli, wachanganuzi fulani wanasema kwamba “kuna watumwa wengi leo kuliko wakati mwingine wowote.”
Masimulizi kuhusu watumwa hao wa leo yanahuzunisha sana. Kila siku, Kanji,a aliye na umri wa miaka kumi tu, huchunga ng’ombe za mabwana wake wakali ambao humchapa. Anasema hivi: ‘Nikibahatika, mimi hupata mkate mdogo uliokauka, la sivyo mimi hushinda na njaa siku nzima. Sijawahi kulipwa mshahara kwa sababu mimi ni mtumwa na mali yao. Watoto wa rika langu wanacheza pamoja. Ni afadhali nife kuliko kuwa na maisha haya ya taabu.’
Kama Kanji, watumwa wengi leo ni watoto au wanawake. Wao hulazimishwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza mikeka, kujenga barabara, kukata miwa, au hata kuwa makahaba. Na wanaweza kuuzwa kwa dola 10 tu za Marekani. Hata wazazi wengine huwauza watoto wao utumwani ili walipe madeni makubwa.
Je, ripoti hizo zinakuudhi? Basi, si wewe tu unayehisi hivyo. Katika kitabu chake Disposable People, mwandishi Kevin Bales anasema hivi: “Utumwa ni jambo linaloudhi. Utumwa sio tu kumlazimisha mtu kufanya kazi; bali ni kumnyang’anya mtu maisha yake.” Kwa sababu ya ukatili ambao mwanadamu anamtendea mwenzake, je, twaweza kutazamia kwamba siku moja utumwa utakwisha? Swali hilo linakuhusu wewe binafsi.
Kama vile tutakavyoona, kuna aina nyingi za utumwa, na nyingine zinaathiri watu wote walio hai. Kwa hiyo, sote tunahitaji kujua ikiwa wanadamu watapata uhuru wa kweli siku moja. Lakini kwanza, hebu tuchunguze kwa ufupi historia ya biashara ya watumwa.
[Maelezo ya Chini]
a Si jina lake halisi.
[Picha katika ukurasa wa 3]
Kwa muda mrefu, wanawake na watoto maskini wamekuwa watumwa
[Hisani]
Picha ya juu: UN PHOTO 148000/Jean Pierre Laffont
U.S. National Archives photo
-
-
Pambano la Muda Mrefu Dhidi ya UtumwaAmkeni!—2002 | Juni 22
-
-
Pambano la Muda Mrefu Dhidi ya Utumwa
“Huu ndio ufafanuzi wa utumwa: kudhulumiwa na kuvumilia, kustahimili udhalimu kwa sababu ya kuogopa kutendewa ukatili.”—Euripides, Mgiriki aliyekuwa mwandishi wa michezo ya kuigiza katika karne ya tano K.W.K.
UTUMWA umekuwepo kwa muda mrefu na mara nyingi umekuwa wenye ukatili. Tangu zama za ustaarabu wa Misri na Mesopotamia, mataifa yenye uwezo yalitumikisha mataifa jirani yasiyokuwa na uwezo. Basi, huo ukawa mwanzo wa mojawapo ya matendo mabaya zaidi ya dhuluma.
Kati ya mwaka wa 2000 na 1000 K.W.K., Misri ilitumikisha taifa zima lenye mamilioni ya watu. (Kutoka 1:13, 14; 12:37) Wakati Ugiriki ilipotawala eneo la Mediterania, familia nyingi za Wagiriki zilikuwa na angalau mtumwa mmoja—kama vile familia za kawaida katika nchi fulani leo zinavyoweza kuwa na gari moja. Mwanafalsafa Mgiriki Aristotle alifanya zoea hilo lionekane kuwa halali aliposema kwamba wanadamu wamewekwa katika vikundi viwili, yaani, kuna mabwana na watumwa, na mabwana huzaliwa wakiwa na haki ya kuamuru, na watumwa huzaliwa tu ili watii.
Waroma waliendeleza utumwa hata kuliko Wagiriki. Katika siku za mtume Paulo, huenda nusu ya idadi ya wakazi wa jiji la Roma—yamkini mamia ya maelfu ya watu—walikuwa watumwa. Na yaonekana kwamba Milki ya Roma ilihitaji watumwa nusu milioni kila mwaka ili kujenga minara ya ukumbusho, kuchimba migodi, kulima, na kufanya kazi katika nyumba kubwa za matajiri.a Kwa kawaida, watu waliotekwa vitani walifanywa kuwa watumwa. Basi, yawezekana kwamba Milki ya Roma iliendeleza vita hasa kwa sababu ilihitaji watumwa wengi zaidi.
Japo utumwa ulipungua kwa kadiri fulani baada ya kuanguka kwa Milki ya Roma, zoea hilo liliendelea. Kitabu Domesday Book (1086 W.K.) kinasema kwamba asilimia 10 ya wafanyakazi huko Uingereza katika Zama za Kati (500-1500 W.K.) walikuwa watumwa. Na bado watumwa walipatikana kupitia vita.
Hata hivyo, tangu wakati wa Kristo, bara la Afrika ndilo limeathiriwa zaidi na matokeo ya biashara ya watumwa kuliko bara jingine lolote. Hata kabla ya wakati wa Yesu, Wamisri wa kale waliwauza na kuwanunua watumwa Waethiopia. Katika kipindi cha miaka 1,250 hivi, inakadiriwa kwamba Waafrika milioni 18 walipelekwa Ulaya na Mashariki ya Kati kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa watumwa huko. Wakati Amerika ilipofanywa kuwa koloni kuanzia miaka ya 1500, watumwa walianza kupelekwa huko pia, na biashara ya kuwasafirisha watumwa kupitia kwenye bahari ya Atlantiki ikawa mojawapo ya biashara kubwa zaidi ulimwenguni. Wanahistoria wanakadiria kwamba kati ya mwaka wa 1650 na 1850, zaidi ya watumwa milioni 12 walihamishwa kutoka Afrika.b Wengi waliuzwa katika masoko ya watumwa.
Mapambano Dhidi ya Utumwa
Katika karne zilizopita, mataifa na watu mbalimbali wamepigania uhuru kutoka utumwani. Katika karne ya kwanza kabla ya Kristo, Spartacus aliongoza jeshi la watumwa Waroma 70,000 ili kupigania uhuru, lakini hakufua dafu. Karne mbili hivi zilizopita, watumwa Wahaiti walifanya mapinduzi yaliyofanikiwa na serikali huru ilianzishwa mnamo mwaka wa 1804.
Utumwa ulidumu kwa muda mrefu zaidi huko Marekani. Watumwa fulani walipambana juu chini ili wao na wapendwa wao wapate uhuru. Na watu fulani waliokuwa huru walipinga sana utumwa kwa kuteta ukomeshwe au kwa kuwasaidia watumwa watoro. Hata hivyo, ni katika miaka ya mwisho-mwisho ya 1800 ndipo utumwa ulipopigwa marufuku hatimaye katika sehemu zote za nchi hiyo. Lakini, vipi leo?
Je, Mapambano Hayo Yameambulia Patupu?
Azimio la Watu Wote la Haki za Binadamu linasema hivi: ‘Hakuna mtu atakayewekwa utumwani wala kutumikishwa; aina zote za utumwa na za biashara ya watumwa hazitaruhusiwa.’ Kwa wazi, mradi huo, ambao ulitangazwa kwa bidii mnamo mwaka wa 1948, ni mradi mzuri. Watu wengi wenye nia njema wametenga wakati wao, nguvu zao, na mali zao ili kufanikisha mradi huo. Hata hivyo, si rahisi kupata mafanikio.
Kama makala iliyotangulia inavyosema, mamilioni ya watu wangali wanafanya kazi kwa jasho bila malipo katika hali mbaya sana, na wengi wao wamenunuliwa au kuuzwa kwa lazima. Japo watu wenye nia nzuri wamejitahidi kukomesha utumwa—na mikataba ya kimataifa imetiwa sahihi ili kuupiga marufuku—bado ni vigumu kwa watu wote kupata uhuru wa kweli. Biashara ya ulimwenguni pote imewezesha biashara haramu ya watumwa kuchuma fedha nyingi. Yaonekana hata utumwa unaendelea kuimarika. Je, kuna tumaini lolote? Hebu tuone.
[Maelezo ya Chini]
a Kitabu kimoja cha kale kinasema kwamba huenda ikawa Waroma fulani matajiri sana walikuwa na watumwa 20,000.
b Wahubiri fulani wa uwongo walidai kwamba Mungu alikubali biashara hiyo ya watumwa yenye ukatili. Hivyo, watu wengi wangali wanadhani kwamba Biblia huunga mkono ukatili huo, na kumbe haifanyi hivyo. Tafadhali ona makala yenye kichwa “Maoni ya Biblia: Je, Mungu Alikubali Biashara ya Watumwa?” katika toleo la Amkeni! la Septemba 8, 2001.
[Picha katika ukurasa wa 4, 5]
Hapo zamani, mara nyingi watumwa waliosafirishwa kwa meli (juu) kutoka Afrika waliuzwa katika masoko ya watumwa huko Amerika
[Hisani]
Godo-Foto
Archivo General de las Indias
-
-
Utumwa Utakapokoma!Amkeni!—2002 | Juni 22
-
-
Utumwa Utakapokoma!
UHURU! Neno hilo ni mojawapo ya maneno yanayowafurahisha sana wanadamu. Watu wamepigana na kuteseka, kuishi na kufa, wakitafuta uhuru. Hata hivyo, inahuzunisha kwamba wengi wamefanya hivyo bila kufanikiwa sana. Je, kuna tumaini lolote kwamba utumwa utakoma—tumaini ambalo halitawafadhaisha wanadamu wala kuwakatisha tamaa? Naam, lipo.
Mtume Paulo aliongozwa na Mungu kuandika ahadi yake inayosema hivi: “Viumbe vyenyewe pia vitawekwa huru kutoka katika utumwa wa uharibifu na kuwa na uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu.” (Waroma 8:21) Lakini tunawezaje kuwa na uhakika kwamba Mungu ataleta ‘uhuru huo wenye utukufu’? Njia moja ni kuchunguza jinsi ambavyo Mungu ameshughulika na wanadamu sikuzote.
Biblia inasema hivi: “Iliko roho ya Yehova, kuna uhuru.” (2 Wakorintho 3:17) Naam, roho ya Mungu, au nguvu yake ya utendaji, ina nguvu nyingi sana. Kwa muda mrefu, ameitumia kuwaweka watu huru kwa njia nyingi. Jinsi gani? Twapaswa kukumbuka kwamba kuna aina nyingi za utumwa. Tayari tumezungumzia aina moja yenye ukatili mwingi sana—jinsi ambavyo watu wenye uwezo huwatumikisha watu wasio na uwezo kwa nguvu au kwa ujeuri. Lakini hebu fikiria aina nyingine za utumwa.
Watu wanaweza kuwa watumwa wa mazoea mbalimbali ambayo ni vigumu sana kuyaacha. Na watu wanaweza kuwa watumwa wa uwongo na udanganyifu, wakidanganywa kuamini mafundisho ya uwongo sikuzote. Zaidi ya yote, kuna aina moja ya utumwa ambayo inatuathiri sote—iwe twajua au hatujui—na matokeo yake husababisha kifo. Hata hivyo, ni lazima tukazie kwamba ijapokuwa tunazungumzia aina mbalimbali za utumwa katika habari hii, hatumaanishi hata kidogo kwamba zote ziko sawa. Aina za utumwa zinatofautiana sana. Hata hivyo, zinafanana katika jambo moja. Hatimaye, Mungu wa uhuru atahakikisha kwamba wanadamu wamewekwa huru kutokana na aina zote hizo za utumwa.
Mazoea Yanapowafanya Watu Kuwa Watumwa
Ona jinsi kitabu When Luck Runs Out kinavyofafanua uchezaji sugu wa kamari: “Ni tatizo linalomchochea sana mtu kucheza kamari bila kuwa na uwezo wa kujidhibiti. Kichocheo hicho huendelea kwa muda mrefu, huongezeka na kuzidisha hamu . . . hadi, hatimaye, kinaingilia, kinadhoofisha na mara nyingi kuvuruga mambo yote ya maana katika maisha ya mtu huyo.” Hakuna ajuaye ni watu wangapi ambao ni watumwa wa kamari. Katika nchi moja tu, Marekani, inakadiriwa kwamba watu milioni sita ni watumwa wa kamari.
Kuwa mtumwa wa kileo kwaweza kusababisha madhara kama hayo, au hata mabaya zaidi, na watu wengi zaidi katika sehemu nyingi ni watumwa wa zoea hilo. Katika nchi moja kubwa, nusu ya idadi ya wanaume ni walevi sugu kwa kadiri fulani. Ricardo, aliyeanza kuwa mlevi sugu miaka 20 iliyopita, anaeleza hivi kuhusu zoea hilo: “Kuanzia wakati unapoamka, mwili wako unatamani kileo—ili utulie, usahau matatizo yako, au kujiamini vya kutosha kuweza kukabiliana na maisha. Mtu hutamani sana kunywa pombe, huku akijaribu kujisadikisha na kuwasadikisha watu wengine kwamba hana tatizo lolote.”
Mbali na kileo, kuna vitu vingine pia vinavyowafanya watu kuwa watumwa. Ulimwenguni pote, mamilioni ya watu hutumia dawa za kulevya. Isitoshe, watu bilioni 1.1 hivi hutumia tumbaku—ambayo ina mojawapo ya dawa za kulevya zinazowafanya watu kuwa watumiaji sugu sana. Watu wengi wangependa kuacha zoea hilo, lakini wanahisi kwamba hawawezi. Je, Yehova amewakomboa watu kutokana na aina hizo za utumwa zenye nguvu?a
Hebu fikiria mfano wa Ricardo. Anasema hivi: “Miaka kumi hivi iliyopita, nilitambua kwamba maisha yangu yaliongozwa na kileo. Jambo hilo lilikuwa likiharibu ndoa yangu, kazi yangu, na familia yangu, na nilijua kwamba singeweza kutatua matatizo yangu pasipo kuacha zoea hilo. Kupitia funzo la Biblia, nilijifunza kwamba umaskini—uwe ni halisi au wa kiroho—humkumba mlevi. (Mithali 23:20, 21) Nilitaka kuwa na uhusiano mzuri na Mungu, na nilipomwomba kwa moyo mnyofu, hilo lilinisaidia kujichunguza waziwazi. Mwanamume mmoja alijifunza Biblia pamoja nami, na akawa rafiki yangu mpendwa. Niliporudia zoea hilo, yeye hakuvunjika moyo, lakini kwa subira na uthabiti alinionyesha jinsi Mungu anavyotaka Wakristo wa kweli watende.”
Akilinganisha maisha yake ya awali na ya sasa, Ricardo anahisi kwamba amewekwa huru kutokana na utumwa huo. Anakubali waziwazi kwamba hapo mwanzoni alirudia zoea hilo mara kwa mara. Anasema hivi: “Lakini kujapokuwa vizuizi hivyo, tamaa yangu ya kumtumikia Yehova kwa uaminifu, na vilevile utegemezo wa mke wangu na Wakristo wenzangu, umenisaidia kukabiliana vema na hali hiyo. Ninatazamia kuona ahadi ya Mungu ikitimia, wakati ambapo ‘hakuna mtu atakayesema, Mimi mgonjwa’ na ulevi sugu utakoma. Kwa sasa, nitaendelea kujitahidi kila siku kutoa mwili wangu kuwa ‘dhabihu iliyo hai, takatifu, yenye kukubalika kwa Mungu.’”—Isaya 33:24; Waroma 12:1.
Maelfu ya watu ulimwenguni pote walisaidiwa na Mungu walipojitahidi kuacha mazoea mabaya. Ni kweli kwamba, wao wenyewe ndio waliojiingiza katika utumwa, labda kwa kujiruhusu washindwe na vishawishi. Hata hivyo, wametambua kwamba Yehova ni Mkombozi mwenye subira nyingi. Yu tayari kuwasaidia na kuwaimarisha wote wanaotaka sana kumtumikia.
“Kweli Itawaweka Nyinyi Huru”
Vipi juu ya utumwa wa uwongo na udanganyifu? Yesu Kristo anatuhakikishia kwamba inawezekana kuwekwa huru kutokana na utumwa huo. Alisema hivi: “Ikiwa nyinyi mwakaa katika neno langu, nyinyi kwa kweli ni wanafunzi wangu, nanyi mtajua kweli, na kweli itawaweka nyinyi huru.” (Yohana 8:31, 32) Wakati huo, watu wengi waliomsikiliza Yesu walikuwa watumwa wa sheria kali za mapokeo ya Mafarisayo. Ndiyo sababu Yesu alisema hivi kuhusu viongozi wa kidini wa wakati wake: “Wao hufunga mizigo mizito na kuiweka juu ya mabega ya watu, lakini wao wenyewe hawataki kuisogeza kwa kidole chao.” (Mathayo 23:4) Mafundisho ya Yesu yaliwaweka watu huru kutokana na utumwa huo. Alifichua uwongo wa kidini, na hata akataja waziwazi chanzo cha uwongo huo. (Yohana 8:44) Alifichua uwongo na kufundisha kweli, akieleza waziwazi matakwa rahisi ambayo Mungu anataka wanadamu watimize.—Mathayo 11:28-30.
Sawa na wanafunzi wa Yesu, maelfu ya watu leo wanaona kwamba kwa msaada wa Mungu wanaweza kuacha uwongo wa kidini na mapokeo ya uwongo ambayo yamewafanya kuwa watumwa. Baada ya kujifunza kweli za Biblia zenye kuburudisha, wao huwekwa huru kutokana na hofu ya wafu yenye kutisha, kutokana na hofu ya kuteketezwa milele motoni, na kutokana na kulazimishwa kulipa fedha wanazochuma kwa jasho eti ndiyo wapate msaada wa kidini kutoka kwa makasisi wanaodai kumwakilisha Kristo ambaye alisema hivi: “Mlipokea bure, toeni bure.” (Mathayo 10:8) Isitoshe, uhuru mkubwa zaidi u karibu.
Utumwa Hatari Zaidi Usioonekana Wazi
Hebu ona jinsi Yesu alivyofafanua utumwa mmoja hatari usioonekana wazi, ambao ulitajwa awali na unaathiri kila mwanamume, mwanamke, na mtoto hapa duniani: “Kwa kweli kabisa mimi nawaambia, Kila mtendaji wa dhambi ni mtumwa wa dhambi.” (Yohana 8:34) Ni nani anayeweza kudai kwamba yeye hatendi dhambi? Hata mtume Paulo alikubali hivi: “Lile jema nitakalo silifanyi, bali lile baya nisilotaka ndilo nazoea kulifanya.” (Waroma 7:19) Ijapokuwa hakuna mtu anayeweza kujiweka huru kutokana na dhambi, bado kuna tumaini.
Yesu aliwahakikishia wanafunzi wake hivi: “Mwana akiwaweka nyinyi huru, mtakuwa huru kikweli.” (Yohana 8:36) Utimizo wa ahadi hiyo utamaanisha uhuru wa kweli kutokana na ule utumwa hatari zaidi. Ili tuelewe namna ambavyo twaweza kuwekwa huru kutokana na utumwa huo, lazima kwanza tuone jinsi tulivyoingia utumwani.
Biblia inaeleza kwamba Mungu alimuumba mwanadamu akiwa na hiari, bila mwelekeo wa kutenda dhambi. Lakini mwana mmoja wa kiroho wa Mungu, asiyeonekana, alitaka kuwatawala wanadamu, bila kujali mateso ambayo yangewapata. Ili kufikia lengo hilo, malaika huyo mwasi, ambaye baadaye aliitwa Shetani Ibilisi, aliwafanya wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa, wamwache Mungu. Adamu alipoasi kimakusudi maagizo ya Mungu yaliyokuwa wazi, akawa mtendaji wa dhambi na akapitisha kutokamilika na kifo kwa wazao wake wote. (Waroma 5:12) Hatimaye, Shetani akawa “mtawala wa ulimwengu,” na ‘dhambi imewatawala wanadamu ikiwa mfalme pamoja na kifo.’—Yohana 12:31; Waroma 5:21; Ufunuo 12:9.
Twawezaje kuwekwa huru? Tunapokuwa wanafunzi wa Yesu, twaweza kufaidika kutokana na kifo cha Kristo cha kidhabihu, ambacho kina uwezo wa “kumfanya kuwa si kitu yule aliye na uwezo wa kusababisha kifo, yaani, Ibilisi” na “kuwaweka huru wale wote ambao kwa hofu ya kifo walitiishwa kwenye utumwa maisha zao zote.” (Waebrania 2:14, 15) Hebu wazia hilo—kuwekwa huru kutokana na dhambi na kifo! Je, uhuru wa aina hiyo haukufurahishi?
Lakini, vipi juu ya utumwa ambao tulizungumzia hapo mwanzoni? Je, kuna wakati ambapo watu hawatatumikishwa tena kwa nguvu?
Msingi Hakika wa Kuwa na Tumaini
Bila shaka, twaweza kuwa na uhakika kwamba utumwa huo wenye kuchukiza utakomeshwa. Kwa nini? Hebu fikiria jambo hili: Yehova Mungu alihusika moja kwa moja katika ukombozi mkubwa zaidi wa watumwa katika historia yote. Huenda ikawa unafahamu simulizi hilo.
Waisraeli walitumikishwa na Wamisri, wakalazimishwa kufanya kazi ngumu na kutendewa kwa ukatili. Wakamlilia Mungu awasaidie, naye, akisukumwa na huruma zake nyingi, akawasikia na kutenda. Yehova akawatumia Musa na Aroni kama wasemaji wake ili kumwamuru Farao Mmisri awaachilie huru Waisraeli. Mfalme huyo mwenye kiburi akakataa katakata, hata baada ya Yehova kuleta mapigo ambayo yaliharibu nchi hiyo. Hatimaye, Mungu akamnyenyekeza Farao. Waisraeli wakaachiliwa huru!—Kutoka 12:29-32.
Ni simulizi lenye kusisimua, sivyo? Hata hivyo, huenda ukajiuliza kwa nini Mungu hajafanya tendo kama hilo katika nyakati zetu. Mbona hajaingilia shughuli za wanadamu na kukomesha utumwa? Kumbuka, Shetani ndiye “mtawala wa ulimwengu” wala si Yehova. Kwa sababu ya masuala yaliyozushwa huko Edeni, Yehova amemruhusu Adui huyo mwovu kutawala kwa kipindi kifupi. Utumwa, uonevu, na ukatili ni ishara za utawala wa Shetani. Kwa sababu ya Shetani, utawala wa wanadamu umeshindwa kabisa. Biblia inaeleza vizuri utawala huo inaposema hivi: “Mtu mmoja anayo mamlaka juu ya mwenziwe kwa hasara yake.”—Mhubiri 8:9, Chapa ya 1989.
Lakini kwa muda gani? Biblia inaeleza kwamba tunaishi katika “siku za mwisho,” wakati ambapo ubinafsi na pupa zingeongezeka sana. (2 Timotheo 3:1, 2) Hiyo inamaanisha kwamba hivi karibuni Ufalme wa Mungu, ambao Yesu alitufundisha tusali juu yake, utaanzisha jamii yenye uadilifu na utumwa utapigwa marufuku. (Mathayo 6:9, 10) Yesu Kristo, Mfalme aliyewekwa rasmi na Mungu, atachukua hatua ya kukomesha utumwa wa aina zote hadi adui wa mwisho, kifo, atakapofanywa kuwa si kitu.—1 Wakorintho 15:25, 26.
Siku hiyo itakapofika, wanadamu waaminifu watatambua kwamba ule ukombozi ambao watu wa Mungu walipata kutoka utumwani huko Misri ulikuwa wonyesho mdogo tu wa ukombozi huo mkubwa zaidi. Naam, muda si muda, “viumbe vyenyewe pia vitawekwa huru kutoka katika utumwa wa uharibifu.” Hatimaye, kila mtu ataweza kufurahia kikamili “uhuru wenye utukufu wa watoto wa Mungu.”—Waroma 8:21.
[Maelezo ya Chini]
a Katika karne ya kwanza, ulafi ulikuwa jambo la kawaida kwenye karamu za Waroma. Hivyo, Wakristo walionywa wasiruhusu chakula au kitu kingine chochote kama hicho kiwafanye kuwa watumwa.—Waroma 6:16; 1 Wakorintho 6:12, 13; Tito 2:3.
[Picha katika ukurasa wa 7]
Inakadiriwa kwamba watu milioni sita ni watumwa wa mchezo wa kamari huko Marekani peke yake
[Picha katika ukurasa wa 7]
Mamia ya mamilioni ya watu ni watumwa wa dawa za kulevya, kileo, na tumbaku
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Kama vile Ricardo, maelfu ya watu wamesaidiwa na Mungu kuacha mazoea mabaya
[Picha katika ukurasa wa 10]
Kama vile Waisraeli wa kale walivyokombolewa kutoka utumwani, hivi karibuni waabudu wa kweli wa Mungu watapata ukombozi mkubwa zaidi
-