Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • yb07 kur. 66-175
  • Afrika Kusini

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Afrika Kusini
  • 2007 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
  • Vichwa vidogo
  • MANDHARI YENYE KUPENDEZA
  • UKUZI KUTOKANA NA MBEGU CHACHE
  • MAENDELEO YA KITHEOKRASI WAKATI WA VITA
  • WAPIGANIA KWELI BILA WOGA
  • KUPANDA MBEGU KATIKA JAMII NYINGINE
  • MAENDELEO YA KITHEOKRASI NYAKATI NGUMU
  • UPANUZI ZAIDI
  • OFISI MPYA YA TAWI
  • ONGEZEKO KUBWA WAKATI WA MIAKA YA VITA
  • MAENDELEO IJAPOKUWA VIKWAZO
  • FAIDA ZA MAZOEZI YA KITHEOKRASI
  • MSAADA WENYE UPENDO WATOLEWA
  • WALIJITOA KWA HIARI
  • KUSANYIKO LA KWANZA LA MZUNGUKO
  • ITIKIO LENYE KUTIA MOYO MIONGONI MWA WAHINDI
  • MATOKEO YA UPENDO NA SUBIRA
  • MRADI MKUBWA
  • KUDUMISHA UMOJA WA KIKRISTO KUJAPOKUWA UBAGUZI
  • KOMBORA LA BLUU LINACHOCHEA ONGEZEKO
  • MSIMAMO WA KUTOKUWAMO UNAJARIBIWA
  • JUMUIYA YA WAKRISTO NA MSIMAMO WA KUTOKUWAMO
  • UTIMILIFU WA NDUGU WEUSI
  • UPINZANI SHULENI
  • MATATIZO MENGINE SHULENI
  • UBAGUZI WA RANGI NA MAKUSANYIKO YETU
  • UBAGUZI HAUKUWAZUIA AKINA NDUGU KUKUTANA
  • SHIRIKA LA KISHERIA LINAANZISHWA
  • MABADILIKO MAKUBWA KATIKA UCHAPAJI
  • KUTAYARISHIA ONGEZEKO
  • KUSHUGHULIKIA UHITAJI WA MAANA
  • ROHO YA KUJIDHABIHU
  • WENGINE PIA WANAONA
  • KUSHUGHULIKIA UHITAJI WA MAJUMBA YA UFALME AFRIKA
  • MATOKEO YA MABADILIKO YA KISIASA
  • UKUZI KATIKA MIOYO
  • “REFUSHA KAMBA ZA HEMA LAKO”
  • MAHALI PANAPOFAA KWA AJILI YA MAKUSANYIKO
  • SHERIA ZA WANADAMU HAZIJAWATENGANISHA
  • BADILIKO LAFAIDI HUDUMA
  • MAENDELEO KATIKA KUTAFSIRI
  • KUPANDA MBEGU ZA KWELI MIONGONI MWA VIZIWI
  • MATOKEO YA KAZI YA UFALME KATIKA NCHI NYINGINE
  • MATARAJIO YA WAKATI UJAO
2007 Kitabu cha Mwaka cha Mashahidi wa Yehova
yb07 kur. 66-175

Afrika Kusini

UKITEMBEA katika barabara yenye shughuli nyingi nchini Afrika Kusini, utaona watu wa rangi mbalimbali, kuanzia walio weusi tititi hadi weupe pepepe. Pamoja na kelele za magari, utawasikia watu wakizungumza lugha nyingi mbalimbali. Kivuli cha majengo marefu chaweza kukukinga na jua kali huku ukitembea kando ya vibanda vya wauzaji wa matunda, vinyago, na nguo. Ukipenda, unaweza kunyolewa na kinyozi aliye kando ya barabara.

Katikati ya mchanganyiko huo na kukiwa na idadi ya watu zaidi ya milioni 44, si rahisi kujua ni nani hasa walio wenyeji asili wa Afrika Kusini. Watu weusi, ambao ni asilimia 75 hivi ya jumla ya watu, ni Wazulu, Wahosa, Wasotho, Wapedi, na Watswana pamoja na makabila mengine madogo-madogo. Nao weupe wengi wanazungumza Kiingereza na Kiafrikana. Hiyo inatia ndani wajukuu wa wakoloni kutoka Uholanzi waliokuja katikati ya karne ya 17 na Wahuguenoti wa Ufaransa waliokuja baadaye. Masetla kutoka Uingereza walifika mapema katika karne ya 19.

Pia kuna Wahindi wengi, wajukuu wa watu waliofanya kazi katika mashamba ya miwa huko Natal (ambako leo huitwa KwaZulu-Natal). Kwa sababu ya mchanganyiko huo wa jamii na utamaduni mbalimbali, Afrika Kusini inaitwa Taifa-Upinde-Mvua.

Wakati uliopita, kulikuwa na mizozo baina ya jamii mbalimbali. Sera ya ubaguzi wa rangi ilifanya taifa hilo lishutumiwe na mataifa mengine. Katika miaka ya karibuni, nchi hiyo imesifiwa kwa kuondolea mbali ubaguzi wa rangi na kuanzisha serikali iliyoteuliwa kidemokrasia.

Sasa, watu wa jamii zote wanaweza kuchangamana kwa uhuru, wanaweza kwenda sehemu zozote za umma, kama kwenye majumba ya sinema au mikahawa. Mtu wa jamii yoyote anaweza kuishi popote apendapo, maadamu ana uwezo wa kifedha.

Hata hivyo, baada ya msisimuko wa awali kutulia, maswali fulani ya msingi yalizuka. Serikali hiyo mpya ingetatua dhuluma zilizoletwa na ubaguzi wa rangi kwa kadiri gani? Ingechukua muda gani? Zaidi ya miaka kumi baadaye, kungali na matatizo mazito. Kuna matatizo makubwa yanayoikabili serikali, kama vile ongezeko la uhalifu, zaidi ya asilimia 41 ya watu hawana kazi, na watu wapatao milioni tano wana virusi vya UKIMWI. Watu wengi wametambua kwamba hakuna serikali ya mwanadamu inayoweza kuondolea mbali matatizo hayo, nao wanatafuta majibu kwingineko.

MANDHARI YENYE KUPENDEZA

Ingawa kuna matatizo nchini, bado watalii wanavutiwa na maumbile ya asili na yenye kupendeza ya nchi hiyo. Watalii huvutiwa na mambo kama vile fukwe zinazopata jua, safu za milima zenye kuvutia, na vijia vingi vya kupanda milima. Katika majiji kuna baadhi ya maduka na mikahawa bora ulimwenguni. Hali nzuri ya hewa pia hufanya Afrika Kusini ivutie.

Aina mbalimbali za wanyama-mwitu huvutia wengi. Nchi hiyo ina aina 200 hivi za wanyama, aina 800 za ndege, na aina 20,000 za mimea inayochanua maua. Watu humiminika kwenye hifadhi za wanyama, kama ile Mbuga ya Kitaifa ya Kruger inayojulikana sana. Unaweza kuwaona wale wanyama watano walio maarufu barani Afrika: tembo, kifaru, simba, chui, na nyati wakiwa katika makao yao ya asili.

Jambo lingine lisiloweza kusahaulika ni misitu ya asili iliyo nchini Afrika Kusini. Imejaa mimea kama vile kangaga, kuvu, na maua yenye kuvutia, hali kadhalika ndege na wadudu wenye kupendeza sana. Pia kuna miti mikubwa sana na yenye kupendeza inayoitwa yellowwood ambayo hukua kutokana na mbegu ndogo sana. Baadhi ya miti hiyo hufikia kimo cha meta 50, nayo huishi kwa miaka elfu moja hivi.

Hata hivyo, kwa karne moja sasa, mbegu tofauti imekuwa ikipandwa na kukuzwa katika nchi hii. Ni habari njema ya Ufalme wa Mungu, ambayo imepandwa katika mioyo ya watu. Mtunga-zaburi aliwalinganisha wanaopendezwa na miti mikubwa alipoandika hivi: “Mwadilifu atachanua kama mtende; kama mwerezi katika Lebanoni, atakuwa mkubwa.” (Zab. 92:12) Waadilifu hao wataishi kwa muda mrefu zaidi kuliko miti ya yellowwood ya kale zaidi, kwa kuwa Yehova amewaahidi uzima wa milele.—Yoh. 3:16.

UKUZI KUTOKANA NA MBEGU CHACHE

Katika karne ya 19, kulikuwa na misukosuko nchini kwa sababu ya vita na mizozo ya kisiasa. Kupatikana kwa almasi na dhahabu katika miaka ya mwisho-mwisho ya karne hiyo kulileta mabadiliko makubwa. Katika kitabu chake (The Mind of South Africa), Allister Sparks aeleza: “Ghafula, nchi iliyokuwa ikitegemea kilimo ikabadilika na kuwa nchi ya viwanda, ikivuta watu kutoka mashambani kuja majijini na kubadili maisha yao.”

Mwaka wa 1902, mbegu za kwanza za kweli ya Biblia zilifika Afrika Kusini katika mizigo ya kasisi mmoja kutoka Uholanzi. Mojawapo ya masanduku yake lilikuwa na baadhi ya vichapo vya Wanafunzi wa Biblia, jina waliloitwa Mashahidi wa Yehova wakati huo. Vichapo hivyo vilipatikana na Frans Ebersohn na Stoffel Fourie, huko Klerksdorp. Walitambua kwamba mambo waliyokuwa wakisoma yalikuwa kweli nao wakaanza kuwahubiria wengine. Watu zaidi ya 80, vizazi vitano vya familia ya Fourie, na wajukuu kadhaa wa familia ya Ebersohn wakawa watumishi wa Yehova waliojiweka wakfu. Mmoja wa wajukuu za Fourie anatumikia katika Betheli ya Afrika Kusini.

Mwaka wa 1910, William W. Johnston kutoka Glasgow, Scotland, alikuja Afrika Kusini akiwa ametumwa afungue ofisi ya tawi ya Wanafunzi wa Biblia. Yamkini akiwa katika miaka yake ya 30 na kitu, Ndugu Johnston alikuwa mkomavu na mwenye kutegemeka. Ofisi ya tawi aliyoanzisha ilikuwa chumba kidogo katika jengo fulani huko Durban. Ofisi hiyo ilipaswa kusimamia kazi katika eneo kubwa sana, sehemu yote ya Afrika iliyo kusini mwa ikweta.

Katika miaka hiyo ya mapema, habari njema ilitia mizizi hasa miongoni mwa wazungu. Wakati huo, vichapo vya Wanafunzi wa Biblia vilipatikana katika Kidachi na Kiingereza tu, na ilichukua muda mrefu kabla ya vichapo kadhaa kutafsiriwa katika lugha za kienyeji. Muda si muda kazi ilisonga mbele katika vikundi vinne—wazungu, weusi, machotara, na Wahindi.

Tangu mwaka wa 1911 na kuendelea, kumekuwa na maendeleo miongoni mwa jamii za weusi nchini. Johannes Tshange alirudi kwao Ndwedwe, karibu na Durban. Aliijua kweli ya Biblia, naye aliwahubiria wengine. Aliongoza mafunzo ya Biblia kwa ukawaida na kikundi kidogo, akitumia kitabu Studies in the Scriptures katika Kiingereza. Yaonekana kikundi hicho ndicho kilichokuja kuwa kutaniko la kwanza la watu weusi nchini Afrika Kusini.

Kikundi hicho kiliwashangaza makasisi wenyeji. Wafuasi wa Kanisa la Kimethodisti la Wesleyan waliwauliza iwapo wanashikamana na mafundisho ya kanisa. Kikundi hicho kikawajibu kwamba kinafundisha mambo yaliyo katika Biblia. Baada ya kujadiliana sana, washiriki wa kikundi hicho wakafukuzwa kanisani. Ndugu Johnston aliwasiliana na kikundi hicho na kuwatembelea kwa ukawaida ili kuongoza mikutano na kuwapa msaada. Ingawa kulikuwa na Wanafunzi wachache wa Biblia, kazi kubwa ya kuhubiri ilikuwa ikifanywa. Ripoti ya mwaka wa 1912 ilionyesha kwamba jumla ya trakti 61,808, ziligawanywa. Pia, kufikia mwishoni mwa 1913, magazeti 11 ya Afrika Kusini yalikuwa yakichapisha katika lugha nne hotuba za C. T. Russell, Mwanafunzi wa Biblia aliyejulikana sana.

MAENDELEO YA KITHEOKRASI WAKATI WA VITA

Mwaka wa 1914 ulikuwa muhimu kwa kikundi kidogo cha watumishi wa Yehova nchini Afrika Kusini, kama ilivyokuwa kwa watu wa Mungu ulimwenguni pote. Wengi walitarajia kupokea thawabu yao mbinguni wakati huo. Katika ripoti ya mwaka ambayo Ndugu Johnston alituma katika makao makuu huko Brooklyn, New York, aliandika hivi: “Katika ripoti ya mwaka uliopita, nilitaja kwamba ninatumainia kutuma ripoti inayofuata katika makao makuu mbinguni. Tumaini hilo halikutimia.” Hata hivyo, aliongeza kusema: “Mwaka ambao umepita umekuwa na shughuli nyingi sana kuliko wakati mwingine wowote katika kazi ya mavuno barani Afrika.” Wengi walikuja kutambua kwamba bado kuna kazi zaidi ya kufanywa, nao walifurahi kushiriki kazi hiyo. Bidii yao ilionekana katika ripoti ya mwaka wa 1915, iliyoonyesha kwamba nakala 3,141 za kitabu Studies in the Scriptures zilikuwa zimegawanywa, mara mbili hivi ya nakala zilizogawanywa mwaka uliotangulia.

Mmoja wa wale waliopata kweli wakati huo ni Japie Theron, wakili stadi. Alisoma katika gazeti la Durban makala iliyokuwa ikizungumzia vichapo vilivyochapishwa na Wanafunzi wa Biblia makumi ya miaka mapema. Makala hiyo ilionyesha kwamba matukio ambayo yamekuwa yakitukia tangu 1914 yalikuwa yametabiriwa katika ule mfululizo wa vitabu Studies in the Scriptures, vilivyokuwa vikifafanua unabii wa Biblia. Japie aliandika hivi: “Niliazimia kuvipata vitabu hivyo, na baada ya kuvitafuta katika maduka yote ya vitabu na kugonga mwamba, mwishowe nilivipata baada ya kuandikia ofisi iliyokuwa Durban. Navyo vilikuwa na ujumbe wenye kusisimua kama nini! Ni shangwe iliyoje kuelewa ‘mambo yaliyofichwa’ ambayo yako katika Biblia!” Mwishowe, Japie akabatizwa, naye aliwahubiria wengine kwa bidii kweli za Biblia hadi alipougua na kufa ghafula mwaka wa 1921.

Mnamo Aprili 1914, Kusanyiko la Wanafunzi wa Biblia la kwanza nchini Afrika Kusini lilifanyiwa Johannesburg. Hudhurio lilikuwa 34, na 16 kati yao wakabatizwa.

Mwaka wa 1916, “Photo-Drama of Creation” ilifika, nayo iliwavutia watu kote nchini. Gazeti Cape Argus liliripoti hivi: “Mafanikio ambayo yamepatikana kufuatia kutolewa kwa mfululizo huo wa pekee wa Filamu za Biblia, yaonyesha kwamba bidii na utambuzi wa Shirika la Kimataifa la Wanafunzi wa Biblia hazikuambulia patupu.” Matokeo ya “Photo-Drama” hayakuonekana mara moja, hata hivyo, filamu hiyo ilivutia watu wengi na kutoa ushahidi mzuri katika eneo kubwa kwa muda mfupi. Ndugu Johnston alisafiri kilomita 8,000 kotekote nchini ili kuwaonyesha watu filamu hiyo.

Kwa muda, kifo cha Ndugu Russell mwaka huo kilipunguza mwendo wa kazi ya kuhubiri nchini Afrika Kusini, kama ilivyokuwa kwingineko pia. Wengine hawakupendezwa na mabadiliko yaliyohitaji kufanywa baada ya kifo chake, nao walisababisha migawanyiko katika makutaniko waliyoshirikiana nayo. Kwa mfano, jijini Durban, wengi katika kutaniko walijitenga na kufanya mikutano yao. Walianza kujiita “Wanafunzi wa Biblia Wanaoshirikiana.” Ni 12 tu waliosalia katika kutaniko la awali, wengi wao wakiwa akina dada. Kwa sababu hiyo, mambo hayakuwa rahisi kwa Henry Myrdal, kijana aliyekuwa amebatizwa karibuni. Baba yake alikuwa amejiunga na upinzani, huku mama yake akiwa amebaki katika kutaniko hilo lililokuwa limepungua sana. Baada ya kufikiri kwa uzito na kusali kuhusu jambo hilo, Henry aliamua kubaki kutanikoni. Kama ilivyo kawaida, kikundi kilichokuwa kimejitenga hakikudumu.

Mwaka wa 1917, ofisi ya tawi ilihamishwa kutoka Durban hadi Cape Town. Idadi ya wahubiri ilizidi kuongezeka. Kufikia wakati huo, kulikuwa na Wanafunzi wa Biblia kati ya 200 na 300 wa ukoo wa Kizungu hali kadhalika makutaniko kadha wa kadha ya watu weusi yaliyokuwa yakisitawi.

Mwaka wa 1917, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini iliripoti hivi: “Ijapokuwa hatuna vichapo katika lugha za kienyeji, inashangaza kuona jinsi akina ndugu wenyeji wanavyoielewa kweli tuliyo nayo. Tunaweza tu kusema kwamba, ‘Ni kazi ya Bwana na inapendeza machoni petu.’” Ndugu kutoka Nyasaland (ambayo leo ni Malawi) walikuja kufanya kazi Afrika Kusini. Baadhi yao ni James Napier na McCoffie Nguluh. Ndugu hao waliwasaidia watu wengi weusi kuwa wanafunzi.

WAPIGANIA KWELI BILA WOGA

Katika miaka hiyo ya mapema, kikosi hicho kidogo cha wahubiri kiliitetea kweli bila woga. Huko Nylstroom, katika mkoa wa Northern Transvaal (ambao leo unaitwa Mkoa wa Limpopo), wanafunzi wawili wavulana walisoma kijitabu What Say the Scriptures About Hell? Walisisimuka sana kujifunza kweli kuhusu wafu. Mmoja wao, Paul Smit,a alisema hivi: “Nylstroom pakawa kituo cha vurugu, kana kwamba pamekumbwa na tufani, wakati ambapo sisi wanafunzi wawili tulipotangaza waziwazi kwamba mafundisho ya kanisa ni ya uwongo. Punde si punde, watu mbalimbali walikuwa wakizungumza kuhusu dini hiyo mpya. Bila shaka, kama ilivyo kawaida yao, makasisi walisema uwongo kuhusu watu wa Mungu na kuwatesa. Kwa miezi kadhaa, hata miaka, mahubiri yao ya kila juma yalikuwa juu ya kitu kimoja tu, eti ‘dini ya uwongo.’” Japo matatizo hayo yote, kufikia 1924, kulikuwa na kikundi kidogo cha wahubiri 13 watendaji huko Nylstroom.

Mwaka wa 1917, Piet de Jager alikuwa akisomea theolojia katika chuo kikuu cha Stellenbosch. Mwanafunzi mwenzake alikuwa akisoma na kuzungumza kuhusu vichapo vilivyochapishwa na Wanafunzi wa Biblia. Jambo hilo liliwahangaisha wakuu wa kanisa, ambao walimwambia Piet azungumze na mwanafunzi huyo na kumwalika ahudhurie funzo la Biblia la kila juma linalofanywa na Shirika la Wanafunzi Wakristo. Matokeo yakawa kinyume na matarajio ya wakuu hao. Piet mwenyewe akakubali kweli. Baada ya kupoteza muda mwingi akijadiliana na maprofesa wake kuhusu nafsi, moto wa mateso, na mambo mengine, aliondoka katika chuo hicho.

Baadaye, mipango ikafanywa kuwe na mjadala kati ya Piet na mtaalamu wa theolojia wa Kanisa la Dutch Reformed, Dwight Snyman, mbele ya wanafunzi 1,500. Ndugu Attie Smit anasimulia mambo yalivyokwenda: “Piet alikanusha kila moja ya hoja za mtaalamu huyo na kuthibitisha kutoka katika Biblia kwamba kanisa lina mafundisho yasiyopatana na Biblia. Mmoja wa wanafunzi alitoa maoni yake kwa kusema, ‘Isipokuwa ni kwa vile naamini Piet de Jager amepotea, ningaliweza kuapa kwamba anasema kweli kwa sababu alithibitisha kila kitu kutoka katika Biblia kwa kutumia maandiko!’”

KUPANDA MBEGU KATIKA JAMII NYINGINE

Alipokuwa akitembelea mji mdogo wa Franschhoek, karibu na Stellenbosch, Ndugu Johnston aliwasiliana na machotara kadhaa waliokuwa wakiishi huko. Miaka mingi kabla, mwalimu mwenyeji, Adam van Diemen, alikuwa ameliacha Kanisa la Dutch Reformed na kuanzisha kikundi kidogo cha kidini. Ndugu Johnston alimtembelea, naye Bw. van Diemen akachukua vichapo kadhaa kwa ajili yake mwenyewe na rafiki zake.

Van Diemen na baadhi ya rafiki zake walikubali kweli na kuwahubiria wengine kwa bidii. Hilo liliweka msingi mzuri wa kuenea kwa habari njema ya Ufalme miongoni mwa machotara. G. A. Daniels, aliyekuwa na umri wa miaka 17, alijifunza kweli na tangu wakati huo akatumia maisha yake yote kumtumikia Yehova.

Baadaye David Taylor, ndugu chotara, alishiriki pia kwa bidii kueneza kweli za Biblia miongoni mwa machotara. Alianza kujifunza Biblia na Wanafunzi wa Biblia alipokuwa na umri wa miaka 17. Mwaka wa 1950, aliwekwa rasmi kutumikia akiwa mwangalizi wa mzunguko naye akapewa mgawo wa kutembelea makutaniko na vikundi vyote vya machotara, jumla ikiwa 24 kufikia wakati huo. Alisafiri sana kwa gari-moshi na kwa basi.

MAENDELEO YA KITHEOKRASI NYAKATI NGUMU

Mwaka wa 1918, Ndugu Johnston alipewa mgawo wa kusimamia kazi ya kuhubiri Ufalme nchini Australia, naye Henry Ancketill, akaombwa atumikie akiwa mwangalizi wa tawi nchini Afrika Kusini. Awali, alikuwa mbunge huko Natal. Alikuwa amestaafu, na ingawa umri wake ulikuwa umesonga, alitimiza mgawo wake vizuri kwa miaka sita iliyofuata.

Licha ya misukosuko iliyokuwako katika miaka hiyo ya vita na marekebisho ya kitengenezo, kulikuwa na ongezeko kadiri wengi zaidi walivyozidi kupendezwa na kweli za Biblia. Mwaka wa 1921, Christiaan Venter, mkubwa wa kikundi cha wafanyakazi waliokuwa wakirekebisha reli, aliona kipande cha karatasi kilichokuwa kimekwama chini ya reli. Ilikuwa trakti iliyochapishwa na Wanafunzi wa Biblia. Aliisoma na kwenda mbio kwa mwana-mkwe wake, Abraham Celliers. Christiaan akamwambia, “Abraham, leo nimeipata kweli!” Wanaume hao wawili walipokea vichapo zaidi vya Biblia na kuvisoma kwa bidii. Wote wawili wakajiweka wakfu na kuwa Mashahidi, nao waliwasaidia wengi kujifunza kweli. Wana na wajukuu wao zaidi ya mia moja ni Mashahidi wa Yehova.

UPANUZI ZAIDI

Kufikia 1924, mashini ya kuchapa ilikuwa imesafirishwa hadi Cape Town. Pia, ndugu wawili waliwasili kutoka Uingereza ili kutoa msaada. Ndugu hao ni Thomas Walder, aliyewekwa kuwa mwangalizi wa tawi, na George Phillips,b aliyepewa wadhifa huo miaka michache baadaye. Ndugu Phillips alitumikia katika wadhifa huo kwa karibu miaka 40, naye alichangia sana kusonga mbele na kuimarishwa kwa kazi ya Ufalme nchini Afrika Kusini.

Kazi ya kueneza injili ilipamba moto mwaka wa 1931 wakati ambapo azimio la kukubali jina Mashahidi wa Yehova lilipopitishwa. Kijitabu The Kingdom, the Hope of the World kilitolewa wakati huo kikiwa na maneno kamili ya azimio hilo. Kiligawanywa kotekote nchini, na jitihada zikafanywa ili kila kasisi, mwanasiasa, na mfanyabiashara maarufu katika eneo hilo apate nakala moja.

OFISI MPYA YA TAWI

Mwaka wa 1933, ofisi ya tawi ilihamia makao makubwa zaidi jijini Cape Town hadi mwaka wa 1952. Kufikia wakati huo, washiriki wa familia ya Betheli walikuwa wameongezeka kufikia 21. Wanabetheli hao walikuwa wakiishi kwa akina ndugu, nao walisafiri kwenda ofisini na kwenye kiwanda cha uchapaji kila siku. Kabla ya kuanza kazi kila asubuhi, walikutana katika chumba cha kubadili mavazi kwenye kiwanda ili kuzungumzia andiko la siku. Kisha, wakaikariri Sala ya Bwana kwa pamoja.

Baadhi yao waliishi mbali sana wasiweze kurudi nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana. Walipewa senti 15 za Afrika Kusini wanunue chakula. Kwa fedha hizo, wangeweza kununua sahani ya viazi vilivyopondwa na soseji ndogo kwenye mkahawa katika kituo cha gari-moshi, au wangeweza kununua mkate na tunda.

Mwaka wa 1935, Andrew Jack, mchapaji stadi, alitumwa akasaidie kazi ya kuchapa katika ofisi ya tawi huko Cape Town. Alikuwa Mskoti, mwembamba, aliyependa kutabasamu. Awali alikuwa mtumishi wa wakati wote katika nchi za Baltiki za Lithuania, Latvia, na Estonia. Baada ya kufika Afrika Kusini, Andrew alipata vifaa zaidi vya kuchapa, na muda si muda mashini hiyo inayoendeshwa na mtu mmoja ikawa ikifanya kazi vilivyo. Mashini ya kwanza inayojiendesha yenyewe, inayoitwa Frontex, ilianza kutumiwa mwaka wa 1937. Kwa miaka zaidi ya 40, ilichapisha mamilioni ya vikaratasi vya ukaribishaji, fomu, na magazeti ya Kiafrikana.

Andrew alitumikia katika Betheli ya Afrika Kusini kwa muda wote uliobaki wa maisha yake. Hata alipokuwa amezeeka sana, aliiwekea familia ya Betheli mfano mzuri, akishiriki kikamili na kwa ukawaida katika huduma ya shambani. Andrew, ndugu mwaminifu mtiwa-mafuta, alikufa akiwa na tumaini la kwenda mbinguni mwaka wa 1984 akiwa na umri wa miaka 89, baada ya kutumikia kwa miaka 58 akiwa amejiweka wakfu.

ONGEZEKO KUBWA WAKATI WA MIAKA YA VITA

Vita vya Pili vya Ulimwengu havikuathiri sana Afrika Kusini kama ilivyokuwa Ulaya, ingawa watu wengi wa Afrika Kusini walipigana barani Afrika na nchini Italia. Vita hivyo vilitangazwa sana ili kuchochea watu waviunge mkono na wengi wajitolee kushiriki. Ijapokuwa roho ya uzalendo ilikuwa imeenea sana wakati huo, mwishoni mwa mwaka wa utumishi wa 1940 kulikuwa na kilele kipya cha wahubiri 881—ongezeko la asilimia 58.7 kuliko kilele cha mwaka uliotangulia cha wahubiri 555!

Januari 1939, gazeti Consolation (ambalo leo huitwa Amkeni!) lilichapishwa katika Kiafrikana kwa mara ya kwanza. Ndilo pia gazeti la kwanza kuchapishwa na Mashahidi wa Yehova nchini Afrika Kusini. Herufi zilipangwa kwa mkono, kazi iliyochukua muda mrefu. Punde baadaye, ikaamuliwa gazeti la Mnara wa Mlinzi lichapishwe katika Kiafrikana. Ijapokuwa akina ndugu hawakujua wakati huo, ulikuwa uamuzi wa hekima kwa kuzingatia mambo yaliyotokea baadaye barani Ulaya. Mashini ya kupiga chapa na ya kukunja magazeti zikaanza kutumiwa. Toleo la kwanza lilitolewa Juni 1, 1940.

Kufikia wakati huo, ndugu walikuwa wakipokea gazeti la Mnara wa Mlinzi la Kidachi kutoka Uholanzi kwa ajili ya wasomaji wa Kiafrikana, kwa kuwa lugha hizo mbili zinafanana. Lakini mwezi wa Mei 1940, kwa sababu Hitler alivamia Uholanzi, ofisi ya tawi ilifungwa ghafula. Hata hivyo, kwa kuwa tayari gazeti la Mnara wa Mlinzi lilikuwa limeanza kuchapwa katika Kiafrikana nchini Afrika Kusini, akina ndugu hawakukosa toleo lolote la gazeti hilo. Magazeti yaliyogawanywa kila mwezi yaliongezeka kufikia 17,000.

MAENDELEO IJAPOKUWA VIKWAZO

Kwa sababu ya uchochezi wa viongozi wa dini zinazodai kuwa za Kikristo na shuku ya serikali kufuatia msimamo wetu wa kutokuwamo, nakala za wale waliokuwa wameandikisha magazeti ya Mnara wa Mlinzi na Consolation zilitwaliwa mwaka wa 1940 na wenye mamlaka waliokuwa wameweka vikwazo. Tangazo rasmi la kupiga marufuku vichapo hivyo likatolewa. Magazeti na vitabu kutoka ng’ambo vilitwaliwa mara tu vilipowasili.

Hata hivyo, bado akina ndugu walipokea chakula chao cha kiroho kwa wakati. Sikuzote, kwa njia moja au nyingine, ofisi ya tawi ilipata nakala ya Kiingereza ya gazeti la Mnara wa Mlinzi, kisha ikaitayarisha na kuichapa. George Phillips aliandika hivi: “Wakati wa marufuku, tulijionea . . . mambo mengi yenye kupendeza yaliyotuthibitishia kwamba Yehova alikuwa akiwatunza na kuwalinda watu wake kwa upendo. Hatukukosa hata toleo moja la Mnara wa Mlinzi. Mara nyingi tulipokea nakala moja tu. Nyakati fulani tungepata tulichohitaji kutoka kwa mwandikishaji aliyekuwa katika mojawapo ya nchi za Rhodesia [ambazo leo zinaitwa Zambia na Zimbabwe] au kutoka katika eneo la Afrika Mashariki lililokuwa likitawaliwa na Wareno [ambalo leo linaitwa Msumbiji] au mashambani nchini Afrika Kusini au kutoka kwa mgeni aliyekuwa akisafiri kwa mashua ambayo ilitia nanga Cape Town.”

Agosti 1941 barua zote zilizotumwa na ofisi ya tawi zilitwaliwa na wenye mamlaka waliokuwa wameweka vikwazo, nasi hatukupewa sababu yoyote. Baadaye, mwaka huohuo, waziri wa mambo ya ndani alitoa amri vichapo vyote vya tengenezo vilivyo nchini vitwaliwe. Saa nne asubuhi moja, maofisa wa Idara ya Upelelezi (CID) walifika kwenye ofisi ya tawi wakiwa na malori ili kuchukua vichapo vyote. Ndugu Phillips aliichunguza hati ya kukamata, akaona kwamba haikupatana kikamili na sheria. Vitabu havikuorodheshwa kulingana na jina, kama ilivyopaswa kuwa kulingana na Gazeti la Serikali.

Kisha Ndugu Phillips akawaomba maofisa wa CID wasubiri awasiliane na wakili, naye akatoa ombi la haraka kwa mahakama kuu itoe amri ya kumzuia waziri wa mambo ya ndani asitwae vichapo hivyo. Ombi lake likakubaliwa. Kufikia alasiri amri hiyo ilitolewa, nao polisi wakaondoka mikono mitupu. Siku tano baadaye waziri huyo alifutilia mbali amri hiyo na kulipia gharama zetu za kisheria.

Kesi kuhusu kupigwa marufuku kwa vichapo vyetu iliendelea kwa miaka kadhaa. Akina ndugu walificha vichapo hivyo nyumbani kwao. Ingawa walikuwa na vichapo vichache vya kutumia shambani, walivitumia kwa busara. Walikuwa wakiwaazima watu waliotaka kujifunza Biblia. Wengi waliikubali kweli wakati huo.

Kuelekea mwishoni mwa mwaka wa 1943, waziri mpya wa mambo ya ndani aliteuliwa. Ombi la kuondolewa kwa marufuku likatolewa, na mambo yakaenda shwari. Mapema katika mwaka wa 1944, marufuku hiyo iliondolewa na vichapo vingi sana vilivyokuwa vimetwaliwa na wenye mamlaka vikarudishwa kwenye ofisi ya tawi.

Wapinzani wa ibada ya kweli walifanikiwa kadiri gani kukomesha utendaji wa kuhubiri Ufalme? Ripoti ya mwaka wa utumishi wa 1945 inaonyesha kwamba Yehova alibariki utumishi mtakatifu wa watu wake waaminifu, nayo kazi ikasonga mbele kwa kiwango kisicho na kifani. Wastani wa wahubiri 2,991 waliwagawia watu vichapo 370,264 na kuongoza mafunzo ya Biblia 4,777. Hilo ni ongezeko kubwa linapolinganishwa na kilele cha wahubiri 881 mwaka wa 1940.

FAIDA ZA MAZOEZI YA KITHEOKRASI

Mtaala wa Huduma ya Kitheokrasi (ambao leo unaitwa Shule ya Huduma ya Kitheokrasi) ulioanzishwa mwaka wa 1943 uliwazoeza ndugu wengi wastahili kuwa wasemaji. Pia, uliwasaidia wengi wawe na matokeo katika huduma ya shambani. Kufikia mwaka wa 1945, kulikuwa na idadi kubwa ya wasemaji waliozoezwa, na kampeni ya Mikutano ya Watu Wote ikaanzishwa. Akina ndugu walitangaza hotuba ambazo zingetolewa katika mikutano hiyo wakitumia mialiko na mabango.

Piet Wentzelc alikuwa kijana painia wakati huo. Akikumbuka kuhusu miaka hiyo ya mapema, anasema hivi: “Nilipewa mgawo wa kwenda Vereeniging, pamoja na Frans Muller akiwa painia mwenzangu. Kabla ya kuanza kampeni yetu ya Mkutano wa Watu Wote mwezi wa Julai 1945, nilitayarisha hotuba mbili kati ya hotuba nne zilizopaswa kutolewa. Nilienda mtoni kila siku wakati wa chakula cha mchana, na kwa saa nzima nikazungumza na mto na miti, nikijizoeza kutoa hotuba yangu kwa mwezi mzima kabla ya kupata ujasiri wa kutosha kuitoa mbele ya watu.” Hotuba ya kwanza ilipotolewa huko Vereeniging, watu 37 wanaopendezwa walihudhuria. Kutokana nao, msingi uliwekwa wa kutaniko lililoundwa baadaye.

Baada ya kutumikia kwa miaka mingi akiwa mwangalizi anayesafiri, Piet, pamoja na mke wake, Lina, walialikwa Betheli. Sasa, akiwa mshiriki wa Halmashauri ya Tawi, amedumisha bidii katika huduma, naye angali mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii. Lina alikufa Februari 12, 2004, baada ya kumtumikia Yehova wakati wote kwa miaka 59.

MSAADA WENYE UPENDO WATOLEWA

Jambo lingine lililofanywa chini ya mwelekezo wa makao makuu huko Brooklyn ni kuwekwa rasmi kwa wanaume walioitwa watumishi wa akina ndugu. Leo, ndugu hao wanaitwa waangalizi wa mzunguko. Ndugu waliowekwa rasmi walikuwa waseja wenye afya nzuri na nguvu nyingi za kuwawezesha kushikamana na ratiba yenye shughuli nyingi.

Mwanzoni, makutaniko makubwa yalitembelewa kwa siku mbili au tatu; navyo vikundi vidogo vikatembelewa kwa siku moja tu. Hivyo, ndugu waliopewa migawo hiyo walisafiri sana. Kwa kawaida walisafiri kwa magari ya umma, mara nyingi wakisubiri magari-moshi na mabasi usiku sana. Wakati wa ziara zao, walikagua kwa uangalifu rekodi za makutaniko. Hata hivyo, lengo lao kuu lilikuwa kwenda shambani pamoja na akina ndugu na kuwazoeza katika huduma.

Mtumishi mmoja wa akina ndugu aliyewekwa rasmi mwaka wa 1943 ni Gert Nel, aliyejifunza kweli mwaka wa 1934 akiwa mwalimu katika shule moja huko Northern Transvaal. Aliwasaidia wahubiri wengi na bado wengi wanakumbuka utumishi wake wa uaminifu. Alikuwa mrefu na mwembamba na alionekana kuwa mkali, naye alipigania kweli kwa bidii. Alikuwa na kumbukumbu nzuri sana na pia aliwapenda watu sana. Alikuwa akihubiri kuanzia saa moja asubuhi mpaka saa moja au mbili jioni bila kupumzika. Katika safari zake akiwa mwangalizi anayesafiri, alikuwa anapanda gari-moshi wakati wowote iwe mchana au usiku; anatembelea kutaniko moja kwa siku kadhaa ikitegemea ukubwa wa kutaniko hilo; kisha anaenda kutaniko linalofuata. Ndivyo alivyofanya juma baada ya juma. Alialikwa Betheli mwaka wa 1946 awe mtafsiri wa Kiafrikana, naye aliendelea kutumikia huko kwa uaminifu hadi alipokufa mwaka wa 1991. Ndiye ndugu mtiwa-mafuta wa mwisho kutumikia Betheli ya Afrika Kusini. Kati ya mwaka wa 1982 na 1985, watiwa-mafuta wengine waaminifu, George Phillips, Andrew Jack, na Gerald Garrard, walifikia mwisho wa utumishi wao duniani.

WALIJITOA KWA HIARI

Watumishi wa Yehova wanathamini utumishi wa waangalizi wanaosafiri na wake zao wanaojitoa kwa moyo wote ili kuyaimarisha makutaniko kiroho. Kwa mfano, Luke Dladla aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa mzunguko mwaka wa 1965 na sasa ni painia wa kawaida. Alisema: “Leo, mwaka wa 2006, nina umri wa miaka 81 na mke wangu ana umri wa miaka 68, hata hivyo bado tunaweza kupanda na kushuka milima, kuvuka mito na kueneza habari njema katika eneo letu. Tumetumia zaidi ya miaka 50 shambani.”

Andrew Masondo aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa mzunguko mwaka wa 1954. Alisema: “Mwaka wa 1965, nilipewa mgawo wa kwenda Botswana, nao ulikuwa kama mgawo wa umishonari. Kulikuwa na njaa nchini humo kwa kuwa mvua haikuwa imenyesha huko kwa miaka mitatu. Mara nyingi mimi na mke wangu Georgina tulilala bila chakula cha jioni na kwenda shambani asubuhi bila kiamsha-kinywa. Kwa kawaida tulipata mlo mmoja tu, mchana.

“Niliporudi Afrika Kusini, niliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa wilaya nami nikazoezwa na Ernest Pandachuk. Maneno ya mwisho aliyoniambia yalikuwa, ‘Usiinue kamwe kichwa chako kuwapita akina ndugu, bali uwe kama mabua ya nafaka yanayoinamisha kichwa yanapoiva, na kuonyesha kwamba yana mazao tele.’”

KUSANYIKO LA KWANZA LA MZUNGUKO

Mnamo Aprili 1947, kusanyiko la kwanza la mzunguko nchini Afrika Kusini lilifanywa jijini Durban. Milton Bartlett, mhitimu wa darasa la tano la Shule ya Gileadi na mmishonari wa kwanza kuja Afrika Kusini, asimulia maoni yake kuhusu akina ndugu waliohudhuria kusanyiko hilo: “Lilikuwa jambo lenye kusisimua sana kuona mtazamo wa Mashahidi weusi. Walikuwa safi, watulivu, na nadhifu sana, tena wanyoofu sana na wenye hamu ya kujifunza mengi zaidi kuhusu kweli na wenye hamu ya kuhubiri.”

Kadiri weusi wengi zaidi walivyozidi kupendezwa, ndivyo usaidizi zaidi ulivyotolewa. Toleo la kwanza la Mnara wa Mlinzi katika Kizulu lilikuwa la Januari 1, 1949. Lilichapwa katika ofisi ya tawi jijini Cape Town kwa kutumia mashini ndogo ya kufanyiza nakala, inayoendeshwa kwa mkono. Gazeti hilo halikuwa na sura yenye kupendeza kama lilivyo leo, hata hivyo lilikuwa na chakula muhimu cha kiroho. Mwaka wa 1950, madarasa ya kujifunza kusoma na kuandika yalianzishwa katika lugha sita. Madarasa hayo yaliwawezesha mamia ya ndugu na dada wenye hamu, kujisomea wenyewe Neno la Mungu.

Kazi ya kueneza injili ilipozidi kusonga mbele, uhitaji wa mahali panapofaa pa kufanyia mikutano ulizuka. Mwaka wa 1948, painia fulani alipewa mgawo wa kwenda Strand, karibu na Cape Town, ambako alikuwa na pendeleo la kusimamia ujenzi wa Jumba la Ufalme la kwanza nchini Afrika Kusini. Dada mwenyeji alilipia mradi huo. George Phillips alisema, “Laiti jumba hilo jipya lingekuwa na magurudumu, ningelizungusha nchini ili kuwatia moyo akina ndugu wajenge Majumba ya Ufalme zaidi.” Miaka kadhaa ilipita kabla ya mpango wa kujenga Majumba ya Ufalme kuanzishwa kote nchini.

ITIKIO LENYE KUTIA MOYO MIONGONI MWA WAHINDI

Kati ya miaka ya 1860 na 1911, wanakandarasi waliletwa kutoka India ili kufanya kazi katika mashamba ya miwa huko Natal. Wengi wao walibaki baada ya kumaliza kandarasi zao, na idadi kubwa ya Wahindi, ambao sasa ni zaidi ya milioni moja, waliamua kuishi nchini. Kufikia miaka ya mapema ya 1950, Wahindi walianza kupendezwa na kweli ya Biblia.

Velloo Naicker alizaliwa mwaka wa 1915, akiwa wa nne katika familia yenye watoto tisa. Wazazi wake walifanya kazi katika mashamba ya miwa, nao walikuwa wafuasi thabiti wa dini ya Kihindu. Masomo ya Biblia yalimchochea Velloo alipokuwa shuleni, na alipokuwa kijana, mtu fulani alimpa Biblia. Aliisoma kila siku, akaimaliza baada ya miaka minne. Aliandika hivi: “Andiko la Mathayo 5:6 lilinivutia. Nilipolisoma, nilitambua kwamba Mungu hufurahi iwapo mtu ana njaa kwa ajili ya kweli na ya kufanya lililo sawa.”

Mwishowe Velloo alitembelewa na Shahidi naye akaanza kujifunza Biblia. Alikuwa miongoni mwa Wahindi wa kwanza kubatizwa Afrika Kusini, mwaka wa 1954. Jamii ya Wahindi, katika eneo aliloishi huko Actonville, Gauteng, iliwapinga vikali Mashahidi wa Yehova, na hata mtu fulani mashuhuri alitisha kumwua Velloo. Kwa sababu ya msimamo wake imara kwa ajili ya kweli ya Biblia, Velloo alipoteza kazi yake ya kusimamia biashara ya udobi. Hata hivyo, aliendelea kumtumikia Yehova kwa uaminifu hadi alipokufa mwaka wa 1981. Kielelezo chake kizuri kilikuwa na matokeo, kwa kuwa washiriki zaidi ya 190 wa familia yake (kutia ndani watu wa ukoo kupitia ndoa) kufikia vizazi vinne wanaendelea kumtumikia Yehova.

Gopal Coopsammy alikuwa na umri wa miaka 14 aliposikia kweli kwa mara ya kwanza kutoka kwa mjomba wake, Velloo. “Velloo alizungumza na vijana kadhaa kati yetu kuhusu Biblia, ingawa sikuwa nikijifunza Biblia rasmi,” akumbuka. “Nikiwa Mhindu, niliiona Biblia kuwa kitabu kigeni. Hata hivyo, baadhi ya mambo niliyojifunza yalionekana kuwa yenye hekima. Siku moja nilimwona Velloo akiondoka kwenda kwenye Funzo la Kitabu la Kutaniko. Nilimwomba niandamane naye. Alikubali, na tangu wakati huo nimekuwa nikihudhuria mikutano. Nilitaka kuongeza ujuzi wangu wa Biblia, hivyo nikaenda kwenye maktaba ya umma na kupata vichapo kadhaa vya Mashahidi wa Yehova. Nilipata upinzani mwingi kutoka kwa familia yangu, lakini sikuzote nilikumbuka maneno ya Zaburi 27:10: ‘Hata ikiwa baba yangu na mama yangu wangeniacha, Yehova mwenyewe angenichukua.’ Nilibatizwa mwaka wa 1955, nikiwa na umri wa miaka 15.”

Gopal ni mwangalizi-msimamizi katika kutaniko analoshirikiana nalo, pamoja na mke wake, Susila. Wamewasaidia watu wapatao 150 kujiweka wakfu na kumtumikia Yehova. Alipoulizwa walitimizaje hilo, alisema: “Kulikuwa na washiriki wengi wa familia waliokuwa wakiishi katika eneo letu, ambao niliwahubiria. Baadhi yao waliitikia. Pia nilikuwa na biashara yangu mwenyewe, na hilo liliniwezesha kuwa na wakati wa kutumia katika huduma. Nilifanya upainia kwa miaka minne. Nilihubiri sana na kufuatia kwa bidii watu wowote waliopendezwa.”

MATOKEO YA UPENDO NA SUBIRA

Doreen Kilgour alihitimu shule ya Gileadi mwaka wa 1956 naye Isabella Elleray akahitimu mwaka wa 1957. Walitumikia kwa miaka 24 katika eneo la Wahindi huko Chatsworth, kitongoji cha Durban.

Doreen alieleza jinsi kazi ya kuhubiri katika eneo hilo ilivyokuwa: “Tulihitaji subira. Baadhi yao hawakuwa wamesikia kamwe kuhusu Adamu na Hawa. Watu walikuwa wakarimu. Wahindu wanaamini kwamba haifai mgeni kusimama mlangoni. Walikuwa wakituambia, ‘Ingieni mnywe chai ndipo mwondoke,’ yaani, tunywe chai kabla ya kwenda kwa jirani. Baada ya muda, tulihisi ni kana kwamba chai itatokea machoni. Ulikuwa muujiza kila mara Mhindi alipoacha imani ya kidini iliyokuwa imetia mizizi na kuwa mwabudu wa Yehova.”

Isabella alisimulia jambo hili lililoonwa: “Nilipokuwa katika huduma ya shambani, nilizungumza na mtu aliyekubali magazeti. Mke wake, Darishnie, aliyekuwa ametoka kanisani, akajiunga naye. Alikuwa amebeba mtoto wao. Tulikuwa na mazungumzo mazuri, nami nikapanga kuwarudia. Hata hivyo, Darishnie hakupatikana nyumbani. Baadaye aliniambia kwamba pasta wao alimwambia awe akitoka kila mara ninapowatembelea. Pasta huyo alijua kwamba akifanya hivyo, basi ningeona kwamba hapendezwi. Nilienda Uingereza kutembelea familia yangu. Nilipokuwa huko, niliendelea kumfikiria Darishnie. Niliporudi Afrika Kusini, nilienda kumwona. Alitaka kujua nilikuwa nimepotelea wapi. Alisema: ‘Nilijua kabisa kwamba ulidhani sipendezwi. Nafurahi sana kukuona tena.’ Tulianza kujifunza, ingawa mume wake hakujiunga nasi. Darishnie alikuwa mwanafunzi makini na muda si muda akabatizwa.

“Kulingana na dini yake, mwanamke aliyeolewa anapaswa kuvaa shanga yenye kidani cha dhahabu na uzi wa manjano shingoni. Shanga hiyo inaitwa tali. Anapaswa kuitoa ikiwa tu mume wake amekufa. Darishnie alipotaka kuanza kuhubiri, alitambua kwamba anahitaji kuvua shanga hiyo. Aliniuliza afanye nini. Nilimshauri azungumze na mume wake kwanza, ajue maoni yake. Alimuuliza, lakini mume wake hakutaka aivue. Nikamwambia awe na subira, angoje kidogo, kisha mume wake atakapokuwa ametulia, amuulize tena. Hatimaye mumewe akamruhusu aivue. Tuliwatia moyo wanafunzi wetu wa Biblia wawe na busara na kuheshimu mafundisho ya Kihindu na wakati huohuo wachukue msimamo kwa ajili ya kweli ya Biblia. Hivyo, waliepuka kuwaudhi marafiki na watu wa ukoo ambao pia wangekubali mabadiliko ya kidini ya wanafunzi wa Biblia.”

Walipoulizwa ni nini ambacho kimewasaidia kuvumilia kwa miaka mingi wakiwa wamishonari, Doreen alisema: “Tuliwapenda watu. Tulijishughulisha kabisa na mgawo wetu nasi tuliufurahia sana.” Isabella aliongezea: “Tulikuwa na rafiki wengi wapendwa. Tulihuzunika tulipoondoka katika mgawo wetu, hata hivyo afya yetu si nzuri. Tulishukuru na kuupokea mwaliko wenye fadhili wa kutumikia Betheli.” Isabella alikufa mnamo Desemba 22, 2003.

Wamishonari wengine pia waliotumikia huko Chatsworth waliona kwamba kwa sababu ya umri wao, hawangeweza kuendelea katika migawo yao na vilevile kuendeleza makao ya wamishonari, hivyo wao pia wakapewa mgawo wa kutumikia Betheli. Wamishonari hao walikuwa Eric na Myrtle Cooke, Maureen Steynberg, na Ron Stephens ambaye alikufa.

MRADI MKUBWA

Nathan Knorr na Milton Henschel, ambao walikuwa wakitumikia katika makao makuu huko Brooklyn, walipotembelea Afrika Kusini mwaka wa 1948, iliamuliwa kwamba uwanja ununuliwe wa kujenga makao ya Betheli na kiwanda cha uchapaji huko Elandsfontein karibu na Johannesburg. Mradi huo ulimalizika mwaka wa 1952. Kwa mara ya kwanza, Wanabetheli wote wangeweza kukaa katika jengo moja. Mashini nyingi zaidi za kuchapisha zilianza kutumiwa, kutia ndani mashini bapa ya kuchapa. Gazeti la Mnara wa Mlinzi lilichapishwa katika lugha nane na Amkeni! katika lugha tatu.

Mwaka wa 1959, makao ya Betheli na majengo ya kiwanda yakapanuliwa. Majengo yaliyoongezwa yalikuwa makubwa kuliko ya awali. Mashini mpya ya kuchapa inayoitwa Timson ilianza kutumiwa. Hiyo ndiyo mashini ya kwanza yenye mtambo wa kuzunguka ambayo ilitumiwa katika ofisi hiyo ya tawi.

Ili kuwasaidia kutumia mashini hizo, Ndugu Knorr aliwaalika vijana wanne kutoka Kanada wahamie Afrika Kusini: Bill McLellan, Dennis Leech, Ken Nordin, na John Kikot. Waliwasili Novemba 1959. Bill McLellan na mke wake, Marilyn, wangali wanatumika katika Betheli ya Afrika Kusini, John Kikot na mke wake, Laura, sasa wanatumikia katika Betheli ya Brooklyn, New York. Ken Nordin na Dennis Leech waliendelea kukaa Afrika Kusini, wakaoa na kupata watoto. Wanaendelea kuchangia pakubwa katika kazi ya Ufalme. Watoto wote wawili wa Ken wanatumikia katika Betheli ya Afrika Kusini.

Betheli iliyopanuliwa na majengo mapya yalitumiwa vizuri kushughulikia ongezeko nchini. Mwaka wa 1952, idadi ya wahubiri nchini Afrika Kusini ilizidi 10,000. Kufikia 1959, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka hadi 16,776.

KUDUMISHA UMOJA WA KIKRISTO KUJAPOKUWA UBAGUZI

Kujua jinsi sera ya ubaguzi wa rangi ilivyofanya kazi hufanya iwe rahisi kuelewa matatizo ambayo akina ndugu walikabili wakati huo. Sheria iliwaruhusu watu weusi, weupe (wa jamii ya Kizungu), machotara (mchanganyiko), na Wahindi kufanya kazi majijini katika majengo yaleyale, kama vile viwandani, ofisini, na mikahawani. Lakini usiku kila jamii ilipaswa kurudi kwao. Hivyo, jamii hizo hazikuruhusiwa kuishi pamoja. Majengo yote yalikuwa na mahali tofauti pa kulia chakula na vyoo kwa ajili ya wazungu na watu wa jamii nyinginezo.

Ofisi ya tawi ya kwanza ilipojengwa huko Elandsfontein, wenye mamlaka hawakuruhusu akina ndugu weusi, machotara, na Wahindi waishi katika jengo moja na ndugu wazungu. Wakati huo, Wanabetheli wengi walikuwa wazungu kwa sababu ilikuwa vigumu kwa watu wa jamii nyingine kupata vibali vya kufanya kazi jijini. Hata hivyo, kulikuwa na ndugu na dada 12 weusi na machotara Betheli, hasa watafsiri wa lugha za kienyeji. Serikali ilitoa kibali ndugu hao wajengewe vyumba vitano nyuma na kando ya majengo makuu ya kukaa. Baadaye, kibali hicho kilifutwa wakati sheria za ubaguzi wa rangi zilipoanza kutekelezwa hata zaidi, na ndugu zetu walilazimika kusafiri hadi maeneo ya watu weusi yaliyokuwa karibu, umbali wa kilomita 20 hivi ili kukaa katika mabweni ya wanaume. Dada wawili weusi waliishi katika nyumba za Mashahidi wengine katika maeneo hayo.

Sheria hata haikuwaruhusu Wanabetheli hao wale chakula pamoja na ndugu zao wazungu katika chumba cha kulia chakula, na wapelelezi wa baraza la jiji walichunguza kuona iwapo sheria hiyo ilivunjwa. Hata hivyo, ndugu hao wazungu hawakuvumilia jambo hilo. Hivyo basi, walibadili vioo vya madirisha na kuweka vioo visivyoonyesha wazi katika chumba hicho ili waweze kula pamoja wakiwa familia nzima bila kusumbuliwa.

Mwaka wa 1966, George Phillips alilazimika kutoka Betheli kwa sababu mke wake, Stella, alikuwa mgonjwa. Harry Arnott, ndugu mwenye uwezo, aliwekwa kuwa mwangalizi wa tawi, naye akafanya kazi hiyo kwa miaka miwili. Tangu mwaka wa 1968, Frans Mullerd ametumikia akiwa mwangalizi wa tawi kisha mratibu wa Halmashauri ya Tawi.

KOMBORA LA BLUU LINACHOCHEA ONGEZEKO

Kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele kilitolewa katika kusanyiko la wilaya la mwaka wa 1968. Wengi walipenda kukiita kombora la bluu nacho kilisaidia sana shambani. Kila mwaka, Idara ya Upakizi na Usafirishaji ilikuwa ikituma vitabu 90,000 hivi kwenye makutaniko, lakini katika mwaka wa utumishi wa 1970, idara hiyo ilituma vitabu 447,000.

Mwaka wa 1971, Ndugu Knorr alitembelea tena Afrika Kusini. Kufikia wakati huo, Betheli ilikuwa imejaa tena. Kulikuwa na Wanabetheli 68. Basi, mipango ya kupanua majengo ilifanywa, na ndugu walijitolea kufanya kazi au kutoa michango kwa ajili ya kazi hiyo. Ujenzi ulimalizika Januari 30, 1972. Baadaye, upanuzi mwingine ulifanywa, nao ukakamilishwa mwaka wa 1978. Upanuzi wote huo ulitia moyo na kuonyesha wazi utegemezo wa Yehova, kwa sababu wakati huo watu wa Mungu walipingwa sana na wenye mamlaka.

MSIMAMO WA KUTOKUWAMO UNAJARIBIWA

Afrika Kusini ilijitenga na Jumuiya ya Madola ya Uingereza na kuwa jamhuri Mei 1961. Wakati huo, kulikuwa na msukosuko wa kisiasa na ongezeko la jeuri nchini. Ili kudhibiti hali, serikali ilichochea roho ya uzalendo, na jambo hilo liliwaletea shida Mashahidi wa Yehova katika miaka iliyofuata.

Kwa miaka mingi, Mashahidi wa Yehova hawakulazimishwa watumikie katika jeshi. Lakini hali ilibadilika mwishoni mwa miaka ya 1960, Afrika Kusini ilipohusika zaidi katika shughuli za kijeshi nchini Namibia na Angola. Sheria mpya ilisema kwamba kila kijana mzungu mwenye afya anapaswa kutumikia jeshini. Ndugu waliokataa walihukumiwa kifungo cha siku 90 katika kambi ya kijeshi.

Mike Marx alikuwa miongoni mwa ndugu waliofungwa na kuagizwa wavae mavazi na kofia za kijeshi. Anakumbuka hivi: “Kwa sababu hatukutaka kuonwa kuwa wanajeshi, tulikataa. Basi, ofisa mkuu, ambaye alikuwa kapteni, akaamuru tunyimwe haki zetu, kila mmoja afungwe peke yake, na kupata chakula kidogo tu.” Kwa hiyo, akina ndugu hawangeweza kuandika wala kupokea barua, kupata wageni, wala kuwa na vichapo vyovyote ila Biblia. Chakula hicho kidogo, kilichokusudiwa hasa wafungwa wenye vichwa vigumu, kilikuwa maji na nusu-mkate kila siku kwa siku mbili halafu chakula cha kawaida cha wanajeshi kwa siku saba, kisha maji na mkate kwa siku mbili tena. Mara nyingi, hata chakula hicho cha kawaida kilikuwa kibovu, nacho hakikutosha.

Utimilifu wa akina ndugu ulijaribiwa vikali. Kila mmoja wao alifungiwa katika chumba kidogo. Wakati mmoja, hawakuruhusiwa kuoga kwa maji yanayotiririka kutoka kwenye mfereji. Badala yake, kila ndugu alipewa ndoo mbili, moja ya kuendea haja na nyingine ya kuogea. Baada ya muda, waliruhusiwa tena kuoga kwa maji yanayotiririka kutoka kwenye mfereji.

Keith Wiggill anakumbuka hivi: “Siku moja, baada ya kuoga kwa maji baridi katika majira ya baridi kali, walinzi walitunyang’anya magodoro na mablanketi yetu. Hawakuturuhusu tuvae mavazi yetu ya raia, hivyo tukavaa suruali fupi na fulana tu. Tulilalia taulo iliyolowa maji kwenye sakafu baridi kama barafu. Asubuhi, ofisa mmoja wa kijeshi alishangaa kuona kwamba tulikuwa wazima na wenye furaha. Alikubali kwamba Mungu wetu alitutunza usiku huo wenye baridi kali.”

Muda mfupi kabla ya kumaliza kifungo chao cha siku 90, ndugu hao walipelekwa mahakamani tena kwa sababu walikataa kuvaa mavazi ya kijeshi na kufanya mazoezi pamoja na wafungwa wengine wa kijeshi. Kisha wakarudishwa gerezani. Wenye mamlaka walisema wazi kwamba lengo lao ni ndugu hao wafungwe tena na tena mpaka watakapokuwa na umri wa miaka 65, wakati ambapo hawangestahili tena kutumikia jeshini.

Mwaka wa 1972, sheria ilibadilishwa baada ya raia na wanasiasa kuteta vikali. Akina ndugu walihukumiwa kifungo kimoja ambacho kinalingana na muda wa kupata mazoezi ya kijeshi. Mwanzoni, kifungo hicho kilikuwa cha kati ya miezi 12 na 18. Halafu, muda huo ukaongezwa kufikia miaka mitatu na mwishowe miaka sita. Baadaye, wenye mamlaka walilegeza mambo kidogo, na ndugu hao wakaruhusiwa kufanya mkutano mmoja kwa juma.

Walipokuwa gerezani, akina ndugu hawakusahau amri ya Kristo ya kufanya wanafunzi. (Mt. 28:19, 20) Waliwahubiria wafungwa wenzao, wenye mamlaka, na watu wengine waliokutana nao. Kwa kipindi fulani, kila Jumamosi alasiri waliruhusiwa kuhubiri habari njema kwa kuandika barua.

Wakati mmoja, wenye mamlaka katika jeshi waliwaamuru Mashahidi hao 350 kula pamoja na wafungwa 170 wa kijeshi. Ni katika kambi hiyo ya kijeshi tu ambapo kulikuwa na Mashahidi wawili kati ya kila mtu mmoja ambaye si Shahidi, na baada ya muda wenye mamlaka waliamua akina ndugu wawe wakila peke yao.

JUMUIYA YA WAKRISTO NA MSIMAMO WA KUTOKUWAMO

Jumuiya ya Wakristo ilionaje suala la kulazimishwa kutumikia jeshini? Mnamo Julai 1974, Baraza la Makanisa la Afrika Kusini (SACC) lilipitisha azimio la kukataa kutumikia jeshini kwa sababu ya dhamiri. Hata hivyo, badala ya kuzungumzia suala hilo kwa upande wa kidini tu, azimio hilo liliingilia mambo fulani ya kisiasa. Liliunga mkono haki ya kukataa kutumikia jeshini kwa sababu jeshi lilikuwa likilinda “jamii isiyofuatia haki na yenye ubaguzi” na hivyo lilikuwa likipigana vita visivyo vya haki. Dini za Kiafrikana, na dini nyingine pia, hazikuunga mkono azimio la baraza hilo.

Kanisa la Dutch Reformed liliunga mkono shughuli za kijeshi za serikali. Kanisa hilo lilipinga azimio la Baraza la Makanisa la Afrika Kusini na kusema kwamba linavunja amri iliyo katika Waroma sura ya 13. Msimamo wa baraza hilo ulipingwa pia na makasisi waliotumikia katika Jeshi la Afrika Kusini, ambalo lilikuwa na makasisi wa makanisa yaliyo katika baraza hilo. Katika taarifa fulani waliyoitayarisha pamoja, makasisi wa makanisa ya Kiingereza walishutumu azimio hilo na kusema: “Tunamsihi kila mfuasi wa makanisa yetu, na hasa vijana, wajitoe kuilinda nchi yetu.”

Isitoshe, makanisa mojamoja ya baraza hilo hayakuchukua msimamo ulio wazi kuhusu suala la kutokuwamo. Kitabu kimoja (War and Conscience in South Africa) kinasema hivi: “Makanisa mengi . . . hayakuwatangazia wafuasi wao msimamo wao wala kuwahimiza wasishiriki vita kwa sababu ya dhamiri.” Kitabu hicho kinasema makanisa yaliogopa kutetea msimamo wao kwa sababu serikali ilipinga vikali azimio la baraza hilo na kutunga sheria kali. Kinasema hivi: “Haikuwezekana kulifanya kanisa lichukue hatua.”

Kwa upande mwingine, kitabu hicho kinasema: “Idadi kubwa ya waliofungwa kwa kukataa kutumikia jeshini kwa sababu ya dhamiri ni Mashahidi wa Yehova.” Kisha kinaongeza hivi: “Mashahidi wa Yehova walitetea haki za mtu za kupinga vita vyote kwa sababu ya dhamiri yake.”

Msimamo wa Mashahidi ulitegemea sababu za kidini tu. Ingawa Mashahidi wanakubali kwamba “mamlaka zilizopo zimesimamishwa na Mungu katika vyeo vyao vya kadiri,” hawaungi mkono upande wowote wa siasa. (Rom. 13:1) Wao wanamtii kwanza Yehova, ambaye katika Neno lake Biblia anasema kwamba waabudu wake wa kweli hawapaswi kushiriki vita.—Isa. 2:2-4; Mdo. 5:29.

Baada ya mfumo huo wa kuwafunga watu wanaokataa kutumikia jeshini kuendelea kwa miaka kadhaa, ilionekana wazi kwamba Mashahidi wa Yehova hawawezi kukana msimamo wao wa kutokuwamo ili waepuke kutendewa kwa ukatili. Zaidi ya hayo, magereza katika kambi za kijeshi yalijaa kupita kiasi na kupata sifa mbaya. Maofisa fulani wa serikali walisisitiza akina ndugu wapelekwe katika magereza ya raia.

Maofisa fulani wa kijeshi wenye nia nzuri walikataa. Waliwaheshimu ndugu zetu vijana kwa sababu ya maadili yao mema. Ikiwa akina ndugu wangepelekwa katika gereza la raia, ingesemekana kuwa wamewahi kutenda uhalifu. Pia, wangefungiwa pamoja na wahalifu wabaya zaidi na kukabili hatari ya kunajisiwa. Basi, ilipangwa wafanye kazi ya kujitolea katika wizara za serikali ambazo si za kijeshi. Hali ya kisiasa ya Afrika Kusini ilipobadilika katika miaka ya 1990, haikuwa lazima tena kutumikia jeshini.

Ndugu zetu vijana waliathiriwaje walipofungwa kwa muda mrefu katika kipindi cha maana maishani mwao? Wengi wao walimtumikia Yehova kwa ushikamanifu na kutumia nafasi hiyo kwa hekima kujifunza Neno la Mungu na kukua kiroho. “Maisha yangu yalibadilika nilipokuwa gerezani katika kambi ya kijeshi,” asema Cliff Williams. “Kuona waziwazi jinsi Yehova alivyonilinda na kunibariki nilipokuwa gerezani kulinichochea nifanye mengi zaidi kuendeleza kazi ya Ufalme. Nilianza upainia wa kawaida muda mfupi baada ya kuachiliwa mwaka wa 1973, kisha mwaka uliofuata nikaingia Betheli, ambako ninaendelea kutumikia hadi leo hii.”

Stephen Venter, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 alipofungwa katika kambi ya kijeshi, alisema hivi: “Nilikuwa mhubiri ambaye hajabatizwa, nami sikuwa na ujuzi mwingi kuhusu kweli. Nilivumilia kwa sababu ya msaada wa kiroho niliopata kupitia mikutano, kufundishwa Biblia na ndugu mwenye uzoefu, na mazungumzo ya andiko la kila siku ambayo tulifanya asubuhi tulipokuwa tuking’arisha sakafu. Ingawa kulikuwa na nyakati ngumu, ni ajabu kwamba sikumbuki sana pindi hizo! Huenda hata ile miaka mitatu niliyokaa gerezani ndiyo miaka bora ya maisha yangu. Mambo niliyokabili wakati huo yalinisaidia kukomaa. Nilipata kumjua Yehova, na hilo lilinichochea kuanza utumishi wa wakati wote.”

Kuna faida iliyotokana na kuwafunga ndugu zetu isivyo haki. Gideon Benade, ambaye aliwatembelea ndugu hao walipokuwa gerezani katika kambi ya kijeshi, aliandika hivi: “Ninapokumbuka yaliyopita, ninatambua kwamba ushahidi mkubwa sana ulitolewa.” Uvumilivu wa ndugu zetu na ripoti nyingi za habari kuhusu kesi na hukumu waliyopata zilionyesha kwa njia isiyosahaulika msimamo wa kutokuwamo wa Mashahidi wa Yehova, ambao ulitambuliwa jeshini na kotekote nchini.

UTIMILIFU WA NDUGU WEUSI

Katika miaka ya mwanzo wa utawala wa ubaguzi wa rangi, ndugu weusi hawakukabili majaribu yaleyale ambayo ndugu wazungu walikabili kuhusu msimamo wa kutokuwamo. Kwa mfano, watu weusi hawakuitwa watumikie jeshini. Hata hivyo, makundi ya kisiasa ya watu weusi yalipoanza kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi, Mashahidi weusi walikabili majaribu makali. Baadhi yao waliuawa, wengine wakapigwa, na wengine wakalazimika kuhama makwao baada ya nyumba na mali yao kuteketezwa. Walikabili yote hayo kwa sababu walikataa kubadili msimamo wao wa kutokuwamo. Naam, waliazimia kutii amri ya Yesu ya ‘kutokuwa sehemu ya ulimwengu.’—Yoh. 15:19.

Makundi fulani ya kisiasa yaliwalazimisha wakaaji wote wa maeneo yao kununua kadi ya chama cha kisiasa. Wawakilishi wa makundi hayo walienda kwenye nyumba za watu kudai pesa za kununua silaha au za kulipia maziko ya wenzao waliouawa wakipambana na majeshi ya ulinzi ya wazungu. Akina ndugu weusi walishtakiwa kuwa wapelelezi wa serikali ya ubaguzi wa rangi kwa sababu walikataa kwa heshima kulipa pesa hizo. Ndugu na dada fulani walipokuwa katika utumishi wa shambani, walishambuliwa na kushtakiwa kwamba wanaeneza propaganda za Waafrikana wazungu.

Fikiria kisa cha Elijah Dlodlo, ambaye aliacha michezo ambayo ingemletea mafanikio ili awe mtumishi wa Yehova aliyejiweka wakfu. Majuma mawili kabla ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini, kulikuwa na wasiwasi mkubwa kati ya jamii za weusi zenye uadui. Kutaniko ambalo Elijah alishirikiana nalo liliamua kuhubiri eneo lao ambalo halikuhubiriwa mara nyingi, lililokuwa umbali wa kilomita kadhaa. Elijah, ambaye alibatizwa miezi miwili tu mapema, aligawiwa kuhubiri pamoja na wavulana wawili waliokuwa wahubiri ambao hawajabatizwa. Walipokuwa wakizungumza na mwanamke fulani mlangoni pake, walivamiwa na kundi la vijana. Vijana hao walikuwa washiriki wa kundi la kisiasa. Kiongozi wao alikuwa na mjeledi mnene wa ngozi unaoitwa sjambok. Akauliza kwa hasira: “Mnafanya nini hapa?”

“Tunaongea juu ya Biblia,” mwenye nyumba akajibu.

Akimpuuza mwanamke huyo, mtu huyo mwenye hasira akamwambia Elijah na wale wavulana wawili: “Tufuateni, ninyi wavulana watatu. Huu si wakati wa kuongea juu ya Biblia; huu ni wakati wa kupigania haki zetu.”

Kwa ujasiri, Elijah akamjibu, “Hatuwezi kufanya hivyo kwa sababu tunafanya kazi ya Yehova.”

Mtu huyo alimsukuma Elijah na kuanza kumpiga kwa ule mjeledi. Kila alipomcharaza, mtu huyo alipaaza sauti akisema, “Jiungeni nasi!” Baada ya kuchapwa mara ya kwanza, Elijah hakuhisi tena uchungu. Aliimarishwa na maneno ya mtume Paulo, ambaye alisema Wakristo wote wa kweli “watateswa.”—2 Tim. 3:12.

Mwishowe mtu huyo alichoka na kuacha kumpiga. Kisha, mmoja wa washambulizi hao akamshutumu yule mtu mwenye mjeledi, akisema kwamba Elijah si wa jamii yao. Washambulizi hao wakagawanyika na kuanza kupigana, naye kiongozi wao akacharazwa vibaya kwa mjeledi wake mwenyewe. Fujo hizo zilipokuwa zikiendelea, Elijah na wenzake wawili wakakimbia. Jaribu hilo liliimarisha imani ya Elijah, naye akaendelea kufanya maendeleo akiwa mhubiri wa habari njema asiye na woga. Kufikia sasa, ameoa, ana watoto, na ni mzee katika kutaniko lao.

Dada zetu weusi pia walikuwa mashujaa kwelikweli walipokabili majaribu ya kuwavunja moyo waache kuhubiri. Hebu ona mfano wa Florah Malinda. Binti yake, Maki, aliyekuwa amebatizwa, aliteketezwa na kuuawa na kundi la vijana kwa sababu alijaribu kumtetea ndugu yake aliyekataa kujiunga na kundi lao la kisiasa. Ijapokuwa alipatwa na msiba huo mkubwa, Florah hakuvunjika moyo bali aliendelea kuhubiri kuhusu Neno la Mungu katika jamii yao. Siku moja, wawakilishi wa kundi la kisiasa lililomuua binti yake walisisitiza ajiunge na kundi hilo, la sivyo aumie. Majirani walimtetea, wakasema kwamba Florah haungi mkono upande wowote wa kisiasa bali anajishughulisha kuwasaidia watu kujifunza Biblia. Wawakilishi hao wakaanza kubishana, na mwishowe wakaamua kumwacha Florah. Katika kipindi hicho chote cha majaribu mpaka leo, Florah ameendelea kutumikia kwa uaminifu akiwa painia wa kawaida.

Ndugu mmoja ambaye ni painia wa kawaida anasimulia yaliyompata alipokuwa akisafiri kwa basi kwenda eneo lake. Kijana mmoja mwanaharakati wa kisiasa alimsukuma na kumuuliza ni kwa nini anabeba vichapo vinavyochapishwa na Waafrikana na kuwauzia watu weusi. Ndugu huyo anaeleza yaliyofuata: “Aliniamuru nitupe vichapo hivyo nje ya basi. Kwa sababu nilikataa, alinipiga kofi usoni na kuizimia shavuni mwangu sigara aliyokuwa akivuta. Sikufanya lolote. Halafu akaninyang’anya mkoba wangu wenye vichapo na kuutupa nje dirishani. Pia, alivuta na kuitoa tai yangu huku akisema kwamba huo ni mtindo wa wazungu wa kuvaa. Aliendelea kunivunjia heshima na kunidhihaki, akisema kwamba watu kama mimi wanapaswa kuteketezwa wakiwa hai. Yehova aliniokoa kwa kuwa nilishuka basi hilo bila kuumizwa zaidi. Kisa hicho hakikunivunja moyo nisiendelee kuhubiri.”

Makutaniko na watu binafsi walituma barua nyingi kwa ofisi ya tawi ya Afrika Kusini kusimulia utimilifu wa ndugu weusi. Barua moja kama hiyo iliandikwa na mzee wa kutaniko fulani huko KwaZulu-Natal. Ilisema hivi: “Tunawaandikia barua hii kuwajulisha kwamba tumempoteza ndugu yetu mpendwa Moses Nyamussua. Alikuwa fundi wa vyuma na magari. Wakati mmoja, washiriki wa kundi la kisiasa walimwomba amalizie kuunda bunduki walizokuwa wamejitengenezea, naye akakataa. Kisha, Februari 16, 1992, kundi hilo lilifanya mkutano wa kisiasa, ambako vita vilizuka kati ya washiriki wake na wale wa kundi pinzani. Jioni ya siku hiyohiyo, walipokuwa wakirudi kutoka kupigana, walikutana na ndugu huyo akienda madukani. Walimuua papo hapo kwa mikuki yao. Kwa nini? Walisema: ‘Ulikataa kutuundia bunduki, na sasa wenzetu wameuawa vitani.’ Kisa hicho kimewashtua sana akina ndugu, lakini tutaendelea kutimiza huduma yetu.”

UPINZANI SHULENI

Matatizo yalitokea katika shule za weusi kwa sababu wanafunzi walipokusanyika asubuhi, kulikuwa na sala na nyimbo za dini, na watoto wa Mashahidi hawakushiriki. Hilo halikuwa tatizo katika shule za wazungu. Katika shule hizo, watoto wangeruhusiwa kutoshiriki ikiwa wazazi wangeandika barua ya kueleza msimamo wao. Lakini katika shule za weusi, kukataa kushiriki sherehe za dini kulionwa kuwa kuasi mamlaka ya shule. Walimu hawakuwa wamezoea kuona watoto wakikataa. Wazazi walipokuja kueleza msimamo wa Mashahidi, walimu walikataa kutoa kibali cha kutoshiriki.

Wakuu wa shule walisisitiza kwamba watoto wa Mashahidi wa Yehova wanapaswa kukusanyika pamoja na wanafunzi wengine asubuhi kwa sababu matangazo ya shule hutolewa wakati huo. Watoto hao walihudhuria, lakini badala ya kushiriki nyimbo na sala, walisimama na kunyamaza. Baadhi ya walimu walitembea katikati ya mistari ya wanafunzi ili waone ikiwa wanafunga macho wakati wa sala na kuimba nyimbo za dini. Ilifurahisha kujua kwamba watoto hao, baadhi yao wakiwa na umri mdogo sana, walidumisha utimilifu bila woga.

Baada ya watoto wengi kufukuzwa shuleni, akina ndugu waliamua kupeleka suala hilo mahakamani. Agosti 10, 1976, Mahakama Kuu Zaidi ya Johannesburg ilitoa uamuzi wa kesi kubwa iliyowahusu wanafunzi 15 wa shule moja. Nakala ya kisheria ilisema hivi: “Washtakiwa . . . walikubali kwamba watoto wa walalamishi wana haki ya kutoshiriki sala na nyimbo za dini, na . . . kwamba walifukuzwa shule . . . kinyume cha sheria.” Huo ulikuwa ushindi mkubwa wa kisheria, na mwishowe suala hilo likatatuliwa katika shule zote zilizohusika.

MATATIZO MENGINE SHULENI

Watoto wengi Mashahidi waliokuwa katika shule za wazungu walikabili jaribu lingine la utimilifu lililofanya wafukuzwe shuleni. Serikali ya ubaguzi wa rangi ilitaka kuwatumia vijana wazungu kuunga mkono sera zake. Mwaka wa 1973, serikali ilianzisha mradi fulani unaoitwa Vijana Kaeni Chonjo (Youth Preparedness). Mradi huo ulitia ndani shughuli mbalimbali za kizalendo kama vile mafunzo ya kutembea kama askari, kujikinga, na mambo mengine ya kizalendo.

Baadhi ya wazazi Mashahidi waliazimia kutatua jambo hilo kisheria. Ingawa suala hilo liliwasilishwa kwa waziri wa elimu, hakuna hatua iliyochukuliwa. Waziri huyo alidai kwamba mradi wa Vijana Kaeni Chonjo ulikuwa sehemu ya elimu tu. Serikali ilitumia suala hilo kueneza maoni mabaya sana kuhusu Mashahidi wa Yehova. Katika shule fulani, wakuu wa shule walikubali kutowashirikisha watoto katika sehemu za mradi huo ambazo hazikupatana na Maandiko, lakini katika shule nyingine watoto walifukuzwa.

Ni wazazi wachache tu Wakristo ambao walikuwa na pesa za kuwapeleka watoto wao katika shule za watu binafsi. Wazazi fulani walipanga watoto wao wapate elimu kwa njia ya posta. Mashahidi ambao ni walimu waliwafundisha watoto nyumbani. Hata hivyo, watoto wengi waliofukuzwa shuleni hawakumaliza masomo ya sekondari. Badala yake, walifaidika kutokana na mazoezi ya Kimaandiko waliyopata nyumbani na kutanikoni. (Isa. 54:13) Baadhi yao walianza utumishi wa wakati wote. Vijana hao wasio na woga walifurahi kwamba walivumilia majaribu, wakimtegemea Yehova kabisa. (2 Pet. 2:9) Baada ya muda, hali ya kisiasa katika nchi hiyo ilibadilika, na watoto wetu hawakufukuzwa shuleni tena kwa kukataa kushiriki shughuli za kizalendo.

UBAGUZI WA RANGI NA MAKUSANYIKO YETU

Ili kutovunja sheria za Afrika Kusini, akina ndugu walilazimika kupangia makusanyiko tofauti kwa ajili ya kila kikundi cha rangi. Vikundi vyote vya rangi vilikutana mahali pamoja kwa mara ya kwanza kwenye kusanyiko la kitaifa lililofanyiwa Uwanja wa Wembley, Johannesburg, mwaka wa 1952. Wakati huo, Ndugu Knorr na Ndugu Henschel walitembelea Afrika Kusini na kutoa hotuba katika kusanyiko hilo. Kupatana na sheria zilizokuwapo wakati wa ubaguzi wa rangi, kila kikundi cha rangi kilipaswa kuketi katika sehemu yake. Wazungu walikalia viti vya magharibi, weusi wakakalia vya mashariki, na Machotara na Wahindi wakakalia vya kaskazini. Pia, ilikuwa lazima mipango ifanywe ili wasichangamane katika mistari ya chakula. Ijapokuwa vizuizi hivyo, Ndugu Knorr aliandika hivi kuhusu kusanyiko hilo: “Inafurahisha kwamba sote tulikusanyika katika uwanja mmoja na kumwabudu Yehova katika pambo takatifu.”

Mnamo Januari 1974, makusanyiko matatu yalifanyiwa Johannesburg, moja la weusi, lingine la Machotara na Wahindi, na la tatu la wazungu. Lakini mpango wa pekee ulifanywa kwa ajili ya siku ya mwisho ya kusanyiko: Watu wa rangi zote hizo wangekusanyika kwenye Uwanja wa Rand huko Johannesburg kwa ajili ya kipindi cha alasiri. Umati wa watu 33,408 walikusanyika katika uwanja huo. Kulikuwa na shangwe nyingi! Wakati huo, watu wa rangi zote walichangamana kwa uhuru na kuketi pamoja. Wageni wengi kutoka Ulaya walikuja, nao walifanya tukio hilo lisisahaulike kamwe. Yote hayo yaliwezekanaje? Bila kujua, wapangaji wa kusanyiko walikuwa wamekodi uwanja uliotengwa kwa ajili ya matukio ya kimataifa na ya watu wa rangi mbalimbali, na kibali hakikuhitajiwa kwa ajili ya kipindi hicho kimoja.

UBAGUZI HAUKUWAZUIA AKINA NDUGU KUKUTANA

Miaka michache mapema, mipango ilifanywa ili kusanyiko la kitaifa lifanyiwe Johannesburg. Hata hivyo, mwakilishi fulani wa serikali kutoka Pretoria alitembelea ofisi za serikali huko Johannesburg ambazo zilishughulikia masuala ya Wabantu (watu weusi), na kutokana na kumbukumbu za mkutano wao, aligundua kwamba Mashahidi wa Yehova wameomba kutumia uwanja wa Mofolo Park kwa ajili ya kusanyiko la ndugu weusi.

Aliripoti jambo hilo kwenye makao yao makuu huko Pretoria, na Wizara ya Masuala ya Wabantu ikafutilia mbali maombi yetu ikisema kwamba sisi si “dini inayotambuliwa.” Ndugu wazungu walikuwa wameomba watumie uwanja wa Milner Park Show Grounds ulio katikati ya Johannesburg ili wautumie wakati huohuo, nao ndugu machotara wangekutania katika Uwanja wa Union, magharibi ya jiji hilo.

Ndugu wawili kutoka Betheli walienda kumwona waziri anayehusika, ambaye zamani alikuwa kasisi wa Kanisa la Dutch Reformed. Walisema kwamba hakuna haja ya kuwazuia ndugu zetu weusi wasikutanie Mofolo Park kwa sababu kwa miaka mingi Mashahidi wamefanya makusanyiko huko, na ndugu wazungu na ndugu machotara wangekuwa pia na makusanyiko yao. Lakini waziri huyo akakataa katakata.

Kwa kuwa uwanja wa Mofolo Park uko magharibi ya Johannesburg, ndugu hao wawili wakaamua wajaribu kufanyia kusanyiko hilo upande wa mashariki wa Johannesburg, ambako pia kulikuwa na weusi wengi. Walienda kumwona msimamizi, lakini hawakumweleza kuhusu mkutano wao pamoja na yule waziri huko Pretoria. Alikuwa mwenye fadhili sana walipomwomba mahali pa kufanyia kusanyiko. Alipanga watumie Uwanja wa Wattville. Tofauti na uwanja wa Mofolo Park, uwanja huo ulikuwa na viti vilivyopangwa katika mistari.

Ndugu wote walielezwa upesi badiliko hilo la mahali pa kusanyiko. Kusanyiko hilo lilifanikiwa, na watu wapatao 15,000 walihudhuria. Hakukuwa na usumbufu wowote kutoka Pretoria. Katika miaka kadhaa iliyofuata, akina ndugu waliendelea kufanyia makusanyiko katika Uwanja wa Wattville bila matatizo yoyote.

SHIRIKA LA KISHERIA LINAANZISHWA

Kufuatia maagizo ya Baraza Linaloongoza, shirika la kisheria lenye washiriki 50 lilianzishwa Januari 24, 1981. Shirika hilo liliitwa Jehovah’s Witnesses of South Africa (Mashahidi wa Yehova wa Afrika Kusini). Shirika hilo lilisaidia kuendeleza mambo ya kiroho kwa njia mbalimbali.

Kwa miaka mingi, akina ndugu kwenye ofisi ya tawi walifanya bidii ili Mashahidi wa Yehova waruhusiwe kuwa na maofisa wao wenyewe wa kuandikisha ndoa, lakini hawakufanikiwa. Frans Muller anakumbuka hivi: “Kila wakati, maofisa wa serikali walikataa maombi yetu na kusema kwamba dini yetu haistahili wala haina uwezo wa kuwa na maofisa wa kuandikisha ndoa.”

Zaidi ya hayo, kwa sababu hakukuwa na shirika la kisheria, haikuwezekana kujenga Majumba ya Ufalme katika maeneo ya weusi. Kila wakati maombi ya akina ndugu yalikataliwa kwa sababu wenye mamlaka walisema: ‘Dini yenu haitambuliwi.’

Hata hivyo, muda mfupi baada ya shirika hilo kuanzishwa, akina ndugu waliruhusiwa kuwa na maofisa wa kuandikisha ndoa. Pia, waliruhusiwa kujenga Majumba ya Ufalme katika maeneo ya weusi. Sasa, wazee zaidi ya 100 ni maofisa wa kuandikisha ndoa nchini Afrika Kusini. Kwa kuwa wazee hao wanaweza kuandikisha ndoa kwenye Jumba la Ufalme, wale wanaotaka kuoana hawahitaji kwenda kwanza kwenye ofisi za sheria ili wapate cheti cha ndoa.

MABADILIKO MAKUBWA KATIKA UCHAPAJI

Njia za uchapaji zilibadilika haraka, na mashini tulizokuwa nazo zilikuwa zimepitwa na wakati. Isitoshe, sehemu za mashini ziliuzwa kwa bei ya juu na hazikupatikana kwa urahisi. Basi, iliamuliwa kwamba tuanze kutumia mashini ambazo zinaendeshwa kwa mifumo ya kompyuta na zinazotumia mabamba ya uchapaji ya mviringo. Mashini za kutayarisha maandishi kwa ajili ya uchapaji zilinunuliwa, na mwaka wa 1979, mashini ya uchapaji ya TKS inayotumia mabamba ya mviringo ilianza kutumiwa. Hiyo ilikuwa zawadi kubwa kutoka ofisi ya tawi ya Japani.

Kwa kuwa Mashahidi wa Yehova wanachapisha vichapo katika lugha nyingi sana, waliona inafaa kutengeneza programu yao ya kompyuta ya kutayarisha maandishi kwa ajili ya uchapaji. Mwaka wa 1979, akina ndugu huko Brooklyn, New York, walianza kutengeneza mfumo ambao baadaye uliitwa MEPS (yaani, multilanguage electronic phototypesetting system). Mfumo wa MEPS ulianza kutumiwa Afrika Kusini mwaka wa 1984. Kwa sababu kompyuta zilitumiwa kutafsiri na kutayarisha maandishi kwa ajili ya uchapaji, vichapo vya lugha mbalimbali viliweza kuchapishwa kwa wakati uleule.

KUTAYARISHIA ONGEZEKO

Mapema katika miaka ya 1980, makao ya Betheli huko Elandsfontein yalikuwa madogo sana na mahitaji ya shambani yaliyoongezeka hayangeweza kushughulikiwa kwa ukamili. Basi, uwanja ulinunuliwa katika mji wa Krugersdorp, umbali wa dakika 30 kutoka Johannesburg ukitumia gari. Shamba hilo la ekari 215 liko katika eneo linalopendeza lenye milima na kijito cha maji safi. Ndugu wengi waliacha kazi zao ili washiriki ujenzi, na wengine walisaidia walipokuwa likizo. Wachache walitoka nchi nyingine, kama vile New Zealand na Marekani, na ujenzi ukamalizika katika muda wa miaka sita.

Bado ilikuwa vigumu kwa Mashahidi weusi, hasa watafsiri, kuruhusiwa kuishi katika eneo hilo. Ni 20 tu walioruhusiwa, na ilikuwa lazima wajengewe makao yao kando. Hata hivyo, baada ya muda, serikali ililegeza msimamo wake kuhusu ubaguzi wa rangi, na akina ndugu wa rangi zote wangeweza kuishi popote Betheli.

Familia ya Betheli ilifurahia makao yao yenye kupendeza na vyumba vyenye nafasi kubwa vilivyojengwa vizuri. Jengo la matofali lenye orofa tatu limezungukwa na bustani maridadi. Ujenzi ulipoanza Krugersdorp, kulikuwa na Mashahidi 28,000 wenye bidii nchini Afrika Kusini. Kufikia wakati wa kuwekwa wakfu, Machi 21, 1987, idadi hiyo ilikuwa imeongezeka kufikia 40,000. Lakini wengine walikuwa na shaka ikiwa jengo hilo kubwa lilihitajiwa. Orofa moja ya ofisi haikutumiwa, na sehemu moja nzima ya vyumba vya kulala haikutumiwa pia. Akina ndugu walikuwa wamejaribu kuona mbele, na walikuwa na uhakika kwamba wametayarishia ongezeko.

KUSHUGHULIKIA UHITAJI WA MAANA

Kwa sababu makutaniko yaliongezeka, kulikuwa na uhitaji wa haraka wa kujenga Majumba mengine ya Ufalme. Akina ndugu katika maeneo yenye weusi wengi walifanya mikutano yao katika hali ngumu. Walitumia magereji, vibanda, na madarasa. Katika madarasa hayo, waliketi kwenye meza ndogo zilizotengenezwa kwa ajili ya watoto wadogo. Pia, walikabili watu wa vikundi vingine vya dini ambao walitumia madarasa ya shule hizo na kuimba kwa sauti kubwa huku wakipiga kelele kwa ngoma zao.

Mwishoni mwa miaka ya 1980, Halmashauri za Ujenzi za Mkoa zilianza kujaribu mbinu mpya za ujenzi ili ziharakishe ujenzi wa Majumba ya Ufalme. Mwaka wa 1992, Mashahidi 11 kutoka Kanada wenye uzoefu wa kujenga majumba haraka, walijitolea kujenga jengo la orofa mbili lenye Majumba mawili ya Ufalme, katika sehemu inayoitwa Hillbrow, jijini Johannesburg. Ndugu hao waliwazoeza akina ndugu wenyeji na kuwasaidia kuwa wajenzi bora.

Jumba la Ufalme la kwanza kumalizwa haraka lilijengwa Diepkloof, Soweto, mwaka wa 1992. Tangu mwaka wa 1962, akina ndugu walikuwa wamejaribu kupata uwanja kwa ajili ya Jumba la Ufalme katika eneo hilo. Zechariah Sedibe, aliyehusika katika kutafuta uwanja huo, alikuwapo wakati Jumba hilo la Ufalme lilipowekwa wakfu Julai 11, 1992. Alisema hivi, huku akitabasamu sana: “Tulifikiri kwamba hatutapata kamwe kuwa na Jumba la Ufalme. Wakati huo tulikuwa vijana. Sasa nimestaafu, lakini tuna jumba letu wenyewe, la kwanza kabisa kujengwa kwa siku chache huku Soweto.”

Kwa sasa, kuna Majumba ya Ufalme 600 katika nchi zinazosimamiwa na ofisi ya tawi ya Afrika Kusini. Majumba hayo ni vituo vya ibada safi ya Yehova. Lakini bado makutaniko 300 hivi yenye wahubiri 30 au zaidi yanahitaji Jumba la Ufalme.

Chini ya usimamizi wa ofisi ya tawi, Halmashauri za Ujenzi za Mkoa 25 zinasaidia makutaniko yanayotaka kujenga jumba. Makutaniko yanaweza kupata mikopo ya ujenzi bila kutozwa riba. Peter Butt, ambaye ameshiriki ujenzi wa Majumba ya Ufalme kwa zaidi ya miaka 18, ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Ujenzi ya Mkoa wa Gauteng. Alisema kwamba ndugu walio katika halmashauri hizo wana familia na wanafanya kazi ya kimwili, hata hivyo, wanatenga wakati mwingi kuwasaidia ndugu zao.

Mshiriki mwingine wa halmashauri ya mkoa, Jakob Rautenbach, alieleza kwamba washiriki wa halmashauri hiyo wanafanya kazi kwenye ujenzi muda wote wa mradi huo. Pia wanashiriki kufanya mipango yote kabla ya ujenzi kuanza. Alisimulia kwa uchangamfu jinsi wafanyakazi wa kujitolea wanavyokuwa na furaha na ushirikiano. Wanasafiri mpaka kwenye eneo la ujenzi kwa gharama yao, na nyakati nyingine wanatoka mbali sana.

Jakob alisema kwamba ndugu wengine wengi wanatenga wakati wao na mali yao kusaidia ujenzi wa Majumba ya Ufalme. Kisha akatoa mfano huu: “Dada wawili wa kimwili wenye kampuni ya usafirishaji hupeleka kontena yetu ya vifaa yenye urefu wa meta 13 kwenye maeneo ya ujenzi kotekote nchini na hata katika nchi jirani, nao wamefanya hivyo tangu mwaka wa 1993. Huo ni mchango mkubwa kwelikweli! Baada ya kuona kazi yetu, makampuni mengi tunayoshughulika nayo yanachochewa kutoa michango au kutupunguzia bei.”

Baada ya kufanya mipango kwa uangalifu na kupanga vikundi vya wajenzi, kwa kawaida inawachukua akina ndugu siku tatu kujenga jumba. Jambo hilo limefanya watazamaji wengi watuheshimu. Siku ya kwanza ya ujenzi katika eneo fulani, wanaume wawili waliokuwa wamekunywa kupita kiasi kwenye baa iliyokuwa karibu waliwaendea ndugu zetu jioni moja. Walisema kwamba kila mara walipokuwa wakirudi nyumbani, walipita katika uwanja fulani ambao haukuwa na nyumba, lakini sasa wanaona jumba hapo. Waliomba waonyeshwe njia kwa sababu walifikiri wamepotea.

ROHO YA KUJIDHABIHU

Mabadiliko ya kisiasa mapema katika miaka ya 1990 hayakuleta amani na utulivu. Badala yake, jeuri iliongezeka kuliko wakati mwingine wowote. Hali zilikuwa ngumu, na watu wanaamini kwamba ongezeko la jeuri limesababishwa na mambo mbalimbali, hasa mizozo ya kisiasa na watu kutoridhika na uchumi.

Hata hivyo, ujenzi wa Majumba ya Ufalme uliendelea. Wafanyakazi wa kujitolea wa rangi mbalimbali walienda katika maeneo ya weusi wakiandamana na ndugu wenyeji. Wengine walishambuliwa na umati wenye hasira. Wakati wa ujenzi wa jumba fulani huko Soweto mwaka wa 1993, umati wenye jeuri uliwarushia mawe ndugu watatu wazungu walipokuwa wakipeleka vifaa kwenye eneo la ujenzi wa Jumba la Ufalme. Madirisha yote ya gari lao yalivunjwa, nao wakajeruhiwa. Waliendelea kuendesha gari mpaka kwenye mahali pa ujenzi. Kisha, ndugu wenyeji wakawapeleka haraka hospitali kupitia njia salama.

Kazi ya ujenzi haikusimama. Akina ndugu walifanya kazi wakiwa macho, na mamia ya akina ndugu wa rangi zote walishiriki ujenzi mwishoni mwa juma lililofuata. Mapainia wenyeji walihubiri barabarani karibu na jumba hilo. Walipoona dalili za matata, waliwaonya ndugu waliokuwa wakijenga. Siku chache baadaye, ndugu waliojeruhiwa walikuwa wamepata nafuu vya kutosha kurudia ujenzi.

Makutaniko yanathamini kazi ngumu na kujidhabihu kwa ndugu wanaojitolea kujenga Majumba ya Ufalme. Kwa miaka 15, Fanie na Elaine Smit wamesaidia makutaniko 46 kujenga Majumba ya Ufalme, na mara nyingi wamesafiri mbali sana kwa gharama yao.

Kutaniko moja mkoani KwaZulu-Natal liliandika barua kwa Halmashauri ya Ujenzi ya Mkoa na kusema: “Mlijinyima usingizi, kuwa na familia zenu, kujifurahisha, na mambo mengine mengi ili mje hapa kutujengea jumba. Isitoshe, tunajua kwamba mlitumia pesa zenu nyingi kwa ajili ya kazi hii. Yehova awakumbuke ‘kwa ajili ya wema.’—Nehemia 13:31.”

Kutaniko likiwa na Jumba la Ufalme, kunakuwa na matokeo mazuri katika eneo. Maelezo haya ya kutaniko moja yanaonyesha inavyokuwa katika sehemu nyingi: “Ongezeko katika hudhurio baada ya ujenzi wa Jumba la Ufalme limefanya kutaniko hili ligawanywe katika vikundi viwili kwa ajili ya hotuba ya watu wote na Funzo la Mnara wa Mlinzi. Tutahitaji kuanzisha kutaniko lingine karibuni.”

Nyakati nyingine si rahisi kwa makutaniko madogo huko vijijini kupata pesa za kujenga jumba. Hata hivyo, makutaniko mengi yametafuta njia za kupata pesa. Katika kutaniko moja, akina ndugu waliuza nguruwe. Walipohitaji pesa zaidi, waliuza ng’ombe-dume na farasi. Kisha wakauza kondoo 15, ng’ombe-dume mwingine, na farasi. Dada mmoja alijitolea kununua rangi, mwingine akanunua zulia, na mwingine mapazia. Mwishowe, ng’ombe-dume mwingine na kondoo watano wengine wakauzwa ili viti vinunuliwe.

Ujenzi wa Jumba lao la Ufalme ulipokwisha, kutaniko fulani mkoani Gauteng liliandika hivi: “Kwa majuma mawili hivi baada ya jumba kujengwa, tulikuwa tukienda kulitazama baada ya utumishi wa shambani. Hatungeenda nyumbani baada ya utumishi wa shambani bila kulitazama Jumba letu la Ufalme.”

WENGINE PIA WANAONA

Mara nyingi jamii inaona jinsi Mashahidi wa Yehova wanavyofanya kila wanaloweza ili kupata mahali pa ibada panapofaa. Kutaniko fulani huko Umlazi, KwaZulu-Natal, lilipokea barua iliyosema: “Shirika la Kudumisha Usafi wa Durban linathamini bidii yenu ya kusafisha eneo lenu na linawatia moyo mwendelee kufanya hivyo. Bidii yenu imefanya eneo hili lipendeze. Shirika letu limejitolea kuondoa takataka na kusafisha mazingira. Tunaamini kwamba usafi huleta afya bora katika eneo. Ndiyo sababu tunawapongeza raia zetu kwa kusafisha eneo letu. Asanteni kwa mfano wenu mzuri. Katika shughuli zenu zote, endeleeni kudumisha usafi katika eneo la Umlazi.”

Kutaniko moja liliandika hivi: “Mwizi anayejulikana sana alipovunja na kuingia Jumba letu jipya la Ufalme, watu wanaoishi karibu walimshambulia. Kwa sababu hakuna jengo lingine la ibada karibu, walisema anaharibu ‘kanisa lao.’ Walimpiga kisha wakampeleka kwa polisi.”

KUSHUGHULIKIA UHITAJI WA MAJUMBA YA UFALME AFRIKA

Mwaka wa 1999, tengenezo la Yehova lilianzisha mpango wa kujenga Majumba ya Ufalme katika nchi zenye uhitaji. Idara ya Ujenzi wa Majumba ya Ufalme ilianzishwa katika ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ili isimamie kazi hiyo katika nchi kadhaa za Afrika. Mwakilishi wa idara hiyo alitumwa katika kila tawi kuwasaidia akina ndugu kuanzisha Dawati la Ujenzi wa Majumba ya Ufalme. Dawati hilo linasimamia Vikundi vya Ujenzi wa Majumba ya Ufalme na pia ununuzi wa viwanja. Watumishi wa kimataifa walitumwa pia kuwasaidia na kuwazoeza ndugu wenyeji.

Idara ya Ujenzi ya Afrika Kusini imeanzisha Madawati ya Ujenzi wa Majumba ya Ufalme katika nchi 25 barani Afrika. Madawati hayo yanasimamia ujenzi wa Majumba ya Ufalme katika nchi 37. Tangu Novemba 1999, Majumba ya Ufalme 7,207 yamejengwa katika nchi zilizo chini ya mpango huo. Kufikia katikati ya mwaka wa 2006, ilionekana bado kuna uhitaji wa kujenga Majumba ya Ufalme 3,305 katika nchi hizo.

MATOKEO YA MABADILIKO YA KISIASA

Fujo na jeuri ilitokea kwa sababu watu walichukizwa na sera za ubaguzi wa rangi za serikali ya zamani, na Mashahidi wa Yehova wengine waliathiriwa. Vita vikali vilitokea katika maeneo ya weusi, na watu wengi walikufa. Hata hivyo, ndugu wengi walikuwa waangalifu na waliendelea kumtumikia Yehova kwa uaminifu wakati huo mgumu. Usiku fulani, bomu la petroli lilirushwa ndani ya nyumba ya ndugu wakati yeye na familia yake walipokuwa wakilala. Walifaulu kutoroka, na baadaye ndugu huyo aliiandikia ofisi ya tawi barua na kusema: “Sasa imani yangu na ya familia yangu imeimarika. Tulipoteza mali yetu yote, lakini tumemkaribia Yehova na watu wake zaidi. Akina ndugu wametupa msaada wa kimwili. Tunapongojea mwisho wa mfumo huu wa mambo, tunamshukuru Yehova kwa paradiso yetu ya kiroho.”

Mei 10, 1994, rais mweusi wa kwanza, Nelson Mandela, aliapishwa. Pia, yeye ndiye rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia, nayo ilikuwa mara ya kwanza kwa weusi kuruhusiwa kupiga kura. Kulikuwa na roho ya uzalendo na msisimuko mwingi. Mambo hayo yaliwaletea baadhi ya ndugu zetu matatizo ya aina nyingine.

Inahuzunisha kwamba baadhi ya watu wa Yehova walivunja msimamo wao wa Kikristo wa kutokuwamo, hata hivyo wengi hawakufanya hivyo. Wengi waliobadili msimamo wao walitambua kosa lao, wakaonyesha toba ya kweli, na kufanya maendeleo walipotiwa moyo kwa Maandiko.

UKUZI KATIKA MIOYO

Ujenzi wa Majumba ya Ufalme unaonyesha baraka za Yehova, lakini ukuzi wa ajabu unatokea katika mioyo ya watu. (2 Kor. 3:3) Watu wenye malezi mbalimbali wanavutiwa na kweli. Ona mifano hii.

Ralson Mulaudzi alifungwa gerezani mwaka wa 1986 na kuhukumiwa kifo kwa sababu ya kuua. Alipata anwani ya ofisi ya tawi katika mojawapo ya broshua zetu, naye akaandika barua ya kuomba afundishwe Biblia. Les Lee, painia wa pekee, aliruhusiwa kumtembelea, naye akaanza kumfundisha Biblia. Baada ya muda, Ralson alianza kuwaeleza wafungwa na walinzi mambo anayojifunza. Alibatizwa gerezani Aprili 1990. Ndugu wa kutaniko la karibu wanamtembelea Ralson kwa ukawaida, naye anapewa ruhusa atoke nje ya jela kwa saa moja kila siku. Anatumia wakati huo kuwahubiria wafungwa wengine. Ralson amewasaidia watu watatu wabatizwe na anaongoza mafunzo mawili ya Biblia. Hukumu yake ya kifo imepunguzwa kuwa kifungo cha maisha gerezani na uwezekano wa kupewa kifungo cha nje.

Wengine ambao wamevutwa kwa Yehova wana hali tofauti kabisa. Mwanamke fulani anayependezwa, ambaye anaitwa Queenie Rossouw, alihudhuria Funzo la Kitabu la Kutaniko na kumwomba mwangalizi wa funzo la kitabu amtembelee mwana wake mwenye umri wa miaka 18, ambaye alikuwa akijitayarisha kwa ajili ya masomo ya katekisimu. Ndugu huyo alifurahia mazungumzo pamoja na kijana huyo, na kijana akaanza kuhudhuria mikutano pamoja na mama yake. Kisha mama huyo akamwomba yule ndugu amtembelee mume wake, Jannie, ambaye alikuwa mzee wa Kanisa la Dutch Reformed na mwenyekiti wa kamati ya kanisa; alikuwa na maswali fulani. Ndugu huyo alizungumza na mwanamume huyo, naye akakubali funzo la Biblia.

Hilo lilikuwa juma la kusanyiko la wilaya, na ndugu huyo alimwalika Queenie ahudhurie. Ndugu huyo alishangaa alipomwona Jannie pia akihudhuria siku zote nne. Programu ya kusanyiko na upendo alioona kati ya Mashahidi ulimchochea sana mwanamume huyo. Mwana wao mwenye umri wa miaka 18 na mwana wao mkubwa ambaye alikuwa shemasi katika kanisa hilo, walianza pia kushiriki funzo hilo la Biblia.

Wote walijiuzulu kanisani, na bila kukawia wakaanza kuhudhuria mikutano. Pia walihudhuria mkutano wa utumishi wa shambani. Ndugu huyo alimweleza Jannie kwamba hawezi kwenda katika utumishi wa shambani pamoja na Mashahidi kwa sababu hajastahili kuwa mhubiri ambaye hajabatizwa. Mwanamume huyo alitiririkwa na machozi na kusema kwamba ametafuta kweli maisha yake yote naye hawezi kujizuia asiongee kuihusu.

Akina Rossouw walikuwa na mwana mwingine mwenye umri wa miaka 22, ambaye alikuwa katika mwaka wa tatu wa masomo ya dini. Jannie alimwandikia mwana huyo na kumwomba aje nyumbani kwa sababu hangemlipia tena mwana huyo masomo yake. Siku ya tatu baada ya mwana huyo kurudi, Jannie na wana wake watatu walifanya kazi na kutaniko kwa siku moja katika Betheli huko Krugersdorp. Mwanafunzi huyo wa masomo ya dini alivutiwa na mambo aliyoona Betheli, naye akakubali kujifunza Biblia pamoja na ndugu zake. Baada ya kujifunza kwa muda, alisema kwamba amejifunza mengi kuhusu Biblia kwa mwezi mmoja kuliko kwa miaka miwili na nusu aliyokuwa chuo kikuu.

Mwishowe, familia yote ikabatizwa. Sasa baba ni mzee, na baadhi ya wana wake ni wazee au watumishi wa huduma. Binti mmoja ni painia wa kawaida.

“REFUSHA KAMBA ZA HEMA LAKO”

Ingawa mwanzoni akina ndugu walijitahidi kujenga Betheli ambayo ingetosheleza mahitaji ya wakati ujao, miaka 12 tu baada ya kuwekwa wakfu kwa majengo mapya huko Krugersdorp, upanuzi mkubwa ulihitaji kufanywa. (Isa. 54:2) Kwa kipindi hicho, kulikuwa na ongezeko la asilimia 62 la wahubiri nchini Afrika Kusini na nchi nyinginezo zilizo chini ya ofisi hiyo ya tawi. Bohari na majengo matatu mapya ya kukaa yalijengwa. Pia, jengo la udobi na majengo ya ofisi yalipanuliwa, na chumba cha pili cha kulia kikajengwa. Mnamo Oktoba 23, 1999, majengo yote hayo yaliwekwa wakfu kwa Yehova. Daniel Sydlik, mshiriki wa Baraza Linaloongoza alitoa hotuba ya wakfu.

Hivi majuzi, kiwanda cha uchapishaji kilipanuliwa kwa mita 8,000 za mraba. Kiwanda hicho kina mashini za uchapaji zinazoitwa MAN Roland Lithoman. Ofisi ya tawi ilipokea pia mashini za kukata, kuhesabu, na kupanga magazeti. Ofisi ya tawi ya Ujerumani ilitoa mashini ya kujalidi, inayowezesha Afrika Kusini kutengeneza vitabu na Biblia zenye jalada jepesi kwa ajili ya maeneo yote ya Afrika yaliyo kusini mwa Sahara.

MAHALI PANAPOFAA KWA AJILI YA MAKUSANYIKO

Kulikuwa na miradi mingi ya ujenzi wa Majumba ya Kusanyiko. Jumba la kwanza lilijengwa huko Eikenhof, kusini mwa Johannesburg, na likawekwa wakfu mwaka wa 1982. Lingine lilijengwa Bellville, huko Cape Town, na hotuba ya wakfu ilitolewa na Milton Henschel, mwaka wa 1996. Katika mwaka wa 2001, jumba lingine pia lilikamilishwa huko Midrand, katikati ya Pretoria na Johannesburg.

Majirani ambao mwanzoni walipinga ujenzi huko Midrand walibadili mtazamo wao walipopata kuwajua akina ndugu na kuona kazi yao. Jirani mmoja alijitolea kuwapelekea matunda na mboga kila baada ya majuma mawili kwa zaidi ya mwaka mmoja. Kampuni kadhaa zilichochewa kutoa michango. Kampuni moja ilitoa mbolea kwa ajili ya bustani bila kutoza chochote. Nyingine iliwapa akina ndugu hundi ya dola za Marekani zipatazo 1,575, kwa ajili ya ujenzi. Bila shaka, akina ndugu pia walitoa michango kwa ukarimu kwa ajili ya ujenzi wa Jumba la Kusanyiko.

Jumba hilo ni maridadi nalo limeundwa vizuri. Guy Pierce, mshiriki wa Baraza Linaloongoza ambaye alitoa hotuba ya wakfu, alizungumzia umaridadi halisi wa jumba hilo, yaani, kumtukuza Mungu wetu Mkuu, Yehova.—1 Fal. 8:27.

SHERIA ZA WANADAMU HAZIJAWATENGANISHA

Kwa miaka mingi haikuwa rahisi kupata mahali panapofaa pa kufanyia makusanyiko katika maeneo ya weusi. Katika Mkoa wa Limpopo, akina ndugu walikuwa wakiishi katika eneo lililotengewa watu weusi peke yao. Corrie Seegers, mwangalizi wa wilaya, hangeweza kupata kibali cha kuingia katika eneo hilo wala mahali pa kufanyia kusanyiko.

Ndugu Seegers alizungumza na mtu fulani ambaye shamba lake lilikuwa karibu na eneo lililotengewa weusi, lakini mtu huyo hakutaka kusanyiko lifanywe katika shamba lake. Hata hivyo, alimruhusu Ndugu Seegers aegeshe gari lake huko. Mwishowe, akina ndugu walifanyia kusanyiko msituni katika mahali palipofyekwa katika eneo hilo lililotengwa. Eneo hilo lilipakana na shamba la mkulima huyo, nalo lilitenganishwa kwa seng’enge. Ndugu Seegers aliegesha gari lake katika shamba la mkulima huyo karibu na mahali palipofyekwa na kutoa hotuba zake kutoka hapo. Ingawa ua liliwatenganisha akina ndugu na “jukwaa,” walihudhuria programu ya kusanyiko, naye Ndugu Seegers aliweza kuwahutubia bila kuvunja sheria.

BADILIKO LAFAIDI HUDUMA

Baraza Linaloongoza lilitoa mwongozo kwamba kuanzia mwaka wa 2000, makutaniko yote nchini Afrika Kusini yangeanza kutoa vichapo bila malipo kwa watu wote wanaopendezwa kikweli. Wahubiri wangewaalika watu kutoa michango kidogo kwa ajili ya kazi ya kuhubiri ya ulimwenguni pote.

Mpango huo wa kutoa michango ya hiari umewafaidi akina ndugu pamoja na wale wanaohubiriwa. Awali, wengi hawakuweza kugharimia vichapo vinavyotumiwa kwa ajili ya Funzo la Mnara wa Mlinzi na Funzo la Kitabu la Kutaniko. Katika makutaniko fulani yenye wahubiri 100, wahubiri kama 10 tu ndio waliokuwa na nakala za Mnara wa Mlinzi. Sasa kila mtu anaweza kupata nakala yake mwenyewe.

Kazi inayofanywa na Idara ya Usafirishaji ya Betheli imeongezeka sana katika miaka ya karibuni. Mnamo Mei 2002, jumla ya tani 432 za bidhaa zilitumwa nchi nyingine za Afrika, nyingi zikiwa vichapo vya Biblia.

Sasa ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ina sehemu iliyotengwa kwa ajili ya vichapo vya ofisi ya tawi ya Malawi, Msumbiji, Zambia, na Zimbabwe. Vichapo hivyo vinatia ndani vile vya lugha mbalimbali zinazotumiwa katika nchi hizo. Magari hupakiwa vichapo vya kila kutaniko kwa njia ya kwamba vinapopelekwa katika ofisi za tawi, vinaweza kuhamishwa moja kwa moja katika magari ya ofisi ya tawi na kupelekwa katika depo mbalimbali.

Tangu mpango wa kutoa vichapo bila malipo uanzishwe, vichapo vingi vinaagizwa. Idadi ya magazeti yanayochapishwa nchini Afrika Kusini imeongezeka kutoka milioni moja hadi milioni 4.4 kila mwezi. Maagizo ya vichapo yameongezeka kufikia tani 3,800 kila mwaka, ikilinganishwa na tani 200 mwaka wa 1999.

Vifaa vya ujenzi pia hutumwa nchi nyingine za Afrika. Isitoshe, ofisi ya Afrika Kusini hutuma misaada kwa akina ndugu walio na uhitaji. Mara nyingi misaada ilitumwa kwa akina ndugu wa Malawi ambao kwa sababu ya mateso makali walitoroka makwao na kuishi kambini. Misaada ilitumwa katika nchi ya Angola, ambayo ilikumbwa na ukame mwaka wa 1990. Pia, kwa sababu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, akina ndugu wengi walikuwa maskini, nao walitumiwa vyakula na mavazi. Katika mwaka wa 2000, akina ndugu nchini Msumbiji walisaidiwa baada ya kukumbwa na mafuriko makubwa. Akina ndugu nchini Zimbabwe ambao waliathiriwa na ukame mkali mwaka wa 2002 na mapema mwaka wa 2003, walitumiwa zaidi ya tani 800 za mahindi.

MAENDELEO KATIKA KUTAFSIRI

Ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ina Idara kubwa ya Tafsiri. Miaka kadhaa iliyopita, ilipanuliwa ili kushughulikia kazi ya kutafsiri Biblia. Kwa sasa kuna watafsiri 102 ambao wanatafsiri vichapo katika lugha 13.

Tafsiri ya Ulimwengu Mpya inapatikana sasa katika lugha saba za kienyeji. Ndugu mmoja alisema hivi kuhusu Biblia ya Kitswana: “Kitswana kimeboreka sana. Kinaeleweka na kinapendeza unapokisoma na unaposikia kikisomwa. Ningependa kumshukuru Yehova pamoja na tengenezo lake linaloongozwa na roho kwa vile tunavyolishwa kiroho.”

Teknolojia ya kisasa imetumiwa vizuri kuwasaidia watafsiri. Akina ndugu nchini Afrika Kusini walipokuwa wakitayarisha programu za kompyuta za kuwasaidia watafsiri, idara yenye lengo hilohilo ilianzishwa Brooklyn. Hatimaye programu mbalimbali zilizobuniwa ziliunganishwa na kufanyiza programu moja inayoitwa Watchtower Translation System. Watayarishaji wa programu hizo nchini Afrika Kusini walichangia sana kuundwa kwa programu hiyo.

Akina ndugu hawakujaribu kuunda programu za kompyuta ili zitafsiri, jambo ambalo kampuni kadhaa zimejaribu bila mafanikio. Badala yake, walijaribu sana kuwapa watafsiri vifaa. Kwa mfano, Biblia zinapatikana kwenye kompyuta. Watafsiri pia wanaweza kujitengenezea kamusi zao kwenye kompyuta. Kamusi hizo ni zenye thamani kwa sababu lugha kadhaa hazina kamusi za kutosha.

KUPANDA MBEGU ZA KWELI MIONGONI MWA VIZIWI

Wahubiri wa Ufalme hujaribu kumfikia kila mtu. Imekuwa vigumu kuwasiliana na viziwi, lakini matokeo yanaridhisha. Katika miaka ya 1960, June Carikas alianza kujifunza Biblia na mwanamke kiziwi. Mwanamke huyo pamoja na mume wake ambaye pia ni kiziwi, walifanya maendeleo wakabatizwa.

Tangu wakati huo viziwi wengi wamekubali kweli, navyo vikundi vya viziwi vimeanzishwa majijini kotekote nchini. Akina ndugu wamezoea kuwa na sehemu ya lugha ya ishara makusanyikoni. Inapendeza sana kuona wahudhuriaji wakiimba katika lugha ya ishara na “kupiga makofi” pamoja na wengine kwa kupunga mikono yao hewani.

Kikundi cha kwanza cha lugha ya ishara kilianzishwa katika Kutaniko la Brixton huko Johannesburg chini ya usimamizi wa mume wa June, George, ambaye ni mzee. Akina ndugu kutanikoni, kutia ndani Wanabetheli kadhaa, walifunzwa lugha ya ishara. Sasa, kuna kutaniko moja la lugha ya ishara na vikundi vitano katika eneo linalosimamiwa na ofisi ya tawi ya Afrika Kusini.

MATOKEO YA KAZI YA UFALME KATIKA NCHI NYINGINE

Ofisi ya tawi ya Afrika Kusini inasimamia kazi ya kuhubiri katika nchi nyingine tano. Ifuatayo ni taarifa fupi kuhusu maendeleo ya kazi ya Ufalme katika nchi hizo.

Namibia

Nchi hii imeanzia Bahari ya Atlantiki mpaka upande wa magharibi wa Botswana. Baada ya Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, Ushirika wa Mataifa uliamuru Namibia iwe chini ya utawala wa Afrika Kusini. Mwishowe, baada ya msukosuko mwingi na umwagaji wa damu, Namibia ilipata uhuru mwaka wa 1990. Ingawa sehemu kubwa ya nchi hiyo ni kame na ina watu wachache, ina sehemu maridadi zilizo na wanyama-mwitu wengi na mimea yenye kuvutia. Jangwa la Namib huvutia wageni wengi ambao huenda wakashangaa kuona wanyama-mwitu wa aina mbalimbali wanaoishi katika hali hizo ngumu. Namibia ina mandhari yenye kuvutia na watu wenye kupendeza wanaozungumza lugha tisa za taifa.

Kazi ya kuhubiri ujumbe wa Ufalme nchini Namibia ilianza mwaka wa 1928. Mwaka huo, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ilituma vichapo vingi vya Biblia kwa watu ambao hawangeweza kufikiwa. Karibu wakati huo, mtu wa kwanza kuwa Mkristo aliyejiweka wakfu nchini Namibia alijifunza kweli kwa njia isiyo ya kawaida. Bernhard Baade alinunua mayai yaliyofungwa kwa karatasi zilizopasuliwa kutoka kwa kichapo chetu kimoja. Alisoma karatasi hizo kwa makini, bila kujua zilitoka wapi. Yai moja lilikuwa limefungwa kwa ukurasa wa mwisho wa kichapo hicho, ambao ulionyesha anwani ya ofisi ya tawi ya Ujerumani. Aliandika kuomba vichapo zaidi. Mwangalizi wa mzunguko ambaye baadaye alitembelea kutaniko ambalo Bernhard alikuwa akihudhuria alisema kwamba kwa miaka yote hadi kifo chake, Bernhard hakukosa kuhubiri hata mwezi mmoja.

Mwaka wa 1929, Lenie Theron alitumwa Windhoek, jiji kuu la Namibia. Dada huyo painia alihubiri katika miji yote mikubwa ya Namibia, akisafiri kwa gari-moshi na gari la kupeleka barua. Kwa miezi minne aliachia watu vitabu na vijitabu 6,388 katika Kiafrikana, Kiingereza, na Kijerumani. Ijapokuwa mapainia walihubiri Namibia mara kwa mara, hakuna aliyebaki kufuatia upendezi. Mambo yalibadilika mwaka wa 1950 wamishonari kadhaa walipowasili. Miongoni mwao ni Gus Eriksson, Fred Hayhurst, na George Koett, ambao walidumisha uaminifu katika utumishi wao hadi kifo.

Kufikia mwaka wa 1953, kulikuwa na wamishonari wanane nchini humo, kutia ndani Dick Waldron na mke wake Coralie.e Walilazimika kuvumilia upinzani mkali kutoka kwa viongozi wa dini zinazodai kuwa za Kikristo na vilevile wenye mamlaka katika eneo hilo. Ingawa Ndugu na Dada Waldron walitaka kuwahubiria wenyeji ujumbe wa Biblia, walihitaji kibali cha kuingia maeneo ya weusi. Dick alituma maombi lakini hakufanikiwa.

Baada ya binti yao kuzaliwa mwaka wa 1955, Ndugu na Dada Waldron waliacha umishonari, lakini Dick aliendelea kufanya upainia kwa muda. Mwishowe, mwaka wa 1960, Dick alipata kibali cha kuingia Katutura, mojawapo ya maeneo ya weusi. Anasema, “Watu walipendezwa sana.” Baada ya muda mfupi, watu wengi kutoka eneo hilo walikuwa wanahudhuria mikutano. Sasa, miaka zaidi ya 50 baadaye, Dick na Coralie wanaendelea kutumikia kwa uaminifu nchini Namibia. Wamesaidia sana kuendeleza kazi ya Ufalme katika eneo hilo.

Haikuwa rahisi kuwapelekea kweli ya Biblia watu wa jamii mbalimbali nchini Namibia. Hakukuwa na kichapo chochote cha Biblia katika lugha za kienyeji, kama vile Kiherero, Kikwangali, na Kindonga. Mwanzoni, wenyeji waliokuwa na elimu na ambao walikuwa wakijifunza Biblia, walitafsiri trakti na broshua kadhaa wakisimamiwa na Mashahidi wenyeji. Esther Bornman, aliyekuwa painia wa pekee wakati huo, alijifunza Kikwanyama na baada ya muda angeweza kukizungumza vizuri hali kadhalika lugha nyingine ya kienyeji. Yeye na Aina Nekwaya, dada anayezungumza Kindonga, walitafsiri gazeti la Mnara wa Mlinzi, ambalo huchapishwa kwa sehemu katika Kikwanyama na Kindonga. Lugha hizo mbili zinatumiwa huko Ovamboland na watu wengi wanazielewa.

Mwaka wa 1990, ofisi ya kutafsiri yenye vifaa vya kutosha ilianzishwa huko Windhoek. Watafsiri zaidi wakaongezwa, na mbali na lugha zilizotangulia kutajwa, vichapo vinatafsiriwa katika Kiherero, Kikwangali, Kikhoekhoegowab, na Kimbukushu. André Bornman na Stephen Jansen wanasimamia ofisi hiyo.

Namibia ina almasi nyingi. Mnara wa Mlinzi wa Julai 15, 1999, lilitaja jambo hilo katika makala yenye kichwa “Kuna Johari Hai Nchini Namibia!” Makala hiyo iliwalinganisha watu wenye mioyo minyoofu na “johari hai” nayo ikasema kwamba ingawa kazi kubwa ya kuhubiri imefanywa, maeneo fulani nchini humo hayajahubiriwa bado. Makala hiyo ilitoa mwaliko huu: “Je, unaweza kutumikia mahali ambapo wapiga-mbiu wa Ufalme wenye bidii wanahitajiwa sana? Basi, tafadhali, vuka uingie Namibia, utusaidie kung’arisha johari zaidi za kiroho.”

Itikio lilikuwa lenye kupendeza. Akina ndugu 130 kutoka nchi mbalimbali, kutia ndani Australia, Japani, na Ujerumani, na nchi nyingine za Amerika ya Kusini, waliomba habari zaidi. Matokeo yakawa kwamba, 83 kati yao walitembelea Namibia na 18 miongoni mwao wakabaki. Kati yao, 16 walikuwa mapainia wa kawaida walipofika, na baada ya muda baadhi yao waliwekwa kuwa mapainia wa pekee. Roho ya wafanyakazi hao wa kujitolea iliwachochea wengine. Hata sasa, ofisi ya tawi hupokea barua za watu wanaotaka kupata habari zaidi kuhusiana na mwaliko uliokuwa katika Mnara wa Mlinzi. William na Ellen Heindel wametumikia wakiwa wamishonari kaskazini mwa Namibia tangu mwaka wa 1989. Walihitaji kujifunza Kindonga kinachozungumzwa na Waovambo, wanaoishi katika eneo hilo. Wamepata baraka nyingi kwa sababu ya uvumilivu na bidii yao ya kuhubiri eneo hilo la ajabu. William anasema: “Tumewaona wavulana, ambao baadhi yao walikuwa wanafunzi wetu wa Biblia, wakikua na kuwa wanaume wa kiroho. Baadhi yao ni wazee na watumishi wa huduma kutanikoni. Sisi hujivunia vijana hao tunapowaona wakitoa hotuba makusanyikoni.”

Katika miaka ya karibuni wahitimu kadhaa wa Shule ya Mazoezi ya Kihuduma wametumwa Namibia, nao wamefanya mengi katika kukuza upendezi na kutumikia makutanikoni. Mwaka wa 2006, kulikuwa na wahubiri 1,264 nchini Namibia, ongezeko la asilimia 3 kuliko mwaka uliotangulia.

Lesotho

Nchi ndogo ya Lesotho yenye watu milioni 2.4 imezingirwa kabisa na nchi ya Afrika Kusini. Iko kwenye Milima inayopendeza ya Drakensberg.

Ingawa kwa kawaida kuna utulivu, nchi hiyo imekuwa na misukosuko ya kisiasa pia. Mwaka wa 1998, mizozo ya uchaguzi ilisababisha vita kati ya wanajeshi na polisi katika jiji kuu la Maseru. Wakati huo, Veijo Kuismin na mke wake, Sirpa, walikuwa wamishonari huko. Veijo anasema: “Ni ndugu wachache tu walioumia wakati wa vita hivyo, nasi tulipanga kuwapa msaada wale ambao hawakuwa na chakula na fueli. Hilo liliimarisha zaidi umoja kutanikoni na hudhurio likaongezeka nchini kote.”

Uchumi wa Lesotho hutegemea hasa kilimo. Kwa sababu ya uchumi mbaya, wanaume wengi huhamia Afrika Kusini kufanya kazi katika migodi. Ingawa nchi hiyo ni maskini, utajiri wa kiroho unapatikana katika nchi hiyo yenye milima mingi, na watu wengi wamekubali kweli ya Biblia. Mwaka wa 2006, kulikuwa na wahubiri wa Ufalme 3,101, ongezeko la asilimia 2 kuliko mwaka uliotangulia. Wamishonari sita, Ndugu na Dada Hüttinger, Ndugu na Dada Nygren, na Ndugu na Dada Paris wanatumikia huko Maseru.

Abel Modiba alikuwa mwangalizi wa mzunguko nchini Lesotho kati ya mwaka wa 1974 na 1978. Sasa yeye na mke wake Rebecca, wanatumikia Betheli ya Afrika Kusini. Kwa utulivu na polepole, anasimulia maoni yake kuhusu Lesotho: “Maeneo mengi ya mashambani hayakuwa na barabara. Wakati mwingine ningetembea kwa saa saba ili kufikia kikundi cha wahubiri waliokuwa mbali. Mara nyingi akina ndugu walileta farasi, mmoja anibebe na mwingine abebe mizigo yangu. Wakati mwingine tulibeba mashini ya kuonyesha slaidi na betri yenye volti 12. Mto ulipofurika, tulingoja siku chache hadi maji yapungue. Katika vijiji fulani, mzee wa kijiji aliwaalika wakaaji waje kusikiliza hotuba ya watu wote.

“Baadhi yao walitembea kwa saa nyingi ili kufika mikutanoni, na kwa sababu hiyo, mwangalizi wa mzunguko alipokuja, waliotoka mbali sana walilala katika nyumba za akina ndugu walioishi karibu na Jumba la Ufalme. Hilo lilifanya iwe pindi ya pekee. Wakati wa jioni, walikusanyika na kuzungumzia mambo yaliyoonwa na kuimba nyimbo za Ufalme. Siku iliyofuata walienda kuhubiri.”

Per-Ola na Birgitta Nygren wametumikia wakiwa wamishonari huko Maseru tangu mwaka wa 1993. Birgitta anasimulia jambo lililoonwa ambalo linaonyesha thamani ya magazeti katika kuwasaidia watu: “Katika mwaka wa 1997, nilianza kujifunza na mwanamke anayeitwa Mapalesa. Alianza kuhudhuria mikutano, lakini nyakati nyingine hakuwa nyumbani kwa ajili ya funzo, na mara nyingi alijificha. Niliacha kujifunza naye lakini nikaendelea kumpelekea magazeti kwa ukawaida. Miaka mingi baadaye, alihudhuria mkutano wetu. Alieleza kwamba siku moja alisoma makala katika Mnara wa Mlinzi kuhusu kuzuia hasira. Aliona hilo kuwa jibu kutoka kwa Yehova kwa kuwa yeye na watu wake wa ukoo waligombana sikuzote. Alianza kujifunza tena, naye hajakosa mikutano tangu wakati huo. Pia, alianza kuhubiri kwa bidii.”

Kwa miaka mingi akina ndugu huko Lesotho walitumia majengo ya muda kama Majumba ya Ufalme. Hata hivyo, katika miaka ya karibuni, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini imesaidia makutaniko ya Lesotho kugharimia ujenzi wa Majumba ya Ufalme.

Jumba la Ufalme katika mji wa Mokhotlong lililo mita 3,000 hivi juu ya usawa wa bahari, ndilo liko juu zaidi barani Afrika. Ili kujenga jumba hili, wajitoleaji walitoka sehemu za mbali kama vile Australia na California, Marekani. Akina ndugu wa Mkoa wa KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini walitoa utegemezo wa kifedha na magari ya kusafirisha bidhaa na vyombo hadi mahali pa ujenzi. Makao ya wajitoleaji yalikuwa duni sana. Walilazimika kujitafutia matandiko na vyombo vya kupikia. Baada ya siku kumi jumba lilikamilika. Ndugu mmoja mzee kwa umri, aliyezaliwa mwaka wa 1910, alikuwapo siku zote za ujenzi kuona jinsi mambo yalivyoendelea. Amekuwa akitamani wawe na jumba lao wenyewe tangu alipokuwa mtumishi wa Yehova katika miaka ya 1920, naye alifurahi kuona maendeleo ya Jumba “lake” la Ufalme.

Mwaka wa 2002, nchi ya Lesotho ilikumbwa na njaa. Unga wa mahindi na bidhaa nyingine zilisafirishwa na kugawiwa Mashahidi katika maeneo yaliyoathiriwa. Barua ya kutoa shukrani ilisema: “Ndugu walipokuja nyumbani kuleta unga wa mahindi, nilishangaa sana. Walijuaje nilichohitaji? Nilimshukuru Yehova kwa msaada ambao sikuutarajia kamwe. Hilo liliimarisha imani yangu kwa Yehova Mungu na tengenezo lake, nami nimeazimia kumtumikia kwa nafsi yote.”

Botswana

Sehemu kubwa ya nchi hii ni Jangwa la Kalahari na ina idadi ya watu zaidi ya milioni 1.7. Kwa kawaida kuna joto na ukavu. Watalii hutembelea mbuga nyingi nchini humo. Delta ya Okavango yenye kuvutia inapendwa sana kwa sababu ya utulivu wake na wanyama-mwitu wengi. Watu hutumia mokoro, mashua zilizochongwa kutoka katika miti ya asili, ili kusafiri mtoni. Botswana imeimarika kiuchumi, hasa kwa sababu ya uchimbaji wa almasi. Tangu almasi ilipovumbuliwa katika Jangwa la Kalahari mwaka wa 1967, Botswana imekuwa mojawapo ya mataifa ambayo huuza almasi nyingi sana ulimwenguni.

Yaelekea ujumbe wa Ufalme wa Mungu ulifika Botswana mwaka wa 1929, wakati ndugu mmoja alipohubiri huko kwa miezi kadhaa. Joshua Thongoana aliwekwa rasmi kuwa mwangalizi wa mzunguko nchini Botswana mwaka wa 1956.f Anakumbuka kwamba wakati huo, vichapo vilivyochapishwa na Mashahidi wa Yehova vilipigwa marufuku huko.

Wamishonari wenye bidii wamekuwa na matokeo mazuri katika eneo hili. Blake na Gwen Frisbee pamoja na Tim na Virginia Crouch wamejitahidi kujifunza Kitswana. Upande wa kaskazini, Veijo na Sirpa Kuismin, wanafurahia kuwasaidia watu kiroho.

Upande wa kusini mwa nchi, Hugh na Carol Cormican wana bidii katika kazi ya umishonari. Hugh anasema: “Katika kutaniko letu kuna ndugu mwenye umri wa miaka 12 anayeitwa Eddie. Tangu alipokuwa na umri mdogo sana, alitaka kujua kusoma ili ajiandikishe katika Shule ya Huduma ya Kitheokrasi na kuhubiri. Mara tu alipostahili kuwa mhubiri ambaye hajabatizwa, alitumia wakati mwingi shambani na kuanzisha funzo la Biblia na mmoja wa wanafunzi wenzake. Tangu abatizwe, Eddie amefanya upainia msaidizi mara nyingi.”

Makutaniko mengi nchini Botswana yako katika au karibu na jiji kuu, Gaborone, lililo karibu na mpaka wa mashariki. Wakaaji walio wengi huishi katika eneo hilo. Wale wengine huishi vijijini kuelekea magharibi na katika Jangwa la Kalahari, ambapo familia za Kisan huzunguka-zunguka, wakitafuta chakula na kuwinda wakitumia upinde na mishale. Wahubiri hujitahidi sana wakati wa kampeni za kuhubiri maeneo ya mbali, wakisafiri maelfu ya kilomita ili kuwapelekea kweli za Biblia wafugaji wenye kuhamahama katika maeneo ya mashambani. Watu hao hukuza chakula, hujenga nyumba kutokana na vifaa vinavyopatikana huko, na kutafuta kuni. Hawana wakati mwingi kwa ajili ya mambo mengine. Hata hivyo, mgeni anapowasili akiwa na ujumbe wa Biblia wenye kuburudisha, wao hukubali kwa utayari kusikiliza wakiwa nje kwenye mchanga mwororo wa jangwani.

Stephen Robbins, mmoja kati ya mapainia sita wa pekee wa muda, alisema: “Sikuzote watu wako mbioni. Ni kana kwamba wao huvuka mipaka kama vile tunavyovuka barabara. Tulikutana na Marks, mmoja wa wanafunzi wetu wa Biblia ndani ya feri tulipokuwa tukivuka Mto Okavango. Tulifurahi kusikia kwamba alikuwa ameomba ruhusa kazini ili asafiri akawahubirie rafiki zake na watu wa ukoo kweli za Biblia. Marks hutumia nafasi zote anazopata katika kazi ya kuhubiri.”

Inafurahisha kwamba habari njema inakubaliwa nchini Botswana. Mwaka wa 2006, kulikuwa na wahubiri 1,497, walioshiriki kazi ya kuhubiri. Hilo ni ongezeko la asilimia 6 kuliko mwaka uliopita.

Swaziland

Nchi hiyo ndogo ina watu milioni 1.1 hivi. Hutegemea hasa kilimo, ingawa wanaume wengi hutafuta kazi Afrika Kusini. Swaziland ina mandhari yenye kupendeza na hifadhi kadhaa za wanyama. Waswazi ni wenye urafiki na bado wanafuata desturi zao nyingi.

Mfalme wa zamani Sobhuza wa Pili, aliwapenda Mashahidi wa Yehova, naye alikuwa na vichapo vyetu vingi. Mbali na kualika viongozi wa kidini katika makao yake ya kifalme kila mwaka, alikaribisha Shahidi wa Yehova ili kuzungumzia Biblia. Mwaka wa 1956, Shahidi aliyealikwa alizungumzia fundisho la kutoweza kufa kwa nafsi na vilevile kutumia majina ya vyeo miongoni mwa viongozi wa dini. Baadaye, mfalme aliwauliza viongozi wa dini ikiwa mambo yaliyosemwa ni kweli. Hawakuweza kukanusha mambo yaliyosemwa na ndugu huyo.

Ndugu walihitaji kuchukua msimamo thabiti dhidi ya desturi za kuomboleza zilizohusianishwa na ibada ya mababu. Katika sehemu fulani za Swaziland, machifu wa kikabila walifukuza Mashahidi wa Yehova kutoka katika nyumba zao wenyewe eti kwa sababu walikataa kufuata desturi za kuomboleza. Sikuzote ndugu zao wa kiroho katika maeneo mengine waliwatunza. Mahakama Kuu ya Swaziland ilitoa hukumu iliyowapendelea Mashahidi wa Yehova katika jambo hilo na kuagiza waruhusiwe kurudi katika nyumba zao na mashamba yao.

James na Dawne Hockett, ni wamishonari katika jiji kuu la Swaziland, Mbabane. James alihitimu Shule ya Gileadi mwaka wa 1971, naye Dawne alihitimu mwaka wa 1970. James alitumia mfano huu kuonyesha jinsi wamishonari wanavyolazimika kujifunza desturi mbalimbali: “Tulikuwa tukihubiri katika eneo ambalo halijagawiwa yeyote, naye chifu akawakusanya watu na kuniomba niwahutubie. Tulikuwa mahali ambapo ujenzi ulikuwa ukiendelea, na mawe ya kujengea yalikuwa yametapakaa. Kulikuwa na unyevunyevu, hivyo nikakalia jiwe moja, naye Dawne akaketi karibu na mimi kwenye jiwe hilo. Dada mmoja Mswazi alimwita Dawne na kumwomba aketi karibu naye. Dawne akamwambia kwamba yuko sawa, lakini dada huyo akasisitiza. Baadaye, tulielezwa kwamba kwa kuwa baadhi ya wanaume walikuwa wameketi chini kabisa, wanawake hawakupaswa kuketi juu kuliko wanaume. Hiyo ndiyo desturi huko mashambani.”

James na Dawne walitembelea shule fulani kuzungumza na mwalimu mmoja anayependezwa. Mwalimu huyo alimtuma mwanafunzi awaambie kwamba hangeweza kuzungumza nao wakati huo. Basi, wakaamua kuzungumza na mvulana huyo, anayeitwa Patrick. Walimuuliza ikiwa anajua ni kwa nini wamekuja. Baada ya mazungumzo, walimpa kitabu Maswali Ambayo Vijana Huuliza—Majibu Yafanyayo Kazi na kuanza kujifunza Biblia pamoja naye. Patrick alikuwa yatima aliyekuwa akiishi katika chumba kilichokuwa karibu na nyumba ya baba yake mdogo. Alilazimika kujitunza, kujipikia, na kufanya kazi ya muda ili ajilipie karo ya shule. Alifanya maendeleo, akabatizwa, na sasa ni mzee kutanikoni.

Tangu kazi ya kuhubiri ilipoanza miaka ya 1930, kumekuwa na itikio zuri sana nchini Swaziland. Mwaka wa 2006, kulikuwa na wahubiri 2,292 waliotangaza habari njema ya Ufalme wa Mungu katika eneo hilo, na mafunzo ya Biblia 2,911 yaliongozwa.

St. Helena

Kisiwa hicho kidogo chenye urefu wa kilomita 17 na upana wa kilomita 10 kiko upande wa magharibi ya pwani ya kusini-magharibi mwa Afrika. Kwa ujumla, kisiwa hicho kina hali ya hewa ya kiasi na yenye kupendeza. Idadi ya watu huko St. Helena ni karibu 4,000, na kuna Wazungu, Waasia, na Waafrika. Kiingereza kinachozungumzwa huko hutamkwa kwa njia ya pekee. Kisiwa hicho hakina uwanja wa ndege; kampuni ya meli za biashara huwawezesha wakaaji kusafiri kwenda na kutoka Afrika Kusini na Uingereza. Katikati ya miaka ya 1990 ndipo matangazo ya televisheni yalipoanzishwa kwa kutumia setilaiti.

Habari njema ya Ufalme wa Mungu ilifika St. Helena kwa mara ya kwanza mapema miaka ya 1930 wakati mapainia wawili walipotembea huko. Tom Scipio, polisi na shemasi wa kanisa la Baptisti, alipokea vichapo kadhaa kutoka kwao. Akaanza kuwaambia wengine mambo aliyokuwa akijifunza, na akiwa kanisani alifundisha waziwazi kwamba hakuna Utatu, moto wa mateso, na kutoweza kufa kwa nafsi. Yeye pamoja na wengine walioitetea kweli ya Biblia waliombwa waondoke kanisani. Punde si punde, Tom na kikundi fulani kidogo wakaanza kuhubiri wakitumia vinanda vitatu. Walihubiri kotekote kisiwani wakitembea kwa miguu na kusafiri kwa punda. Pia, Tom aliiwekea msingi mzuri wa kweli familia yake kubwa yenye watoto sita.

Mwaka wa 1951, Jacobus van Staden alitumwa kutoka Afrika Kusini kukitia moyo na kukisaidia kikundi hicho cha Mashahidi washikamanifu kisiwani. Aliwasaidia kuwa na matokeo zaidi katika huduma na akapanga mikutano ya ukawaida ya kutaniko. George Scipio,g mmoja wa wana wa Tom, anakumbuka mojawapo ya magumu waliyokabili ili kumfikisha kila mtu mikutanoni: “Kulikuwa na magari mawili tu. Njia zilikuwa mbovu na zenye milima mingi, na ni barabara chache tu zilizokuwa nzuri wakati huo. . . . Wengine walianza kutembea mapema asubuhi. Nilibeba watu watatu katika gari langu na kuwaacha mahali fulani barabarani. Waliendelea kutembea, huku nikirudi kuwachukua wengine watatu, na kuwaacha baada ya muda fulani, na kurudi. Mwishowe wote walifika mkutanoni kwa njia hiyo.” Baadaye, ingawa George alikuwa na mke na watoto wanne, alitumikia akiwa painia kwa miaka 14. Watatu kati ya wana wake ni wazee kutanikoni.

Katika miaka ya 1990, Jannie Muller akiwa na mke wake Anelise, alitembelea St. Helena mara kadhaa akiwa mwangalizi wa mzunguko. Anasema: “Unapoambatana na mhubiri shambani, atakuambia ni nani anayeishi katika nyumba inayofuata na jinsi atakavyoitikia. Tulipotembelea kisiwa hicho na kugawanya trakti Habari za Ufalme yenye kichwa “Je, Watu Wote Watapata Kupendana?” tulimaliza kisiwa chote kwa siku moja, kati ya saa 2:30 asubuhi na saa 9:00 alasiri.”

Jannie hasa anakumbuka jinsi walivyowasili na kuondoka kisiwani humo. Anasema: “Mashua ilipowasili, ndugu wengi walikusanyika bandarini kutukaribisha. Walisema kwamba siku ya kuondoka ilikuwa ya machozi, na ndivyo ilivyokuwa tulipowaona wote wakiwa bandarini kutuaga.”

Mwaka wa 2006, wahubiri 125 walishiriki kueneza kweli ya Biblia katika kisiwa hicho. Watu 239 walihudhuria Ukumbusho. Kati ya kila watu 30 kisiwani humo, mmoja ni mhubiri, na huo ndio uwiano bora zaidi ulimwenguni.

MATARAJIO YA WAKATI UJAO

Ijapokuwa tofauti za kijamii nchini Afrika Kusini, Mashahidi wa Yehova wa jamii zote wanafurahia ‘kifungo cha muungano’ kisicho na kifani. (Kol. 3:14) Watu fulani wamezungumzia jambo hilo. Mwaka wa 1993, wajumbe wengi walikuja kutoka ng’ambo kuhudhuria makusanyiko ya kimataifa. Mashahidi 2,000 hivi walienda kwenye uwanja wa ndege wa Durban kuwapokea wageni kutoka Marekani na Japani. Waliimba nyimbo za Ufalme walipowaona wageni. Ndugu walisalimiana kwa shauku na kukumbatiana. Kiongozi mashuhuri wa kisiasa alikuwa miongoni mwa watu walioshuhudia hilo. Akizungumza na baadhi ya akina ndugu, alisema: “Kama tungekuwa na roho kama yenu, tungesuluhisha matatizo yetu kitambo.”

Makusanyiko ya Kimataifa ya “Mtukuzeni Mungu” ya 2003 yaliwachochea kiroho wahudhuriaji. Afrika Kusini ilikuwa na makusanyiko ya kimataifa katika miji yake mikubwa, na pia makusanyiko mengi ya wilaya. Washiriki wawili wa Baraza Linaloongoza, Samuel Herd na David Splane, walikuwa wawakilishi katika makusanyiko hayo ya kimataifa. Wajumbe kutoka nchi 18 walihudhuria. Baadhi yao walivalia mavazi ya kwao ya kitamaduni, na kufanya makusanyiko hayo kuwa ya kimataifa kwelikweli. Hudhurio katika makusanyiko yote lilikuwa 166,873, na 2,472 wakabatizwa.

Janine, aliyehudhuria kusanyiko la kimataifa huko Cape Town, alishukuru kwa sababu ya kutolewa kwa kitabu Jifunze Kutoka kwa Mwalimu Mkuu: “Sina maneno ya kuonyesha jinsi ninavyohisi kuhusu zawadi hii. Kitabu hiki kimekusudiwa kufikia mioyo ya watoto wetu. Yehova anajua kile ambacho watu wake wanahitaji, naye Yesu, Kichwa cha kutaniko, anajua jinsi ilivyo vigumu kuwalea watoto katika ulimwengu huu usiomwogopa Mungu. Kwa moyo wote, ninamshukuru Yehova pamoja na watumishi wake walio duniani.”

Tunaposoma historia ya Mashahidi wa Yehova nchini Afrika Kusini katika karne iliyopita, tunafurahi kuona jinsi ambavyo waaminifu wamevumilia na kubaki imara. Mwaka wa 2006, kulikuwa na wahubiri 78,877 ambao waliongoza mafunzo ya Biblia 84,903. Watu 189,108 walihudhuria Ukumbusho mwaka wa 2006. Inaonekana bado maneno ya Yesu yanatimizwa leo katika eneo hili: “Tazama! Ninawaambia ninyi: Inueni macho yenu myatazame mashamba, kwamba ni meupe kwa ajili ya kuvunwa.” (Yoh. 4:35) Bado kazi nyingi inahitaji kufanywa. Kwa kuwa tunaona waziwazi mwongozo wa Yehova, tunachochewa kusema hivi pamoja na ndugu zetu katika pembe zote za dunia: “Mpigieni Yehova kelele za ushindi, enyi nyote watu wa dunia. Mtumikieni Yehova kwa kushangilia”!—Zab. 100:1, 2.

[Maelezo ya Chini]

a Masimulizi ya maisha ya Paul Smit yalikuwa katika gazeti la Kiingereza la Mnara wa Mlinzi la Novemba (Mwezi wa 11) 1, 1985, ukurasa wa 10-13.

b Masimulizi ya maisha ya George Phillips yalikuwa katika gazeti la Kiingereza la Mnara wa Mlinzi la Desemba (Mwezi wa 12) 1, 1956, ukurasa wa 712-719.

c Masimulizi ya maisha ya Piet Wentzel yalikuwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Julai 1, 1986, ukurasa wa 9-13.

d Masimulizi ya maisha ya Frans Muller yalikuwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Aprili 1, 1993, ukurasa wa 19-23.

e Masimulizi ya maisha ya Ndugu na Dada Waldron yalikuwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Desemba 1, 2002, ukurasa wa 24-28.

f Masimulizi ya maisha ya Joshua Thongoana yalikuwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Februari 1, 1993, ukurasa wa 25-29.

g Masimulizi ya maisha ya George Scipio yalikuwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi, la Februari 1, 1999, ukurasa wa 25-29.

[Blabu katika ukurasa wa 174]

Kati ya kila watu 30 nchini St. Helena, mmoja ni mhubiri, na huo ndio uwiano bora zaidi ulimwenguni

[Picha katika ukurasa wa 68, 69]

Sera ya Ubaguzi wa Rangi

Neno apartheid linalotafsiriwa ubaguzi wa rangi linamaanisha “kutenga” nalo lilitumiwa kwa mara ya kwanza na chama cha National Party wakati wa uchaguzi wa kisiasa uliofanywa mwaka wa 1948. Chama hicho kilishinda uchaguzi mwaka huo, nao ubaguzi wa kijamii ukawa sera rasmi ya serikali ya Afrika Kusini, iliyoungwa mkono kabisa na Kanisa la Dutch Reformed. Sera hiyo iliyoanzishwa ili kuimarisha mamlaka ya wazungu, ilichangia kuanzishwa kwa sheria zilizoweka mipaka kuhusu mambo ya msingi maishani, kama vile makao, kazi, elimu, rasilimali za umma, na siasa.

Watu waligawanywa katika vikundi vifuatavyo: wazungu, Wabantu (Waafrika weusi), machotara (mchanganyiko wa rangi), na Waasia (Wahindi). Watetezi wa ubaguzi wa rangi walitangaza kwamba jamii mbalimbali ziwe na maeneo yao wenyewe ambako wangeweza kuishi na kuendeleza utamaduni na mila zao. Ingawa jambo hilo lilionekana kuwa rahisi, halikufaulu. Kwa sababu ya kuogopa bunduki, gesi za kutoa machozi, na mbwa wakali, weusi wengi walifukuzwa kutoka makwao na kuhamishiwa kwingineko wakiwa na vitu vichache tu. Sehemu nyingi za umma kama vile benki na posta, zilikuwa na vitengo vya wazungu na vya jamii nyingine. Mikahawa na majumba ya sinema yalikuwa ya wazungu peke yao.

Weusi waliwafanyia wazungu kazi katika biashara zao na nyumbani, nao walilipwa mishahara midogo. Hilo lilitenganisha familia. Kwa mfano, wanaume weusi waliruhusiwa kwenda majijini kufanya kazi katika migodi au viwandani nao walikaa katika mabweni ya wanaume huku wake zao wakiwa nyumbani. Hilo lilivuruga maisha ya familia na kusababisha uasherati. Kwa kawaida watumishi weusi waliokuwa wakifanya kazi katika nyumba za wazungu waliishi katika chumba kwenye boma la mkubwa wao. Familia zao hazingeweza kuishi katika ujirani huo wa wazungu, kwa hiyo wazazi hawakuona familia zao kwa muda mrefu. Weusi walipaswa kubeba vitambulisho nyakati zote.

Kulikuwa na ubaguzi katika sehemu nyingi za maisha, kutia ndani elimu, ndoa, kazi, na kumiliki mali. Ingawa Mashahidi wa Yehova walijulikana kuwa watu wasio na ubaguzi, walitii sheria za serikali maadamu hazikuwazuia kutoa utumishi mtakatifu kwa Mungu. (Rom. 13:1, 2) Walijitahidi kushirikiana na waabudu wenzao wa jamii mbalimbali kadiri ambavyo wangeweza.

Kuanzia miaka ya katikati ya 1970, serikali ilifanya mabadiliko kadhaa, na hivyo sera zake za ubaguzi wa rangi zikalegezwa. Mnamo Februari 2, 1990, Rais F. W. de Klerk, alitangaza mikakati mbalimbali ya kukomesha ubaguzi wa rangi, kama vile kuidhinisha vyama vya kisiasa vya weusi, na kuachiliwa kutoka gerezani kwa Nelson Mandela. Kufuatia ushindi wa serikali ambayo walio wengi walikuwa weusi katika uchaguzi wa kidemokrasia uliofanywa 1994, ubaguzi wa rangi ulikoma rasmi.

[Sanduku/Ramani katika ukurasa wa 72, 73]

Maelezo Mafupi Kuhusu Afrika Kusini

Nchi

Pwani ya Afrika Kusini ni ukanda mwembamba unaozingirwa na milima iliyoinuka kando ya nyanda za ndani ambazo hufanyiza sehemu kubwa ya nchi hiyo. Nyanda hizo ndizo zilizo juu zaidi upande wa mashariki, upande wa Bahari ya Hindi, ambapo safu ya Mlima wa Drakensberg hufikia urefu wa zaidi ya mita 3,400. Eneo la nchi ya Afrika Kusini ni kubwa mara nne hivi kuliko Visiwa vya Uingereza.

Watu

Wakaaji milioni 44 wa nchi hiyo wanatoka katika jamii mbalimbali. Mwaka wa 2003, serikali ilichapisha matokeo ya hesabu ya watu iliyogawa raia wa nchi hiyo katika vikundi vinne: Waafrika weusi, asilimia 79; wazungu, asilimia 9.6; machotara, asilimia 8.9; na Wahindi au Waasia, asilimia 2.5.

Lugha

Kuna lugha rasmi 11, ingawa wengi wanazungumza Kiingereza. Lugha zinazozungumzwa, kuanzia inayozungumzwa na watu wengi zaidi, ni Kizulu, Kihosa, Kiafrikana, Kisepedi, Kiingereza, Kitswana, Kisotho, Kitsonga, Kisiswati, Kivenda, na Kindebele.

Kazi

Nchi hiyo ina mali nyingi za asili nayo ndiyo nchi yenye dhahabu na platinamu nyingi zaidi ulimwenguni. Mamilioni ya watu wa Afrika Kusini wanafanya kazi katika migodi, mashamba, au viwanda vya chakula, magari, mashini, nguo, na bidhaa nyinginezo.

Hali ya hewa

Sehemu ya kusini ya nchi hiyo, kutia ndani jiji la Cape Town, huwa na majira ya baridi kali yenye mvua nyingi hali kadhalika majira ya kiangazi. Nyanda za ndani zina hali tofauti ya hewa; mvua ya radi huandamana na baridi yenye kuburudisha wakati wa kiangazi, na wakati wa majira ya baridi kali siku haziwi na baridi sana na anga haliwi na mawingu.

[Ramani]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NAMIBIA

JANGWA LA NAMIB

Katutura

WINDHOEK

BOTSWANA

JANGWA LA KALAHARI

GABORONE

SWAZILAND

MBABANE

LESOTHO

MASERU

Teyateyaneng

AFRICA KUSINI

Mbuga ya Kitaifa ya Kruger

Nylstroom

Bushbuckridge

PRETORIA

Johannesburg

Klerksdorp

Dundee

Ndwedwe

Pietermaritzburg

Durban

MIL. YA DRAKENSBERG

Strand

Cape Town

PRETORIA

Midrand

Krugersdorp

Kagiso

Johannesburg

Elandsfontein

Soweto

Eikenhof

Heidelberg

[Picha]

Cape Town

Rasi ya Tumaini Jema

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 80]

Mara ya Kwanza Nilipojaribu Kuwa Shahidi

ABEDNEGO RADEBE

ALIZALIWA 1911

ALIBATIZWA 1939

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alitumikia kutaniko la kwanza la weusi huko Pietermaritzburg, KwaZulu-Natal, naye akafa mwaka wa 1995 akiwa mwaminifu.

NILIZALIWA na kulelewa karibu na Pietermaritzburg. Baba yangu alikuwa mhubiri Mmethodisti. Katikati ya miaka ya 1930, nilipokea vichapo vilivyochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Ingawa nilikubali mambo niliyosoma, sikuwa na nafasi ya kushirikiana na Mashahidi.

Mtu fulani katika jengo nililokuwa nikiishi alinipa kijitabu Heaven and Purgatory. Sikuwa nimewahi kukisoma. Kilinisaidia kuelewa yale ambayo Biblia inasema kuhusu ufufuo na tumaini la kuishi duniani. Niliandikia ofisi ya tawi huko Cape Town na kuagiza vitabu kadhaa.

Niliogopa kuzungumza na Mashahidi niliokutana nao mjini. Desturi ya Wazulu ilikuwa “Usimwendee mzungu kwanza. Subiri aje ulipo.”

Jioni moja nilipokuwa nikirudi nyumbani kutoka kazini, niliona gari la Mashahidi lililokuwa na kipaza-sauti likiwa limeegeshwa nje ya jengo nilimokuwa nikiishi. Nilipokaribia lango, mzee mmoja mnene aliyevalia suti alinikaribia. Akajitambulisha kwa jina Daniel Jansen. Basi nikaamua kutumia nafasi hiyo kuwajua Mashahidi. Nikamwomba nisikilize mojawapo ya hotuba za Ndugu Rutherford. Watu wengi walikusanyika. Hotuba hiyo ilipokwisha, Jansen aliweka maikrofoni mkononi mwangu na kusema, “Waambie watu hawa katika Kizulu yale ambayo umesikia katika hotuba hii ili nao pia wafaidike.”

Nikamjibu, “Siwezi kukumbuka kila jambo ambalo msemaji alisema.”

Jansen akasema, “Sema tu yale unayokumbuka.”

Huku mkono wangu ukitetemeka, nilisema maneno machache. Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kujaribu kuwa Shahidi wa Yehova. Kisha, Jansen akanialika niambatane naye katika kazi ya kuhubiri. Kwanza, alichunguza ikiwa ninaelewa mambo ya msingi ili aone kama ninakubali kabisa mafundisho ya Biblia. Aliridhika. Nilishirikiana na kampuni, au kutaniko, la wazungu kwa miaka minne, ambamo mimi tu ndiye niliyekuwa mtu mweusi. Tulikuwa kikundi kidogo na tulifanya mikutano katika nyumba ya ndugu.

Siku hizo, kila mhubiri alipewa kadi ya kutoa ushahidi ili aitumie kumtolea mwenye nyumba utangulizi wa ujumbe wa Biblia. Pia, tulibeba kinanda cha kucheza sahani za santuri, hotuba zilizorekodiwa za dakika nne, na mkoba wenye vichapo.

Ili kuokoa wakati, mhubiri alihakikisha kwamba sahani ya santuri imerudishwa hadi mwanzo na sindano mpya ya kinanda iko tayari. Mwenye nyumba alipofungua mlango, mhubiri alimsalimu na kumpa kadi ambayo ilikuwa na utangulizi wa hotuba iliyorekodiwa. Hotuba ilipofika nusu, mhubiri alifungua mkoba wake ili hotuba hiyo inapokwisha, amtolee mwenye nyumba kitabu kilichozungumziwa katika hotuba hiyo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 88, 89]

Kielelezo cha Uaminifu

GEORGE PHILLIPS

ALIZALIWA 1898

ALIBATIZWA 1912

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alianza upainia wa kawaida mwaka wa 1914. Alitumikia akiwa msimamizi wa tawi ya Afrika Kusini kwa karibu miaka 40. Alikufa mwaka wa 1982.

GEORGE PHILLIPS alizaliwa na kulelewa huko Glasgow, Scotland. Alianza upainia mwaka wa 1914, akiwa na umri wa miaka 16. Katika mwaka wa 1917, alikamatwa kwa sababu ya kudumisha msimamo wa Kikristo wa kutokuwamo. Mnamo 1924, Ndugu Rutherford alimwomba atumikie Afrika Kusini. Alisema, “George, huenda ikawa kwa mwaka mmoja, au labda kwa muda mrefu zaidi.”

Haya ndiyo maoni ya George baada ya kufika Afrika Kusini: “Ikilinganishwa na Uingereza, hali zilikuwa tofauti kabisa na bado kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya. Wakati huo, kulikuwa na watumishi 6 tu wa wakati wote na watu wasiozidi 40 hivi walishiriki kazi ya kuhubiri kwa kadiri ndogo. Eneo letu lilianzia Cape hadi Kenya. Watu katika maeneo hayo wangehubiriwaje na kutolewa ushahidi kamili kwa mwaka mmoja tu? Hakukuwa na haja ya kuwa na wasiwasi. Tulihitaji tu kuanza kuhubiri kwa kadiri ambayo tungeweza, tutumie njia tulizo nazo, kisha tumwachie Yehova matokeo.

“Afrika Kusini ni nchi kubwa iliyo na jamii na lugha mbalimbali. Ilikuwa shangwe kupata kuwajua watu hao tofauti. Haikuwa rahisi kupanga na kuweka msingi kwa ajili ya kazi katika eneo hilo kubwa.

“Kwa muda wote huo, Yehova ametosheleza mahitaji yangu yote, amenilinda, ameniongoza, na amenibariki sana. Nimejifunza kwamba ‘utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa’ na kwamba ili mtu abaki katika ‘mahali pa siri pa Aliye Juu Zaidi,’ ni lazima awe karibu sana na tengenezo lake na ajitahidi sana kufanya kazi yake kulingana na mapenzi yake.”—1 Tim. 6:6, Union Version; Zab. 91:1.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 92-94]

Kusaidia Familia Yangu Kiroho

JOSEPHAT BUSANE

ALIZALIWA 1908

ALIBATIZWA 1942

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Mtu mwenye familia aliyejifunza kweli akiwa kazini jijini Johannesburg, mbali na nyumbani kwake huko Zululand, KwaZulu-Natal.

NILIZALIWA huko Zululand, Afrika Kusini, mwaka wa 1908. Ingawa familia yetu iliridhika na maisha rahisi ya ukulima, nikiwa na umri wa miaka 19, nilianza kufanya kazi ya kuuza dukani katika mji wa Dundee. Baada ya muda, nilisikia kwamba vijana wengi walikuwa wakichuma pesa nyingi huko Johannesburg, kwenye migodi mingi ya dhahabu ya Afrika Kusini. Basi, nilihamia huko na kwa miaka mingi nikafanya kazi ya kubandika matangazo katika sehemu za umma. Kulikuwa na sehemu nyingi za anasa na nafasi nyingi za kujiendeleza kimaisha, lakini nilitambua kwamba maadili ya watu wetu yalikuwa yakizorota kwa sababu ya maisha jijini humo. Ingawa vijana wengi walisahau familia zao huko mashambani, sikuisahau familia yetu kamwe nami nilikuwa nikiwatumia pesa kwa ukawaida. Mwaka wa 1939, nilimwoa Claudina, msichana kutoka Zululand. Hata baada ya kuoa, niliendelea kufanya kazi huko Johannesburg, umbali wa kilomita 400 kutoka nyumbani. Wengi wa rafiki zangu walifanya hivyo pia. Ijapokuwa sikufurahia kutengana na familia yangu kwa muda mrefu, nilihisi nina jukumu la kuwasaidia waishi maisha bora.

Nikiwa Johannesburg, mimi na rafiki yangu Elias tuliamua kutafuta dini ya kweli. Tulitembelea makanisa mbalimbali katika ujirani wetu lakini hayakuturidhisha. Kisha, Elias akakutana na Mashahidi wa Yehova. Nilijiunga na Elias kushirikiana kwa ukawaida na kutaniko la kwanza la Mashahidi wa Yehova la watu weusi huko Johannesburg. Mwaka wa 1942, baada ya kujiweka wakfu kwa Yehova, nilibatizwa huko Soweto. Kila wakati niliporudi nyumbani huko Zululand, nilijaribu kumweleza Claudina imani yangu lakini alikuwa amejiingiza sana katika mambo ya kanisa.

Hata hivyo, alianza kulinganisha vichapo vyetu na Biblia yake, na hatua kwa hatua kweli ya Neno la Mungu ikafikia moyo wake. Alibatizwa mwaka wa 1945. Akawa mhudumu Mkristo mwenye bidii, akiwahubiria majirani kweli ya Biblia na kuikazia katika mioyo ya watoto wetu. Wakati huohuo, nilikuwa na pendeleo la kuwasaidia watu fulani kupata ujuzi wa kweli ya Biblia jijini Johannesburg. Kufikia mwaka wa 1945, kulikuwa na makutaniko manne ya watu weusi katika maeneo ya Johannesburg, nami nilitumikia nikiwa mtumishi wa kampuni (mwangalizi-msimamizi) katika Kutaniko la Small Market. Baada ya muda, mwelekezo wa Kimaandiko ulitolewa kwa wanaume waliokuwa wameoa na ambao walifanya kazi mbali na nyumbani warudi kwa familia zao ili watimize majukumu yao wakiwa vichwa vya familia.—Efe. 5:28-31; 6:4.

Basi, mwaka wa 1949, niliacha kazi huko Johannesburg ili kutunza familia yangu kulingana na njia ya Yehova. Huko nyumbani, mkaguzi wa mifugo aliniandika kazi ya kuwa msaidizi katika kidimbwi cha kuoshea mifugo kwa dawa. Ilikuwa vigumu kutegemeza familia yenye watoto sita kwa mshahara mdogo niliopata. Kwa hiyo, ili kugharimia matumizi, niliuza mboga na mahindi tuliyokuza nyumbani. Ingawa familia yetu haikuwa tajiri kimwili, tulikuwa na hazina za kiroho kwa sababu tulitii mwongozo wa Yesu kwenye Mathayo 6:19, 20.

Bidii inahitajiwa kupata hazina hizo za kiroho sawa na inavyohitajiwa wakati wa kuchimba dhahabu katika migodi huko Johannesburg. Kila jioni nilisoma Biblia pamoja na watoto wangu na kumwomba kila mmoja wao anieleze alichojifunza. Mwishoni mwa juma, nilihubiri pamoja nao kwa zamu. Tulipotembea kutoka nyumba moja ya mkulima hadi nyingine, nilizungumza nao mambo ya Kimaandiko na kujaribu kukazia mioyoni mwao viwango vya juu vya Biblia.—Kum. 6:6, 7.

Kwa miaka mingi, familia yetu tu ndiyo iliyoweza kuwaalika waangalizi wanaosafiri. Ndugu hao pamoja na wake zao waliwawekea watoto wetu kielelezo kizuri na kuwasaidia kutamani kuwa wahubiri wa wakati wote. Tulikuwa na wavulana watano na msichana mmoja. Wote sita sasa ni watu wazima na wenye nguvu kiroho. Ninamshukuru Yehova kama nini kwa mwongozo kutoka kwa tengenezo lake uliotia moyo akina ndugu kama mimi kukazia uangalifu zaidi mahitaji ya kiroho ya familia zetu! Baraka ambazo nimepata ni nyingi sana kuliko kitu chochote kinachoweza kununuliwa.—Met. 10:22.

Ndugu Josephat Busane aliendelea kumtumikia Yehova kwa uaminifu hadi alipokufa mwaka wa 1998. Watoto wake ambao sasa ni watu wazima wanaendelea kufurahia urithi wao wa kiroho. Theophilus, mmoja wa wana wake, ni mwangalizi anayesafiri. Habari zaidi kuhusu Ndugu Busane zinaweza kupatikana katika gazeti la “Amkeni!” la Oktoba 8, 1993, ukurasa wa 19 mpaka 22.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 96, 97]

“Utumishi wa Ufalme Umenisaidia Kumkaribia Yehova”

THOMAS SKOSANA

ALIZALIWA 1894

ALIBATIZWA 1941

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alijifunza lugha tano ili awasaidie watu kiroho katika migawo yake akiwa painia.

KATIKA mwaka wa 1938 mwalimu fulani alinipa vijitabu kadhaa vilivyochapishwa na Mashahidi wa Yehova. Wakati huo, nilikuwa mhubiri katika kanisa la Wesleyan huko Delmas, karibu kilomita 60 mashariki mwa Johannesburg. Kwa muda mrefu nilikuwa nimependezwa na Biblia. Kanisa hilo lilifundisha kwamba nafsi haiwezi kufa na eti waovu wanateswa katika moto. Lakini, vijitabu hivyo vilionyesha kupitia Biblia kwamba hilo si kweli. (Zab. 37:38; Eze. 18:4) Pia, nilijifunza kwamba badala ya kwenda mbinguni, watu wengi wa Mungu watapata uzima wa milele duniani.—Zab. 37:29; Mt. 6:9, 10.

Nilifurahi sana kujifunza kweli hizo na nilitaka kuwahubiria watu katika kanisa letu, lakini wahubiri wenzangu walikataa na wakapanga nifukuzwe. Hivyo, niliacha kanisa hilo nikaanza kushirikiana na kikundi kidogo cha Mashahidi wa Yehova huko Delmas. Nilibatizwa mwaka wa 1941 na kuanza upainia mwaka wa 1943.

Nilihamia Rustenburg, ambapo kulikuwa na uhitaji wa wahubiri wa Ufalme. Kwa kuwa nilikuwa mgeni, nilihitaji kumwandikia chifu wa eneo hilo ili kumwomba makao na kibali cha kukaa huko. Aliniambia nilipe pauni 12 ili kupata kibali cha kukaa huko. Nilishindwa kulipa pesa hizo, lakini ndugu mzungu wa huko mwenye fadhili alinilipia na akanisaidia niendelee na utumishi wa upainia. Mmoja wa wanaume niliojifunza nao alifanya maendeleo, na baada ya kutoka katika mgawo huo, aliwekwa rasmi kuwa mtumishi wa kutaniko.

Kisha, nikahamia upande wa magharibi huko Lichtenburg. Wakati huo nilipaswa kuomba kibali kutoka kwa ofisa fulani mzungu, ili nikae katika eneo la mji lililokaliwa na weusi. Alikataa kunipa kibali. Nilimsihi ndugu mzungu painia aliyeishi Mafikeng, mji uliokuwa karibu, anisaidie. Tulimtembelea ofisa huyo pamoja, lakini akasema: “Siwataki hapa. Ninyi watu mnafundisha kwamba hakuna moto wa mateso. Watu wanaweza kufanyaje mema ikiwa hawaogopi moto wa mateso?”

Kwa sababu msimamizi huyo alikataa kunipa kibali, nilihamia Mafikeng, ambapo bado ninatumika nikiwa painia wa kawaida. Lugha yangu ni Kizulu, lakini muda mfupi baada ya kujifunza kweli, niliamua kwamba ni lazima nijifunze Kiingereza ili niweze kusoma vichapo vyote vya Mashahidi wa Yehova. Kufanya hivyo kulinisaidia kukua kiroho.

Ili nifanikiwe katika utumishi, nimejifunza Kisesotho, Kihosa, Kitswana, na Kiafrikana kidogo. Kwa miaka fulani sasa, nimekuwa na pendeleo la kuwasaidia wengi kujiweka wakfu kwa Yehova, kutia ndani wanne ambao sasa ni wazee wa kutaniko. Utumishi wa wakati wote umenisaidia sana kuwa na afya nzuri.

Namshukuru Yehova kwa kuniruhusu nifikie umri mwema wa uzee katika utumishi wake. Si kwa nguvu zangu kwamba nimeweza kupata ujuzi na mafanikio katika huduma. Yehova amenisaidia kupitia roho yake takatifu. Zaidi ya yote, kufanya utumishi wa Ufalme wa wakati wote kwa ukawaida kumenisaidia kumkaribia Yehova nami nimejifunza kumtegemea.

Mahojiano hayo yalifanywa mwaka wa 1982. Akiwa mmoja wa watiwa-mafuta wa Mungu, Ndugu Skosana aliendelea kutumikia kwa uaminifu mpaka alipokufa mwaka wa 1992.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 100]

Mwangalizi wa Wilaya wa Kwanza wa Afrika Kusini

MILTON BARTLETT

ALIZALIWA 1923

ALIBATIZWA 1939

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alikuwa mmishonari wa kwanza kutumwa Afrika Kusini kutoka shule ya Gileadi. Alijitahidi sana kuendeleza mambo ya Ufalme, hasa katika maeneo hayo ya weusi.

MNAMO Desemba 1946, Milton Bartlett aliwasili Cape Town akiwa mmishonari wa kwanza wa Shule ya Gileadi kutumwa Afrika Kusini. Mgawo wake ulikuwa kuanzisha kazi ya mzunguko na ya wilaya, naye alifanya hivyo. Wakati huo, Ndugu Bartlett tu ndiye aliyekuwa mwangalizi wa wilaya. Miaka iliyofuata, waangalizi wanaosafiri walijitahidi sana kuendeleza kazi ya Ufalme nchini Afrika Kusini, hasa miongoni mwa watu weusi.

Milton alipendwa sana na ndugu wa Afrika Kusini. Alikuwa mtu mwenye subira aliyesikiliza kwa makini akina ndugu walipomweleza matatizo yao. Hivyo, aliweza kutuma ripoti kamili na sahihi kwenye ofisi ya tawi ya Afrika Kusini kuhusu matatizo ambayo huenda yangewakumba akina ndugu katika maeneo mengine pia. Kufanya hivyo kulisaidia kufanya mwenendo na njia ya ibada ya akina ndugu ipatane zaidi na kanuni za Biblia.

Milton aliweza kuwasaidia ndugu zake kwa sababu aliyajua Maandiko vizuri na alikuwa mwalimu mwenye ustadi. Pia, alikuwa mwenye bidii na mvumilivu, sifa zilizomwezesha kupata vibali kutoka kwa maofisa wa serikali ili aingie maeneo ya watu weusi, ingawa alikuwa mzungu. Mara nyingi maofisa wenye upendeleo wangekataa kumpa kibali. Ilipokuwa hivyo, Milton alitafuta msaada kutoka kwa mamlaka za juu, kama vile mabaraza ya miji. Kisha, angesubiri mpaka wakati baraza lingefanya mkutano wao uliofuata ambapo maamuzi mazuri yalifikiwa. Kwa njia moja au nyingine, aliingia katika maeneo mengi ya watu weusi.

Nyakati nyingine, polisi wa siri walitumwa kuchunguza hotuba za Milton. Sababu moja ya kufanya hivyo ni kwamba wahudumu wa dini zinazodai kuwa za Kikristo walisema kwa uwongo kuwa Mashahidi wa Yehova walichochea Ukomunisti. Wakati fulani polisi mweusi alitumwa anukuu habari kusanyikoni. Milton aliandika hivi miaka 20 baadaye: “Hilo lilikuwa na matokeo mazuri, kwa kuwa polisi huyo alikubali ibada ya kweli kwa msingi wa yale aliyosikia mwishoni mwa juma hilo, na bado ana bidii katika imani.”

Milton alipofika Afrika Kusini akiwa mseja mwenye umri wa miaka 23, kulikuwa na wahubiri 3,867. Baada ya Milton kutumika nchini Afrika Kusini kwa miaka 26, idadi ya wahubiri ilikuwa imefika 24,005. Mwaka wa 1973, Milton, mke wake, Sheila, pamoja na Jason, mwana wao mwenye umri wa mwaka mmoja, walirudi Marekani kuwatunza wazazi wa Milton waliokuwa wazee. Picha katika ukurasa huu ni ya Milton na Sheila wakiwa Afrika Kusini mwaka wa 1999, walipohudhuria kuwekwa wakfu kwa ofisi ya tawi ya Afrika Kusini baada ya kufanyiwa upanuzi. Walifurahi kama nini kurudi baada ya miaka 26 na kukutana tena na wahudumu wa muda mrefu ambao wanakumbuka kazi yao ya upendo!

[Picha]

Milton na Sheila Bartlett, 1999

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 107]

Mandhari ya Pekee

Jiji la Cape Town linatambuliwa kwa Mlima Table wenye kuvutia. Watu fulani husema kwamba Cape Town ndilo jiji maridadi zaidi Afrika.

Nyakati nyingine katika majira ya kiangazi sehemu ya juu ya mlima hufunikwa na wingu zito linaloonekana kama “kitambaa cha meza.” Wingu hilo hufanyizwa kutokana na unyevu unaoletwa na pepo zenye nguvu zinazovuma na kuinuka juu ya Mlima Table.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 114-117]

Kudumisha Utimilifu Gerezani

MAHOJIANO NA ROWEN BROOKES

ALIZALIWA 1952

ALIBATIZWA 1969

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alikuwa gerezani kuanzia Desemba 1970 hadi Machi 1973 kwa sababu ya kutokuwamo kwa Kikristo. Alianza upainia wa kawaida mwaka wa 1973 na kwenda Betheli mwaka wa 1974. Sasa ni mshiriki wa Halmashauri ya Tawi.

Hali zilikuwaje gerezani?

Kambini kulikuwa na majengo makubwa, kila moja likiwa na safu mbili za vyumba 34, na mtaro wa maji katikati ya majengo. Katika vifungo vya upweke, kila mmoja wetu alikuwa na chumba chenye urefu wa mita 2 na upana wa mita 1.8. Tuliruhusiwa kutoka katika vyumba vyetu mara mbili tu kwa siku: asubuhi ili kunawa, kunyoa ndevu, na kuosha ndoo zetu tulizotumia kama vyoo na wakati wa alasiri ili kuoga. Hatukuruhusiwa kuandika wala kupokea barua. Hatukuruhusiwa kuwa na vitabu vyovyote ila Biblia na hatukuruhusiwa kuwa na kalamu wala penseli zozote. Hatukuruhusiwa kuwa na wageni wowote.

Kabla ya kufungwa, ndugu wengi walikuwa na Biblia zilizounganishwa na vitabu vingine, kama vile Aid to Bible Understanding. Walinzi hawakutambua kwa kuwa zilifanana na Biblia zao za zamani za Kiafrikana au Kidachi.

Je, mlikuwa mkipata vichapo vya Biblia?

Ndiyo, wakati wowote ambapo ingewezekana, tuliviingiza kisiri. Vitu vyote tulivyokuwa navyo, kutia ndani sabuni, mafuta, dawa ya meno, na kadhalika, vilikuwa ndani ya mifuko katika mojawapo ya vyumba ambavyo havikuwa na mtu. Mara moja kwa mwezi, mlinzi alituruhusu kwenda katika jela hilo kuchukua vitu tulivyohitaji. Pia, tuliweka vichapo katika mifuko hiyo.

Mmoja wetu alimkengeusha mlinzi kwa kuzungumza naye, huku ndugu mwingine akificha kitabu ndani ya suruali au fulana. Tuliporudi katika vyumba vyetu tulitenganisha visehemu vidogo-vidogo vya vitabu hivyo, ili iwe rahisi kuvificha. Tulipokezana visehemu hivyo ili wote wavisome. Tulipata sehemu nyingi za kuvificha. Vyumba kadhaa vilikuwa vimeharibika sana, navyo vilikuwa na mianya kila mahali.

Vyumba vyetu vilipekuliwa kila wakati, nyakati nyingine hata usiku wa manane. Sikuzote walinzi walipata baadhi ya vichapo lakini kamwe hawakupata kila kitu. Mara nyingi askari mmoja aliyetujali alitutahadharisha wakati ambapo upekuzi ungefanywa. Kisha, tungefunga vichapo hivyo katika plastiki na kuvishindilia katika mabomba ya kuondoa maji machafu. Siku moja kulikuwa na mvua kubwa, na ajabu ni kwamba kifurushi kimoja kilikuja kikielea katika mtaro uliokuwa katikati ya majengo. Baadhi ya wafungwa waliokuwa wanajeshi walianza kukichezea kama mpira. Ghafula mlinzi alikuja na kuwaambia warudi katika vyumba vyao. Tulifurahi kwamba hakuna mtu aliyejishughulisha na kifurushi hicho, na hivyo tuliweza kukichukua tuliporuhusiwa kutoka nje ya majela yetu muda mfupi baadaye.

Je, utimilifu wenu ulijaribiwa mlipokuwa gerezani?

Wakati wote. Kila wakati maofisa wa gereza walijaribu njama fulani. Kwa mfano, wangejifanya wazuri kwetu, yaani, wangetupatia chakula cha ziada, wangetupeleka kufanya mazoezi, na hata kuturuhusu tuote jua. Kisha, baada ya siku chache wangetuamuru tuvae nguo za kijeshi. Tulipokataa, walitutendea kikatili kama mwanzoni.

Baada ya hayo, tuliambiwa tuvae kofia za plastiki za kijeshi, nasi tukakataa. Msimamizi alikasirika sana hivi kwamba kuanzia wakati huo hata hakuturuhusu tuoge kwa maji yanayotiririka. Kila mmoja wetu alipewa ndoo ambayo angetumia kuoga ndani ya chumba chake.

Kwa sababu hatukuwa na viatu, miguu ya akina ndugu fulani ilikuwa na vidonda. Ilitubidi tujitengenezee viatu. Tuliokota vipande vya mablanketi makuukuu yaliyotumiwa kung’arisha sakafu. Halafu tukapata waya wa shaba, tukatandaza mwisho mmoja, na kunoa ule mwingine. Tulitumia pini kutoboa shimo katika sehemu iliyotandazwa ya waya na kuitumia waya hiyo kama sindano ya kushonea. Tulitoa nyuzi kwenye mablanketi yetu na kuzitumia kushona viatu tukitumia vipande vya blanketi.

Bila kujua sababu, tuliamuriwa tukae watatu-watatu katika chumba kimoja. Ingawa tulisongamana, tulifaidika. Tulipanga kwamba ndugu walio dhaifu kiroho wakae na wenye uzoefu. Tuliongoza mafunzo ya Biblia na kufanya mazoezi ya kuhubiri. Msimamizi alishangaa kuona kwamba tulikuwa na uhakika zaidi.

Alipotambua kwamba mbinu hiyo iliambulia patupu, msimamizi huyo aliamuru kwamba kila Shahidi akae na watu wawili wasio Mashahidi. Ingawa walikuwa wameonywa vikali wasizungumze nasi, walianza kuuliza maswali na tulikuwa na wakati wa kutosha kutoa ushahidi. Matokeo yakawa kwamba mmoja au wawili kati ya wafungwa wenzetu walikataa kujihusisha katika utendaji fulani wa kijeshi. Punde si punde, tulianza tena kuishi kila mtu katika chumba chake.

Je, mliweza kufanya mikutano?

Tulifanya mikutano yetu kwa ukawaida. Juu ya mlango wa kila chumba kulikuwa na dirisha lenye wavu wa waya na fito saba zilizo wima. Tulikalia kiti cha kuning’inia tulichotengeneza kwa kufunga miisho miwili ya blanketi kwenye fito mbili. Tukiwa huko juu tungeweza kumwona ndugu katika chumba kilichokuwa upande ule mwingine, nasi tungeweza kupaaza sauti na kusikiwa na wengine katika jengo hilo. Tulichunguza andiko la kila siku, na pia tulijifunza Mnara wa Mlinzi iwapo tungekuwa na gazeti hilo. Kila siku tulimalizia kwa sala ya hadharani tuliyotoa kwa zamu. Hata tulijitayarishia programu ya kusanyiko la mzunguko.

Hatukuwa na uhakika iwapo mzee angeruhusiwa kuja kuhudhuria Ukumbusho pamoja nasi. Hivyo, tulifanya matayarisho yetu wenyewe. Tulitengeneza divai kwa kulowesha zabibu kadhaa ndani ya maji, na kutandaza na kuukausha mkate tuliopokea. Wakati mmoja tuliruhusiwa kupokea chupa ndogo ya divai na mikate kadhaa isiyotiwa chachu kutoka kwa akina ndugu huko nje.

Je, mambo yalibadilika?

Ndiyo, baada ya muda mambo yalikuwa afadhali. Sheria ilibadilishwa na kikundi chetu kikaachiliwa. Kuanzia wakati huo na kuendelea, watu waliokataa kutumikia jeshini kwa sababu ya dini walihukumiwa kifungo kimoja kwa kipindi hususa bila kuhukumiwa tena. Baadaye, baada ya kikundi chetu cha ndugu 22 kuachiliwa, ndugu 88 waliobaki gerezani walitendewa kama wafungwa wengine. Wangeweza kutembelewa mara moja kwa mwezi na hata kuandika na kupokea barua.

Je, baada ya kuachiliwa, ilikuwa rahisi kurudia maisha ya kawaida?

Hapana, ilichukua muda kuzoea maisha tukiwa huru. Kwa mfano, hatukuhisi huru tulipokuwa mahali penye watu wengi. Hatua kwa hatua wazazi na ndugu zetu walitusaidia kwa fadhili kukubali mapendeleo zaidi kutanikoni.

Ingawa huo ulikuwa wakati mgumu, tulifaidika kutokana na mambo tuliyokabili. Majaribu ya imani tuliyokabili yalituimarisha kiroho na kutufunza uvumilivu. Kwa kweli, tulijifunza kuithamini Biblia na kuona faida ya kuisoma na kuitafakari kila siku. Na bila shaka tulijifunza kumtegemea Yehova. Baada ya kujidhabihu hivyo ili kubaki waaminifu kwa Yehova, tuliazimia kuendelea kuvumilia, tukijitoa kabisa kwake kwa kutumikia katika utumishi wa wakati wote ilipowezekana.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 126-128]

Tulimtumaini Yehova Wakati wa Taabu

ZEBLON NXUMALO

ALIZALIWA 1960

ALIBATIZWA 1985

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Alikuwa mfuasi wa dini ya rasta kabla ya kujifunza kweli. Muda mfupi baada ya kubatizwa, alianza utumishi wa wakati wote. Sasa ni mwangalizi wa mzunguko, naye anatumikia pamoja na mke wake, Nomusa.

BAADA ya kusaidia katika ujenzi wa Betheli ya Krugersdorp, mimi pamoja na painia mwenzangu tulipewa mgawo wa kutumikia mahali penye uhitaji katika eneo la KwaNdengezi karibu na jiji la bandarini la Durban. Siku chache baada ya kuwasili, kikundi fulani cha kisiasa kilituma vijana watano wa kikundi chao nyumbani kwetu ili kupeleleza. Walituomba tuwasaidie kulinda eneo hilo lisishambuliwe na kikundi fulani cha upinzani. Uadui kati ya vikundi hivyo viwili vya Kizulu ulikuwa umesababisha umwagikaji mwingi wa damu nchini Afrika Kusini. Tuliwauliza maoni yao kuhusu suluhisho la jeuri hiyo. Walisema kwamba utawala wa wazungu ndio uliosababisha hali hiyo. Tulitaja nchi nyingine za Afrika zilizokumbwa na vita na ambazo raia zake walikuwa maskini. Kisha, tukawakumbusha msemo huu, Historia hujirudia. Wakakubali kwamba uhalifu, jeuri, na magonjwa yataendelea kuwapo hata watu weusi wakitawala. Halafu, tukafungua Biblia na kuwaonyesha kwamba Ufalme wa Mungu ndio serikali pekee inayoweza kusuluhisha matatizo ya wanadamu.

Siku chache baadaye, tulisikia umati wa vijana wakiimba nyimbo za ukombozi na tukaona wanaume wakiwa wamebeba silaha. Nyumba ziliteketezwa na watu wakauawa. Tuliogopa sana, tukamwomba Yehova atupe nguvu ili tusiruhusu vitisho au ukatili utuvunje moyo au kuvunja utimilifu wetu. Pia, tuliwakumbuka wale waliofia imani bila kumkana Yesu walipokuwa chini ya hali kama hizo. (Mt. 10:32, 33) Ghafula, kikundi cha vijana na watu wazima wakabisha mlango wetu. Hata bila salamu, walidai tuwape pesa za kununua intelezi, ambayo kulingana na Wazulu ni dawa inayopatikana kwa mchawi ambayo inaaminiwa kuandaa ulinzi. Tuliwasihi wawe na subira kisha tukawauliza, “Je, mnafikiri kwamba wachawi wanafanya vizuri kwa kuunga mkono mauaji wakitumia uchawi?” Pia tukawauliza: “Namna gani ikiwa mtu wa ukoo mnayempenda sana angeuawa kwa sababu ya uchawi. Mngehisije?” Wote wakakubali kwamba hawangefurahi. Kisha, tukafungua Biblia na kumwomba kiongozi wao asome maoni ya Mungu kuhusu uchawi kwenye Kumbukumbu la Torati 18:10-12. Alipomaliza kuisoma, tukawauliza maoni yao kuhusu habari hiyo. Walinyamaza kimya. Tukatumia pindi hiyo kuwauliza iwapo ni jambo la hekima sisi kumtii Yehova au kuwatii wao. Wote wakaondoka bila kusema lolote.

Tuliponea hali nyingi kama hizo nasi tukatambua kwamba Yehova alikuwa pamoja nasi. Kwa mfano, jioni moja kikundi kingine kilikuja nyumbani kwetu wakitaka pesa za kununua silaha za “kuwalinda” wakaaji. Walidai kwamba hakukuwa na usalama kwa sababu ya kikundi cha kisiasa cha upinzani na kwamba suluhisho ni kufanya mashambulizi kwa silaha kali zaidi. Walidai tuwape pesa, la sivyo tuone cha mtema kuni. Kisha tukawakumbusha kwamba shirika lao lilikuwa limetia sahihi mkataba wa haki za kibinadamu na kuheshimu dhamiri za wengine. Tuliwauliza ikiwa mtu anapaswa kuwa hata tayari kufa badala ya kutenda kinyume na katiba yao. Wakasema ndiyo. Kisha tukawaeleza kwamba sisi ni wa tengenezo la Yehova, “katiba” yetu ni Biblia, nayo inashutumu kuua. Mwishowe, kiongozi wa kikundi hicho aliwaambia hivi wenzake: “Ninaelewa msimamo wa watu hawa. Wamesema waziwazi kwamba ikiwa pesa hizo ni za kuboresha eneo letu, kama vile kujenga makao ya wazee, au ikiwa jirani anahitaji pesa za kwenda hospitali, wako tayari kuzitoa. Lakini hawako tayari kutupa pesa za kuua.” Waliposikia hivyo, walisimama, tukawaaga na kuwashukuru kwa kutusikiliza.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 131-134]

Dada Waseja Ambao kwa Pamoja Wametumikia Wakiwa Watafsiri kwa Miaka 100

Ndugu na dada kadhaa katika familia ya Betheli ya Afrika Kusini wametumia vipawa vyao vya useja kwa faida za utumishi wa Ufalme. (Mt. 19:11, 12) Dada watatu wafuatao wametumia jumla ya miaka 100 wakitafsiri chakula cha kiroho kutoka kwa “mtumwa mwaminifu na mwenye busara.”—Mt. 24:45.

Maria Molepo

Nilizaliwa katika eneo la Molepo katika Mkoa wa Limpopo nchini Afrika Kusini. Dada yangu mkubwa Aletta alinifundisha kweli nilipokuwa ningali shuleni. Nilipomaliza shule, dada yangu mwingine, ambaye si mmoja wa Mashahidi wa Yehova, alijitolea kunilipia karo kwa miaka mitatu katika chuo ili niwe mwalimu aliyehitimu. Nilikataa fadhili zake kwa sababu nilitaka kumtumikia Yehova pamoja na dada zangu wawili wakubwa, Aletta na Elizabeth, waliokuwa mapainia. Nilibatizwa mwaka wa 1953, nami nikawa natimiza takwa la saa la painia mara kwa mara kwa miaka sita kabla ya kujaza ombi na kuwekwa rasmi kuwa painia wa kawaida mwaka wa 1959.

Mwaka wa 1964, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini ili- nialika nifanye kazi ya kutafsiri kwa muda chakula cha kiroho katika Kisepedi. Nilifanya hivyo huku nikiendelea katika utumishi wangu wa upainia. Kisha, mwaka wa 1966, nikaalikwa niwe mshiriki wa familia ya Betheli ya Afrika Kusini. Utumishi wa Betheli haukuwa nilivyofikiri. Nilitamani kwenda katika utumishi wa shambani kila siku. Hata hivyo, muda si muda nilibadili maoni yangu na kuiona miisho ya juma, kuanzia Jumamosi alasiri hadi Jumapili jioni, kuwa wakati wa upainia, ingawa singeweza kutimiza takwa la saa la painia. Nilifurahia sana utumishi wangu wa shambani mwishoni mwa juma hivi kwamba mara nyingi nilichelewa kurudi kwa wakati kwa ajili ya chakula cha jioni Jumamosi au Jumapili. Mabadiliko yalipofanywa ili dada wenye umri mkubwa wawe wakipumzika Jumamosi asubuhi, nilifurahi sana kwamba ningeweza kuutumia muda huo wa ziada katika utumishi wa shambani.

Miaka ya kwanza minane nikiwa Betheli, mimi na mtafsiri mwingine tulikaa katika chumba kimoja katika jengo lingine mbali na makao ya Betheli. Mwanzoni, wenye mamlaka walituruhusu tuishi karibu na ndugu zetu wazungu, lakini kuanzia mwaka wa 1974 hatukuruhusiwa tena kamwe. Watafsiri weusi kama mimi walilazimika kuishi katika maeneo yaliyotengewa watu weusi. Nilikaa pamoja na familia ya Mashahidi huko Tembisa na kulazimika kusafiri mwendo mrefu kwenda na kurudi kutoka Betheli kila siku. Betheli mpya ilipojengwa Krugersdorp, serikali ilikuwa imeanza kulegeza sera zake, nami ningeweza tena kuishi na Wanabetheli wengine.

Namshukuru sana Yehova kwa kuniwezesha niendelee na kazi yangu nikiwa mtafsiri Betheli hadi leo hii. Kwa kweli, amenibariki sana kwa kutumia zawadi yangu ya useja katika utumishi wake hivi kwamba hata dada yangu mdogo, Annah, aliamua kubaki mseja naye amekuwa akifurahia kazi ya kuhubiri wakati wote kwa miaka 35 ambayo imepita.

Tseleng Mochekele

Nilizaliwa katika mji wa Teyateyaneng nchini Lesotho. Mama yangu alipenda sana mambo ya dini, naye alikuwa akinilazimisha mimi na wadogo zangu tuandamane naye kwenda kanisani. Nilichukia kwenda kanisani. Kisha, mamangu mdogo akawa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, naye akawa akimhubiria mamangu mzazi. Nilifurahi sana mama yangu alipoacha kwenda kanisani, hata hivyo, nilipuuza kweli kwa sababu nilivutiwa na ulimwengu na burudani zake.

Mwaka wa 1960, nilihamia Johannesburg ili kumalizia masomo yangu huko. Nilipoondoka nyumbani, mama yangu alinisihi, “Tafadhali, Tseleng, utakapokuwa Johannesburg, watafute Mashahidi na ujaribu kuwa mmoja wao.” Nilipofika Johannesburg, mwanzoni nilivutiwa sana na burudani mbalimbali zilizokuwako jijini humo. Hata hivyo, nilipochunguza kwa makini maisha ya watu, nilishangaa kuona upotovu wa adili uliokuwa umeenea. Kisha nikakumbuka maneno ya mama yangu na kuanza kuhudhuria mikutano ya Mashahidi wa Yehova huko Soweto. Katika mkutano wa kwanza niliohudhuria, nakumbuka nikisali: “Nisaidie, Yehova, kwa sababu nataka kuwa mmoja wa Mashahidi wako.” Punde si punde nikaanza kushiriki katika huduma na kubatizwa mwezi wa Julai mwaka huohuo. Baada ya kumaliza masomo, nilirudi nyumbani kwa mama yangu huko Lesotho. Wakati huo, yeye pia alikuwa amebatizwa.

Mwaka wa 1968, ofisi ya tawi ya Afrika Kusini iliniomba niwe mtafsiri wa Kisesotho. Kwa miaka mingi, nilifanya mgawo huo nikiishi nyumbani kwa mama yangu. Nyakati zilipokuwa ngumu niliipendekezea familia yetu kwamba afadhali niache utumishi wa wakati wote, nitafute kazi ili niwategemeze. Hata hivyo, mama yangu na dada yangu mdogo zaidi, Liopelo, hawakutaka kamwe kusikia hilo. Walithamini sana pendeleo la kunitegemeza katika mgawo wangu nikiwa mtafsiri wa wakati wote.

Mwaka wa 1990, nilijiunga na familia ya Betheli ya Afrika Kusini katika makao mapya ya ofisi ya tawi katika eneo la Krugersdorp, ambapo naendelea kufurahia pendeleo langu la kufanya kazi ya kutafsiri. Sijutii kamwe uamuzi wangu wa kubaki mseja. Badala yake, namshukuru sana Yehova kwa kunibariki kwa maisha yenye furaha na kusudi.

Nurse Nkuna

Nilizaliwa kaskazini-mashariki mwa Afrika Kusini, katika mji wa Bushbuckridge. Akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, mama yangu alinilea katika kweli huku akifanya kazi wakati wote ili kumsaidia baba kuiruzuku familia. Mama alinifundisha kusoma hata kabla sijaenda shule. Hilo lilinisaidia kushiriki kazi ya kuhubiri katikati ya juma pamoja na dada mkongwe aliyekuwa painia wa kawaida. Hangeweza kuona vizuri, kwa hiyo uwezo wangu wa kusoma ulimsaidia katika huduma yake. Hata baada ya kuanza kwenda shule, niliendelea kuhubiri pamoja naye alasiri. Kushirikiana na watumishi wa wakati wote kulinifanya nipendezwe na huduma. Mimi hufurahi ninapoona watu wakichukua msimamo katika kweli. Nilipokuwa na umri wa miaka kumi hivi, nilisali kwa Yehova kuhusu tamaa yangu ya kutumia maisha yangu katika kazi ya kuhubiri ya wakati wote. Nilibatizwa mwaka wa 1983, na miaka michache iliyofuata nilifanya kazi ili kusaidia kushughulikia mahitaji ya kimwili ya familia yetu. Ili kuhakikisha sikuzi tamaa ya pesa ambayo ingenizuia nisifikie mradi wangu wa kuingia katika utumishi wa wakati wote, nilimwomba mama yangu awe akipangia jinsi mshahara wangu utakavyotumika. Kisha, mwaka wa 1987, niliacha kazi wakati ombi langu la kuwa mtafsiri wa Kizulu katika Betheli ya Afrika Kusini lilipokubaliwa.

Kutumikia Betheli nikiwa dada mseja kumeniletea shangwe nyingi. Maelezo yanayotolewa wakati wa ibada ya asubuhi yamenisaidia kuboresha huduma yangu ya shambani. Kutumikia bega kwa bega na waabudu wenzangu wenye malezi tofauti kumenisaidia kuboresha utu wangu wa Kikristo. Ni kweli kwamba sina watoto wangu mwenyewe, hata hivyo nina watoto na wajukuu wengi wa kiroho ambao huenda singepata iwapo ningeamua kuolewa na kuwa na familia yangu mwenyewe.

Wanapoendelea kufanya kazi kwa bidii katika migawo yao ya kutafsiri katika Betheli, wote pamoja, dada hao watatu waseja wamewasaidia watu 36 kuwa waabudu wa Yehova waliojiweka wakfu na kubatizwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 146, 147]

Milima Yenye Fahari

Safu ya Milima ya Drakensberg iliyo nchini Afrika Kusini ina upana wa kilomita 1,050. Hata hivyo, sehemu inayopakana na KwaZulu-Natal na Lesotho ndiyo yenye kuvutia zaidi. Mara nyingi huitwa Uswisi ya Afrika Kusini.

Wapandaji milima huvutiwa na vilele vyake visivyo rahisi kupandwa kama vile kilele cha Sentinel; kilele cha Monk’s Cowl kilicho laini na hatari; na kilele cha Devil’s Tooth chenye utelezi na miinuko mikali. Kupanda milima hiyo kunaweza kuwa hatari. Hata hivyo, ingawa vijia kadhaa vya kwenda kwenye magenge vina mwinuko mkali, si hatari kupanda wala mpandaji hahitaji kutumia vifaa vya pekee vya kupanda milima. Bila shaka, ni muhimu kutii sheria za milima. Ni muhimu kuwa na mavazi ya baridi, hema, na chakula cha kutosha. Kunaweza kuwa na baridi kali na pepo zenye nguvu wakati wa usiku kwenye magenge hayo.

Kila mwaka, maelfu ya watu huacha mikazo na uchafuzi wa hewa ulio majijini na kuja kupanda milima hiyo, kupiga kambi milimani, kupunga hewa safi ya milimani, kunywa maji matamu, na kufurahia milima hiyo yenye fahari.

[Picha]

Picha zilizochorwa na wawindaji wa Afrika Kusini kwenye majabali

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 158, 159]

Anyakuliwa Kutoka Katika Kuwasiliana na Roho na Ndoa ya Wake Wengi

ISAAC TSHEHLA

ALIZALIWA 1916

ALIBATIZWA 1985

MAELEZO MAFUPI KUMHUSU Akiwa amechanganyikiwa kwa sababu ya mafundisho ya dini zinazodai kuwa za Kikristo, alikuwa mganga tajiri wa kienyeji kabla ya kujifunza kweli.

ISAAC na rafiki zake watatu—Matlabane, Lukas, na Phillip—walilelewa katika Milima ya Sekhukhune iliyo upande wa kaskazini-mashariki mwa Afrika Kusini. Vijana hao wanne waliamua kuliacha Kanisa la Apostolic kwa sababu ya unafiki walioona miongoni mwa wafuasi wa kanisa hilo. Walianza kuitafuta dini ya kweli wakiwa pamoja. Baada ya muda, wakapoteza mawasiliano.

Mwishowe, watatu kati ya rafiki hao wanne wakawa Mashahidi wa Yehova, pamoja na wake zao. Namna gani Isaac? Alifuata hatua za baba yake aliyekuwa mganga maarufu. Isaac aliazimia kupata pesa, naye akawa tajiri. Alikuwa na ng’ombe mia moja na pesa nyingi katika benki. Kama ilivyo desturi ya matajiri wengi, Isaac pia alikuwa na wake wawili. Wakati huohuo, Matlabane akaamua kumtafuta Isaac na kumwonyesha jinsi rafiki zake watatu walivyopata dini ya kweli.

Isaac alifurahi kukutana na Matlabane, naye alikuwa na hamu ya kujua kwa nini rafiki zake wa jadi walikuwa Mashahidi wa Yehova. Isaac akaanza kujifunza Biblia akitumia broshua Furahia Milele Maisha Duniani! Katika chapa ya lugha ya kienyeji aliyokuwa akitumia, picha namba 17 inaonyesha mganga wa Kiafrika akitupa mifupa chini ili kutabiri jibu la swali la mteja wake. Isaac alishangaa sana kujifunza katika andiko linalotajwa, Kumbukumbu la Torati 18:10, 11, kwamba mazoea hayo ya kuwasiliana na pepo hayampendezi Mungu. Alihangaishwa na picha namba 25 ya mwanamume mwenye wake wengi. Picha hiyo ina andiko la 1 Wakorintho 7:1-4 linaloonyesha kwamba Mkristo wa kweli hapaswi kuwa na wake wengi.

Isaac alitaka sana kutii Maandiko. Akiwa na umri wa miaka 68, alimwacha mke wake wa pili na kuhalalisha ndoa yake na mke wake wa kwanza, Florina. Pia, aliacha kazi yake ya uganga na kutupa mifupa aliyotumia kutabiri. Pindi moja Isaac alipokuwa akijifunza Biblia, wateja wawili walikuja kutoka mbali. Walikuwa wamekuja kumlipa randi 550 (dola 140 za Marekani wakati huo) alizokuwa akiwadai kwa sababu ya huduma zake za uganga. Isaac alizikataa pesa hizo na kuwahubiria watu hao akiwaeleza kwamba ameacha zoea lake la awali na sasa anajifunza Biblia ili awe mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Muda si muda, Isaac akafikia mradi wake. Mwaka wa 1985, yeye na mkewe Florina wakabatizwa, na kwa miaka kadhaa sasa, Isaac, ambaye sasa ana umri wa miaka 90, amekuwa akitumikia akiwa mzee katika kutaniko la Kikristo.

[Chati/Grafu katika ukurasa wa 124, 125]

MFUATANO WA MATUKIO—Afrika Kusini

1900

1902 Vichapo vya Biblia vyafika Afrika Kusini.

1910 William W. Johnston afungua ofisi ya tawi jijini Durban.

1916 “Photo-Drama of Creation” yafika.

1917 Ofisi ya tawi yahamishiwa Cape Town.

1920

1924 Mashini ya uchapaji yasafirishwa hadi Cape Town.

1939 Gazeti Consolation lachapwa kwa mara ya kwanza katika Kiafrikana.

1940

1948 Jumba la Ufalme lajengwa karibu na Cape Town.

1949 Gazeti la Mnara wa Mlinzi lachapwa katika Kizulu.

1952 Betheli mpya huko Elandsfontein.

1979 Mashini ya uchapaji ya TKS yaanza kutumika.

1980

1987 Betheli mpya yajengwa Krugersdorp; yapanuliwa mwaka wa 1999.

1992 Jumba la Ufalme la kwanza kujengwa haraka Soweto.

2000

2004 Eneo la uchapaji lapanuliwa. Mashini ya uchapaji ya MAN Roland Lithoman yaanza kutumiwa.

2006 Kilele cha wahubiri chafikia 78,877.

[Grafu]

(See publication)

Jumla ya Wahubiri

Jumla ya Mapainia

80,000

40,000

1900 1920 1940 1980 2000

[Chati/Picha katika ukurasa wa 148, 149]

Lugha Chungu Nzima

Kiwanda cha Afrika Kusini huchapisha gazeti la “Mnara wa Mlinzi” katika lugha 33

Mitindo Mbalimbali ya Mavazi

Barani Afrika kuna mavazi na mapambo mengi ya kitamaduni yenye kupendeza

Kizulu

SALAMU “Sanibona”

WANAOKIZUNGUMZA 10,677,000h

WAHUBIRI 29,000i

Kisesotho

SALAMU “Lumelang”

WANAOKIZUNGUMZA 3,555,000

WAHUBIRI 10,530

Kisepedi

SALAMU “Thobela”

WANAOKIZUNGUMZA 4,209,000

WAHUBIRI 4,410

Kitsonga

SALAMU “Xewani”

WANAOKIZUNGUMZA 1,992,000

WAHUBIRI 2,540

Kihosa

SALAMU “Molweni”

WANAOKIZUNGUMZA 7,907,000

WAHUBIRI 10,590

Kiafrikana

SALAMU “Hallo”

WANAOKIZUNGUMZA 5,983,000

WAHUBIRI 7,510

Kitswana

SALAMU “Dumelang”

WANAOKIZUNGUMZA 3,677,000

WAHUBIRI 4,070

Kivenda

SALAMU “Ri a vusa”

WANAOKIZUNGUMZA 1,021,800

WAHUBIRI 480

[Maelezo ya Chini]

h Takwimu zote ni za wastani.

i Takwimu zote ni za wastani.

[Picha ya ukurasa mzima katika ukurasa wa 66]

[Picha katika ukurasa wa 71]

Mti wa “yellowwood”

[Picha katika ukurasa wa 74]

Stoffel Fourie

[Picha katika ukurasa wa 74]

“Studies in the Scriptures”

[Picha katika ukurasa wa 74]

Kutaniko la Durban na William W. Johnston, 1915

[Picha katika ukurasa wa 74, 75]

Johannes Tshange na familia yake

[Picha katika ukurasa wa 75]

Ofisi ya tawi ya kwanza ilikuwa chumba kidogo katika jengo hili

[Picha katika ukurasa wa 77]

Japie Theron

[Picha katika ukurasa wa 79]

Henry Myrdal

[Picha katika ukurasa wa 79]

Piet de Jager

[Picha katika ukurasa wa 82]

Henry Ancketill, 1915

[Picha katika ukurasa wa 82]

Grace na David Taylor

[Picha katika ukurasa wa 82]

Kijitabu hiki cha mwaka wa 1931 kilikuwa na azimio la kukubali jina Mashahidi wa Yehova

[Picha katika ukurasa wa 84]

Familia ya Betheli huko Cape Town mwaka wa 1931, kutia ndani George na Stella Phillips

[Picha katika ukurasa wa 87]

Kunasa sauti katika Kihosa

[Picha katika ukurasa wa 87]

Andrew Jack na mashini ya kuchapisha inayoitwa Frontex, 1937

[Picha katika ukurasa wa 87]

Magazeti ya “Consolation” na “Mnara wa Mlinzi” ya kwanza kuchapishwa katika Kiafrikana

[Picha katika ukurasa wa 90]

Wajumbe wa kusanyiko, Johannesburg, 1944

[Picha katika ukurasa wa 90]

Kutangaza hotuba kwa mabango, 1945

[Picha katika ukurasa wa 90]

Frans Muller na Piet Wentzel wakiwa na vinanda, 1945

[Picha katika ukurasa wa 95]

Gert Nel, mtumishi wa akina ndugu, 1943

[Picha katika ukurasa wa 95]

Kuhubiri mashambani, 1948

[Picha katika ukurasa wa 99]

Andrew Masondo na mke wake wa pili, Ivy

[Picha katika ukurasa wa 99]

Luke na Joyce Dladla

[Picha katika ukurasa wa 99]

“Mnara wa Mlinzi” la kwanza katika Kizulu

[Picha katika ukurasa wa 102]

Mfano wa Velloo Naicker ulisaidia washiriki 190 wa familia yao kukubali kweli

[Picha katika ukurasa wa 102]

Gopal Coopsammy akiwa na umri wa miaka 21, na leo akiwa na mke wake, Susila. Wamesaidia watu 150 kujiweka wakfu

[Picha katika ukurasa wa 104, 105]

Isabella Elleray

Doreen Kilgour

[Picha katika ukurasa wa 108, 109]

ya awali, 1952

Betheli, Elandsfontein, 1972

[Picha katika ukurasa wa 110]

Mambo Makuu ya Kusanyiko

(Juu) Kutolewa kwa kitabu “Children,” 1942; (katikati) wanaotaka kubatizwa, 1959; (chini) Waimbaji wa Kihosa wakaribisha wajumbe wa kusanyiko, 1998

Watu 3,428 walibatizwa mwaka jana!

[Picha katika ukurasa wa 120]

Elijah Dlodlo alivumilia alipopigwa

[Picha katika ukurasa wa 121]

Florah Malinda, painia wa kawaida. Binti yake aliuawa kikatili

[Picha katika ukurasa wa 122]

Moses Nyamussua aliuawa na umati

[Picha katika ukurasa wa 140, 141]

Majumba ya Ufalme Yajengwa Haraka

Kutaniko lililoko Kagiso lilisaidiwa kupata jumba jipya la ibada

Kabla ya ujenzi

Wakati wa ujenzi

Baada ya ujenzi

Kutaniko la Rathanda huko Heidelberg linapenda Jumba lao jipya la Ufalme

Katika nchi 37 za Afrika, majumba 7,207 yamejengwa, na mengine 3,305 yanahitajiwa!

[Picha katika ukurasa wa 147]

Familia ya Rossouw leo

[Picha katika ukurasa wa 150]

Jumba la Kusanyiko la Midrand

[Picha katika ukurasa wa 155]

Msaada unapelekwa Zimbabwe, 2002

[Picha katika ukurasa wa 155]

Watafsiri wameandaliwa programu za kompyuta zinazowasaidia

[Picha katika ukurasa wa 156, 157]

Ofisi ya Tawi ya Afrika Kusini, 2006

Majengo ya makao na ofisi, kiwanda kipya cha uchapaji, na Idara ya Upakizi na Usafirishaji

[Picha katika ukurasa wa 156, 157]

Halmashauri ya Tawi

Piet Wentzel

Loyiso Piliso

Rowen Brookes

Raymond Mthalane

Frans Muller

Pieter de Heer

Jannie Dieperink

[Picha katika ukurasa wa 161, 162]

Namibia

William na Ellen Heindel

Coralie na Dick Waldron, 1951

Ofisi ya kutafsiri ya Namibia

[Picha katika ukurasa wa 167]

Lesotho

(Juu zaidi) Abel Modiba alipokuwa mwangalizi wa mzunguko; (juu) wakaaji wa mapango wanamzingira mmishonari; (kushoto) Per-Ola na Birgitta Nygren

[Picha katika ukurasa wa 168]

Botswana

Ndugu na Dada Thongoana wamhubiria mchuuzi

Kuhubiri kibanda kwa kibanda

[Picha katika ukurasa wa 170]

Swaziland

James na Dawne Hockett

Kuhubiri katika soko la sanaa, Mbabane

[Picha katika ukurasa wa 170]

St. Helena

Kampeni ya “Habari za Ufalme” ilikamilishwa kwa siku moja; (chini) jiji la Jamestown lenye bandari

[Picha katika ukurasa wa 175]

Kusanyiko la kimataifa la 1993

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki